Monday, 3 June 2019

Rais Magufuli akutana na Askofu Gwajima Ikulu

RAIS John Magufuli amekutana na kuzungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dkt. Josephat Gwajima leo Juni 3, 2019, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kumaliza mazungumzo yao, Gwajima amempongeza Magufuli kwa ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge akisema umeme wa mradi huo utakuwa mkubwa kuliko umeme wowote ambao Tanzania ilishawahi kuzalisha tangu uhuru, hivyo yatakuwa ni manufaa makubwa kwa taifa letu.

“Tuelewe ili ule chips yai lazima uvunje mayai, namshukuru rais kwa juhudi za Stiegler’s Gorge, tutakapozalisha umeme mwingi kuliko tuliozalisha zamani.  Kama unavyojua watu wengi wa Magharibi wanasema eneo hilo ni la mazingira lakini ukweli ni siasa tu.




Share:

Waziri Mkuu: Kamilisheni Ujenzi Wa Magereza Za Wilaya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Magereza nchini ukamilishe mkakati wa ujenzi wa magereza za wilaya kwa wilaya zisizokuwa na magereza.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 3, 2019) wakati akifungua Gereza la wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja vya gereza hilo.

Waziri Mkuu amesema uwepo wa magereza katika wilaya zote nchini utasaidia kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza ya jirani.

“Kutokuwepo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki.”

Waziri Mkuu amesema kwamba ufunguzi wa gereza la Ruangwa utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la wilaya ya Nachingwea

Awali wakazi wa wilaya hiyo waliokabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa vifungo walikuwa wakipelekwa katika Gereza la wilaya ya Nachingwea.

Amesema kitendo cha kupelekwa Nachingwea kilikuwa kikiwanyima wafungwa na mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliokuwepo.

“Mbali na ndugu na jamaa kushindwa kwenda kuwaona ndugu zao pia Jeshi la Polisi lilikuwa likilaumiwa kuwa linawachelewesha mahubusu kuja kusikiliza mashauri yao.”

Waziri Mkuu amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Ruangwa umeipunguzia Serikali gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa kwenda Nachingwea.

Awali, Waziri waMambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Gereza la Wilaya ya Ruangwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya hiyo.

Amesema gereza hilo ni chachu ya kuimarika kwa uchumi wa wilaya hiyo kwa kupitia sekta ya kilimo kwani kutakuwa na kambi za kilimo, hivyo wananchi nao watajifunza. 

 “Wananchi msilione gereza hili kama adui kwenu, halijaja kuwafunga bali lipo kwa ajili ya kuimarisha amani, ulinzi na usalama wa wilaya yetu pamoja na kutoa elimu mbalimbali.”

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike amesema ujenzi huo umefanywa na kikosi cha ujenzi cha Magereza kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa.

Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa gereza hilo imekamilika na imegharimu sh. bilioni 1.5 hivyo umekamilisha uwepo wa magereza katika wilaya zote za mkoa wa Lindi.

Kamishna huyo amesema ujenzi huo ungefanywa na mkandarasi wa nje ungegharimu sh. bilioni 2.226, hivyo kwa kutumia kikosi cha Magereza wameokoa sh. milioni 635.675.

Amesema kwa sasa gereza hilo lina uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 250 hadi 280 na likikamilika itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi wahalifu 500.

Kamishna Kasike amesema gereza hilo lina ardhi yenye ukubwa wa ekari 80, ambapo ekari saba zitatumika kwa ajili ya majengo ya gereza, maegezo ya magari na karakana.

“Ekari 56 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 100 za makazi, ekari sita ujenzi wa majengo ya huduma kama zahanati na ekari nane zitatumika katika kilimo cha bustani.”

Baadhi ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha huduma za jamii.

