Saturday, 25 May 2019

MWENYE JINSIA MBILI AGOMA KUNYOA NYWELE

Alok Vaid-Menon ni mshairi na mwana harakati wa kutetea wanamitindo waliozaliwa na jinsia mbili (kiume na kike) katika mitandao ya kijamii. Lakini mara nyingi watu hukemjeli.

Mara ya kwanza alipoifahamisha familia yake kuwa ana jinsia mbili na kwamba angelipendelea kuangazia zaidi jinsia ya kike, swali la kwanza lilikua , "Lakini una nywele nyingi sana mwilini! Utapata tabu sana kuzitoa zote ili upate muonekano wa kike, kwa hivyo achana na wazo hilo."

Familia yake iliangazia zaidi nywele nyingi alizokuwa nazo mwilini kiasi cha kumzuia kujitambulisha kwa umma kama mwanamke.

''Watu bado wana uelewa mdogioo kuhusu masuala ya watu waliyozaliwa na jinsia mbili'' alisema Alok Menon.

Jamii imetawaliwa na dhana ya kuwa watu waliozaliwa na jinsia mbili ima wanataka kuwa mwanamume au mwanamke lakini haijawahi kutathmini mahitaji mingine ya watu hao linapokuja suala la jinsi wao wanavyotaka kutambulisha jinsia yao kwa hadharani.

Alipoamua kuangazia jinsia yake ya kike zaidi japo muonekano wake ni wa kiume alijiunga na kikundi cha watu waliyozaliwa na jinsia mbili kama yeye ili kubadilishana mawazo na pia kupeana motisha kuhusu hali wanazokumbana nazo katika jamii.

''Nimekuwa nikibadilisha mavazi yangu kulingana na hisia zangu wakati mwingine navaa mavazi ya kiume na mara nyingine navalia mavai ya kike, hali hiyo ilikuwa ikiwakanganya watu sana'' alisema.

Kwa mfano akivalia rinda, wanawake walikuwa wakimchukulia kama mwanamke mwenzao na umuliza kwa mshangao "Alaa, sasa umekuwa mwenzetu?"
Baadhi ya wenzake katika kikundi alichojiunga nacho walimwambia, ni vyema achague moja kati ya jinsia hizo mbili.
"Ikiwa unataka watu wabadili msimamo wao kukuhusu kama mtu aliyezaliwa na jinsia mbili basi unahitaji kunyoa nywele zote mwilini na kutafuta ushauri wa kitaalamuli upete matibabu itakayokusaidia kusalia na jinsia moja."

Lakini wazo hilo lilimkera sana kwasabau tayari alikuwaakipata ushauri kutoka kwa kila mtu kuhusu maisha yake. Anasema alijiunga na kundi hilo ikidhani kuwa wenzake wataheshimu uamuzi wake.

''Bado kuna dhana kuhusu urembo ambayo ni kigezo kinachoongoza jinsia ya kike - kwamba haiwezekani uwe mwanamke ukiwa na nywele kila mahali mwilini'', alisema Menon.

Hata hivyo bado anakabiliana na changamoto ya kujieleza yeye ni nani huku wale wanaomuelewa hasa katika mitandao ya kijamii wakimshauri aachane na juhudi za kutafuta muonekano wa kuwa mwanamke.

Wanafanya hivyo kwa kumjali lakini anasema kuwa yeye hujiuliza maswali mengi sana kama vile "Wananitakia nini wakati ni uamuzi wa kibinafsi?"

Mara ya kwanza alipogundua kuwa anastahili kuchukia nywele na nyingi mwilini alikuwa na miaka 10.

Dada yake mkubwaa mbaye wakati huo alikuwa na miaka 13 alikuwa na nywele kidogo tu zilizomea makwapani.

''Nywele zangu zilipoanza kumea zilinijaa kila sehemu mwilini'', alisema Menon.

Anaongeza kuwa alishangazwa na jinsi kila mtu katika familia yake alivyokuwa akijitolea kumnyoa.

Ni hapo alianza kuwa kujiuliza maswali kuhusu nywele zake na alipouliza maswali zaidi alifahamishwa kuwa zilitokana na maumbile yake.
Nywele ziliendelea kumea kadri alivyokua mkubwa na alihisi uchungu wakati wa kunyolewa hadi baba yake akaamua kuwa asinyolewe tena kutokana na matatizo aliyokuwa akipata.

''Nilimraia baba aniruhusu kunyoa nywele zangu mwilini lakini alikataa kabisa''

Watoto shuleni walikuwa wakimkejeli kwa kuwa na nywele nyingi mwilini, huku wengine wakimfananisha na "mnyama" au uchafu.

Alipofikisha miaka 11, kejeli kutoka kwa watu zilizidi kiasi cha wengine kuitenga familia yake wakidai ni ''magaidi''

Alikuwa akiishi na jamaa zake katika mji mmoja jimboni Texas Marekani katika moha ya maeneo yaliokuwa na jamii ya wahindi waliokuwa wachache.

Watu walianza kuwaita magaidi na wakati kuna mmoja mtu alimuuliza, "Kwanini watu wako wamekufanyia hivi?"

Alipofikisha umri wa miaka 13 hatimae baba yake alimruhusu kunyoa nywele zake mwilini.

''Nakumbuka hiyo siku, nilijihisi vizuri sana kwasababu sasa nitafanana na wasichana wenzangu darasani'', alisema.

''Kwa kweli hatua hiyo ilinisaidia kwasababu kejeli zao zilipungua.''

Alipojiunga na shule ya upili hali ilibadilika kabisa kwani wanafunzi wenzake walishangazwa na uwezo wake wa kufuga ndevu hadi zikawa kubwa kiasi hicho.

''Hata nilijiunga na kundi lililojiita ''ndevu za amani''ambapo tulikua tukijadili masuala kama kujiepusha na ghasia na vurugu shuleni- Nakumbuka nilipewa tuzo kutokana na ndevu zangu nyingi.''

Hatua hiyo ilimfanya ajipende na kujithamini zaidi na ni hapo anasema ''Niliamua kufanya maamuzi yangu mwenyewe kuhusu muonekano unaoniridhisha''
Anasema kuwa na nywele nyingi mwilini hakustahili kuhusishwa na jinsia ya mtu kwasababu kila mtu ana kiwango fulani cha nywele mwilini mwake.

''Sioni kwanini kitu ambacho kinatokana na maumbile yamtu kinaweza kuwafanya watu kumhukumu muathiriwa''

Menon anasema watu wanaofanya biashara ya kuuza wembe na krimu za kuondoa mwele mwili hawangelipata umaarufu kama kila mtu angelizipenda nywele zake mwilini.

''Napenda kuchezea nywele zangu za mwilini kwasababu zinaniliwaza, wakakati mwingine nahisi kana kwamba ni blanketi inayoniongezea joto mwilini''

Anaongezea kusema kuwa anapendelea kuona nywele zake zikichomoza nje ya nguo yake ''Nazichukulia kama sehemu ya urembo wangu'' alisema.

Lakini suala la kufuga nywele kwa watu waliozaliwa na jinsia mbili lina madhara makubwa kama vile kunyanyaswa na watu.

Wataalau wa tiba kwa watu hao wanasema kufanya hivyo ni kuhatarisha maishakwani popote wanapoenda wanavutia hisia za watu ambao wakati mwingine hufikiria wao ni wapenzi wa jinsia moja.

Suala la kutaka kujionesha ndio linachangi wao kuvamiwa hadharani na kutusiwa mitabndaoni kila siku.

Utafiti unaonesha watu waliozaliwa na jinsia mbili wanakabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo kutokana na kejeli zawatu wengine katika jamii.

Alok Menon anasema Pengine maisha yangekuwa tofauti kama ningelinyoa,lakini kwanini iwe hivyo?'

Kuwa na nywele mwilini anasema ni sehemu ya maumbile yake na kwamba ni uamuzi wa kibinafsi wa kuuambia ulimwengu, "Niko hapa kuishi!"

Picha za zimepigwa na Brian Vu.

Chanzo- BBC
Share:

MAREKANI YATISHIA KUIWEKEA VIKWAZO UTURUKI KUHUSIANA NA MAKOMBORA YA URUSI


Marekani imetishia kuiwekea vikwazo Uturuki endapo haitoacha kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 kutoka Urusi.

 Uturuki inakusudia kulilinda anga lake kwa kutumia mfumo huo wa ulinzi uliotengenezwa Urusi, lakini maafisa mjini Washington wanaitaka Uturuki ambayo ni mshirika wake katika ya Jumuiya ya kujihami NATO kununua mfumo kama huo wa ulinzi uliotengenezwa Marekani. 

Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha CNBC, serikali ya Marekani imeipatia Uturuki muda wa wiki mbili kuachana na mfumo kutoka Urusi la sivyo itakabiliwa na vikwazo ikiwa ni pamoja na kuacha kuiuzia ndege za kivita za F-35. 

Hata hivyo mapema wiki hii waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar alisema vikosi vyake tayari vinapokea mafunzo ya kutumia mfumo wa S-400 nchini Urusi na kuwa mfumo huo ulitarajiwa kuwasili nchini Uturuki mwezi Juni au Julai.


Share:

AJIFUNGUA MTOTO CHOONI BILA KUJUA KAMA ANA MIMBA

Mwanamke mmoja amepata zaidi ya alichokuwa amekinunua alipoenda dukani kununua mahitaji yake. Alitoka dukani akiwa mama wa mtoto wa kiume.

Kylie Hagger, mwenye umri wa miaka 21, alikuwa hafahamu kuwa yeye ni mjamzito na muda mfupi baada ya kufika dukani alijihisi anahitaji kwenda chooni kujisaidia.

Lakini kumbe alikuwa anataka kujifungua jambo ambalo hata yeye mwenyewe alikuwa halifahamu.

Wafanyakazi wa dukani hapo iliwabidi wamsaidie kabla ya mhudumu wa afya hajafika.

Mwanamke alieleza hali iliyomtokea kuwa ni ya kushangaza lakini ilikuwa ni siku ya maajabu kwake na kuwashukuru wafanyakazi wa dukani hapo na watu wengine waliokuepo kumsaidia na mahitaji ya mtoto kwa haraka.

Bi. Hagger , ambaye ana watoto wengine wawili, alikuwa hana wazo kuwa ana ujauzito, alisema mama yake Hagger.

Uzazi huo wa kustahajabisha ulitangazwa kwenye mitandao ya kijamii wa jumuiya ya Wisbech; " Tunahitaji watu wenye ukarimuwa kama wa watu wa Wisbech , alijifungua mtoto wake chooni- Alikuwa hafahamu chochote kuwa ana ujauzito, mahitaji yoyote ya mtoto yanapokelewa- Asanteni sana."

Wakazi wa Cambridgeshire walijitokeza kumsaidia mahitaji mbalimbali ya mtoto.

Na jana mama huyo aliweka picha yake akiwaa na mtoto katika mitandao ya kijamii.

"Ninataka kuwashukuru kila mmoja aliyejitokeza kunisaidia kwa kuchangia nguo, vyombo vya mtoto na vitu vingine vingi, ninashukuru sana." aliandika mama huyo aliyejifungua bila kutarajia.

Mmiliki wa duka lililomsaidia mwanamke huyo kujifungua aliwasifu wafanyakazi wake wawili waliomsaidia Hagger kujifungua mtoto salama."Mimi na mtoto wangu tuko salama na afya njema,"aliandika Hagger.

"Sijui ni namna gani mliweza kufanya kazi hiyo ya ukunga lakini labda inawezekana tukawasaidia mama wengine wengi kujifungua hapa pia" mmiliki wa duka.
Chanzo - BBC
Share:

Makampuni Matatu Yatakayosafirisha Mashabiki Wa Soka Kulekea Misri Na Taifa Stars Yatangazwa

SERIKALI kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) imeyataja Makampuni matatu yatakayotumika kusafirisha Mashabiki wa Soka na Watanzania kwa ajili ya kuishangilia Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakati wa Michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Mwezi Juni, mwaka huu nchini Misri.

Akizungumza na Waandishi wa Vyombo ya Habari leo Jumamosi (Mei 25, 2019), Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo aliyataja Makampuni hayo kuwa ni pamoja na Clouds Entertainment Group Ltd, Travel Link na World Link, ambayo yalishinda mchakato wa ushindani na makampuni mengine kutokana na kukidhi vigezo mbalimbali vilivyoanishwa.

Kwa mujibu wa Singo alisema Serikali na kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) waliamua kusimamia mchakato wa kupata makampuni hayo ili kuzuia aina yoyote ya utapeli kwa Watanzania hususani Mashabiki wa Soka wa hapa nchini watakaojitokeza kwenda Nchini Misri kuipa nguvu ya ushingiliaji Taifa Stars.

“Katika miaka ya nyuma kulikuwa na utapeli katika haya makampuni ya usafirishaji, hivyo Serikali kwa kushirikiana na TFF tumeyapata Makampuni matatu, bei zao zitakuwa rahisi na wamepanga kuwa na nembo ya pamoja ambayo wataitangaza ili iweze kujulikana na Watanzania” alisema Singo.

Aidha Singo alisema kuhusu utaratibu wa visa za kusafiri makampuni hayo kwa kushirikana na TFF yatatoa taarifa ya jinsi Mashabiki wa Soka watavyoweza kupata huduma hiyo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi tarehe 21 Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Clouds Entertainment Group Ltd, Shaffih Dauda alisema Kampuni yao imejipanga vyema kuhakikisha kuwa inatoa huduma zote muhimu kwa Watanzania watakaosafiri kwenda Nchini Misiri kuishangalia Taifa Stars ikiwemo visa, usafiri wa ndani, malazi katika kipindi cha siku 10 za mechi tatu za makundi itayocheza Taifa Stars.

“Clouds Entertainment Ltd kila mwaka tuna msimu wa kulevya wa soka, mwaka jana tulikuwa na  Msimu wa kulevya wa Kombe la Dunia kule nchini Urusi, na sasa tunarudi Afrika na tutawahudumia vyema mashabiki watakaojitokeza kwa kiasi cha Dola za Kimarekani 1650 na pia tutaoa ofa ya Mashabiki hao kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini Misri” alisema Dauda.

Aliongeza kuwa katika kutoa urahisi wa huduma kwa Watanzania hususani suala la malazi, Kampuni yao tayari kwa kushirikiana na wakala wao aliyopo nchini Misri, wamepata mmoja wa Mitaa maarufu nchini Misri ujulikanao Kilimanjaro ambapo utawezesha Mashabiki wa Watanzania kupata huduma zote muhimu kuwafanya Mashabiki hao huko kujiona kuwa wapo nyumbani.

Kwa upande wake, Meneja Maendeleo ya Masoko wa Kampuni ya World Link, Zaki Admani alisema kampuni hiyo itatoza kiasi cha Dola za Kimarekani 1550 kwa Mashabiki wa Soka, ambayo watasafiri kuelekea Nchini Misri pamoja na kutoa ofa ya kuchagua mechi moja yoyote ambayo mshabiki wa Soka atapenda kuingalia katika timu zitakazochuana na Taifa Stars.

Aliongeza kuwa kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo Kampuni hiyo itatoa kifurushi kitakachomwezesha Shabiki wa Soka hapa nchini kuweza kuchagua idadi ya mechi ambazo atapenda kuziangalia wakati akiwa na Timu ya Taifa Stars nchini Misri.

“Wapo wengine watapenda kuangalia mechi moja, na hili tumeliangalia na mapema wiki ijayo kuanzia jumatatu tutatoa utaratibu wake wa namna ya kuwasaidia mashabiki wa aina hii” alisema Admani.

Naye Meneja Utawala wa Kampuni ya Travel Link, Ephrem Mtuya alisema kuwa kwa miaka 15 sasa Kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi pamoja na TFF kwa ajili ya kuwasifirisha wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania katika nchini mbalimbali na hivyo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kusafiri na Kampuni hiyo ili kwenda kuipa nguvu Timu ya Taifa ya Tanzania ikiwa nchini Misri.

Alisema Kampuni imeweka kiwango cha Dola za Kimarekani 1300 pekee kwa Mtanzania yotote atayapenda kusafiri na Timu hiyo hususani Mashabiki wa Soka ikihusisha Gharama za Tiketi ya Ndege, usafiri, pamoja na huduma za malazi.


Share:

Maelfu ya Wananchi waAfrika Kusini Walipuka Kwa Shangwe Baada ya Rais Magufuli Kuingia Uwanjani

Umati mkubwa wa wananchi umelipuka kwa shangwe na chereko wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipowasili  katika uwanja wa michezo wa Loftus Versfeld jijini Pretoria kuhudhuria sherehe za kuaishwa kwa Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa leo Jumamosi Mei 25, 2019



Share:

JE ULISHAWAHI KUSIKIA HABARI ZA MWANAMALUNDI?? YULE MSUKUMA MWENYE MIUJIZA?? ....SOMA HAPA


Mwanamalundi ni jina ambalo lilikuwa maarufu sana karne ya 18 na 19 (enzi za mkoloni) maeneo ya kanda ya ziwa; hususani Mwanza na Shinyanga. Habari za huyu mtu zimewahi kuandikwa kwenye kitabu kiitwacho "MWANAMALUNDI: Mtu maarufu katika Historia ya Usukuma". Ni kitabu ambacho kiliingizwa kwenye mtaala wa elimu ya msingi miaka ya 1970-80. Wazee wenzangu watakuwa wanakumbuka. Hivi sasa habari za mtu huyu ni Kama vile zimepotea kabisa.

MWANAMALUNDI NI NANI HASA?

Mwanamalundi ni jina la mtu wa miujiza kutoka kabila la Wasukuma. Matamshi sahihi ya jina hili Ni "Ng'wanamalundi" na sio "Mwanamalundi" kama ambavyo wengi hutamka.

Mwanamalundi alizaliwa kijiji cha Ng'wakwibilinga, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mwaka 1892. Baba yake aliitwa Bugomola na mama yake aliitwa Ngolo. Wazazi hawa wawili hawakujaaliwa kupata watoto kwa muda mrefu sana. Uzee uliwakaribia bila hata kupata mtoto. Jambo hili liliwakosesha sana raha, hasa Mzee Bugomola ambae alitamani sana japo apate mrithi wa mali zake. Hali hii ilimfanya Bugomola kuwa mtulivu na mpole muda mwingi katika maisha yake.

Katika jamii ya wasukuma wakati huo, mwanamke asiposhika mimba ndani ya kipindi cha miezi 6 hadi 12 tangu aolewe, ilikuwa ni lazima aende kwa mganga kujua kinachomsumbua. Ni nyakati ambazo hakukuwa na makanisa ya maombezi kama ilivyo leo hii, misikiti ya kuomba dua wala hospitali. Waganga ndio watu pekee waliotatua matatizo mbalimbali ya jamii zao.

Mzee Bugomola na mke wake Ngolo wakaamua kwenda kwa mganga upande wa mashariki ya kijiji walichokuwa wakiishi (Ng'wakwibilinga) ili wapate ufumbuzi wa tatizo lao. Mganga aliwaambia ujio wao hata kabla hawajajieleza wenyewe. Mganga akawatengenezea dawa kisha akawaambia kuwa Ngolo (mama/mke) atashika mimba na atazaa mtoto wa kiume ambae atakuja kuwa mashuhuri siku za hapo baadae lakini kwa bahati mbaya Bugomola (baba/mume) hatoweza kumuona mtoto huyo; yaani Bugomola atafariki kabla mtoto hajazaliwa.

Habari hii ilimfurahisha sana Bugomola pamoja na kwamba aliambiwa atakufa bila kumuona mtoto. Mkewe pia alifurahi kusikia kuwa atashika mimba. Bugomola hakujali kifo chake sababu hata umri wake ulikuwa umeenda kidogo. Furaha yake kubwa ilikuwa ni kumpata mrithi wake. Walirudi nyumbani wakiwa na furaha kubwa. Bugomola hakuweza kuificha furaha yake. Muda mwingi alionekana ni mwenye tabasamu na vicheko vingi tofauti kabisa na vile watu wavyomzoea kumuona.

Baada ya wiki kadhaa Ngolo alishika mimba. Mimba ilipotimiza miezi mitatu tu, Bwana Bugomola aliaga dunia bila hata kuugua. Ngolo ambae alikuwa mjane wakati huo aliilea mimba hiyo hadi ilipofikisha miezi 9.

Siku moja kabla Ngolo hajajifungua mtoto, wingu kubwa lilitanda angani. Mvua kubwa na yenye radi kali ikaanza kunyesha. Mtoto aliyekuwa tumboni akaruka mruko usio wa kawaida na kisha ikaskika sauti ya kitoto kutoka tumboni ikisema, "máyù nibyalage, yaani mama nizae!" Ngolo akashtuka na kuingiwa hofu baada ya kuskia sauti hiyo, hivyo akamuita mama mkwe wake na baadhi ya majirani ili nao waweze kuwa mashahidi wa sauti hiyo. Kwa bahati nzuri sauti ile ikajirudia tena na ghafla uchungu ukamshika Ngolo. Ilikuwa ni mwaka 1892 Ngolo alipojifungua mtoto wa kiume mwenye maajabu tangu akiwa tumboni mwake. Mtoto huyo akaitwa Igulu, yaani Mbingu.

Igulu (Mwanamalundi) alizaliwa akiwa mwenye afya njema kabisa isipokuwa tu miguu yake ilikuwa myembamba na yenye nyayo kubwa tangu alipozaliwa. Kutokana na wembamba wa miguu yake, jamii ikampa jina la utani "Mamilundi" likimaanisha "mamiguu membamba".

Igulu alikuwa ni mtu mwenye aibu sana enzi za utoto wake. Alikuwa akiwakimbia wageni wasimuone na kuuficha uso wake kwa aibu. Pamoja na aibu alizokuwepo nazo, alipenda sana kuzurura mitaani akiwa ameambatana na marafiki zake. Baadhi ya wazazi hawakupendezwa na tabia yake ya uzururaji akiwa ameambatana na watoto wao. Mara kadhaa wazazi wa marafiki wa Igulu walimtamkia Igulu (Mwanamalundi) maneno mabaya kila Igulu (Mwanamalundi) alipotoka kuzurura na watoto wa majirani zake, walimwambia, “Mamirundi galyo lilihumbura bana bise”, ikiwa na maana "mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.

Katika ujana wake Igulu, alipenda sana kucheza ngoma aina ya Kahela. Kila aliposhiriki kucheza ngoma hiyo, alipenda sana kuuficha uso wake kwa kitambaa cheusi. Katika mashindano ya kucheza ngoma hiyo, Igulu na marafiki zake walishindwa kuwa washindi. Watu kama Samíke, Ng'wanikinga, Ng'wanilong'ho na Gíndù Nkíma walikuwa si rahisi kuwashinda katika uchezaji wa ngoma. Ni watu ambao walijua kucheza ngoma kwa umahili kuliko Igulu (Mwanamalundi). Mara nyingi matumizi ya uchawi yalihusika katika kuwapa ushindi wa kucheza ngoma hiyo na kukubalika kwa watu mbalimbali.

Kutokukubalika kwa Igulu (Mwanamalundi) na marafiki zake mbele ya jamii hasa katika uchezaji wa ngoma kulipelekea achukue uamuzi wa kwenda kwa mganga. Igulu aliwashawishi vijana wenzie waende kwa mganga atakaewapa dawa ya mvuto kwa watu na kuwa washindi nyakati zote za mashindano ya ngoma. Vijana wenzie walikubali sababu kwa nyakati zile suala la kwenda kwa mganga lilikuwa ni jambo dogo sana.

Safari ya kuelekea mashariki zaidi mwa kijiji chao ikawadia. Mganga alikuwa ni mwanamke, mwenye umri ufaao kuitwa bibi ndani ya kijiji cha Nyaraja, wilaya ya Iramba mkoa wa Singida. Walipokelewa vizuri na mwenyeji wao. Iliwachukua wiki moja bila kuhudumiwa chochote kile, siku ya nane mganga akawaamuru wachukue panga na majembe kuelekea porini ili wakachimbe dawa itakayowasaidia kupendwa na watu.

Wakiwa porini, yule bibi mganga alitafuta vinyonga watatu kwa idadi ya vijana hao wanaotaka dawa kisha akawaambia wachimbe mashimo yenye nusu ya urefu wao. Vijana wakachimba mashimo hayo huku wakiwa na vinyonga vichwani mwao. Walipomaliza kuchimba, bibi mganga akawaambia wafunike mashimo hayo kwa kuni kavu. Vijana hao wakatii maagizo ya bibi mganga na kisha bibi akawatoa vinyonga waliokuwa wameng'ang'ania kwenye vichwa vya vijana hao watatu na kisha akawatia dawa midomoni vinyonga hao na kisha akawaweka juu ya kuni zilizofunika mashimo yale yaliyochimbwa na vijana wale watatu. Mara baada ya kuwaweka vinyonga hao juu ya kuni zile, moto ukawashwa ili kuwachoma vinyonga hao.

Hazikupita dakika kadhaa wakiwa wanashuhudia kuteketea kwa vinyonga hao, ghafla akatokea kifaru katika mazingira ya kutatanisha na akaanza kuwafukuza watu wote, akiwemo yule bibi mganga. Igulu (Mwanamalundi) ilimlazimu apande juu ya mti kujinusuru na madhira hayo. Wale vijana wawili walitimka mbio na hawakurudi tena. Bibi mganga akararuliwa na yule kifaru mpaka akapoteza maisha na kisha kifaru akamjia Igulu (Mwanamalundi) aliekuwa juu ya mti na kuanza kuudhuru ule mti kwa pembe yake. Kifaru hakufanikiwa kuuangusha mti aliopanda Igulu zaidi ya kuubandua magome yake. Kifaru alipochoka akaamua kuondoka na kutokomea kusikojulikana.

Igulu (Mwanamalundi) akashuka juu ya ule mti na kumwendea bibi mganga ambae muda huo alikuwa ni marehemu. Igulu akaubeba mwili wa yule bibi mganga na kuurudisha nyumbani. Akiwa njiani, ule mwili wa bibi mganga uliokuwa mabegani mwake ukaonesha kuwa ni kama vile unavuta pumzi mapafuni. Ghafla yule bibi akapiga chafya na kuamka kisha akamuuliza Igulu (Mwanamalundi), "Bhaja hálí abhayanda abhalaha" akimaanisha kuwa wako wapi vijana waliokuwa hapa? Igulu akamwambia kuwa wale vijana wenzie wamekimbia baada ya kumuona yule kifaru. Bibi mganga ambae muda huu alionekana kuwa ni mzima kabisa na hana majeraha tena akaomba warudi eneo la tukio ili wachukue dawa. Wakiwa njiani kurudi eneo la tukio, yule bibi mganga akamsifia sana Igulu kwa kumuita "Ni mwanaume kamili" aliekuja kweli kutafuta dawa. Bibi akaokota yale magome yaliyobanduliwa na kifaru na kisha kuondoka nayo.

Walipofika nyumbani, yule bibi akaamua kumwambia ukweli Igulu (Mwanamalundi) kuwa yule kifaru ni yeye mwenyewe bibi. Aliamua kujibadili ili kuwapima uwezo wao wa kuvumilia magumu. Kwa kuwa Igulu pekee ndio alionesha yuko imara, bibi yule alimtunuku dawa nzuri zitakazompa mvuto na nguvu katika ngoma zake. Wale vijana wawili walipitiliza hadi kwao bila kurudi tena kwa mganga. Bibi mganga alimpa masharti Igulu baada ya kumpa dawa. Bibi mganga alimzuia Igulu (Mwanamalundi) kumparaza mtu yeyote au kumnyooshea kidole. Iwapo atafanya hivyo basi alieparazwa au kunyooshewa kidole atakufa hapohapo.

Igulu (Mwanamalundi) aliporudi kijijini kwake na kisha kucheza ngoma ya kwanza baada tu ya kurudi kutoka kwa mganga, alishinda. Kuna nyakati Igulu aliamua kucheza ngoma akiwa juu ya jiwe kubwa. Wakati akicheza ngoma hizo, nyazo zake zilionekana juu ya mawe aliyokuwa akitumia kucheza ngoma. Ni alama za nyayo ambazo zipo mpaka leo pale kijiji cha Nyandekwa, wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga. Ni kama km 10 tu kutoka makao makuu ya wilaya. Kuna nyakati Igulu alitengeneza mashimo ya mchezo wa bao juu ya jiwe kwa kutumia kisigino chake. Ni alama ambazo pia bado zipo kijiji cha Nyandekwa, Kahama-Shinyanga.

Igulu aliposhinda mashindano ya ndani ya kijiji, akaamua kuomba kushindana na wapinzani wakubwa zaidi walioishi kijiji cha Ng'wagala wilaya ya Maswa; yaani akina Samíke, Ng'wanikînga, Ng'wanilog'ho na mwanamke mwenye nguvu za kiganga aitwae Gíndü Nkíma. Hawa watu wanne walikuwa hawana mpinzani katika ngoma lakini Igulu (Mwanamalundi) akajitosa kushindana nao kwa mara nyingine.

Mwanamalundi alipofika kwenye mashindano, akafanya miujiza kwa kujirefusha kama ngongoti asiye na magongo yoyote yale na kisha akaanza kucheza huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa cheusi kama kawaida yake. Wakati anacheza ngoma akiwa ana urefu wa ngongoti, baadhi ya watu walijaribu kugusa na kuifunua miguu yake ili wajue kulikuwa kuna nini. Wote waliothubutu kuigusa walikufa baada ya muda mfupi. Katika ngoma hiyo, Gíndü Nkíma akatumia nguvu zake za kiganga kumrudisha Igulu (Mwanamalundi) kama alivyokuwa awali; yaani pasipo kurefuka kama ngongoti. Kwa kufanya hivyo, Mwanamalundi alipoteza pambano hilo.

Mwanamalundi akaondoka Maswa na kwenda kijiji cha Nela ambako lilipangwa shindano jingine. Shindano hili Mwanamalundi alishinda. Kwa kuwa katika safari zake zote huambatana na jopo la wapishi wa chakula, ushindi huu ulimkwaza Gíndü Nkíma, mpinzani wake mkubwa ambae aliamua kuloga chakula anachoandaliwa Mwanamalundi ili kisiive hata kikipikwa wiki nzima.

Ni kweli kabisa, wapishi wa Mwanamalundi walilalamika kuhusu chakula kutoiva kabisa kwa muda mrefu na kuni zinakaribia kuisha. Hivyo wapishi wakaomba msaada wa kuni kwa Mwanamalundi. Baada ya wapishi kulalamika, Mwanamalundi akasonta/akanyoosha kidole kwenye pori fulani eneo hilo na kuwaambia wapishi waende wakakate kuni alikonyooshea kidole. Kwa bahati mbaya wakati ananyoosha kidole hicho hakujua kama ndani ya pori hilo kulikuwa kuna mifugo na wachungaji kadhaa ambao wote walikufa na kukauka kama kuni.

Tukio hili la kukausha miti na kuua ng'ombe na wachungaji wake lilimuudhi sana Mtemi Masanja wa III ambae aliamuru askari wake waende kumkamata Mwanamalundi haraka iwezekanavyo ili awajibishwe. Askari wa Mtemi Masanja waliogopa sana kumkamata Mwanamalundi wakihofia kufa. Iliwalazimu kumkamata tu sababu walimuogopa zaidi mtemi kuliko Mwanamalundi.

Kabla Mwanamalundi hajakamatwa, alijua jambo hilo lingetokea. Hivyo akaenda haraka kumuaga mama yake mzazi na kumuachia maagizo. Mwanamalundi alikamua maziwa kiasi fulani kwenye kikombe na kisha akampa mama yake na kumwambia, "Iwapo maziwa haya yataanza kuganda, ujue kuwa nipo katika hali mbaya, iwapo yataganda kabisa, ujue kuwa nimekufa!", Mwanamalundi akachukua shoka isiyo na mpini kisha akaiegamisha ukutani na kumwambia mama yake, "Iwapo nitakamatwa na kupelekwa kuuliwa, shoka hii itakuwa ikipanda ukutani nikiwa napelekwa kuuliwa, tukifika eneo nitakalouliwa, basi hii shoka itapandisha hadi mwisho wa ukuta kuonesha kuwa tumefika mwisho wa safari!" Mama yake alipokea maagizo hayo na haikuchukua muda Mwanamalundi akakamatwa na askari wa Mtemi Masanja.

Mtemi Masanja III aliamua kupeleka shauri hilo kwa watawala wa kizungu (Wajerumani) ili wamchukulie hatua Mwanamalundi. Uchunguzi ukafanyika na Mwanamalundi akaonekana ana hatia ya mauaji ya watu wasio na hatia. Adhabu ya kosa hili ilikuwa ni kunyongwa.

Katika safari hii ya kunyongwa, Mwanamalundi aliambatana na Makongoro Igana ambae alikuwa ni Mtemi wa Ilemela. Mtemi huyu alikuwa ana hatia ya kuwachapa fimbo wajerumani baada ya kupita upande usio sahihi katika njia kadiri ya utaratibu wa utawala wake. Mtemi Makongoro Igana kila alipokuwa akisafiri juu ya punda, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshika fimbo ndefu. Fimbo hiyo hutumika kumchapia kila atakaepita upande wa kuume katika safari zake. Kwa bahati mbaya wajerumani hawakujua utaratibu huo wa Mtemi Makongoro. Siku wajerumani walipopishana safarini na Mtemi Makongoro, walipita upande wa kuume wenye fimbo. Mtemi Makongoro akawachapa fimbo wazungu hao kama ilivyo jadi yake. Wazungu hao walishindwa kumvumilia, wakamkamata na kumfungulia mashtaka yaliyoamuru Mtemi anyongwe.

Kaliyaya ni mtu wa pili alieambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa. Huyu Kaliyaya alikuwa ni mtu alieonekana ni mwenye ushawishi mkubwa kwa watu wa jamii yake. Kukubalika kwake kulimfanya apate wafuasi wengi ambao walihofiwa kumpindua mjerumani. Hivyo wajerumani wakaona ni bora wamfungulie mashtaka ili wamnyonge kabla hajawapindua. Kaliyaya alikuwa ni mtu wa kawaida tu ila ni mwenye ushawishi na kipenzi cha watu wengi.

Mtu wa tatu alieambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa ni Mtemi Italange wa Bugando. Mtemi huyu aliingia mgogoro na Wajerumani baada ya kuhodhi eneo kubwa la pwani ya ziwa Victoria na bandari zake kisha akakataa kuwapa Wajerumani. Ili kumnyang'anya utajiri huo, wajerumani wakaamua kumfungulia mashtaka ili wamnyonge.

Zoezi la kunyongwa lilipofika, Mwanamalundi alikuwa ndio mtu wa kwanza kuvishwa kitanzi. Kamba ilipofyatuliwa tu ili kumuua, kamba ikakatika yenyewe. Zoezi la kumuua likaahirishwa, badala ya kunyongwa akabadilishiwa adhabu.

Ikaja zamu ya Mtemi Makongoro Igana. Mtemi alipowekewa tu kitanzi shingoni na kisha kuifyatua kamba hiyo ili kumuua, ghafla kukatokea mfano wa sinema kwenye ukuta. Ni sinema ya kimiujiza iliyoonesha matukio ya kivita miaka ya nyuma. Askari wakageuka kuitazama sinema hiyo. Sinema haikuchukua zaidi ya dakika moja, ikaisha. Walipomgeukia yeye (Mtemi Makongoro Igana) wakaona hana kamba shingoni. Huyu nae akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu.

Akaja Mtemi Italange. Huyu alipowekewa kitanzi shingoni, nae pia kamba ilifyatuka. Akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu. Ilipofika zamu ya Bwana Kaliyaya, kitanzi kilipofyatuliwa ili kumnyonga, hakika kitanzi kilimuua. Huyu hakuwa mwenye ulinzi wowote ule kishirikina; yaani alikuwa ni mtu wa kawaida tu.

Ndipo mamlaka za mjerumani zikaamuru askari wawapeleke watu hao watatu Tabora. Wakiwa njiani kuelekea Tabora, walifika Nzega na kuamua kupumzika kidogo chini ya mti mkubwa nje ya Shule ya Sekondari Chama. Askari wakijerumani wakawa wakimuuliza maswali Mwanamalundi kuhusu nguvu zake na kisha wakamuomba afanye muujiza wa mwisho kabla hajafikishwa gerezani. Mwanamalundi akawaambia askari kuwa bado ana uwezo mkubwa, hata huo mti waliopumzikia anaweza kuukausha. Aliongea maneno hayo huku akiupigapiga mti huo. Kabla hajamalizia sentensi yake kuwa anaweza kuukausha, mti ulikauka palepale na majani makavu yakaanza kudondoka. Askari wa kijerumani waliogopa sana tukio hilo.

Walipofika Tabora mjini, Mwanamalundi na wale watemi wawili waliunganishwa na watu wengine wenye makosa ya uhaini na uhujumu uchumi na kisha kupelekwa kisiwa cha Mafia kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

Akiwa gerezani, Mwanamalundi aliwekwa chumba kimoja na mtemi Makongoro Igana. Mtemi Makongoro akamuuliza Mwanamalundi, "Hivi huna namna ya kujiokoa mahali hapa?" Mwanamalundi akamjibu kuwa kwa wakati huo hangeweza kujiokoa, ila kuna miujiza ya shoka na maziwa amemuachia mama yake nyumbani. Mtemi akamuuliza, "Una miujiza mingine yoyote?" Mwanamalundi akamwambia Mtemi Makongoro kuwa yeye (Mwanamalundi) anaweza kupanda viazi na mihogo na ikavunwa ndani ya dakika kadhaa tu na ikawa tayari kabisa kwa chakula. Wakiwa kisiwani hapo, wakakubaliana kwenda ng'ambo ya kisiwa (bara) kisha wakachukue mbegu za viazi na mihogo ili washuhudie miujiza hiyo ya kupanda na kuvuna ndani ya dakika kadhaa.

Kwa kuwa nyakati hizo wafungwa wa visiwani walikuwa wakiachwa huru sababu hawataweza kutoroka, Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walienda mpaka baharini ndani ya kisiwa hicho. Makongoro akiwa ameshika jiwe na Mwanamalundi akiwa ameshika fimbo. Makongoro aliporusha jiwe umbali mrefu baharini, Mwanamalundi aliyapiga maji kwa fimbo na kisha maji yakajitenga na kuacha njia mpaka pale lilipotua jiwe. Walifanya hivyo mpaka walivyofika bara (mainland). Wakatafuta mbegu za mihogo na viazi na kuonesheana miujiza.

Kila walipokuwa wakitoroka gerezani, waliacha vivuli vyao vilivyoonekana kama watu halisi. Kuna nyakati Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walionekana wakiwa Mwanza au Shinyanga na gerezani pia muda huohuo. Jambo hili liliwachanganya sana wajerumani.

Walipomaliza kifungo chao walirudishwa nyumbani kwao kwa ndege. Jamii ya Mwanamalundi ilipoona ndugu yao amerudishwa kwa ndege wakaamua kumpa jina jipya, "Ng'wenhwandege", wakimaanisha "aliyerudishwa kwa ndege". Mwanamalundi anaaminika kuwa ndie msukuma wa kwanza kupanda ndege.

Wakati anarudishwa nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake, mama yake alifurahi sana. Mama yake alifurahi kwa sababu maziwa hayakuganda kwa miaka mitatu jambo ambalo lilionesha kuwa huko aliko alikuwa hai. Maziwa yalibaki katika ubora uleule kwa miaka mitatu. Shoka ilianza kuteremka taratibu kwenye ukuta kadiri Mwanamalundi alivyokuwa akikaribia kufika nyumbani. Alivyofika tu, shoka ilikuwa tayari imefika ardhini kuashiri kuwa muda wowote Mwanamalundi atafika hapo. Na ndivyo ilivyokuwa.

Aliporudi mtaani, Mwanamalundi hakuacha asili yake. Aliendelea kucheza ngoma maeneo mbalimbali. Mtemi Masanja ambae ndie aliesababisha Mwanamalundi kunusurika kunyongwa na hatimae kufungwa, aliamua kumfukuza Mwanamalundi katika himaya ya utawala wake. Mwanamaundi akaamua kuhamia kijiji kiitwacho Seke kwa Mtemi Mahizi ambako akiendelea kucheza ngoma na kufanya miujiza yake.

Akiwa Seke wilayani Kishapu ,mkoani Shinyanga; Mwanamalundi alifanya muujiza uliomuongezea heshima kijijini Seke. Wanakijiji cha Seke waliibiwa ng'ombe wengi sana na Wamasai kutoka Tabora. Wanakijiji wakataka kwenda kufuatilia ng'ombe hao usiku huo huo jambo ambalo Mwanamalundi alikataa. Mwanamalundi aliwahakikishia wanakijiji kuwa ng'ombe hao wapo salama na watarudishwa salama tu kesho asubuhi na sio usiku huo. Wanakijiji walikubali kutokana na kumuamini Mwanamalundi.

Usiku wa siku hiyo, Mwanamalundi akatuma nguvu zake zilizowazingira Wamasai na kisha kuwafanya wasinzie na mifugo hiyo. Hata walipofuatwa asubuhi, walikutwa wamelala fofofo. Wanakijiji wakawaua Wamasai hao na kisha wakarudi na mifugo yao. Mwanamalundi akapewa jina jingine ugenini na kuitwa "Kishosha mang'ombe nga Seke", ikimaanisha "Alierudisha ng'ombe za Seke".

Kuna kipindi, Mwanamalundi alivamia pori la Mtemi wa Ng'hung'hu aitwae Chalya ili achimbe mizizi fulani ya dawa. Mtemi Chalya alipata machale kuwa kuna mvamizi katika mapori yake anachimba mizizi ya dawa. Mtemi akaondoka na kuelekea kule ambako machale yalimuelekeza. Ni kweli, akamkuta Mwanamalundi akichimba mizizi ya dawa fulani. Mtemi akamuuliza Mwanamalundi, "ni kwanini umeingia katika utemi wangu bila kunijulisha?" Mwanamalundi akajibu, "Wewe ni mtemi wa watu wote ila mimi ndie mtemi wa miti yote!" Jibu hilo lilimkwaza Mtemi Chalya ambae aliamua kurudi kwenye himaya yake kwa ghadhabu na kuwaamuru askari wake wamkamate Mwanamalundi ili aadhibiwe.

Askari wakiwa wameambatana na Mtemi Chalya walipofika porini eneo alilokuwepo Mwanamalundi, hawakumkuta. Badala yake waliwakuta simba wengi wakiwa wamelala eneo hilo. Ilibidi watimue mbio kujiokoa wenyewe dhidi ya simba hao walioanza kuwafukuza. Walipofika kwenye himaya ya Mtemi wakiwa salama, walimkuta Mwanamalundi amemaliza kula chakula chao na anaondoka. Ilibidi mtemi amuache tu Mwanamalundi aondoke bila kumbughudhi kwa lolote.

Mwanamalundi alifariki mwaka 1936 kwa maradhi ya kawaida na kuzikwa Ididí Jihū huko kijiji cha Seke wilaya Kishapu mkoa wa Shinyanga akiwa ana umri wa miaka 44. Tukio la kifo chake liliitwa "hang'witulo gwa shigela" ikimaanisha "Vita ya kuwakimbia wamasai". Hii ni kwa sababu wakati Mwanamalundi anakata roho, kulitokea kishindo kikubwa kama tetemeko la ardhi. Watu wengi walikimbia ovyo kwa hofu kuwa labda wamasai wamevamia eneo lao ili kuwaua. Baada ya kishindo hicho, giza likaingia ghafla, giza ambalo hata kuku wakaanza kurudi nyumbani, fisi wakaanza kutembea mitaani wakidhani ni usiku. Hata baada ya mazishi yake, kaburi lake lilifuka moshi mwingi sana uliopanda mpaka juu mawinguni na kutengeneza giza la muda mfupi. Mwanamalundi anakumbukwa pia kwa kuweza kutembea hewani bila kukanyaga ardhi, kujibadili na kuwa kiumbe tofauti kama mnyama, ndege, majani, mti au jiwe na uwezo wake wa kutembea juu ya maji au kuwa ndani ya maji kwa muda mrefu. Mwanamalundi ni mmoja tu wa watu mashuhuri katika tawala za Kisukuma. Kuna watu mashuhuri kabla yake kama akina Níndwa, Italange na Sïta. Hawa wote walikuwa ni watu wa miujiza kama alivyokuwa Mwanamalundi.

Makala hii inasimuliwa na Msukuma halisi na mwanahistoria ya Wasukuma Nghwana Ibengwe Shileki Mazege katika kitabu chake kiitwacho "Miujiza ya akina NG'WANA MALUNDI", toleo la kwanza 2015. Huyu Bwana ana vitabu vingi sana kuhusu historia ya wasukuma.

Kwa maswali yoyote kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana nae kupitia:

+255 763 379 387
Share:

Tanzania Yashiriki Kongamano La Matumizi Endelevu Ya Rasilimali Za Bahari Nchini Msumbiji.

Na Edward Kondela
Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi zikiwemo Tanzania, Kenya, Msumbiji na Afrika ya Kusini na Visiwa vya Ushelisheli zimepewa rai ya kuhakikisha zinafanya kila njia kulinda rasilimali za pamoja hususan zinazopakana na bahari ili ziweze kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rai hiyo imetolewa (24.05.2019) na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili matumizi endelevu ya rasilimali za bahari linaloendelea katika mji wa Maputo nchini humo.

Rais Nyusi amesema kongamano hilo la siku mbili lina umuhimu mkubwa kwa kuwa linafanyika wakati huu ambapo uvunaji holela na usiofuata utaratibu wa rasilimali za bahari umeshamiri katika nchi nyingi za bara la Afrika na Asia.

Akihutubia washiriki wa Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameelezea hatua mbalimbali ambazo nchi ya Tanzania imepiga katika kuhakikisha malengo ya milenia kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili yanafikiwa.

Mhe. Ulega amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupambana na uvuvi haramu na biashara haramu ya utoroshwaji wa mazao ya uvuvi, kudhibiti uvuvi wa mabomu katika pwani ya Bahari ya Hindi, kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira ya bahari kwa lengo la kuinua maisha ya jamii za wavuvi, kulinda maeneo tengefu ya bahari, kufanya utafiti na kuzuia uharibifu wa bahari unaotokana na matumizi ya bidhaa za plastiki.

Aidha, Mhe. Ulega amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi kuhakikisha rasilimali zilizopo zinalindwa na zinazinufaisha nchi wanachama.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo umeangazia mchango wa sekta zingine ambazo kwa pamoja zinachochea ukuaji wa uchumi wa bluu ambao unahimiza matumizi ya bahari katika kukuza uchumi wa nchi.

Sekta hizo ni pamoja na usafirishaji, utalii wa bahari, uhifadhi wa mazingira, utafutaji na uchimbaji wa gesi, pamoja na usalama wa chakula na ajira.

Kwa pamoja washiriki wa kongamano hilo wamekubaliana katika kuimarisha ushirikiano, kuendelea kubadilishana uzoefu na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kulinda rasilimali za bahari kwa kuwa baadhi ya rasilimali hizo hazina mipaka kama ilivyo kwa samaki aina ya jodari ambao huhama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Kongamano hilo limeandaliwa na nchi ya Msumbiji kwa kushirikiana na Norway pamoja na mashirika mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, ambapo zaidi ya washiriki 300 kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wataalam wa sayansi za bahari, mazingira, usafirishaji majini, viongozi wa
kisiasa, wakuu wa mashirika ya fedha na mashirika binafsi yanayojihusisha na uhifadhi wa rasilimali za bahari wanahudhuria kongamano hilo.

Tanzania, imewakilishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na wengine ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Mmanga Mjengo Mjawiri, Mkurugenzi wa Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe na maofisa kutoka Mamlaka ya Bahari Kuu nchini.


Share:

JINSI DUNIA YA INTANETI ILIVYOINGILIA MVUTANO KATI YA NDUGAI NA MASELE


Dunia ya sasa, ukisema kitu bila kueleweka vizuri, watu wa mitandaoni watatengeneza tafsiri yao. Utabaki unashangaa, mbona maana yako haikuwa inavyotafsiriwa na wengi?

Dunia ya intaneti, hasa unapokuwa kiongozi, unatakiwa ufafanue vizuri mawazo yako, vilevile utazame kipindi ambacho unajenga hoja, vinginevyo intaneti itakupeleka mahali ambako hukutaka.

Ndugai Vs Masele

Job Ndugai ni Spika wa Bunge la Tanzania. Stephen Masele ni mbunge wa Shinyanga Mjini. Masele pia ni mbunge wa Bunge la Afrika, vilevile Makamu wa kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika.

Sifa ya kuwa mbunge katika Bunge la Afrika ni lazima uwe mbunge katika nchi yako ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Ukiwa mbunge, ndiyo unaomba kuchaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Afrika. Ukipoteza ubunge kwenye nchi yako, moja kwa moja unakosa sifa za ubunge Bunge la Afrika.

Hapa ndipo kwenye mamlaka ya Ndugai. Kwamba Masele ni kiongozi wa juu kabisa Bunge la Afrika, lakini Ndugai anaweza kumfanya asiwe mbunge katika Bunge la Afrika kwa sababu ‘chaneli’ ya ubunge wake ni Bunge la Tanzania.

Ndani ya Bunge la Afrika kuna kashfa kumhusu Rais wa Bunge hilo, Roger Dang, raia wa Cameroon kutumia madaraka yake vibaya – kuhusika na rushwa ya upendeleo wa ajira na unyanyasaji wa kingono kwa watumishi.

Tuhuma dhidi ya Rais Dang (Spika) ni rasmi. Bunge la Afrika limezifanyia kazi na kamati ya uchunguzi imemtia hatiani Dang, ambaye alikuwa anajaribu kujinasua. Inadaiwa Dang baada ya kumuona Masele ni tatizo, alimshtaki kwa Ndugai.

Na Ndugai alimwita Masele nyumbani (Bunge la Tanzania) ajieleze. Awali, inadaiwa Masele alikaidi wito na akasema kwamba aliagizwa na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa, apuuze wito wa Ndugai.

Kutokana na mvutano huo, Ndugai alitangaza kusimamisha kwa muda ubunge wa Masele kwenye Bunge la Afrika. Alimtuhumu kuwa anafanya mambo ya hovyo kugonganisha mihimili.

Baada ya kauli ya Ndugai na uamuzi wake, intaneti ilikuwa kinyume naye. Watoa maoni mitandaoni walimshambulia. Kwa mitazamo ya wengi, Masele yupo sahihi, maana tuhuma dhidi ya Dang ni nzito na anatakiwa kuwajibishwa.

Watu hawakuangalii kosa lililosemwa “kuchonganisha mihimili”, walijikita kwenye tuhuma za msingi zinazomkabili Dang.

Baada ya nivute nikuvute, Masele aliitikia wito. Kamati ya Maadili ya Bunge ilimkuta na hatia ya kugonganisha mihimili na kupendekeza aadhibiwe kwa kuzuiwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge. Hata hivyo Ndugai aliamua kumsamehe.

Pamoja na kutoa msamaha, mitandaoni Ndugai ameshahukumiwa kuwa anamtetea Dang, mwenye tuhuma. Akawa anamdhibiti Masele, anayepigania misingi.

Silioni kosa la Ndugai kumwita Masele alieleze Bunge la Tanzania kinachoendelea katika Bunge la Afrika. Nauona utovu wa nidhamu wa Masele kusema aliambiwa na Waziri mkuu akaidi wito wa Spika Ndugai. Matamshi hayo ni uchonganishi kwa Serikali na Bunge.

Pamoja na hivyo, Ndugai alipaswa kukumbuka yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti. Angekumbuka hilo, angekuwa na angalizo kuhusu matamshi yake na uamuzi wake wa jumla kuhusu Masele.

Angejiuliza, je, tuhuma zipi ni nzito? Masele kukaidi wito au Dang kufanya unyanyasaji wa kingono na rushwa? Ukaidi wa Masele umeibukia wapi? Kabla, baada au katikati ya tuhuma za Dang? Majibu ni kuwa tuhuma za Dang ni nzito zaidi. Ukaidi wa Masele ulitokea katikati ya tuhuma za Dang.

Ndugai kwa kutambua yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti, alipaswa kufahamu kwamba uamuzi wake kuhusu Masele ungesababisha sababu ya msingi izungumzwe. Na kwa sababu hiyo, alitakiwa kufahamu kwamba mitandao ingemhukumu kwa kumtetea Dang na kumdhibiti Masele.

Kuna swali; katika ulimwengu huu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, ilishindikana vipi Ndugai kumpigia simu kuzungumza na Masele mpaka amwite nyumbani aache shughuli muhimu za Bunge la Afrika ikiwemo tuhuma za Dang?

Dunia ya intaneti yenye Skype, ilishindikana kufanya mkutano (Skype Meeting) kuondoa utata? Mwisho, Ndugai angeweza kulitatua suala la Masele kimyakimya, badala ya kupaza sauti. Kwa kuwa alizungumza, intaneti ikashtuka, ikatafuta sababu, ikaibuka na tafsiri kwamba Ndugai anamtetea Dang.

Busara za uongozi katika ulimwengu wa intaneti, zinataka ukumbuke kuwa kila unachofanya na unachosema, watu mitandaoni watapokea wanavyojua wao na watatafsiri kwa namna yao. Tafsiri yao itakuhukumu na itakukwaza. Hivyo, lazima uwe makini sana.
Via>>Mwananchi
Share:

MFANYABIASHARA WA NGUO AUAWA NDANI YA DUKA LAKE


Duka la nguo

Mkazi wa Kijiji cha Katoro na mfanyabiashara wa duka la nguo katika Kijiji jirani cha Nyarugusu mkoani Geita, Deus Mwenda(36) ameuawa kikatili kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni akiwa ndani ya duka lake.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja baada ya watuhumiwa 17 wa makosa mbalimbali waliokuwa wamehifadhiwa kwenye ukumbi wa jengo jipya la Mahakama ya Mkoa wa Geita wakisubili mashauri yao kutajwa, kudaiwa kutoroka.

Aidha tukio hilo limetokea majira ya mchana na kuacha maswali mengi kwa baadhi ya wafanyabiashara wenzake, kutokana na duka la mfanyabiashara huyo kuwa maeneo yenye msongamano wa watu na pembezoni mwa soko la kijiji hicho, ambapo wafanyabiashara hao sasa wameamua kufunga maduka kwa kuhofia usalama.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarugusu, Amosi Yunge, mbali na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo amesema tukio hilo limetokea saa chache baada ya mwanamke mwingine kubakwa na majambazi, huku mjane wa marehemu na ndugu wengine wakielezea jinsi walivyopokea taarifa za tukio hilo.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI MEI 25,2019


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger