Tuesday, 8 October 2019

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne Ya October 8




Share:

Monday, 7 October 2019

Benki Ya Dunia Yaipatia Tanzania Mkopo Nafuu Wa Dola Milioni 450 Kusaidia Kaya Masikini

Na Eva Valerian, WFM, Dar es Salaam
Benki ya Dunia imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 450 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.035, kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfumo wa Maendeleo ya Jamii- TASAF, awamu ya tatu.

Tukio hilo limefanyika Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu-Hazina Bw. Doto James na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.

Bw. James amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kupatikana kwa mafanikio makubwa ya awamu mbili zilizopita kwa kusaidia kaya masikini kwa kuongeza kipato na huduma za kijamii, kiuchumi ikiwemo kuwaendeleza watoto wao.

“Mpango huu katika kipindi cha pili ni kuwezesha kaya masikini kutumia fursa ya kuongeza kipato na huduma za kijamii na kiuchumi na kuwekeza katika maendeleo ya watoto wao” alisema Bw. James

Alisema malengo mengine yatakuwa ni kutekeleza miradi inayotoa ajira za muda ikihusisha ujenzi wa miundombinu hususan kwenye sekta mahususi kamavile afya, elimu, maji, kuimarisha taasisi na mifumo.

“Awamu hii ya pili inakwenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mkakati wa Kukuza Uchumi na na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) utakao iwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025” aliongeza Bw. James

Katika hafla hiyo Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Dkt. Moses Kusiluka, alisema kuwa kaya masikini watumie fursa hii kwa kuongeza kipato na huduma za jamii kwa lengo la kupunguza umasikini uliokithiri.

Alisema nia njema ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwajali wanyonge na kwa kupitia fedha hizo anaamini jamii itanufaika na ameahidi kuzisimamia fedha hizo kikamilifu ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema TASAF itahakikisha kuwa kaya zinazoishi katika umasikini uliokithiri zinapata stadi na elimu ya utunzaji wa fedha na hatimaye kupata fursa ya kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha na hivyo kukuza uchumi wa kaya zao na kujenga rasilimali watu hasa watoto wanaohudhuria kliniki na wale walioko shuleni ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird amesema Benki yake imefurahishwa na namna Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa fedha na  ilivyotekeleza kwa ufanisi mpango huo wa kunusuru kaya masikini katika awamu zote za uwepo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF

Alisema kuwa kupitia fedha hizo, jamii itaimarisha lishe, maisha ya watu na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari darasani pamoja na huduma za afya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Shaaban Mohamed, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo huo wenye masharti nafuu na kueleza kuwa Zanzinbar imekuwa mnufaikaji mkubwa wa mpango huo wa kunusuru Kaya Masikini.

Mwaka 2000, Serikali ilianzisha Mfumo wa Maendeleo ya jamii –TASAF kwa madhumuni ya kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umasikini. Awamu ya kwanza (TASAF I) ilitekelezwa mwaka 2000 – 2005 ambapo jumla ya miradi ya kijamii 1,704 yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa ikiwemo ujenzi wa madarasa, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mabwawa ya kuhifadhi maji wakati wa mvua, ujenzi wa barabara vijijini, vituo vya afya, nyumba za walimu kwenye Halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mwaka 2005 – 2013 awamu ya pili (TASAF II) ilitekeleza miradi ya kijamii 12,347 yenye thamani ya shilingi bilioni 430 katika Halmashauri 126 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, na kuwanufaisha watu 18,682,208.

“Mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote mbili imepelekea Serikali kutekeleza awamu ya tatu (TASAF III) mwaka 2012, ambayo itatekelezwa kwa miaka 10 mpaka 2023 katika vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza kitafikia ukomo mwaka huu 2019, na Awamu ya Pili ambayo mkatabata wa mkopo umesainiwa, utakamilika mwaka mwaka 2023.

Mwisho


Share:

Picha : BENKI YA CRDB YAZINDUA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA...MKURUGENZI AGAWA CHAKULA KWA WATEJA


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akiwahudumia baadhi ya wateja wa benki hiyo tawi la Kariakoo jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja.
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amewaongoza baadhi ya watendaji wa benki hiyo kugawa chai kwa wateja wao.

Akizungumza akiwa kwenye tawi la Kariakoo jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, Nsekela alisema ni wiki muhimu kwa wateja wa CRDB.

Alisema ni wiki ya viongozi wa benki hiyo kutoka matawi yote kuwafuata na kuwahudumia wateja kwa upendo chini ya kaulimbiu ya 'Ulipo tupo kukupa Magic'.

"Hii ni wiki ya huduma kwa wateja duniani kauli mbiu ya dunia ni 'The magic of service' na sisi benki yetu tunashiriki kwa kuwahudumia wateja wetu.

"Tunawaambia ulipo tupo kukupa Magic. Tumeandaa vitu vingi vizuri naamini wateja wetu watafurahia," alisema Nsekela.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, TullyEsther Mwambapa, alisema wafanyakazi wa benki hiyo watafanya shughuli za kijamii kwa kushtukiza na kuwashukuru wateja wao.

"Ni wiki hii ya huduma kwa wateja, tunaitumia kushukuru wafanyakazi wetu kwa huduma wanazozitoa na kushukuru wateja wetu kwa kutuchagua.

"...Tutawafikia na kuwahudumia wateja wetu kwa kuwashtukiza hivyo wajiandae kwa mambo mazuri," alisema Mwambapa.



Share:

RC MAKONDA AWATAKA TBA KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA HALMASHAURI YA UBUNGO KABLA YA DISEMBA 30


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewataka Wakala wa Majengo Tanzania TBA kuhakikisha ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo unakamilika na kuanza kutumika kabla ya Disemba 30 Mwaka huu likiwa Viwango na Ubora unaotakiwa.

Makonda ameeleza kuchukizwa kuona mkataba wa ujenzi huo umesainiwa tangu Disemba 13 mwaka jana na kazi inatakiwa kukamilika Disemba 13 mwaka huu lakini hadi sasa ujenzi umefikia 35% huku muda wa mkandarasi kuwa site ukiwa mkubwa kuliko kazi aliyoifanya.

Makonda amebaini kuwa ujenzi ulisimama kwa zaidi ya Miezi miwili kwa kigezo cha Manispaa kuchelewa kutoa fedha huku muhusika akikaa kimya pasipo kutoa taarifa kwenye ngazi ya Mkoa ili mkoa uweze kuingilia kati fedha itoke kwa wakati.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Kisasa la Juu (Interchange) Ubungo ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo na kumuelekeza mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Pamoja na hayo Makonda pia amefanya ziara ya Ukaguzi wa Maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha na kueleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Katika ziara hiyo Makonda ametembelea Ujenzi wa Kituo cha Afya Kimara na kumuelekeza Katibu tawala wa Mkoa huo kutuma timu ya kufuatilia upya ujenzi wa Jengo la gorofa katika kituo hicho linalogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 baada ya kubaini gharama za ujenzi ni kubwa kuliko idadi ya majengo wakati Wilaya ya Kigamboni imetumia Bilioni 1.5 kujenga majengo saba ya kisasa.
Share:

Aliyekuwa Mkurugenzi Usalama wa Taifa Afariki Dunia

Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, nchini Apson Mwang’onda amefariki Dunia leo Oktoba 7, 2019 akiwa Afrika Kusini alipokuwa akiatiwa matibabu dhidi ya maradhi yaliyokuwa yakimsimbua.

Apson Mwang’onda alistaafu kazi hiyo Agosti 21, mwaka 2006 kwa mujibu wa sheria.


Share:

KOROGWE MINI MARATHON KUTUMIKA KUMUENZI BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE, KUTIMUA VUMBI OCTOBA 13 MWAKA HUU MJINI KOROGWE

Share:

KIJAZI AMFAGILIA GASPARA KASHAMBA KUANZISHA SHULE


Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tano ya  Shule ya Sekondari ya St. Catherine's iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Oktoba 5, 2019. (Picha na Yusuph Mussa).

Na Yusuph Mussa, Lushoto



KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi amesema kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya St. Cathetine's iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kutawasaidia watoto wa kike kupata elimu, sio kwa wilaya hiyo pekee, bali Taifa zima la Tanzania.


Aliyasema hayo Oktoba 5, 2019 alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tano ya kidato cha nne ya shule hiyo iliyopo kwenye viunga vya Mji wa Lushoto nakusema anaunga mkono mawazo ya muanzilishi wa shule hiyo Mtawa Gaspara Kashamba ambaye kwa sasa ndiyo Mkuu wa Masista wa Usambara (COLU) chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, ambapo Makao Makuu yao yapo Kwamndolwa wilayani Korogwe.


"Nashukuru mawazo ya Sista Gaspara Kashamba kwa kuanzisha shule hii. Hakika atawasaidia watoto wengi wa kike kupata elimu, sio kwa Lushoto tu bali Taifa zima litafaidika. Hivyo naahidi kumuunga mkono kwa nguvu zangu zote kuhakikisha taasisi hii anaikuza na kuwa chachu ya maendeleo nchini" alisema Dkt. Kijazi.


Dkt. Kijazi aliwataka wanafunzi kujali na kuthamini mchango wa wazazi wao kwa kufanya vizuri kwenye masomo, kwani wazazi wao wanahaha usiku kucha ni namna gani watoto wao watapata elimu nzuri, hivyo katika kulipa fadhila hizo, anataka kuona wanafunzi wote 33 kidato cha nne kwenye shule hiyo wanapata daraja la kwanza.


"Moja ya jambo ambalo mnatakiwa kuwatendea wazazi, na ninyi kufika salama kwenye safari yenu ya maisha ni kufanya vizuri kwenye mitihani yenu kwa ninyi wote kupata division one (daraja la kwanza). Nitafuatilia kuona ndoto zenu zinatimia baada ya wote kuniahidi mtafanya vizuri" alisema Dkt. Kijazi.


Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Frank Maduga, ambaye ni Meneja wa NSSF mstaafu wa Mikoa ya Arusha na Tanga, alisema kila siku wanaongeza miundombinu kuona shule hiyo changa inapata mafanikio, na kukiri kwa taaluma si haba, kwani wanafunzi wanaosoma hapo wanajitahidi kufanya vizuri mwaka hadi mwaka.


Akisoma risala yake kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule hiyo Fokas Mjema alisema shule hiyo iliyoanzishwa Januari 12, 2012 na Mtawa Gaspara Kashamba ikiwa na wanafunzi 29 na walimu sita, ilitokana na maombi ya wazazi, kwani tayari alikuwa ana Shule ya Awali na Msingi ya St. Chatherine's, hivyo wazazi wakataka na sekondari iwepo.


"Mama Gaspara Kashamba kama mdau wa elimu, mpenda maendeleo na mkereketwa wa elimu, akaanzisha O-Level (kidato cha kwanza hadi cha nne) hapa mwaka 2012. Na mwaka jana 2018 alianzisha A-Level (kidato cha tano na sita) kwa combination (mchepuo) za PCM, PCB na HGL. Leo shule ina wanafunzi 272. Lengo la mwanzilishi wa shule hii ni kumwelimisha mwanamke  apate elimu bora ya kumfanya akubalike katika jamii. 


"Na lengo letu tunaofanya kazi kwa sasa ni pamoja na kufanya St. Catherine's kutoa elimu bora kwa mtoto wa kike, kuifanya shule yetu kuwa miongoni mwa shule bora kitaifa, kutengeneza mabinti ambao wameiva kitaaluma, kiakili, kiroho na kimaadili, kuhakikisha kwamba ufaulu wa shule yetu unaongezeka siku hadi siku ili wanafunzi wetu wafaulu kwa daraja la kwanza na la pili tu, ili wale wa kidato cha nne wajiunge na kidato cha tano, na wale wanaohitimu kidato cha sita, waweze kujiunga na vyuo vikuu  vizuri hapa nchini na nje ya nchi" alisema Mtawa Mjema.


Mjema ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Masista wa Usambara (COLU), alisema tangu shule hiyo ilipoanza kufaulisha mwaka 2015, wanafunzi watano walipata ufaulu wa daraja la kwanza, 19 daraja la pili, watano daraja la tatu, na hakukuwa na daraja la nne wala sifuri, huku wakishika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya shule 74, na nafasi ya 42 kitaifa kati ya shule 1,162.


Mwaka 2016 daraja la kwanza wanne (4), la pili 12, la tatu 13 na wawili daraja la nne, na kuwa shule ya tatu kimkoa kati ya 99 na 63 kati 1,439 kitaifa. Mwaka 2017 daraja la kwanza wawili, la pili 17, la tatu saba. Nafasi ya pili kimkoa kati ya shule 133, na ya 36 kitaifa kati ya 1,738.


"Mwaka 2018 wanafunzi watano walipata daraja la kwanza, wanafunzi 27 daraja la pili, wanane (8) daraja la tatu na mmoja daraja la nne. Tulishika nafasi ya nane (8) kimkoa kati ya shule 188, na nafasi ya 188 kati ya shule 3,488 kitaifa" alisema Mtawa Mjema.


MWISHO.
Share:

Lukuvi Aahirisha Sherehe Za Siku Ya Makazi Na Kuagiza Fedha Iliyotengwa Kuboresha Mapato Ya Sekta Ya Ardhi

Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameahirisha sherehe za maadhimisho siku ya Makazi Dunia na kuagiza fedha iliyopangwa kwa ajili ya sherehe hiyo shilingi milioni 23 kutumika kuboresha mfumo wa mapato na utoaji huduma za ardhi.

Katika salamu zake za siku ya Makazi Duniani yenye kauli mbiu ‘Matumizi ya Teknolojia Bunifu Kubadili Taka kuwa chanzo cha Mapato’ Lukuvi ametaka maadhimisho ya mwaka huu kutofanyika sherehe na badala yake yatumike kutafakari kauli mbiu ya na kujipanga upya kutekeleza agizo la rais alilolitoa muda mrefu la kuwataka wananchi kujitolea kufanya kazi za usafi katika maeneo ya miji na wanayoishi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaelekeza kutafakari kwa kina namna changamoto ya uwepo wa taka mijini kuwa fursa ya kujiongezea kipato kwa kutumia teknolojia rahisi.

Alisema, mwaka huu inaelekezwa kuingia kwa undani zaidi kutumia ubunifu kubadili taka kuwa mtaji na kuongeza kipato kwa wananchi bila kuathiri afya za wakazi wa mijini na mazingira na hatimaye kupunguza gharama za udhibiti taka.

 ‘’Mamlaka za miji zina wajibu wa kukusanya taka kama mojawapo ya huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi na kwa upande mwingine wananchi wanao wajibu wa kulipia huduma hiyo kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mamlaka za mitaa’’ alisema Lukuvi.

Aliwaasa wananchi kuepuka kutupa taka kando ya mito , maeneo ya wazi , barabarani na katika mitaro ya maji ya mvua kwa kuwa kufanya hivyo kunasababisha uharibifu wa mazingira , kuziba kwa mitaro ya maji ya mvua  na kutengeneza mafuriko.

Aidha, ameaalika wadau wote wenye teknolojia rahisi ya kuchakata taka ngumu kushirikiana na mamlaka za miji nchini ili kutumia ujuzi huo kupambana na changamoto ya wingi wa taka ngumu na kwa njia hiyo wataweza kutengeneza ajira kwa jamii huku miji ikiendelea kuwa safi na afya za wananchi kuimarika.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Makazi Duniani (UN Habitat) kupitia azimio Namba 40/202 la Baraza la Umoja wa Mataifa la mwezi Desemba mwaka 1985 limetenga jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kuwa siku ya Makazi Duniani. Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yalifanyika jijini Nairobi, Kenya mwaka 1986. Mwaka huu Maadhimisho hayo yanafanyika kimataifa katika jiji la younde Cameroun.


Share:

Michael Wambura Aachiwa Huru

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa (TFF), Michael Wambura amebadilishiwa mashtaka na kukabiliwa na shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na amechiwa kwa makubaliano ya kulipa shilingi milioni 100 na laki tisa kwa awamu tano ambapo leo amelipa milioni 20,249,531


Share:

Waziri Mkuu Amuagiza Mkurugenzi Manispaa Ya Singida Awaondoe Wakusanya Mapato Watatu Walioajiriwa KINDUGU na wanatumiwa kuiba mapato.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Manispaa ya Singida, Bw. Bravo Lyapembile awaondoe kazini watumishi watatu wanaokusanya mapato kwenye stendi ya mabasi ambao wameajiriwa kindugu na wanatumiwa kuiba mapato.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 7, 2019), akizungumza na madiwani na watumishi wa Manispaa ya Singida pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Roman Catholic, mjini Singida.

“Kuna vijana watatu pale stendi ambao mmewaweka kindugu. Yupo Kennedy Francis (mtoto wa Mkurugenzi); Selemani Msuwa (ndugu yake diwani) na Salehe Rajab Kundya (shemeji yake diwani mwingine). Andika barua leo hii, hawa vijana waondoke kwenye hiyo kazi, na upeleke timu nyingine ya watu waaminifu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kuna mchezo unachezwa wa kukusanya mapato lakini hayapelekwi benki na wahusika wakuu ni  mweka hazina wa Manispaa, Bw. Aminieli Kamunde na Mkaguzi wa Ndani, Bw. Ibrahim Makana.

Amewaonya watendaji wa kata wanaohusika kukusanya mapato wahakikishe kuwa kila wanapokamilisha makusanyo, wanazipeleka fedha hizo benki na kupatiwa risiti. “Kuna wakusanyaji wanaoshirikiana na baadhi ya Wakurugenzi na Waweka Hazina. Waheshimiwa Madiwani hakikisheni mnasimamia hizo mashine zinazokusanya mapato na mjue ni nani amepatiwa. Ombeni taarifa mjue nani anayo na yuko wapi.”

“Ninawasihi Mstahiki Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri msiingie kwenye huu mkumbo kwa sababu tunataka fedha zilizokusanywa kutoka kwa wananchi zirudi kuwahudumia wananchi.”

Waziri Mkuu amekemea tabia ambayo ameikuta kwenye Halmashauri nyingine ya kubadilisha matumizi ya fedha ambako Mkurugenzi au Mweka Hazina wanawadai watendaji wa kata wawapatie shilingi milioni mbili. “Kwenye eneo hilo, msikubali kupeleka fedha mkononi kwa afisa yoyote. Ninyi pelekeni benki na mpatiwe risiti,” amesisitiza.

Amesema tabia nyingine ambayo ameikuta katika ziara hii, ni kubadilishwa kwa matumizi ya fedha na kuacha malengo kusudiwa ya fedha zilizotumwa. “Fedha inayotoka Serikali kuu ikiletwa inakuja na maelekezo mahsusi. Unakuta fedha inakuja kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, wao wanahmisha na kujilipa posho au inahamishiwa kwenye mradi mwingine.”

“Au unakuta fedha la kulipa likizo za walimu inatumika kwenye miradi ya afya, na Afisa Elimu upo. Na unajua kwamba walimu wanadai likizo zao, unaona sawa tu. Ni lazima tuchukue hatua kwa sababu huu ni mwaka wa nne wa Serikali ya awamu ya tano, na wanajua nini Serikali hii inataka. Tukiwaachia, wataendelea kufanya ubadhirifu tena na tena.”

“Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, simamieni mapato ya ndani na siyo muwe sehemu ya ulaji wa fedha za umma. Waheshimiwa Madiwani simamieni sheria inayosimamia utoaji iwa asilimia 10 ya mapato kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kila mmoja apate haki yake,” alisisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida, Bw. Rashid Mandoa akamilishe malipo ya madiwani ambayo ni malimbikizo. “Nenda kalipe malimbikizo ya wadiwani ambayo yanafikia shilingi milioni 104,” alisema.

Pia amemtaka awasilishe kwenye mfuko wa Hifadhi ya jamii, michango ya madereva ya sh. 15,000 ambayo wamekuwa wakikatwa tangu mwaka 2015/2016 lakini haijawasilishwa. “Hawa walikuwa LAPF, wamekatwa hela zao lakini bado hazijapelekwa.”

“Watu hao pia wamekuwa wakikatwa sh. 5,500 za Bima ya Afya tangu wakati huo lakini hadi sasa michango yao haijawasilishwa na matokeo yake wakienda hospitali hawatibiwi. Hakikisha malipo yao yanaenda,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

WAZIRI MKUU: UAGIZAJI BIDHAA ZA NJE UTAENDELEA KUPUNGUA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano ni bidhaa za mbao na mafuta ya kula.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, bidhaa zetu ni nzuri na zinapendwa na watu wengi hata wa nje ya nchi. Mnachotakiwa kukifanya ni kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo yenu, hii itawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko."

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 7, 2019) wakati akifungua Maonesho ya Sido Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya BomberdiaManispaa ya Singida. Amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini.

“Niwasihi Watanzania wote hasa wale wanaofikiria kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kuachana na dhana hiyo potofu, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili.”

Amesema wakizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi za ndaniitawezesha ajira endelevu kuwepo kwa vijana, itasaidia malighafi kutoharibika lakini pia bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na thamani kubwa badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Amesema uanzishwaji wa viwanda umejikita zaidi katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na maliasili yanayopatikana nchini, kama, kilimo, mifugo, misitu, uvuvi na madini kwani wananchi wengi wanategemea mazao na rasilimali hizo kwa maisha yao.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhimiza uongezaji thamani wa mazao husika kwa kuwa ndiyo njia sahihi.  “Kwa misingi hiyo, usindikaji, uchakataji na uchenjuaji, vitachangia kupunguza upotevu unaotokea msimu wa mavuno, kuongeza ajira na thamani ya mazao kwa lengo la kuwapatia wazalishaji kipato.”

Amesema uongezaji thamani utahitaji teknolojia (mashine na ujuzi), ambapo baadhi ya teknolojia hizo zimeoneshwa kwenye maonesho hayo. “Vilevile, maonesho hayo yametoa fursa ya kuonesha teknolojia zinazoweza kurahisisha uzalishaji na kuleta ufanisi zaidi ili kuongeza tija na kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.”

Mapema, akitoa taarifa kuhusu maonesho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SIDO, Prof. Elifas Bisanda alisema wamekuwa wakiandaa maonesho hayo ili kuwahamasisha wajasiriamali wadogo na wa kati wapate mbinu mpya juu ya viwanda vidogo.

"Pia tumekuwa tukifanya maonesho haya ili kuwapa wananchi uelewa kuhusu bidhaa zinazozalishwa nchini. Tangu mwaka 2006, yalikuwa yakifanyika kikanda, lakini kwa sasa yanafanyika kitaifa," alisema.

Alisema kupitia maonesho hayo, wajasiriamali  hupata mafunzo ya ufungashaji wa bidhaa lakini pia hupata fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwao na kupata taarifa kutoka kwenye taasisi zinazojihusisha na viwanda vidogo na vya kati.

Alisema anaiomba Serikali iwapatie fedha zaidi ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imepeleka umeme hadi vijijini lakini wananchi wengi hawanufaiki na uwepo wa umeme huo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alisema hii ni mara ya pili maonesho hayo yanafanyika mkoani humo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger