Friday, 11 January 2019
MWALIMU ATEKWA,ANYWESHWA SUMU NA KUFARIKI AKIJIANDAA KUOA
Mwalimu Nocka Mwaisango (28) wa Shule ya Sekondari Kibwe, jijini Dodoma, amefariki dunia baada ya kunyweshwa sumu na watu wasiofahamika.Alikufa wakati akitokea mkoani Dodoma kwenda kijijini kwao mtaa wa Mtakuja, Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa lengo la kumuoa mchumba wake wa muda mrefu.
Baba mzazi wa mwalimu huyo, Oddy Mwaisango, alisema alipigiwa simu Desemba 20, mwaka jana na mtoto wake huyo kuwa anatarajia kwenda Mbeya kwa mapumziko ya sikukuu na kwamba atatumia mapumziko hayo kumuoa mchumba wake wa muda mrefu.
Alisema baada ya kupigwa simu hiyo, alishangaa kuona muda mrefu unapita bila kumuona na wiki moja baadaye alipigiwa simu na watu wasiofahamika waliotumia namba ya simu ya mtoto wake wakisema kuwa wanamshikilia kwa kazi maalum.
Alisema baada ya kauli hiyo aliamua kwenda Kituo cha Polisi Mbalizi, kuripoti tukio hilo.
Alisema siku iliyofuata mama yake alienda Dodoma katika shule aliyokuwa akifundisha kukutana na Mwalimu Mkuu ambaye alimjibu kuwa mtoto wake hakumuaga alipoondoka.
Alisema, ilibidi aende kuripoti Polisi Dodoma na Kitengo cha Uchunguzi wa Mawasiliano mkoani humo kiligundua kuwa mwalimu huyo yuko mkoani Morogoro.
“Ilibidi mama yake asafiri hadi Morogoro na aliripoti kituo cha polisi na kukabidhiwa mtu wa uchunguzi wa mitandao ndipo katika kuchunguza wakabaini wahalifu hao na mwalimu huyo wako mkoani humo, lakini ghafla wakawa hawaonekani kwenye mtandao,” alisimulia.
Alisema baadaye wahalifu hao walimpigia simu (baba) wakihitaji Sh. 5,000,000 kama kikombozi, lakini kwa sababu hakuwa na fedha aliwatumia Sh. 500,000 ili wamwachie.
Aliongeza kuwa siku iliyofuata mtoto wake aliwapigia simu mwenyewe na kuwaambia kuwa yuko kituo cha daladala cha Tazara Mbeya na walipoenda kumfuata walikuta hajitambui.
Aidha, alisema waliamua kumkimbiza hospitali ya Ifisi iliyoko Wilaya ya Mbalizi na baadaye walimhamishia Hospitali ya Rufani Mbeya.
Alisema akiwa wodini aliongezewa maji ya kutosha, lakini alikuwa analalamika kuumizwa kwenye koo na kifuani na katika uchunguzi wa madaktari ilibainika amenyweshwa sumu.
Alisema siku iliyofuata mwalimu huyo alifariki akiwa hajawataja waliomfanyia unyama huo huku chanzo cha kifo kikitajwa kuwa ni dawa aina ya ‘Asphxia Due Mothorax’ aliyonyweshwa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibwe, Dodoma, Mwasiti Msokola, alikiri kupata taarifa za kifo cha mwalimu wake na kwamba suala hilo linashughulikiwa na mkurugenzi ambaye ndiye mwajiri wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Chanzo:Nipashe
TUNDU LISSU AU ZITTO KABWE LAZIMA ASHINDE URAIS 2020 - ADO

Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT Wazalendo, Ado Shaibu ameweka wazi kuwa akipewa nafasi ya kuchagua kati ya Tundu Antiphas Lissu (CHADEMA)na Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) kugombea urais itakuwa ngoma droo kwa kuwa ni viongozi wenye misimamo na kusimamia kilicho sahihi.
Ado amesema kwamba anaamini kupiti muungano wa vyama vya upinzani uliofanyika, kiongozi yoyote atakayesimamishwa kugombea urais 2020 lazima ashinde.
Akiwachambua viongozi hao wawili kwenye www.eatv.tv, Ado amesema kwamba kutokana na ukaribu wake wa kufanya kazi na Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini na hata kwenye masuala mbalimbali tofauti na kazi anamtambua ni kiongozi mwenye maono makubwa sana na Tanzania hivyo akipatiwa nafasi atafanya mambo makubwa.
Akimzungumzia Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, Ado amemuelezea kama Mwanaharakati wa siku nyingi asiyeogopeshwa lakini mwenye uwezo wa kusimama na kuikosoa Serikali ya Rais Magufuli.
"Kwa kufanya kazi nyingi na Zitto Kabwe, naweza kusema Zitto yupo tayari kubeba majukumu makubwa ya kuiongoza Tanzania. Mimi ni zao la Zitto kwenye siasa lakini pia namjua vizuri. Lakini kwa upande wa Lissu namna ninavyomtambua sina budi kusema wote wawili ni ngoma droo", ameongeza Ado.
Mbali na hayo, Ado ameshauri vyama vya upinzani kuwa havipaswi kusimamisha mgombea kila chama bali wanapaswa kuteua kiongozi mmoja atakayepewa nguvu na vyama vingine ili kuweza kuitoa serikali ya CCM madarakani.
Chanzo- EATV
MBUNGE LUPEMBE APELEKA MABILIONI YA FEDHA JIMBONI KWAKE WAPIGAKURA WAELEZA.
Na Maiko Luoga Njombe Wananchi wa Jimbo la Lupembe katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mkoani Njombe Wamempongeza Mbunge wa Jimbo Hilo Mh. Joramu Hongoli Kwakile walichoeleza Kuwa Mbunge Huyo Anafanya Kazi kwa Umoja na Mshikamano na Wananchi wake Ikiwemo Kufika Mara kwa Mara Jimboni humo na Kusikiliza Kero zinazowakabili. Wakizungumza na Mwandishi wetu Aliyetembelea Baadhi ya Kata jimboni humo Ikiwemo kata za Lupembe, Matembwe, Ikuna, Kidegembye Pamoja na Idamba Wananchi hao Walisema Kuwa Kupitia Msukumo na Ufuatiliaji wa Mbunge Huyo Tayari Serikali Kupitia Rais Magufuli Imetoa Fedha Kiasi cha…
MAMA AJIFUNGUA WATOTO WANNE KWA MPIGO MWANZA
Picha hazihusiani na habari hapa chini
Jenipher Juma (23), mkazi wa Ibanda jijini Mwanza amejifungua watoto wanne miezi miwili kabla ya siku ya makadirio aliyotarajiwa kujifungua.
Jenipher ambaye huo ni uzao wake wa pili alijifungua mchana wa juzi Jumatano Januari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure.
Mama huyo amejifungua watoto wawili wa kiume na wawili wa kike ambao hali zao zinaendelea vizuri.
Huo ni uzao wake wa pili baada ya ule wa kwanza wa Aprili, 2018 ambapo pia alijifungua watoto wanne kwa wakati mmoja kwa njia ya upasuaji.
“Bahati mbaya watoto wangu wa kwanza walifia tumboni miezi mitatu kabla ya muda wa kujifungua ikabidi nifanyiwe operesheni,” alisema Jenipher.
Muuguzi kiongozi wa wodi ya wazazi, Tatu Lusesaamesema safari hii Jenipher amejifungua salama kwa njia ya kawaida na watoto wote wanaendelea kuwa chini ya uangalizi maalumu kutokana na kuzaliwa wakiwa chini ya uzito wa kawaida.
Via Mwananchi
NDUGAI AAMUA KULA SAHANI MOJA KIMATAIFA NA ZITTO KABWE SAKATA LA CAG
Unaweza kusema Spika wa Bunge, Job Ndugai ameamua kula sahani moja kimataifa na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hiyo ni kutokana na jana Alhamisi Januari 10, 2019, Ndugai naye kuandika waraka kwenda kwa katibu mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) kutoa ufafanuzi kuhusu barua iliyoandikwa na Zitto jana kwenda katika jumuiya hiyo.
Katika barua hiyo, ambayo Zitto amewatumia pia maspika wote wa nchi wanachama wa CPA na wanasheria wakuu, amesema sakata hilo lilianza baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusema anaamini kuwa kutotekelezwa kwa ripoti anazozitoa, ni udhaifu wa Bunge.
Wakati barua ya Zitto kwenda kwa katibu mkuu wa CPA, Akbar Khan ikieleza mzozo ulioibuka kati ya Ndugai na Profesa Assad, waraka wa Ndugai umesema Bunge hilo haliwezi kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, amesema maoni hayo yamemfanya Spika Ndugai kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwe na kujieleza.
“Mimi binafsi nimeguswa na suala hili. Naomba mabunge ya Jumuiya ya Madola muingilie kati si tu kwa sababu agizo la Spika Ndugai linavunja Katiba bali pia ni hatari kwa mustakabali wa Jumuiya ya Madola kwa ujumla,” ameandika Zitto katika barua hiyo.
Zitto amesema kama CAG ataadhibiwa na kamati ya Bunge kwa kutoa maoni yake, basi ni wazi kwamba uhuru wa Taasisi ya Juu ya Ukaguzi (SAI) utakuwa umevunjwa, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 2013.
Na Cledo Michael, Mwananchi
HABARI KUBWA KWENYE MAGAZETI YA LEO YA TANZANIA JANUARI 11,2019.
Fahamu yote yaliyojiri katika Magazeti ya Tanzania leo Januari 11, 2019. Hapa unapata habari zote zilizopewa uzito katika kurasa za mbele na kurasa za nyuma za habari za michezo na burudani.
Thursday, 10 January 2019
BODABODA AUAWA KWA KUPIGWA NA ABIRIA KISA KAKATAA NAULI YA 500
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamsaka mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi kwa tuhuma za kumuua dereva bodaboda Salumu Ramadhan (40).
Tukio hilo lilitokea Jumatatu ya Januari 7, 2019 majira ya saa nne usiku eneo la Foren Pub - Mawenzi katika Manispaa ya Morogoro ambapo mtuhumiwa alimpiga bodaboda huyo kichwani baada ya kukataa kumpakia mwanamke aliyekuwa naye kwenye pikipiki kwa nauli ya Sh500.
Na Hamida Shariff, Mwananchi
FUGA MENDE UTAJIRIKE
Mende ni mdudu anayechukiwa na watu wengi katika jamii kwa kuwa anahusishwa na uchafu sambamba na kusambaa kwa maradhi mbalimbali licha ya wadudu hawa kuwa na manufaa makubwa kwa binadamu ambayo hayajajulikana kwa wengi.
Lucius Kawogo ni mkazi wa wilayani Njombe akijishughulisha na ujasiriamali wa namna tofauti ukiwemo wa kufuga samaki, kuku, sungura, nyuki na pia, anafuga mende kwa ajili ya chakula cha samaki na kuku anaowafuga sambamba na mende kwa ajili ya biashara (kuuza).
Kawogo anayefanyia ufugaji wake wa mende katika Kijiji cha Igawisega, Kata ya Wino wilayani Madaba mkoani Njombe, anasema japo amefanya shughuli hiyo kwa takribani miezi sita iliyopita, anaona ufugaji wa mende ni kazi ndogo na rahisi, lakini yenye faida.
“Nimeanza kuongeza uzalishaji wa kuku na samaki kwa kufuga mende kwa ajili ya chakula cha mifugo hao kwa kuzingatia lishe na matunzo ya wadudu hao ambao bado kwa watu wengi hawafamu kuwa ni chakula kizuri… Mende wana kiasi kikubwa sana cha protini.” anasema.
“Kwa kweli, watu hawajajua tu, lakini ufugaji wa mende ni biashara inayolipa sana na ndiyo maana ninatamani wengi waifanye kazi hii ili hata ninapokuwa na oda nyingi kiasi cha mimi kupungukiwa, wateja wangu wasikose mzigo, bali nichukue kwa wafugaji wengine na kutimiza mahitaji ya wateja wangu huku pia, nikiwa nimesaidia biashara kwa wafugaji wenzangu.”
Anapozungumza katika mafunzo kwa wajasiriamali 1,000 yaliyoandaliwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) mjini Njombe hivi karibuni, Kawogo anasema anajuta kuchelewa kurasimisha miradi yake hali ambayo ingemwezesha kupata mtaji mkubwa na mapema zaidi.
“Kuchelewa kurasimisha miradi yangu kumenikosesha fursa nyingi maana siwezi hata kupata mkopo na kama ningekuwa nimerasimisha, ningepata soko na wateja wengi na ningetambulika na kujitangaza zaidi.” anasema.
“Nimewaomba Mkurabita wanisaidie kuniunganisha na benki ili benki inikopeshe mtaji wa kufanya ufugaji wangu mkubwa wa samaki, kuku, mende na vingine, lakini kwa masharti nafuu; yaani, nipewe muda wa kutosha kuanza marejesho tofauti na hali ilivyo kwa taasisi nyingi, unapewa leo mkopo, wiki hii hii unatakiwa uanze marejesho sasa unajiuliza kama sijaanza uzalishaji, hayo marejeso nitayatoa wapi, labda nikate pesa zilezile walizonipa, niwarejeshee…” anasema.
Mratibu wa Kitaifa wa Mkurabita, Seraphia Mgembe anasema: “Baada ya kumsikia akisema anatafuta namna ya kupata mkopo benki ukiwa na masharti nafuu, tuliwasiliana na kumuunganisha na benki ya CRDB, Tawi la Njombe nao wakasema, wako tayari kumsikiliza aende wazungumze.”
Meneja Urasimishaji Biashara wa Mkurabita, Harvey Kombe, anasema walipomtembelea Kawogo kuona namna anavyofanya shughuli zake hivi karibuni, walibaini maendeleo katika ufugaji wa samaki sambamba na ufugaji wa memde anaotumia kulishia samaki na kuonesha manufaa makubwa. Mintarafu mazungumzo na CRDB kuhusu mkopo huo, Kombe anasema: “Bado wapo kwenye mazungumzo…”
Kawogo amekiri kuwa katika mazungumzo hayo na CRDB. Anasema: “Bahati nzuri Mkurabita hao hao, wamenikutanisha pia na SIDO ambao wamekubali kunikopesha Sh 5,000,000 ili marejesho yaanze baada ya miezi 12….”
Mjasiriamali huyu anasema alianza na mtaji wa mende wa Sh 150,000 aliponunua boksi moja la mende wazazi 100 kutoka Kenya na sasa anafuga takriban mende 50,000 katika maboksi matano yenye takriban mende 10,000 kila moja na anakusudia kuongeza mengine.
Anasema asili ya wazo la ufugaji mende ni picha ya video aliyoona katika mitandao ya kijamii na kisha, akafuatilia na kusoma kwenye mitandao kwamba kuna uwezekano wa kufuga mende na funza ndipo akabaini uwezekano huo na manufaa yake. “… Nilikwishauza mende zaidi ya 600. Mende mmoja anauzwa kwa Sh 500 na yai moja la mende, linatoa watoto takriban 50…”.
Anabainisha kuwa, wateja wake wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Dodoma, Mwanza, Bukoba (Kagera), Mkuranga (Pwani), Dar es Salaam na Kigoma na kwamba, hajawahi kupata mteja kutoka Njombe.
Mkazi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam, Judica Losai anasema amevutiwa na bidhaa hiyo ya mende na kuweka oda ya mende 50 na maboksi mawili kwa mfugaji huyo ili kulishia bata anaowafuga.
Losai anasema: “Nitamshauri hata mwanangu Enoth Lyimo anayefuga pelege (samaki) na kuku huko Mlandizi (mkoani Pwani) ili naye aanzishe ufugaji wa mende kulishia samaki wake.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Menardy Mlyuka anampongeza Kawogo kwa ubunifu wa kufuga vitu (mende) ambavyo faida zake hazijafahamika vema kwa jamii.
Kawogo anasema ili mende wasisambae na kuwa kero kwa wakazi na maeneo jirani, huwajengea maboksi yasiyoruhusu hata mende mdogo kutoka, lakini akizingatia kuwaacha mianya ya kupitisha hewa ili wasife.
“Hapo ninapowafugia, pia kuna kuku wengi hivyo, ikitokea mende akatoroka, hawezi kufika mbali maana atagombaniwa na kuku. Unajua kuku wanapenda sana kula mende,”anasema.
MANUFAA Anapozungumzia manufaa aliyokwisha yapata katika ufugaji wa mende, Kawogo anasema:
“Mende ambao nimewauza, nimefanikiwa kutumia fedha kuchonga maboksi mengine, nimenunua sungura ninaowafuga na wengine nimekuwa nikiwatumia kukausha na kuwasaga kwa ajili ya kutengeneza chakula cha samaki na kuku ambao tangu waanze kula mende, wamekuwa na afya bora na uzalishaji mayai umeongezeka maradufu… wanataga sana”.
Anapoulizwa kama wateja au walaji wa kuku na samaki anaowafuga hawachukii wanaposikia wanakula chakula kinacholishwa kwa mende,
Kawogo anasema: “Wateja wanaposikia hivyo, wanafurahi kweli maana kwanza wanajua mende wanaprotini nyingi, na pia hawana chemikali kwa hiyo wanakula vyakula ambavyo havijalishwa kemikali. Watu hawataki kula kuku waliokuzwa kwa kulishwa kemikali…”
SOMA ZAIDI HAPA
Via Habarileo
Via Habarileo
Updates : DC MBONEKO AWATEMBELEA HOSPITALI WANAFUNZI WALIOPATA AJALI SHINYANGA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko amefika katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kuwajulia hali wanafunzi waliopata Ajali ya basi la Shule ya msingi Little Treasures iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga.
Ajali hiyo imetokea leo Alhamis Januari 10,2019 majira ya saa tisa alasiri wakati basi hilo lenye namba za usajili T183 AFE likitoka shuleni eneo la Bugayambelele kata ya Kizumbi kuelekea Ushirika likirudisha wanafunzi majumbani.
Akiwa hospitalini hapo Bi. Mboneko amewaagiza madaktari na wauguzi wote waliokuwa wamemaliza muda wao wa kuwepo kazini kurudi mara moja kwa ajili ya kutoa huduma ya dharula kuwahudumia majeruhi hao.
“Kuna Watoto wengine naona wana tatizo la meno hivyo Madaktari waliotoka warudi kusaidia kuwahudumia watoto , hii dharura imetokea ni lazima ifanyike vizuri” alisema Mboneko.
Aidha Bi. Mboneko amewapongeza wauguzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Wa Shinyanga kwa kutoa huduma ya haraka kwa majeruhi wa ajali hiyo huku akimsisitiza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dokta Harbet Masigati kusimamia vyema majeruhi waliobaki wamelazwa hospitalini hapo .
“Ila niwapongeze sana kwa namna mlivyojitolea kuwahudumia hawa watoto mmewahudumia vizuri na kwa haraka , naombeni muendelee hivyo hivyo kwa hawa waliobaki” alisema Mboneko
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dokta Herbet Masigati amesema wamepokea watoto 30 baada ya kuwahudumia na wengi wao wamewaruhu na kubaki na wanafunzi takribani wanne huku akiweka wazi kuwa hali zao zinaendelea vizuri.
Kwa Mujibu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule chanzo cha ajali hiyo ni dereva kuendesha gari huku akichezea simu/akichat huku akiongeza kuwa mara baada ya ajali kutokea dereva alikimbia.
ANGALIA PICHA
Kwa Mujibu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule chanzo cha ajali hiyo ni dereva kuendesha gari huku akichezea simu/akichat huku akiongeza kuwa mara baada ya ajali kutokea dereva alikimbia.
ANGALIA PICHA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko (kushoto
)akiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kuwajulia hali wanafunzi waliopata ajali ya basi la Shule ya msingi Little Treasures iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga.Picha zote na Steve Kanyefu Malunde1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwajulia hali baadhi ya wanafunzi waliopata ajali ya bali la Shule ya msingi Little Treasures
ASILIMIA 52 YA WATANZANIA WAMEPIMA VVU

Dkt. Faustine Ndugulile
Na WAMJW-DOM
SERIKALI imesema kuwa Watanzania wapatao 2,405,296 hadi kufikia tarehe Oktoba 2018 walipima VVU kupitia Kampeni ya ‘Furaha Yangu’ ambao ni sawa na asilimia 52 ya lengo la kuwapima watanzania wapatao 4,638,639 hadi Desemba 2018.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika kikao cha kamati ya bunge ya huduma za jamii kilichofanyika leo jijini Dodoma.
“Hadi kufikia tarehe 31 Oktoba 2018, jumla ya watanzania 2,405,296 walikuwa wamepima VVU kupitia Kampeni ya ‘Furaha Yangu’ ambao ni sawa na asilimia 52 ya lengo la kuwapima watanzania wapatao 4,638,639 hadi Desemba 2018” Alisema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa Miongoni mwa wote waliopima, wanaume walikuwa ni asilimia 44 huku wanawake wakiwa ni asilimia 56. Kati yao, watu 70,436 (2.9%) walikutwa na maambukizi ya VVU, ambapo wanaume 27,984 (2.6%) na wanawake ni 42,452 (3.2%).
Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya UKIMWI namba 28 ya mwaka 2008 ili kupendekeza marekebisho yatayoruhusu upimaji Binafsi wa VVU (HIV Self-testing).
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kupunguza umri ya kupima VVU kwa ridhaa ya mzazi au mlezi kutoka miaka 18 hadi 15, hii ni kutokana na kasi ya maambukizi kuongezeka katika umri huo.
Pia, aliendelea kusema kuwa Wizara imeendelea kutoa huduma za Tohara ya Kitabibu kwa Wanaume kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mwanamke kwenda kwa mwanaume katika mikoa ya kipaumbele ambayo haina utamaduni wa kutahiri na ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU.
“Hadi kufikia Septemba, 2018 Mikoa kumi na saba (17) inatoa huduma za Tohara ambayo ni Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Singida, Kigoma, Mara na Morogoro” Alisema Dkt. Ndugulile
Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali inaendelea kutoa Huduma ya tohara kwa wanaume bila malipo katika vituo vya huduma za afya na kupitia huduma mkoba ngazi ya jamii ambapo hadi kufikia Septemba 2018, jumla ya watu 3,702,387 wamefanyiwa tohara nchini ambao ni wanaume, vijana na watoto wa kiume.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile alisema kuwa Hadi kufikia mwisho wa Desemba 2018, Wizara iliweza kuwaandikisha katika huduma za tiba na matunzo watu wanaoishi na VVU wapatao 1, 087,382. Watu 68,927 waliandikishwa katika kipindi cha robo ya mwaka cha Juai hadi Septemba 2018 ambapo kati yao, 1,068,282 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU, ambapo watoto walikuwa ni 58,908.
Idadi ya vituo vinavyotoa huduma na matunzo vimeongezeka hadi kufikia 6,206 Desemba 2018. Sawa na asilimia 72.7 ya vituo vyote vya huduma za afya nchini. Miongoni mwa vituo hivyo, vituo kamili vinavyotoa huduma za tiba na matunzo ni 2,103 wakati vituo vinavyotoa huduma ya afya mama na mtoto (RCH) ni 4,103.
TCAA YAZINDUA MNARA WA KUONGOZEA NDEGE KATIKA UWANJA WA NDEGE PEMBA, ZANZIBAR
Mgeni rasmi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof.Makame Mbarawa, akikata utepe kuzindua mnara wa kuongozea ndege wa Pemba, baada ya kufanyiwa Ukarabati mkubwa. Hafla hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania Prof. Makame Mbarawa akizungumza mbele ya umati uliofika katika hafla ya uzinduzi wa mnara wa kuongozea ndege katika uwanja wa ndege Pemba.
Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba Dr. Sira Ubwa Mamboya akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa mnara wa kuongozea ndege katika uwanja wa ndege Pemba.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari akihutubia katika katika hafla ya uzinduzi wa mnara wa kuongozea ndege katika uwanja wa ndege Pemba.
Mgeni rasmi Waziri wa Maji na Umwangiliaji, Pro. Makame Mbarawa, Katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa serikali wakaribishaji wa hafla ya Uzinduzi wanara wa kuongozea ndege wa Pemba.
Mnara wa kuongozea ndege katika uwanja wa ndege Pemba.
Baadhi ya wageni waliohudhuria uzinduzi mnara wa kuongozea ndege wa Pemba, baada ya kufanyiwa Ukarabati mkubwa. Hafla hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mgeni rasmi akiwasili Katika hafla ya Uzinduzi mnara wa Kuongozea ndege Pemba.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imezindua mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Pemba, Zanzibar.
Mradi huu umegharimiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, mgeni rasmi Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania Prof. Makame Mbarawa amesema mnara huo umezinduwa mara baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ulioanza Novemba 2017 hadi Agosti 2018.
Amesema mradi huu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 300 ni miongoni mwa miradi inayozinduliwa katika wiki ya maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mradi unalenga kuboresha huduma za uongozaji ndege katika uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na kuimaimarisha usalama wa abiria na vyombo vinavyotumia uwanja huu.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba Dr. Sira Ubwa Mamboya ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu inayopelekea kupata matokeo chanya.
"Binafsi sina la kusema leo nimefurahi sana kuona jinsi serikali zetu zinavyopambana kuleta miundo ya kisasa ili kuweza kwenda na teknolojia ya kisasa," amesema.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari amesema ukarabati umefanywa na Kampuni ya kitanzania ya M/s Future Century Limited ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na kubadilisha vioo vinavyozunguka mnara wa kuongozea ndege, kurekebisha paa na kuzuia kuvuja, kuweka vizuizi vya usalama (guard rails) na kuweka upya mfumo wa viyoyozi (Air conditioning), kuweka upya mfumo wa umeme, kuweka upya mfumo wa simu na taarifa za kieleckroniki na kupaka rangi upya.
Ameongeza kuwa TCAA ina jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri wa anga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya kisheria ya Mamlaka ni pamoja na kudhibiti masuala ya ki-usalama, ki-uchumi katika usafiri wa anga na kutoa huduma za uongozaji ndege.
TCAA inatoa huduma za uongozaji ndege kwenye vituo kumi na nne (14) ambavyo ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dodoma, Iringa, Songwe, Songea, Mtwara, Zanzibar na Pemba.
MWANAMKE APEWA DAWA YA KUSIMAMISHA UUME BADALA YA KUTIBU MACHO

Mwanamke mmoja nchini Uingereza amepata majeraha ya kemikali baada ya kupewa kwa makosa dawa ya kusimamisha uume badala ya dawa ya kutibu macho.
Mwanamke huyo kutoka Glasgow, Uskochi alipewa dawa ya kupaka ya Vitaros badala ya VitA-POS.
Daktari wake alimuandikia dawa sahihi ya kutibu matatizo ya macho ya VitA-POS, ambayo ipo katika mfumo wa kiminika kilaini.
Hata hivyo, kulitokea mkanganyiko wa kusoma maandishi ya daktari na mfamasia akatoa dawa ya Vitaros, ambayo pia ipo katika mfumo wa kiminika laini, lakini yenyewe huchochea kusimama kwa uume.
Baada ya kupaka dawa hiyo, alipata maumivu makali, jicho kuvimba hali iliyompelekea kushindwa kuona vizuri.
Majeraha hayo ya kemikali hata hivyo yaliweza kutibika, na jicho lake kusafishika baada ya siku chache.
Mkasa wa mwanamke huyo umeandikwa kwenye jarida la BMJ Case Reports. Jarida hilo limewataka madaktari kutumia herufi kubwa ili kuepuka makosa kama hayo kutokea.
Maandishi yalofanana
Daktari Magdalena Edington, ambaye ameandika ripoti hiyo amesema: "Makosa katika kutoa dawa ni jambo la kawaida. Dawa zenye vifungashio na majina yafananayo zinaongeza hatari za kutokea makosa hayo.
"Hata hivyo, ni jambo la kustaajabisha katika mkasa huu kuwa hakuna hata mtu mmoja, akiwemo mgonjwa mwenyewe, daktari na mfamasia ambaye alijiuliza iweje mgonjwa mwanamke apewe dawa ya matatizo ya kiume.
"Tunaamini kuwa mkasa huu ni muhimu sana kuuripoti ili kukuza uelewa wa kutoa dawa kwa njia salama."
NDEGE NYINGINE MPYA YA SERIKALI AINA YA AIRBUS A220-300 KUTUA TANZANIA KESHO
Ndege nyingine mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300 iliyopewa jina la Ngorongoro inatarajia kuwasilini nchini kesho Ijumaa mchana, ambapo itafanya idadi ya ndege zilizonunuliwa na Serikali kufikia sita.Ndege hiyo ambayo tayari inanakshi za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) itafanya jumla ya ndege za ATCL kufikia 7, ikijumlishwa na ndege yao ya zamani aina ya Bombardier Q300 ambayo sasa ipo katika matengenezo.
Ndege inayotarajiwa kutua kesho ni ya pili ya aina hiyo, kwani Desemba 23 iliwasili ya kwanza ambayo ilipewa jina la Dodoma.
Ndege nyingine zinazomilikiwa na shirika hilo ni Bomberdier Q400-8 tatu na Boeing 87-8 (Dreamliner) moja.
MAHAKAMA YAAMURU KUFUKULIWA KWA MWILI ULIOZIKWA MWAKA JANA

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, imeamuru kufukuliwa kwa mwili wa marehemu Benedict Msote (68), aliyefariki dunia miezi minne iliyopita ili ufanyiwe uchunguzi wa chanzo cha kifo chake.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kuwepo ubishani kati ya taarifa zilizoandikwa na Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kuhusu chanzo cha kifo cha Msote aliyefariki dunia Oktoba 5, 2018.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Pascal Mayumba, aliamua kutoa kibali hicho kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuchanganya kuhusu chanzo kifo cha marehemu huyo.
Aidha Hakimu Mayumba ameiambia mahakama hiyo kwamba polisi wilayani hapa walitoa ombi la kufukuliwa mwili wa Msote baada ya kuwepo kwa malalamiko ya kuwa kifo chake kilitokana na kipigo na si shinikizo la damu kama inavyodaiwa.
Ofisa Upelelezi wa Polisi Mjini Mpwapwa, Makubura Kati alisema, ndugu wa marehemu walipeleka malalamiko kuwa kifo cha ndugu yao kilitokana na kipigo.
Pia ulizikwa kabla mwili huo haujafanyiwa uchunguzi. Hadi sasa kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Emanuel Sindato amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kusababisha kifo hicho.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Julius Msote alisema waliamua kufukua mwili wa baba yao baada ya kubaini kuwa kifo chake hakikutokana na shinikizo la damu kitu alichokisema kilitokana na kipigo.
“Mwili wa baba tangu unafikishwa hospitalini ulitokana na kipigo na hata Fomu ya Polisi namba tatu (PF3) tulijaza, sasa ninashangazwa kuambiwa mzee alifariki dunia kwa shinikizo la damu, tatizo ambalo hajawahi kuwa nalo katika maisha yake yote,” alisema.
Aidha alisema wanasubiri taarifa ya daktari aliyefanya uchunguzi huo na kubaini chanzo cha kifo cha baba yao.
Uchunguzi huo ulifanywa na Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya, Dk Hamza Mkingule na Bibi Afya wa Wilaya, Merry Mabangwa chini ya uangalizi wa Polisi wa Kituo Kikuu cha Wilaya.
Uchunguzi huo uliofanywa na Mganga Mfawidhi na watendaji wengine utawasilishwa Januari 25,kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani.
Chanzo-Habarileo