Mmoja wa wananchi hao Zena Selemani amesema kabla ya ujenzi wa gereza hilo walikuwa wanashindwa kuwatembelea ndugu zao walofungwa katika gereza la Nachingwea.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Picha : RAIS MAGUFULI ATUMIA KIKAPU CHA ASILI KUNUNUA SAMAKI AKIPIGA MISELE LEO JIONI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akinunua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wafanyabiashara wa Samaki katika Soko la Samaki la Ferry jijini Dar es salaam kuhusu umuhimu wa kutumia mifuko mbadala na kuachana na kutumia mifuko ya plastiki wakati alipopita katika matembezi ya jioni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akinunua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akinunua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipatana bei ya Samaki aina ya Lobster na mmoja wa wachuuzi katika Soko la Ferry mara baada ya kufika eneo hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipatana bei ya Samaki na wachuuzi katika Soko la Ferry mara baada ya kufika eneo hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akinunua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiondoka baada ya kununua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua Samaki kabla ya kumnunua kutoka kwa mfanyabiashara wa Samaki Abraham Kaberege wakati alipkuwa katika matembezi ya jioni katika maeneo ya Soko hilo la Ferry jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akinunua samaki na kuwahifadhi katika kikapu chake cha kiasili wakati alipokuwa matembezini katika maeneo hayo ya Ferry.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wauza kahawa katika eneo la Soko la Ferry ambapo aliagiza kuboreshwa kwa sehemu ya biashara hiyo kuanzia siku ya kesho. PICHA NA IKULU
Share:

MTUHUMIWA ATINGA MAHAKAMANI AKIWA AMEVAA NGUO ALIZOMWIBIA HAKIMU ANAYESIKILIZA KESI

Hakimu katika Mahakama ya Wilaya ya Otuke huko Uganda Kaskazini Alhamisi iliyopita aliachwa na mshangao baada ya mtuhumiwa kuingia mahakamani hapo akiwa amevaa nguo zake zilizoibiwa ambapo  kufuatia tukio hilo Hakimu alilazimika kuahirisha usikilizwaji wa kesi zote za siku ile kwa wiki moja kwa ajili ya kuimarika kutokana na mshtuko alioupata.

Imeelezwa kuwa mshukiwa huyo aliyeingia mhakamani hapo aliachiwa huru na jaji Benjamin Seruru tarehe 24 Mei baada ya kukutwa na hatia za kuiba mabegi, mtuhumiwa huyo Jimmy Oteng (34) mkazi wa Okelo katika kijiji cha Amone alikutwa na hatia za kuiba begi moja la ufuta kutoka nyumba moja huko Okelo mwaka 2018 na akahukumiwa kifungo cha miezi 6 gerezani.

Hata hivyo Mei 24 hakimu Seruru aliamua kumwachia huru baada ya kushindwa kupatikana kwa baadhi ya ushahidi dhidi yake.

Siku moja baada ya kuachiwa kutoka jela Oteng alifanya tukio la wizi nyumbani kwa hakimu huyo kwa kuiba suti jozi nne na nguo nyingine pamoja na madumu mawili ya lita 20 aliyodhani ni ya mafuta ya kupikia na alikamatwa siku ya jumatano wiki iliyopita.

Kamanda wa polisi wa Otuke alilieleza gazeti la Daily Monitor kuwa mtuhumiwa huyo amewahi kuiba katika nyumba mbili za watumishi wa mahakama ambao walieleza kuwa Oteng amewahi kuiba mafuta ya kupikia pamoja na vifaa vingine vya nyumbani na baadaye kwenda nyumbani kwa hakimu kufanya wizi huo.

Imeripotiwa kuwa Oteng amekuwa akifanya matukio hayo wakati mvua ikinyesha au wahusika wakiwa wameenda katika shughuli zao.

Imeelezwa kuwa baada ya kuiba katika nyumba ya hakimu alikutwa na wawindaji wawili amejificha katika kichaka huko Odugu katika kata ya Otuke ambao waliwaita polisi na akakamwatwa akiwa na vitu mbalimbali vilivyoibiwa katika nyumba ya hakimu zikiwemo suti jozi nne.

Kamanda wa polisi alieleza kuwa Oteng alifikishwa mahakamani siku ya alhamisi ambapo hakimu Seruru alihairisha kusikiliza kesi hiyo na kuamuru mtuhumiwa kubaki rumande hadi Juni 11 ambapo kesi hiyo itasikilizwa tena.

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
Share:

ASKOFU GWAJIMA ATINGA IKULU KUONANA NA JPM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dkt. Josephat Gwajima Ikulu jijini Dar es Salaam.

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dk.Josephat Gwajima ametinga Ikulu ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza wazi kwamba ili ule Chips Mayai ni lazima baadhi ya mayai yavunjike.

Ameeleza namna ambavyo anafurahishwa na jitihada za Rais Dk.John Magufuli za kuleta maendeleo huku akitumia nafasi hiyo kumshukuru kwa jitihada zake za ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika Bonde la Mto Rufuji maarufu kwa jina la Stiegler.

Akizungumza leo Juni 3,2019 akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, Askofu Dk.Gwajima amesema ni jambo nzuri kutoa shukrani kwa Rais Dk.John Magufuli kwa jitihada zake za kuleta maendeleo na hasa katika kuimarisha sekta ya nishati ya umeme.

"Kwanza ni jambo nzuri kuelewa ili ule Chips Mayai lazima uvunje baadhi mayai. Kuna mayai lazima yavunje.Namshukuru Rais kwa juhudi zake katika mradi wa umeme wa Stiegler, mahala ambapo tutazalisha umeme mwingi tofauti na hapo zamani.

"Kumbuka wakati wa Mwalim Nyerere,wakati wa Mwinyi, wakati wa Mkapa na wakati wa Jakaya Kikwete tulikuwa tunazalisha umeme kiasi lakini kupitia .... tutazalisha umeme mwingi kuliko Tanzania ilipoanzia,"amesema Askofu Gwajima.

Ameongeza kama ambavyo inafahamika watu wengi wa nchi za Magharibi wanasema eneo hilo ni kwa ajili ya mazingira pamoja na mambo mengine lakini ukweli hizo ni siasa za kimataifa.

"Kwa mfano ukiangalia miaka iliyopita kulikuwa na mkataba kule Japani uliokuwa unafahamika Mkataba wa Kioto na Marekani walikataa kusaini ule mkataba.Hivyo hata sisi tunatakiwa kulinda Interest zetu,"amesema Askofu Gwajima.

Kuhusu ujumbe wake kwa Watanzania,Askofu Gwajima amesema huu ni wakati wa kukimbia na si kutembea hivyo lazima twende na kasi ya dunia."Dunia inakimbia hivyo lazima nasi Watanzania tukimbie ili twende pamoja na dunia."
Share:

Picha: RC TELACK AFUNGUA KIKAO CHA WADAU KUJADILI RASIMU YA SHERIA NDOGO KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI NA MTOTO

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amefungua mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto kwa ajili ya kujadili Mapendekezo ya sheria ndogo za vijiji/halmashauri za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga.

Mkutano huo uliolenga kujadili kwa pamoja mikakati inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga,umefanyika leo Jumatatu Juni 3,2019 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Telack alisema ili kuondoa vifo hivyo ni vyema akina mama wajawazito wanahudhuria kliniki akibainisha kuwa pia ni jukumu la baba kumhamasisha mkewe kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya.

“Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi mkoani Shinyanga vilipungua hadi 56 kutoka vifo 73 mwaka 2017,vifo vya watoto wachanga vilipungua kutoka 915 mwaka 2017 hadi 913 mwaka 2018”,alieleza.

“Ingawa takwimu za vifo zinaonesha kupungua.Nia ya serikali ni kuhakikisha mama mjamzito anajifungua salama na mtoto wake anakua,Sote tutambue kuwa hakuna mama anayestahili kufa wakati wa uzazi wala mtoto mchanga,hivyo ni lazima wadau wote tusongeze jitihada,mikakati na rasilimali ili kuhakikisha tunakuwa na vifo 0”,aliongeza Telack.

Mkuu huyo wa mkoa alisema,Rasimu ya mapendekezo ya uundwaji wa sheria ndogo za kuboresha afya ya uzazi na mtoto imejumuisha mawazo kutoka kwa watendaji wa sekta ya afya ngazi za halmashauri na kusititiza kuwa sheria ndogo zitakazoundwa zisikinzane na Sheria mama,sera na miongozo katika sekta ya afya.

“Ninafurahi kuona kwamba moja ya mkakati katika makubaliano yetu wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ unatekelezwa.Nawaelekeza wanasheria wa halmashauri na Mwanasheria wa mkoa ambao pia ni washiriki wa mkutano huu kutumia weledi wao kushauri na kuhakikisha kwamba kazi hii inakamilika kwa wakati”,aliongeza.

Akiwasilisha rasimu ya sheria ndogo za vijiji/halmashauri za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Rashid Mfaume alivitaja visababishi vinavyochangia vifo vya mama na mtoto kuwa ni kutokuhuduria kliniki kwa wakati na mfumo dume unaosababisha mwanamke kutokuwa na maamuzi.

Alisema sababu zingine kuwa ni kutokufuata ushauri unaotolewa na wataalamu,mila na desturi potofu pamoja na jamii kukosa elimu ya kutosha kuhusu dalili za hatari za mjamzito,mzazi ana watoto wachanga.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akifungua mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kujadili Mapendekezo ya sheria ndogo za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza katika mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto.Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko,kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kujadili Mapendekezo ya sheria ndogo za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Rashid Mfaume akiwasilisha Mapendekezo/rasimu ya sheria ndogo za vijiji/halmashauri za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kujadili Mapendekezo ya sheria ndogo za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga.
Mratibu wa Huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Shinyanga,Joyce Kondoro akitoa taarifa ya huduma za afya ya mama na mtoto mkoa wa Shinyanga.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akiongoza majadiliano wakati wa mkutano wa wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kujadili Mapendekezo ya sheria ndogo za uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga.
Wadau wa huduma za afya ya uzazi na mtoto wakiwa ukumbini.
Wadau wakiwa kwenye mkutano huo.
Wenyeviti wa halmashauri za wilaya wakiwa ukumbini.
Mkutano unaendelea.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Boniface Butondo akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akichangia hoja wakati wa mkutano huo.
Katibu Tawala Msaidizi Serikali za Mitaa Mkoa wa Shinyanga,Alphonce Kasanyi akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya sheria.

Mwenyekiti wa wanasheria wa serikali mkoa wa Shinyanga, Stephen John Magalla akielezea mchakato wa uundwaji sheria ndogo za vijiji na halmashauri.
Mkurugenzi wa shirika la  DSW, Peter Owaga akichangia hoja kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala Simon Berege akichangia hoja ukumbini.

Wadau wakiwa ukumbini.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko akiwa ukumbini.
Mkutano unaendelea.
Wadau wakiwa ukumbini.
Mkutano unaendelea.
Wadau wakiwa ukumbini.

Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akiwa ukumbini.
Mkutano unaendelea.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Rashid Mfaume wakiteta jambo ukumbini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

Mama Aliyetelekezwa Na Mmewe Baada Ya Kujifungua Mapacha Wanne Atua Bungeni Dodoma Ambapo Bunge Limeridhia Kukata Posho Ili Kumchangia Fedha Za Kujikimu.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Mama aliyejifungua watoto Mapacha wanne Radhia Solomon[24] mkazi wa Chemchemi  Magomeni  jijini Dar ES salaam na kutelekezwa na mmewe kwa madai ya kukwepa majukumu leo Juni 3,2019 amewasili bungeni jijini Dodoma ambapo bunge limeridhia kila mbunge wa kiume kumchangia Sh.Laki moja na  kila mbunge wa kike kumchangia Sh.elfu hamsini fedha ambazo zitatumika kumsaidia kujikimu na kuwatunza watoto hao.
 
Akizungumza leo Juni,3,Bungeni jijini Dodoma Spika wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Job Ndugai amesema  jukumu la utunzaji wa watoto ni la kila jamii hivyo bunge limeamua kufanya mchango huo kwa wabunge ili kumsaidia mama na watoto huku akiwaasa wanaume kuacha tabia ya kutelekeza familia zao.
 
Ikumbukwe kuwa Radhia Solomon alijifungua watoto mapacha wanne Januari 8,2019 katika  hospitali ya Muhimbili Dar Salaam ,watoto wa kike wawili Faudhia  na Fardhia  pamoja na wa kiume wawili Suleiman na Aiman  ni pacha wanne ambao  kila mmoja alikuwa na mfuko wake wa uzazi  na gharama ya kuwanunulia maziwa ya SMA ya Kopo  ni Sh.Elfu 40 kwa siku  kwani  alipojifungua afya yake haikuwa nzuri kunyonyesha hali iliyosababisha Mmewe kushindwa kumudu gharama na kuwatelekeza .


Share:

Kanuni bora za ufugaji wa kuku wa kienyeji(kuku Asili)....Soma Hapa Uwe Tajiri

Ufugaji wa kuku wa asili ni nyenzo muhimu katika kupambana na wimbi la umasikini kwa kuongeza kipato cha kaya. 

Hata hivyo, pamoja na soko la uhakika, bado ufugaji kuku haujaweza kutumika ipasavyo kupambana na umaskini unaowakabili Watanzania wengi.

 Ni mazoea kwa jamii nyingi hapa Tanzania kufuga kuku wa asili kama sehemu ya mila na desturi zao. Kuku wa asili amekuwa akifugwa bila ya kupatiwa huduma muhimu kama makaazi bora, chakula cha ziada, tiba, kinga za magonjwa mbali mbali. 

Muhtasari huu unatoa muongozo wa ufugaji wa kuku wa asili ili uweze kuzalisha na hatimae kukuza kuku kwa wingi.

Usafi wa vyombo na mazingira ya kuku
Uchafu ni mama wa magonjwa, hivyo zingatia haya;
1.  Vyombo vya chakula na maji visafishwe mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.

2. Pumba au chakula kilicholowana na kuchanganyika na kinyesi cha kuku kitolowe na kufukiwa.

3.  Choma moto au zika kwenye shimo refu kuku waliokufa kwa ugonjwa.

4.  Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine kwa mfano bata katika banda moja.

5.  Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka katika banda la kuku.

6.  Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia banda na upake chokaa angalau mara moja kwa mwaka.

7.Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu panya na wanyama wakali kama vicheche kuingia katika banda la kuku.


Magonjwa na kinga kwa kuku wote

1.Ndui ya kuku
Huathiri sana vifaranga wanaokua na ujitokeza kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu. Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na hata sehemu nyengine zisizo na manyoya.

2.Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina mengine lufuo, au kideri ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa asili. Ni ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote kijijni.

3.Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu husababisha macho kuvimba na kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana. Kuku wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa. Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.

4.Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri wowote lakini huuwa zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au kinyesi cha kahawia na huzubaa na kuonekana kama wamevaa koti.

5.Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje wanaoshambulia ngozi. Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na kunyonya damu. Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto huuwa vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.

6.Minyoo
Minyoo huweza kudhofisha kuku na kuwafanya waweze kuugua maradhi mengine kirahisi. Muone mtaalaam ukihisi kuku wako wana minyoo.


Chakula cha ziada
1.Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwachanganyia vumbi la dagaa au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye pumba za mahindi.

2.Changanya kikombe kimoja cha vumbi la dagaa na vikombe vitano vya pumba za mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).

3.Mchwa na wadudu wengine wanaweza kutumika kama nyongeza ya protini.

4.Vuna mchwa kwenye vichuguu au tengeneza mchwa katika njia za mchwa.

5. Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi cha ng’ombe na majani makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao katika chungu au ndoo ya zamani.

6Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane kisha weka katika chombo kama ndoo au chungu. Weka chombo chako katika njia ya mchwa ukikigeuza juu chini na subiri hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote vilivyomo na uwamwagie kuku mahali walipo.

Utotoleshaji wa vifaranga
Chagua jogoo bora na tetea bora kuzalisha kuku.

Sifa za jogoo bora
1.  Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na usioangukia upande mmoja.

2.  Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata jogoo mwenye sifa hizi mueke yeye na matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea ishirini jogoo wawili wanatosha.

Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule mwenye umbo kubwa, mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha, kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga.

Uhifadhi wa mayai
1.  Weka mayai mahali safi na penye hewa ya kutosha.

2.  Tumia kasha lililokatwa na kujaza mchanga mkavu na safi au kasha la kuhifadhia mayai.

3.  Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa juu na ile iliyochongoka itizame chini.

4.  Andika namba au tarehe katika siku lilipotagwa.

5.  Mayai yakishatagwa yatolewe na kuhifadhiwa na moja liachwe kwenye kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho yake.

Kuatamiza mayai
1.  Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na uwezo wa kuyaatamia na kuyatotoa yote.

2.  Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.

3.  Mayai ya kuatamiza yasizidi wiki 2 toka kutagwa.

4.  Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza kuchaguliwa hadi yapatikane mayai 10 mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.

5.  Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa kitambaa kikavu na safi au kilichowekwa spiriti

Kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja
1.  Kama unataka kuku zaidi ya mmoja watamie na kutotoa kwa mpigo fanya yafuatayo;

2.  Kuku wa kwanza akianza kuatamia muwekee mayai yasiyo na mbegu mfano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.

3.  Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.

Matunzo ya vifaranga ili kuzuia vifo
Vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa na wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili zingatia yafuatayo;

Ulinzi dhidi ya mwewe na wanyama wengine
1.  Weka vifarang kwenye tega na kuwafunika ili wasiende mbali wakati wa mchana. Wape maji na chakula. Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua. Wakati wa usiku walale na mama yao.

Chanjo ya mdondo kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa kabla ya kuanza kutaga vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya mdondo ya kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya mdondo wafikishapo umri wa siku 18.

Vifaranga ambao historia ya chanjo ya mama haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu baada ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi 3

Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi kwa vifaranga, itolewe hata kama ugonjwa haujajitokeza.

1.  Wape dawa ya amprolium kwa muda wa siku tatu mfululizo mara wafikishapo siku saba tokea waanguliwe kama kinga ya kosidiosisi.

2.  Dawa inaweza kutolewa hata kama wamevuka umri huo. Fuata maelekezo ya mtaalam juu ya kiasi cha dawa kinachopaswa kuchanganwa katika maji au pumba

3.  Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili za kuzubaa kama kuvaa koti wapewe dawa ya amprolium kwenye maji kwa utaratibu ufuatao;

Dawa siku tatu mfululizo: usiwape kwa siku mbili; gawa tena kwa siku tatu

Hitimisho
1.  Hakikisha banda na vyombo vya chakula cha kuku ni visafi kuepusha magonjwa.

2.  Usichanganye kuku na bata katika banda moja

3.  Lisha chakula cha ziada hasa kwa vifaranga.

4.  Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa vitamini A ni vyanzo vikuu vya vifo vya kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako dhidi ya magojwa haya.

5.  Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza kama ilivyoelekezwa ili kuepuka kupata mayai viza.

6.  Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji matunzo mazuri, fuata maelezo kuzuia vifo.

7.  Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo utaongeza mapato yako, jitahidi kuzalisha vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi baadae.

8.  Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae kwa ushauri zaidi.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger