Tuesday, 2 April 2019

CCM KIBONDO YAAGIZA MRADI WA MAJI ULIOKWAMA TANGU 2014 KAGEZI NA MLANGE UKAMILIKE NDANI YA MWEZI MMOJA

Wananchi wa vijiji vya Kagezi na Mlange Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma, wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita mbili kufuata maji katika chanzo cha maji kutokana na mradi wa maji uliogharimu zaidi ya bilioni moja kutokamilika tangu mwaka 2014 hadi sasa.

Wakizungumza jana kijijini hapo wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani kwa baadhi ya miradi ya serikali uliofanya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya wilaya hiyo, baadhi ya wananchi hao waliokuwa wakigombania maji katika chanzo cha mto Kagezi, walisema wanapata shida sana ya kuchota maji na hasa ukizingatia Mlima uliopo katika chanzo hicho unawachosha.

Mmoja wa wananchi hao,Agnes Kunjira alisema wanalazimika kuamka asubuhi sana kuwahi kuchota maji ndipo waende mashambani, kutokana na kero hiyo wanashindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa wakati kwa kuwa maji ni uhai na wanahitaji maji.

Aidha aliiomba serikali kufuatilia kwanini mradi huo hautoi maji kwa kuwa kero waliyonayo inawatesa sana na endapo mradi huo ukikamilika na wakaanza kuchota maji vijijini itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao za maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Kagezi mwenyekiti wa kijiji hicho,Zabroni Ntimba, alisema tangu mradi huo uanze kujengwa ni muda mrefu na mpaka sasa ulitakiwa uwe umekamilika lakini mwaka 2018 wananchi walipata maji kwa muda wa miezi mitatu tu na baada ya hapo maji hayakutoka tena.

Alisema wananchi wanalalamika sana na hasa kwa kuwa walichangia asilimia 20% ya mradi hali hiyo inasababisha wananchi kushindwa kuchangia hata shughuli zingine za maendeleo, kwa kuwa wamechangia mradi wa maji lakini hawaoni mradi ukifanya kazi.

Akitoa ufafanuzi juu ya mradi huo Mhandisi wa maji wilaya ya Kibondo Michael Nguruwe alisema mkandarasi wa mradi huo aliingia mkataba ,wa shilingi bilioni moja na milioni (244,629,764/=)  mradi ulitakiwa kuwa umekamilika 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha kulipa kwa wakati kwa mkandarasi mradi uliongezewa muda hadi 2018 lakini mpaka sasa haujakabidhiwa kwa wananchi.

Alisema tatizo kubwa lililopelekea mpaka sasa mradi huo kutokamilika kwa wakati, ni changamoto ya mfumo wa umeme, ambalo mkandarasi alishindwa kulikamilisha na kama halmashauri wamezuia kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji wa mradi huo.

Alisema mpaka sasa wanaendelea kutafuta mkandarasi wa mfumo wa umeme katika mradi huo kwa ajili ya kuweka kifaa kitakachosaidia kuongoza mfumo wa umeme katika mradi huo na mradi ukabidhiwe kwa wananchi kwa ajili ya kutumika.

Kutokana na changamoto zilizopo katika mradi huo na kero wanayoipata wananchi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kibondo Hamisi Tahilo alisema chama kinaagiza mradi huo kukamilika kwa kipindi cha mwezi mmoja na baada ya mwezi mmoja watafika katika mradi huo kuangalia kama kweli wananchi wameanza kupata maji.

Alisema serikali imetoa zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya mradi wa Wananchi lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika, serikali iliahidi kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani ni lazima watendaji kuhakikisha wanasimamia miradi ya serikali inafanyiwa kazi.

"Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na fedha zinatolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi wananchi wataiamini serikali baada ya kuona miradi hii inakamilika niombe ndani ya mwezi huo mmoja mradi huu uwe umekamilika", alisema Tahilo.

Hata hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira na kuendelea kujenga imani na CCM kwa kuwa imejipanga kuhakikisha wananchi wote wa vijijini na mijini wanapata huduma sawa sawa na wanaondokana na changamoto zote.

Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Kibondo wakiwasaidia wananchi kubeba maji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kagezi wakichota maji katika chanzo cha mto Kagezi baada ya kero kubwa ya maji kijijini humo.
Share:

MAJAMBAZI WANYOFOA MASHINE YA ATM KWA TINGATINGA

Majambazi wamenyofoa na kutokomea na mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa nchini Ireland ya Kaskazini.

Majambazi hao walitumia tingatinga ambalo pia waliliiba katika kunyofoa ATM hiyo kutoka kwenye ukuta wa duka moja katika Kaunti ya Antrim.

Tukio hilo limetokea saa tisa ya usiku wa Jumatatu. Polisi wamethibitisha kuwa jengo hilo limeharibiwa vibaya.

Mmiliki wa duka hilo Walter Millar amesema kuwa ATM hiyo "itakumbukwa sana" na jamii ya eneo hilo na sasa kuna "hofu" juu ya kupatiwa mashine nyingine baada ya wizi huo.

Awali alipopokea taarifa juu ya wizi huo, mmiliki wa duka hilo bwana Millar alidhani ni uzushi tu wa Siku ya Wajinga, Aprili mosi.

"Nachoweza kusema ni kuwa, wametumia tingatinga ambalo waliliiba kwenye eneo moja la ujenzi mwishoni mwa mtaa, wakainyofoa mashine na kuipakia kwenye gari na kuondoka nayo," amesema.

"Ukuta wa jikoni umeharibiwa kabisa...tumekuwa na wakati mgumu, na ukijumlisha na hali ya kiuchumi iliyopo, vitu kama hivi vinatumaliza kabisa."Mmiliki wa duka Walter Millar awali alihusisha taarifa za tukio hilo na Siku ya Wajinga, Aprili 1.

Majambazi wa ATM

"Tulipokea simu kuhusu tukio hilo mishale ya saa 9:25 usiku kuwa tingatinga linaungua moto nje ya duka ambalo ATM imechomolewa," Inspekta wa Polisi Richard Thornton amesema.

"ATM imenyofolewa ukutani na kuharibu jengo ilipokuwa imewekwa...tunawataka mashuhuda wajitokeze, hususan walioiona gari ya rangi ya fedha."

Mwezi uliopita, polisi walitangaza kuundwa kwa kikosi kipya cha kupambana na wizi wa mashine za ATM.

Toka ulipoanza mwaka 2019, mashine saba za ATM zimeibiwa. Polisi pia wanaamini kuna makundi kadhaa ya majambazi ambayo yanajihusisha na wizi wa mashine hizo.

Wamiliki wa maduka sasa wanaonesha uoga wao juu ya kuweka mashine hizo kwenye maeneo yao ya biashara na tayari watu kadhaa wametahadharisha endapo wizi huo utaendelea basi watalazimika kuzitoa mashine hizo.
Chanzo - BBC
Share:

BABA AUA MTOTO KWA KUMNYONGA AKIDAI 'AMEBAMBIKIZIWA'


Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia mkazi wa mtaa wa Vitendo katika kata ya Misugusugu wilayani Kibaha, Pwani, Robison Ernest (33) kwa tuhuma za kumwua kwa kumnyonga mtoto wake wa Modesta Robison miezi sita akidai kuwa si mwanae.

Inadaiwa kuwa Ernest ambaye ni fundi ujenzi alifanya kitendo hicho cha kinyama wakati mama wa mtoto huyo akiwa sokoni kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho, aliuficha mwili chini ya uvungu wa kitanda kisha huku baba huyo akihamia chumba kingine.

Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha leo Jumanne (Aprili 2, 2019), Kamanda Nyigesa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili Mosi, mwaka huu majira ya saa 4:30 asubuhi kwenye mtaa huo.

Na John Gagarini- Habarileo 
Share:

RAIS MAGUFULI AWASAMEHE WALIONUNUA KOROSHO KWA MTINDO WA KANGOMBA


Rais Dkt.John Pombe Magufuli ametoa msamaha kwa watu walionunua korosho kwa mtindo wa Kangomba iwapo watakiri kujihusisha na mtindo huo na kuwaonya wasirudie tena kosa hilo kwa msimu ujao.
Share:

WABUNGE WA UPINZANI WATOKA NJE YA BUNGE KUPINGA MDEE KUSIMAMISHWA


Wabunge wa upinzani wametoka nje ya bunge kupinga hatua iliyochukuliwa na Bunge ya kumsimamisha Mhe.Halima Mdee mikutano miwili ya bunge kuanzia leo kutokana na kulidharau Bunge.
Share:

MAMA AAMUA KUMZALIA MTOTO MWANAWE SHOGA

Mwanamke mmoja nchini Marekani amejifungua mjukuu wake wa kike ambaye alikuwa amembebea kwa miezi tisa mwanawe ambaye ni shoga. 

Kwa maneno rahisi ni kwamba, mtoto wa kiume wa mwanamke huyo ni shoga na mama yake kubeba mimba ilikuwa ndiyo njia ya rahisi kwa 'mume na mke' wake kupata mtoto. 

Matthew Eledge, 32, na Elliot Dougherty, 29, walimkaribisha mtoto wao ulimwenguni kwa jina Uma Louise Dougherty -Eledge baada ya mama ya Mathew, Cecile Eledge kuchukua jukumu la kuibeba mimba hiyo.

 Katika ripoti ya CNN, mama huyo alipata ujauzito kupitia njia ya kitaalamu na Mathew aliwasilisha mbegu ya kiume naye dada ya 'mke' wake Lea Yribe akawasilisha yai. 

"Wakati wewe ni shoga na umeolewa na unataka kuwa na mtoto, ni lazima kufahamu utahitaji njia maalum ya kujenga familia," Matthew alisema kupitia mahojiano na CNN. 

Mama huyo, 61, alijifungua Uma Louise jijini Omaha, Nebraska wiki moja iliyopita na mtoto huyo aliwa na uzani wa kilo 2.6.

 Kulingana na Mathew, mwalimu, walijaribu njia nyingi lakini zilizokuwapo zilikuwa ghali mno na hawakufahamu wafanye nini.

 "Nilikuwa na watu wengi chuoni waliosema (wangezaa mtoto), lakini wakati ukifika, ni jukumu kubwa," Matthewalisema.

 "Zaidi ya yote, tunahisi wenye bahati kubwa kupata wanawake wakarimu sana wanaoweza kufanya hivyo," alisema. 

Wawili hao walisema wana shukrani tele kwa kuwa na familia zenye kujali zaidi na zilizo tayari kuwasaidia kwa lolote.
Share:

BUNGE LARIDHIA KUTOFANYA KAZI NA CAG KWA KUDHALILISHA BUNGE


Bunge limepitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Uamuzi huo umepitishwa leo Jumanne Aprili 2, 2019 baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka kuwasilisha na kusoma bungeni taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji CAG, kumtia hatiani baada ya kubaini kauli aliyoitoa kuwa Bunge ni dhaifu, amelidhalilisha Bunge.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alitoa nafasi kwa wabunge kujadili jambo hilo huku wabunge wakipishana maoni yao, kukubaliana na uamuzi huo na wengine kupinga akiwemo Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.


Baada ya wabunge kutoa maoni yao, Dk Tulia amelihoji Bunge kuhusu hoja hiyo, akiwakata wanaokubaliana na jambo hilo kusema ndio na wasiokubaliana na suala hilo kusema sio, "waliosema ndio wameshinda. "

Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Share:

KAMATI YAPENDEKEZA HALMA MDEE KUSIMAMISHWA KUHUDHURIA BUNGENI KISA CAG


Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imependekeza Bunge kumsimamisha mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia tarehe ya azimio hilo kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG.
Share:

BUNGE LAMKATAA CAG...KUMBE PROF. ASSAD ALIGOMA KUOMBA RADHI AKAKOMAA 'BUNGE DHAIFU'


Prof. Assad
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad amesema kwamba hatoacha kutumia neno dhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia na hakujutia kulitumia dhidi ya Bunge.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maadili, Emmanuel Mwakasaka , ambaye ameeleza bungeni kwamba Kamati imejiridhisha CAG Assad amelidhalilisha Bunge na Kamati imemtia hatiani kwa kulidharau Bunge na kudhalilisha shughuli za chombo hiki.

Mbele ya Bunge, Mwakasaka ameeleza kwamba Prof. Assad alikiri mbele ya kamati kuliita Bunge dhaifu lakini alipingana na tafsiri ya neno 'dhaifu' iliyopo kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu inayosema 'goigoi, hafifu, isiyo imara' akisitiza kiuhasibu udhaifu ni 'upungufu'.

Mwakasaka amesema, "tuliangalia maana ya neno upungufu kwenye kamusi tukabaini ni 'isiyo kamili, isiyo imara', hivyo alidhamiria kulidhalilisha Bunge. CAG hakuomba msamaha wala kujutia na akasisitiza ataendelea kulitumia neno hilo".

"Kamati imependekeza Bunge lisifanye kazi na CAG Prof. Mussa Assad", Mwakasaka amesisitiza.

Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe amelionya Bunge kwamba historia ambayo itaandikwa leo kuhusu CAG itawahukumu, "Bunge mnajipa utukufu ambao ni wa Mungu pekee".

"Azimio mnalotaka kulifanya leo dhidi ya CAG mmeshalifanyia kazi. Mnataka kuwanyima watu haki na uhuru wa mawazo ilhali Katiba imeruhusu kila mtu, akiwamo CAG ana uhuru wa kutoa mawazo na kueleza fikra zake, kufanya mawasiliano na kutoingiliwa kuhusu taarifa yake", ameongeza.

Utata wa kauli ya CAG ulianzia pale CAG alipokuwa akijibu swali la Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwamba kitendo cha ofisi yake kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea ni kutokana na 'udhaifu wa bunge'.
Share:

BABA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMCHOMA MWANAE PANGA LA MOTO

Picha haihusiani na habari hapa chini
Mkazi wa mtaa wa Fisi, kata ya Igunga mjini mkoani Tabora, Nyalagi Simon amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Igunga kwa tuhuma za kumuunguza mwanae kwa upanga wa moto.

Simon amefikishwa leo Jumatatu Aprili 1, 2019 katika mahakama hiyo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya, Lydia Ilunda.

Mwendesha mashtaka wa Polisi, Ellymajid Kweyamba alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo saa tatu usiku Machi 17, 2019.

Amesema siku hiyo, mshitakiwa akiwa baba wa mtoto (jina linahifadhiwa) alimfanyia vitendo vya ukatili kwa kutumia upanga aliouweka kwenye moto.

Amebainisha kwamba mshitakiwa alikuwa akiutoa upanga kwenye moto na kumuunguza kwenye miguu yote miwili.

Mshitakiwa amekana shitaka lake na amepelekwa mahabusu hadi Aprili 14, 2019 shauri lake litakapotajwa tena.

Na Robert Kakwesi, mwananchi 
Share:

DC WA RUANGWA AWATAKA TAMWA KURUDISHA WATOTO SHULE...APIGA MARUFUKU UNYAGO

Na Bakari Chijumba,Lindi.

katika kuendeleza kusaidia watoto wa kike, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hashim Mgandiliwa  amewaomba Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) kuchukua jukumu la kuwasaidia kuwaendeleza kimasomo watoto walioacha shule na wana nia ya kuendelea na masomo.

Amesema hayo 30 Machi 2019, wakati wa muendelezo wa  kikao cha kujadili jinsi ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kilichofanyika ukumbi wa Rutesco mjini Ruangwa.

"TAMWA bebeni hawa watoto wenye nia  ya kurudi shuleni hawajachelewa wanaweza kusaidiwa na wakafikia malengo yako kama watoto wengine waliopata bahati ya kusoma kwa wakati" amesema Mgandilwa.

Pia amewataka TAMWA kuhakikisha katika kila mikutano yao wanayofanya wanahamasisha wazazi kufanya shughuli za unyago wakati wa likizo ili kutomnyima haki ya mtoto kupata elimu.

"Serikali haipingi unyago mimi pia sipingi unyago hizo ni mila na desturi zipo katika kila kabila nchini, ila mfanye jambo hilo kwa kufuata maelekezo yanayotolewa, narudia serikali haina tatizo na mila na desturi " DC Mgandilwa na kuongeza kuwa;

"Hakuna ujanja zaidi ya elimu Elimu ndiyo kila kitu hata mie kuwa hapa ni kwasababu ya elimu sasa mkitoka hapa nyie wanafunzi mliopata mafunzo haya mkawe mabalozi kwa wenzenu muwaeleze umuhimu na faida ya elimu"

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAMWA Bi Rose Reuben, amewataka watoto wakike kuamka na kutambua thamani yao na kuacha tabia za kuiga mambo yasiyo na maana katika maisha yao.

"Mkianza kujitambua nyie hata watu wengine wataanza kuwatambua jisimamieni katika vitu vyenye manufaa umeshindwa kumaliza masomo kwa ajili ya ujauzito basi msimamie mtoto uliyenaye aje kuwa kiongozi mkubwa baadae" Amesema Bi Rose

Aidha kwa niaba ya wenzake, Mwanafunzi Amina Omari Makota, ameuomba uongozi kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao hawawapi ushirikiano watoto wanaoitaji kusoma  na wanapopeleka malalamiko sehemu husika basi mzazi huyo achukuliwe hatua kwa haraka.

Amina amesema siyo watoto wote wanaoacha masomo ni kwasababu hawataki kusoma, wapo wanaoacha kusoma kwasababu wazazi wao hawawatimizi mahitaji muhimu yanayoitajika shuleni .


Share:

VITUO 41 VYA BODABODA NJOMBE VYAPEWA ASKARI WA USALAMA BARABARANI KWA AJILI USIMAMIZI

Na Amiri kilagalila

Jeshi la Polisi Kupitia Kitengo Cha Usalama Barabarani Limepeleka Askari Polisi Katika Vituo 41 Vya Boda boda Mkoani Njombe Ambao Watakuwa Wakifanya Kazi ya Ulezi Kwa Madereva Hao Kwa Lengo la Kuwasaidia Kufanyakazi Hiyo Kwa Weledi na Nidhamu.


Hii Itasaidia Kupunguza Ajali za Barabarani Kwa Kuwa Elimu Itakuwa Ikitolewa Mara Kwa Mara Kwa Madereva Pikipiki Wawapo Katika Vituo Vyao Ikiwa ni Pamoja na Kuwa na Kofia Ngumu Yaani Helmet Kwa Dereva na Abiria Wake na Usafi Kwa Ujumla.

Mkuu wa Kikosi Cha Usalama  Barabarani Mkoa wa Njombe Kelvin Ndimbo Amezungumza na mtandao huu juu ya Hatua Hiyo huku Akisema kuwa huu ni Kwa Mujibu wa Sheria na Kwamba Tayari Tangu Askari Hao Wapelekwe Kwenye Vituo Mafanikio Yameanza Kuonekana Huku Akitoa Wito Kwa Abiria Hususani Wanawake Ambao Wanagoma Kuvaa Kofia Ngumu Kwa Kisingizio Cha Kuchafuka  Nywele.

"Natoa wito na rai kwa abiria wote wanaopakizwa kwenye hizi piki piki wahakikishe wanavaa kofia kwasababu wanapanda kwenye pikipiki ambazo waendeshaji wote wamevaa hizi kofia kwa kuwa sio sale ni usalama,niwaombe abiria wavae kofia la sivyo kwa maana sheria haitasita kuwachukilia sheria wote wanaokiuka sheria"alisema Ndimbo
  
Madereva Bodaboda Mjini Njombe Akiwemo Kenedy Mligo na Kenedy  Mkonga Wanakiri Kuwapo Kwa Mabadiliko Makubwa Tangu Askari Walezi Kuwepo Katika Vituo Vyao na Kwamba Hata Usafi Umeimarika Kwani Sasa Wanavaa Reflector Pamoja na Kuwa na Kofia Ngumu Kwa ajili Yao na Abiria Wao Licha ya Baadhi ya Akina Dada Kugoma Kuvaa Kofia Hizo.

"Askari walezi wananvyokuwepo wanafanya kweli madereva wajitambue ikiwamo kuwa na leseni,kuvaa vikinga upepo pamoja nakofia kwa kweli hii inasaidia na sisi kila wakati tunatoa elimu kwa hawa abiria wetu kwa kuwa wakati mwingine wamekuwa hata wakigoma kuvaa hizi kofia ngumu"alisema Kenedy mligo mmoja wa dereva boda boda.

Baadhi ya wanawake Akiwemo Honey Mnenuka  Licha ya Kukiri Kuhofia Usafi Hasa Katika Nywele Zao Pamoja na Suala Zima la Urembo Wengine Wanashauri Sheria Kuchukua Mkondo Wake.

"Uvaaji wa kofia uwepo maana ni usalama wetu kwa hiyo ni lazima abiria kwa anayegoma lazima sheria zichukuliwe na alipe yeye na sio dereva,ila tatizo kwenye usalama unakuwa mdogo zile kofia zikiwa chafu tungeomba ziwe zinafanyiwa usafi"alisema Honey mnenuka

Neema ni Miongoni Mwa Abiria Aliyekutwa na mtandao huu Akipanda Bodaboda Ambaye Baada ya Kuvalishwa Kofia Alianza Kwa Kusita.

"Mimi siendi mbali jamani nitavaaje naenda jirani tu hapo"alisikia mmoja wa abiria wa kike akigoma kuvaa kofia ngumu.

Mtandao huu umezungumza na Baadhi ya Wanaume Mjini Njombe Akiwemo Reginald Danda na Obeid Ngailo Juu ya Suala la Kofia Ngumu Kwa Abiria Ambao Wanaeleza Umuhimu wa Kuvaa Kofia Hizo Huku Wakiwataka Akina Dada Kutumbua Thamani ya Uhai Wao Badala ya Urembo.

"Mimi nimewahi kupata ajali ya boda boda nikiwa nimevaa kofia ngumu na kofia ngumu ilipasuka huku mimi nikiwa nimepoteza fahamu siku mbili kwa hiyo kama ningekuwa sikuvaa kofia na maisha yangu yangekuwa yamekwisha,kofia hizi ni muhimu sana na watu kwa kweli waache kisingizio cha nywele ukiona nywele ni muhimu basi bora utumie gari" alisema Reginald Danda  

Suala la Usalama Katika Maisha Ni Muhimu Kuliko Urembo.


Share:

Watu 28 wakamatwa na polisi kwa kupiga askari wakiwa kazini

Watu 28 wamekamatwa na polisi wilayani Nyang'hwale, Geita kwa tuhuma za kuwajeruhi askari polisi watatu kwa silaha za jadi wakati askari hao wakizuia wananchi wenye hasira kumshambuliwa mtu aliyedhaniwa ni mwizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu Aprili mosi 2019 kamanda wa polisi mkoani Geita, Mponjoli  Mwabulambo amethibitisha askari wake kujeruhiwa na kuwataja waliojeruhiwa kuwa ni Omari ambaye ni mkaguzi wa Polisi tarafa ya Nyangwale.

Mwingine ni askari H16 D/C Yusuph aliyejeruhiwa mguu wa kulia na H4311 D/C Joseph aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.

Akielezea tukio hilo, Mponjoli amesema Jumamosi Machi 30, 2019 kundi la majambazi wakiwa na silaha za jadi walivamia nyumba za wakazi wawili kijiji cha Nyijundu na kumuua mkazi mmoja na kujeruhi wengine watatu kisha kupora fedha.

Amesema kufuatia hali hiyo, wananchi walipiga yowe na kuanza msako kwa kushirikiana na polisi na walipomkamata mmoja waliyedhani ni mtuhumiwa na kumhoji kisha kukiri walitaka kumuua na walipozuiwa na polisi wakawageuzia kibao. 


==>>Msikilize hapo chini


Share:

LIVE: Fuatilia kipindi cha maswali na majibu kutoka bungeni Jijini Dodoma.

LIVE: Fuatilia kipindi cha maswali na majibu kutoka bungeni Jijini Dodoma.


Share:

TAKUKURU Dodoma Yaokoa Milioni 152....Milioni 900 Zinachunguzwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dodoma imesema inachunguza ufisadi wa shilingi Milioni 900  baada ya kuwa na viashiria vya rushwa katika miradi mbalimbali.

Pia taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh152.3 milioni ambazo zingelipwa kwa wakandarasi ambao ufuatiliaji wa ukaguzi wa miradi ya maji umebaini hawakutimiza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yamebainishwa jana  mkoani Dodoma na kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU, mkoa wa Dodoma Sosteth kibwengo wakati akitoa taarifa ya robo ya mwaka kwa wanahabari.

Ambapo alisema kwa robo ya mwaka taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi  milioni 152.3, zilizokuwa zilipwe kwa wakandarasi ambao hawakutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Taasisi hiyo  pia imemtaka mkurugenzi wa kampuni ya Global Space East Africa Limited, inayojenga kituo cha afya Mima kilichopo Wilayani Mpwapwa mkoani hapa kulipoti katika ofisi ya zake zilizopo wilayani humo kwa mahojiano.

Vile vile alibainisha kuwa katika kipindi husika, TAKUKURU ilipokea jumla ya taarifa 96 za rushwa na makosa yahusianayo ambapo sekta  ziliongoza kwa tuhuma ni;

Serikali za mitaa (25%), Ardhi (17%), Elimu (16%), Afya (8%), Maji, Ujenzi na Mahakama (kila moja asilimia 7), na Polisi (6%), taarifa hizo zilifanyiwa kazi kwa njia mbalimbali na majalada nane (8) ya uchunguzi yalikamilika ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.5 ya majalada yaliyokamilika kwa kipindi hicho mwaka 2018.



Share:

Vyama vya Ushirika Vyashauriwa kukopa fedha kwenye Mabenki kwa ajili ya wanachama wao

Bashiri Salum,Wizara ya Kilimo Arusha
Vyama vya Ushirika vimeshauriwa kukopa fedha kwenye Mabenki kwa ajili ya  wanachama wao kwa kuwa waliowengi hawakopesheki hivyo kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu.

Akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha Maafisa Ushirika, umwagiliaji na afisa kilimo  Mkoani Arusha Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba amesema miundombinu mingi ya umwagiliaji inahitaji marekebisho makubwa  ili kuweza kutumiwa na wakulima.

Aidha miundombinu hiyo imekosa ukarabati kutokana na wakulima kutokuwa na mitaji ya kutosha na kutoaminiwa na taasisi za fedha kusaidia ukarabati huo.

Ameshauri tume ya Ushirika kuvisimia vyama vya ushirika ili viweze kukopa fedha Benki Kwa ajili ya wanachama lengo likiwa ni kufanya ukarabati Wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo kila mwanachama atawajibika kuchangia huduma hiyo.

Hatuwezi kufanya Kilimo cha kibiashara Kwa kutegemea mvua ambazo Nazo zimekuwa haziyabiriki nawashauri tume ya Ushirika na tume umwagiliaji kusimamia vyama hivyo kwenye skimu mbalimbali za umwagiliaji kukopa fedha ambazo zitatumika kurekebisha miundombinu ya umwagiliaji badala ya kutegemea serikali .alisema Mhe. Naibu Waziri

Naibu Waziri aliwataka maafisa ugani kuwafikia wakulima na kuelimisha namna ya kutumia na kutoa elimu juu ya matumizi bora ya viuatilifu vya mimea ili kupambana na visumbufu vya mazao ambavyo vimekuwa vikimsababishia mkulima hasara kubwa.

Naye afisa Umwagiliaji wa kanda mhandisi Juma Mdete amesema katika ukanda huo eneo ambalo linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta elfu 40 kati ya hilo linalotumika ni  hekta elifu 24 tu

Amesisitiza kwamba pamoja na matumizi kidogo ya eneo la umwagiliaji lakini maeneo yanayomwagiliwa yanasaidia upatikanaji wa chakula wakati wa ukame.

Akichangia wakati wa mjadala huo Afisa Kilimo Mkoa wa Arusha Bwana Daniel Loiruck amethibitisha kwamba ukiondoa Magonjwa ya mlipuko na uvamizi wa visumbufu vya mimea  maafisa kilimo wamekuwa wakijitahidi kuwafikia wakulima ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Naye mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoani Arusha bwana Loata Erasto Sanare  akamueleza Mhe. Naibu waziri kwamba hali ya ukame mkoani humo ni kubwa hivyo kuishauri serikali kuanza kufikiri njia mbadala ya kupambana na hali hiyo.

‘Msimu wa kilimo upo katikati lakini mpaka sasa hakuna mvua na tumezunguka sehemu mbalimbali hapa arusha mahindi yamekauka hata mvua ikinyesha  haiwezi kuleta mabadiliko tunaishauri serikali kufikiri mbinu za kukabiliana na hali hiyo’. Alisisitiza bwana Loata  Sanare


Share:

Taarifa kuhusu kuanza kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma Leo tarehe 2 Aprili

Leo Jumanne tarehe 2 Aprili 2019 Bunge la Tanzania linatarajia kuanza Mkutano wa Kumi na Tano utakaomalizika tarehe 28 Juni 2019 Mjini Dodoma.

Mkutano huu utakuwa ni mahsusi kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.

Katika Mkutano huo, wastani wa maswali 515 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na  kujibiwa na Serikali Bungeni.

Aidha, wastani wa Maswali 88 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa kwa siku za Alhamisi.

Pia, Bunge litajadili Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika hatua nyingine Bunge pia linatarajia kujadili na kupitisha Miswada Miwili  (2) ya Sheria ambayo itasomwa kwa hatua zake zote ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa mwaka 2019 (The Appropriation Bill, 2019), na Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 (The Finance Bill, 2019.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger