Tuesday, 15 January 2019

MBOWE ANYANG'ANYWA OFISI NA KUPEWA UHAMIAJI

Mwenyekiti wa (CHADEMA) taifa, Freeman Mbowe.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, amenyang'anywa Ofisi yake ya Ubunge na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kuagiza itumiwe na Idara ya Uhamiaji.

Ole Sabaya amefikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa ameelezwa kuwa Mbowe hajaitumia ofisi hiyo tangu mwaka 2010, hivyo haina haja kuendelea kuwepo na kutotumika katika matumizi yaliyo kusudiwa.

"Tangu Mbowe achaguliwe Mwaka 2010 hajawahi kuingia katika Ofisi hiyo kusikiliza kero za wananchi, sijui yupo wapi namsikia huko maeneo mengine akifanya vurugu, sasa ofisi hii itatumika kusaidia wananchi", amesema Ole Sabaya.

Mbowe amenyang'anywa ofisi hiyo akiwa gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23, 2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana ikiwemo kutoka nje ya nchi bila kibali, yeye pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko.

Mbowe na Matiko wako mahabusu baada ya kufutiwa dhamana kwenye kesi yao ya msingi inayowakabili juu ya kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa NIT, Akwilina Akwilini baada ya kufanya maandamano kuelekea katika ofisi za Mkurugenzi wa Kinondoni Februari 2018.

Chanzo:Eatv
Share:

MANJI KUSUBIRIWA LEO OFISINI JANGWANI

Makao Makuu ya klabu ya Yanga.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, Novemba mwaka uliopita kufuatia sintofahamu juu ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.

Mkuchika alisema kuwa, Manji aliliambia baraza hilo la wadhamini wa Yanga kuwa tarehe ya leo ndipo ataanza kwenda ofisini kwake Yanga, alipokuwa akijibu barua ambayo aliandikiwa na Baraza hilo.

Ikumbukwe kuwa mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo umesimamishwa na Mahakama kufuatia baadhi ya wanachama kushtaki juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi huo ambao ulitakiwa kufanyika wikiendi iliyopita.

Mashabiki na wanachama wa Yanga, wanasubiri endapo Mwenyekiti wao wa zamani, Yusuph Manji atarejea katika nafasi yake hii leo ama la!.

Chanzo:Eatv
Share:

MAPYA YAIBUKA KISA CHA MTOTO ALIYEFUNGIWA KABATINI

Neema Matimbe (15) akiwa na mwanaye.

Uongozi wa hospitali ya Mkoa wa Dodoma umesema kuwa tayari wamemruhusu, Neema Matimbe (15) ambaye inadaiwa mwanaye wa miezi mitano alifungiwa kabatini na mwajiri wake tangu alipozaliwa, lakini hajapata mtu wa kumchukua hivyo atakaa hospitali wakati uongozi ukiwasiliana na
Idara ya Ustawi wa Jamii ili waishi nae kwa sasa.

Imebainika kuwa mama mzazi wa Neema (15) naye ni mfanyakazi wa ndani kama alivyo mwanaye, hivyo kutokana na sababu hiyo, hospitali hiyo imesema ni vigumu kumruhusu binti huyo kwa sababu ya usalama wake.

Akizungumza na www.eatv.tv leo Januari 15, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Ernest Ibenzi amesema mama wa binti huyo yupo lakini naye anafanya kazi za ndani jijini Dodoma, jambo ambalo ni ngumu kwa binti huyo kuruhusiwa kuishi naye.

Mwalimu Anitha Kimako anayedaiwa kuwa mwajiri wa binti huyo ambaye anatuhumiwa kumpiga na kumshinikiza kumuweka mwanaye kabatini tangu alipozaliwa, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Januari 7 na kusomewa shtaka la kushambulia mwili ambalo alilikana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Februari 7.

Wakati hayo yakiendelea, kijana anayedaiwa kumpa ujauzito binti huyo na kumkataa, Salum Waziri atafikishwa mahakamani muda wowote kujibu mashtaka ya kumpa mimba mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18.

Chanzo:Eatv
Share:

B.O.T YAIFUNGA BENKI NYINGINE

Naibu Gavana Dk. Bernad Kibese.

Benki Kuu ya Tanzania BOT imehamishia mali na madeni yote ya Bank M kwenda Azania Bank baada ya benki hiyo kushindwa kuwahudumia wateja wake pamoja na kulipa madeni yao.
Akitangaza taarifa hiyo asubuhi ya leo Januri 14, Naibu Gavana Dk. Bernad Kibese amesema kwamba baada ya kutafuta njia mbalimbali za ufumbuzi wa matatizo ya Benk M, muafaka uliopatikana ni kuhamisha mali zote kwenda Benki ya Azania Bank Limited kwa mujibu wa sheria.

Aidha Dk. Kibese ameeleza kwamba wateja wenye mikopo wametakiwa kuendelea kulipa mikopo yao kulingana na mikataba yao huku benki kuu ikiahidi kufuatilia suala hili kwa ukarubu zaidi.

Aidha Dk Kibese amewatoa wasiwasi wateja wanaohamishiwa Azania Bank, kwamba Benki hiyo inatarajia kuwa na mtaji wa shilingi bilioni 164, ambayo ni kiwango cha juu cha mtaji unatakiwa kuendesha shughuli za kibenki ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 15 hivyo itaweza kuhudumia wateja wake wa zamani na wapya.

Benki kuu itaendelea kulinda maslahi ya wateja wa huduma za kibenki na kuimarisha uhimilivu wa sekta ya fedha nchini.

Chanzo:Eatv
Share:

NECTA YATOA UFAFANUZI KUHUSU MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2018


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Charles Msonde amesema bado hawajatangaza matokeo ya kidato cha nne na kuwataka Wananchi kuachana na taarifa feki zilizosambazwa katika mitandao.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Charles Msonde amesema bado hawajatangaza matokeo ya kidato cha nne na kuwataka Wananchi kuachana na taarifa feki zilizosambazwa katika mitandao.

Akizungimza na Nipashe Msonde alisema kuna baadhi ya watu ambao sio waaminifu na kazi yao ni kutengeneza taharuki kwa wananchi pasipo na sababu za msingi.

"Bado hatujatangaza matokeo na muda ukifika tutawatangazia kama ilivyo kwa miaka mingine na wananchi mtapata taarifa naomba muachene na taarifa feki katika mitandao," alisema Dk Msonde.

Via Nipashe

MALUNDE1 BLOG ITAKUTUMIA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MARA TU YATAKAPOTANGAZWA... 

Tembelea Mara kwa mara Mtandao huu...Lakini kama wewe ni  mjanja pakua App Yetu ...Ingia Play store kisha Andika Malunde 1 blog halafu bonyeza Install 

https://bit.ly/2Qb7qyF

Share:

KINA MAMA NA WATOTO WAJITOLEA KUIMARISHA ULINZI MITAANI

Wanawake wanaoishi maeneo ya mabanda nchini Kenya wamejitolea kukabiliana na ukosefu wa usalama katika maeneo yao, jukumu ambalo kwa muda mrefu liliachiwa wanaume.

Wanawake wanaoishi maeneo ya mabanda nchini Kenya wamejitolea kukabiliana na ukosefu wa usalama katika maeneo yao, jukumu ambalo kwa muda mrefu liliachiwa wanaume.

 Kupitia mpango walioupa jina ‘wamama na usalama' wanawake hao wanasema wanatambua jukumu lao kubwa la kuielekeza jamii ndiposa wanataka kuwa mstari wa mbele katika harakati za kukabiliana na ukosefu wa usalama. 

Maeneo ya mabanda yanasifika kwa kila aina ya uhalifu hali inayochangiwa na wingi wa watu, umasikini na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.

 Kina mama na watoto huathirika zaidi kutokana na visa vya uhalifu katika maeneo hayo huku vijana wakilaumiwa zaidi kwa kusababisha uhalifu.

Chanzo:Dw
Share:

MAHAKAMA YA KATIBA IMEANZA KUSIKILIZA RUFAA YA KUPINGA MATOKEO NCHINI DRC

Mahakama ya Katiba katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo leo inaanza kusikiliza rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30.


Mahakama ya Katiba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo inaanza kusikiliza ombi la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi kiongozi wa upinzani, Felix Tshisekedi.

Ombi hilo limewasilishwa na mgombea mwengine wa upinzani, Martin Fayulu, aliyetangazwa kushika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Desemba 30 ulioitishwa kumrithi Joseph Kabila.

Fayulu ameyaita matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, CENI, kuwa ni mapinduzi ya uchaguzi. Tshisekedi alitangazwa kupata asimilia 38.57 ya kura dhidi ya asilimia 34.8 za Fayulu.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzio, CENI, mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na Kabila alishika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 23.8.

Hata hivyo, akitegemea matokeo yanayosemekana kukusanywa na mawakala wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, CENCO, Fayulu anasema ni yeye aliyechaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura. Mahakama ya Katiba ina wiki moja ya kuamua juu ya madai ya Fayulu.

Chanzo:Dw
Share:

MBIVU NA MBICHI KUJULIKANA LEO.. UINGEREZA KUJITOA UMOJA WA ULAYA AMA LA

Wabunge Uingereza wanajitayarisha kupiga kura kwa iwapo kuunga au kutounga mkono mpango wa Theresa May wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.


Kura hiyo inayotajwa kuwa  Kura yenye umuhimu itafanyika baadaye leo wakati mjadala wa siku tano kuhusu Brexit ukikamilika.

Bi May amewataka wanasiasa kuunga mkono mpango wake au kuhatarisha kuwavunja moyo raia wa Uingereza.

Lakini huku wabunge wake mwenyewe wakitarajiwa kujiunga na wa vyama vya upinzani kupiga kura dhidi ya mpango huo, inatarajiwa pakubwa kwamba mpango huo hautofaulu.

Wabunge pia watapata fursa ya kutoa mapendekezo ya marekebisho ambayo yanaweza kuunda upya mpango huo kabla ya kura kuanza 19:00 kwa saa ya GMT.

Chanzo:Bbc
Share:

RAIS BONGO AREJEA NCHINI BAADA YA JARIBIO LA MAPINDUZI

Rais wa Gabon Ali Bongo anarejea nchini mwake leo Jumanne baada ya kuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi miwili akipokea matibabu nchini Morocco.

Bw Bongo anarejea wiki moja tu baada ya jeshi nchini humo kufanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi ya serikali yake.

Kiongozi huyo mwenye miaka 59 amekuwa akipokea matibabu nchini Morocco tangu Oktoba 24 alipopata kiharisi akihudhuria mkutano mkuu wa kiuchumi nchini Saudi Arabia.

Baada ya utata kuhusu hali yake, makamu wake hatimaye alitangaza mwezi Desemba kwamba alipatwa na kiharusi.

Mara pekee kwake kuonekana na umma ilikuwa ni wakati wa hotuba ya kila mwaka ya Mkesha wa Mwaka Mpya ambayo ilirekodiwa akiwa Morocco.

Chanzo:Bbc
Share:

BODI YA MIKOPO HESLB YATANGAZA NJIA MPYA KWA WANAODAIWA MIKOPO


Mkurugenzi wa bodi ya mikopo nchini, Abdulrazack Badru .

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, HESLB imekuja na mfumo mpya wa kielektoniki wa ulipaji madeni ya waliyokuwa wanufaika wa mikopo, ambapo mfumo huo utajulikana kwa jina la 'Goverment Electronic Payment Getway' (GEGP).

Akitangaza mfumo huo, Mkurugenzi wa bodi ya mikopo nchini, Abdulrazack Badru amesema mfumo utarahisisha uwazi wa kwenye ukusanyaji wa fedha hizo, utamfanya mdaiwa kulipa mahali popote alipo pamoja na kutoa fursa ya kuongezeka kwa mapato ya bodi hiyo.

"Tumekamilisha utaratibu mfumo wa serikali wa kukusanya mapato (GEPG), mwajiri na wanufaika watatakiwa kujiunga kwenye mfumo huu mpya wa GEPG ili kulipa madeni wanayodaiwa na serikali," amesema Badru.

Aidha amesema, "waajiri ambao watashindwa kulipa madeni ya wafanyakazi ambao walikuwa ni wanufaika, tutawaanzishia operesheni maalumu ya kupitia maofisini kwao ili kuwabaini wasiolipa mikopo ya bodi".

Akifafanua mfumo huo mpya mtaalamu wa GEPG, Baziri Bajunia amesema, "mfumo huu umekuwa ukitumika sasa hivi na taasisi nyingi ambazo zinafanya malipo kwa taasisi za serikali, ni utaratibu ambao hata taasisi nyingine za kifedha wanautumia".
Share:

WAZIRI LUKUVI ATOA HATI MILIKI ZA KIMILA KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA MAPOGOLO

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akitoa hati kwa mmoja ya mwananchi wa kijiji cha Mapogolo wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mapogolo waliohudhulia mkutano wa kutoa hati miliki.

 Na Fredy Mgunda- Iringa

NA FREDY MGUNDA,IRINGA

ZAIDI ya Kaya 200 za wafugaji wa kabila la Wamasai na Wamang’ati wamemilikishwa ardhi katika kijiji cha Mapogolo wilayani Iringa, hatua iliyoelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwamba “itamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji na kukuza utanzania.”

Kaya hizo zilikabidhiwa hatimiliki za ardhi za kimila juzi katika hafla iliyohusisha ugawaji wa jumla ya hati 2,404 za mashamba kwa wananchi wa kijiji hicho kinachopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Hati hizo zimetolewa kupitia mradi wa Urasimajishaji Ardhi Vijijini (LTA) unaotekelezwa kupitia  mpango wa Kupunguza Njaa na Utapiamlo (Feed The Future) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

“Leo tumeshuhudia makabila mbalimbali, wakiwemo ndugu zetu wamasai na wamang’ati wakipata ardhi katika ardhi ya wahehe. Hii ndio Tanzania, haina ubaguzi, mtu yoyote ana uwezo wa kufanya shughuli yoyote ya kimaendeleo mahali popote ili mradi havunji sheria,” alisema.

Alisema watanzania hawatarajii tena kusikia ugomvi baina ya wakulima na wafugaji katika kijiji hicho kwani mradi huo umeyawezesha makundi hayo kumiliki ardhi watakayoitumia kwa maendeleo yao endelevu katika jamii.

Mmoja wa wafugaji wa kabila la wamasai aliyemilikishwa ardhi katika kijiji hicho, Liwau Shang’ali aliwashukuru wenyeji wa kijiji hicho kwa kuikaribisha familia yake kijijini hapo akisema; “kama isingekuwa hivyo nisingewe kupata na kumiliki kisheria zaidi ya ekari saba za ardhi.”

Baada ya kupata shamba hilo, alisema hatarajii  kuepeleka mifugo yake kwenye mashamba ya watu wengine kwa kuwa shamba alilonalo linaweza kukidhi mahitaji ya mifugo yake kama ataliendeleza na kufuga kisasa baada ya kupata elimu.

Pamoja na kupata kipande hicho cha ardhi aliishukuru serikali ya kijiji kwa kupitia mradi huo kutenga eneo kubwa la malisho kwa ajili ya wafugaji akisema uamuzi huo unaongeza usalama wa mifugo yao, utalinda mashamba ya wakulima na hatimaye kukuza amani na ushirikiano miongoni mwao.

Awali Mkurugenzi wa LTA, Tressan Sulivan alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi na upimaji ardhi una manufaa makubwa katika kupunguza umasikini na njaa katika jamii hasa za vijijini.

Alisema wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanawake na wanaume wana haki ya kupata, kutumia, kumiliki na kugawa ardhi ili mradi wafuate sheria na taratibu zilizowekwa.

Sullivan alisema kwa kupitia mradi huo uelewa wa haki za wanawake na jamii katika kumiliki ardhi umeongezeka na umesaidia kuwahamasisha kutumia nafasi waliyopewa kuomba ardhi ambayo ni rasilimali muhimu katika kukuza kipato chao.

Katika kijiji hicho alisema mradi uliwezesha uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kukarabati masijala ya ardhi na kutoa mafunzo juu ya haki za ardhi na matumizi ya rasilimali ardhi kiuzalishaji ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema waliopata hatimiliki za kimila wanaweza pia kuzitumia kama dhamana mahakamani na katika taasisi za fedha kupata mikopo itakayowawezesha kushughulikia changamoto walizonazo.

Alisema jumla ya vijiji 36 kati ya vijiji 133 vya wilaya hiyo vimenufaika na mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2015 na ambao utakamilika mwakani, 2019.

Mmoja wa wanawake walionufaika na mpango huo, Sakina Mlelwa alisema wanafurahi kuona mila na desturi zilizokuwa zikiwanyima haki ya kumiliki ardhi katika jamii zao zinapoteza nguvu zake mbele ya sheria mbalimbali za ardhi.  

“Tumeelimishwa jinsi sheria hizo zinavyoondoa tofauti za umiliki wa ardhi baina ya mwanamke na mwanaume, jamii inajua na imeanza kuuona umuhimu wa mwanamke kutobaguliwa katika umiliki wa ardhi,” Mlelwa alisema.

Alisema tatumia kipande chake cha ardhi chenye ukubwa wa heka tatu kutafuta mikopo atakayoitumia kuwekeza katika shughuli za kilimo na ufugaji.
Share:

MPIRA WA KOMBE LA DUNIA WASHINDANISHWA NA YAI


Mpira wa Kombe la Dunia 2018 na picha ya yai iliyoweka rekodi.

Shirikisho la soka duniani (FIFA), kupitia ukurasa wake wa 'Instagram' limeanza mchakato wa kuisaka rekodi ya picha iliyopendwa zaidi (Likes) kwenye mtandao huo ili kuvunja rekodi ya picha ya yai.

FIFA wameomba wafuasi wao na wapenzi wa mpira duniani kuipenda picha hiyo ili iweze kuweka rekodi ya pekee katika mtandao huo.

''Mapema leo picha ya yai imeweka rekodi ya kuwa chapisho lililopendwa zaidi na ndipo tukafikiria kuwa picha ya mpira wa kombe la dunia iweze kuweka rekodi ya kupenda zaidi'', amesema.

Picha ya yai iliyopandishwa Januari 4, 2019 mapema leo ikafikisha 'likes' zaidi ya milioni 18 ambazo zilikuwa ndio nyingi zaidi kwa picha ya Kylie Jenner.

Mpaka sasa picha hiyo ya yai imependwa mara milioni 28.
Share:

NDEFU ZAIDI DUNIANI ‘AIRLANDER 10’ NDEGE YAPATA KIBALI CHA KUANZA MATENGENEZO

Sampuli ya awali ya Airlander iikiwa katika majaribio

Ndege ndefu zaidi duniani ipo tayari kwa ajili ya kuanza kutengenezwa kibiashara na kupakia abiria.

Hatua hiyo inakuja baada ya sampuli ya awali ya Airlander 10 yenye thamani ya pauni milioni 32 - ambayo ni mjumuiko wa ndege na meli inayopaa - kustaafishwa rasmi baada ya kufaulu majaribio ya mwisho.

Kutokana na mafanikio hayo, kampuni iliyobuni ndege hiyo ya Hybrid Air Vehicles (HAV) yenye maskani yake Bedford, Uingereza imepewa ruhusa na mamlaka ya usafiri wa anga wa kiraia wa nchi hiyo Civil Aviation Authority (CAA) kuanza uzalishaji wa aina hiyo ya ndege.

Kampuni hiyo awali mwezi wa Oktoba 2018 ilipewa kibali cha usanifu kutoka kwa mamlaka ya usalama wa usafiri wa kiraia barani Ulaya European Aviation Safety Agency (Easa).
Airlander 10 baada ya kuanguka Novemba 18, 2017 wakati wa safari ya majaribio

Stephen McGlennan, ambaye ni mtendaji mkuu wa kampuni ya HAV amesema mwaka 2018 ulikuwa mzuri sana na kusema kibali cha Easa kilikuwa ni ishara kubwa.

Amesema kwa sasa azma ya kampuni yake ni kutengeneza ndege aina ya Airlander 10 kwa ajili ya biashara na kupakia abiria.

"Sampuli ya awali imetimiza kazi yake kwa kutusaidia kupata takwimu na taarifa muhimu tulizokuwa tukizihitaji ili kuvuka kutoka hatua ya sampuli mpaka utengenezwaji wa ndege halisi," amesema.

Kwa sasa matarajio ni kwamba ndege ya kibiashara itakamata mawingu ikiwa na abiria waliolipia safari yao miaka ya mwanzoni ya 2020.

HAV ilitenga kitita cha pauni milioni 32 baada ya sampuli ya awali kudondoka, na kuwaarifu wanahisa wake kuwa hiko ndicho "kiwango cha juu zaidi cha bima".

Vibali kutoka kwa CAA na Easa sasa vinaipa kampuni hiyo "nafasi imara ya kuanza uzaishaji".

HAV ilifanya majaribio ya awali ya Airlander 10 kutoka katika eneo lake la awali la uwanja wa ndege wa Cardington mwezi Agosti 2016 lakini walihama eneo hilo Juni mwaka jana.

Mwezi Julai wakatangaza mipango yao ya kutoa "huduma za kifahari" pale ambapo majaribio yote yatakapomalizika kwa mafanikio.
Chanzo - BBC
Share:

MASHAHIDI 15 KUTOA USHAHIDI KESI YA UCHOCHEZI INAYOMKABILI ZITTO KABWE

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi wa mashahidi 15 katika kesi ya uchochezi na kusababisha chuki ndani ya jamii inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

Hatua hiyo ilifikiwa na mahakama hiyo Dar es Salaam jana kesi hiyo ilipopelekwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali Adofu Kisima, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuiomba kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, mwaka huu na mshtakiwa yuko nje kwa dhamana.

Zitto ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, anadaiwa kuwa Oktoba 28, mwaka jana, maeneo ya Kijitonyama wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, aliitisha mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho kwa lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwamba kinyume na sheria alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Anadaiwa kutamka kuwa; “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua.”
Share:

NDEGE YAANGUKA NA KUUA WATU 15


Watu 15 kati ya 16 wamekufa baada ya ndege ya mizigo kuanguka magharibi mwa mji mkuu wa Iran jana kufuatia hali
mbaya ya hewa.

Jeshi la Iran limesema ndege hiyo ya kijeshi aina ya Boeing 707 ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa Fath uliopo katika jimbo la Alborz nchini humo.

Mhandisi wa ndege hiyo, ndiye pekee aliyenusurika na alikimbizwa hospitali.

Taarifa ya jeshi imetolewa baada ya mkanganyiko kuhusu mmiliki wa ndege hiyo.

Mapema msemaji wa mamlaka ya anga ya Iran alikiambia kituo cha televisheni cha serikali kuwa ndege hiyo ni mali ya Kyrgyzstan huku msemaji wa uwanja wa ndege wa Manas nchini Kyrgyzstan akisema inamilikiwa na Payam, shirika la ndege la Iran.

Kulingana na kituo hicho cha televisheni timu ya wataalamu tayari imepelekwa kwenye eneo hilo la ajali.
Share:

DEREVA ALIYEPIGANA NA TRAFIKI WATATU AFIKISHWA MAHAKAMANI

Jeshi la Polisi mkoani Songwe limemfikisha mahakamani dereva Mawazo Jairos (29) kwa kosa la kupigana na askari watatu wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Licha ya dereva huyo kufikishwa mahakamani, amelalamikia kitendo cha kung’atwa eneo la shingoni na mgongoni na mmoja wa askari wakati wakipambana naye kwa madai alishindwa kutii amri bila shuruti.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Yusuf Sarungi jana alisema tukio la dereva na askari hao lilitokea Januari 12, mwaka huu saa 2:30 asubuhi Mtaa wa Transfoma mjini Tunduma.

Kamanda Sarungi alisema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kuzuia askari kufanya kazi yao na shambulio la kudhuru mwili.

Alidai siku ya tukio, askari hao walikuwa na maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) ambao walikuwa na operesheni ya ukaguzi wa magari.

Kamanda Sarungi alidai katika ukaguzi huo walisimamisha gari lenye namba za usajili T 842 AAC aina ya Mistubishi Fuso, likiendeshwa na Jairos mkazi wa Mbeya.

Alisema baada ya kusimamishwa Jairos anadaiwa kutoa lugha chafu za kashfa na matusi kwa askari na maofisa wa Sumatra.

Alidai kuwa dereva huyo akiwa kwenye njia ya vumbi kutoka eneo la Mwaka kwenda Songea, aliondoa gari hilo bila kuruhusiwa kitendo kilichowalazimu maofisa hao kulikimbiza na walipofika eneo la Makambini walifanikiwa kumkamata.

Kamanda Sarungi alidai kuwa baada ya gari hilo kukamatwa, Jairos alishuka akiwa amehamaki na kuanza kutoa lugha za matusi kwa maofisa.

Alidai kuwa dereva huyo ghafla alianza kuwashambulia askari, lakini wakafanikiwa kumdhibiti.

Kamanda Sarungi alidai kuwa dereva huyo alianza kupiga kelele kuwa askari hao wanamuua na wananchi wakajaa na kuwazuia askari wasiendele kumpiga.

Alidai kuwa baada ya askari hao kumwachia, alipata upenyo na kuingia katika gari, kisha kutoka na panga akaanza kuwatishia baadaye alifanikiwa kuondoka na gari hilo kabla ya kukamatwa katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi.
Share:

BILIONI 18 KUKARABATI UWANJA WA NDEGE WA SONGWE

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya, unatarajia kutumia Sh bilioni 18 kwa ajili ya ukarabati mkubwa.

Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila (pichani) wakati wa mapokezi ya ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya AIRBUS A 220-300 ambayo imeanza safari zake za Dar es Salaam kwenda Mbeya

Alisema mbali na uwanja huo, kuendelea kutumika kwa ndege mbalimbali,imeelezwa bado uwanja huo unahitaji kufanyiwa maboresho makubwa yatakayoendana na hadhi ya kamataifa ukiwemo ukarabati wa njia za kurukia ndege.

“Hatuna neno kuu kwa Rais, zaidi tunasema ‘asante na Mungu ambariki’, ndege hii imeleta neema kubwa hapa Mbeya, hivi karibuni uwanja huu utaanza kukarabatiwa,huo ni uamuzi wenye tija na upendo kwa Tanzania uliofanywa na Rais wetu, John Magufuli,”alisema.

Alisema hatua stahiki zitachukuliwa kwa baadhi ya watumishi na watu wote waliohusika na upotevu wa mabilioni ya fedha wakati wa ujenzi wa uwanja huo ambao hadi sasa kiwango chake hakina ubora unaostahili.

Hata hivyo, wakizungumzia ujio wa ndege hiyo baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya, walimuomba rais kuangalia njia mbadala itakayosaidia kupunguza gharama za usafiri huo wa
anga ili kila mmoja aweze kumudu hasa wasafirishaji wa mizigo na mazao.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger