Monday, 7 January 2019

NAHODHA WA SIMBA ATOA SIRI ZA AUSSEMS KWA WAARABU

Nahodha wa klabu ya soka ya Simba, John Bocco amesema kocha Patrick Aussems anatumia michuano ya mapinduzi kwa kutengeneza ushindani kwa kila mchezaji kwaajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya JS Souara.

Bocco ameysema hayo akiwa visiwani Zanzibar ambako Simba inashiriki michuano hiyo ambayo imeshuhudiwa kocha Patrick Aussems akibadilisha wachezaji wake katika mechi mbili ambazo tayari ameshacheza.

''Haya mabadiliko anayoyafanya kocha ni kuelekea mechi yetu ya kimataifa, kila mchezaji anatakiwa kuwa imara na tayari kwa mchezo maana timu nyingine inaweza kubaki huku Zanzibar wengine wakaenda kucheza mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya JS Souara'', amesema Bocco.

Katika michuano ya Mapinduzi Simba ilishinda mchezo wake wa kwanza kwa mabao 4-1 dhidi ya Chipukizi ya Zanzibar kabla ya jana usiku kuifunga KMKM kwa bao 1-0.

Kwa mujibu wa ratiba ya kikosi hicho endapo kitafuzu nusu fainali ya Mapinduzi Cup watabaki wachezaji wa kikosi cha pili huku wale wa kikosi cha kwanza wakirejea Dar es salaam tayari kwa mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi.

Chanzo:Eatv
Share:

RAIS BONGO APINDULIWA NA WANAJESHI GABON

Kundi la maofisa wa jeshi nchini Gabon limetangaza kwamba limetekeleza mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ali Bongo.

Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vimesema kwamba taarifa ya wanajeshi hao kufanya mapinduzi imetangazwa katika kituo cha redio cha serikali majira ya saa kumi na mbili alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Imeelezwa kwamba wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita yanaendelea na doria katika barabara za mji mkuu Libreville. Shirika la habari la AFP inasema milio ya risasi imesikika jijini humo.

Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo "kurejesha demokrasia" na wametangaza kwamba wanataka kuunda 'Baraza la Taifa la Ufufuzi/Ukombozi' huku wakikosoa hotuba ya Mwaka Mpya iliyotolewa na Rais Bongo mnamo 31 Desemba.

Mapinduzi hayo yamefanywa wakati Rais Bongo akiwa nje ya nchi hiyo kwa zaidi ya miezi miwili, akipokea matibabu nchini Morocco kutokana na maradhi ambayo hayajafichuliwa baada ya kuugua akiwa ziarani Saudi Arabia, 24 Oktoba.

Rais Ali Bongo alianza kuiongoza Gabon 2009 kwa mara ya kwanza na baadaye katika uchaguzi wa marudio uliofanyika 2016 ambapo inaelezwa kuwa alipokea madaraka kutoka kwa baba yake Omar Bongo ambaye aliiiongoza nchi hiyo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 40.

Chanzo:Eatv
Share:

WAZIRI APIGA MARUFUKU HALMASHAURI KUTUMIA WAKANDARASI

Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza watendaji wa halmashauri zote nchini kutotumia wakandarasi kujenga miradi mbalimbali inayohusu sekta ya afya.

Ametoa agizo hilo mkoani Ruvuma wakati alipotembelea na kujionea ukarabati na ujenzi wa Chuo cha Wauguzi Songea na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Amesema kuwa miradi hiyo inatakiwa kutumia mtindo wa 'Force Account', ambao unatumia mafundi wa kawaida kujenga miradi hiyo.

"Fedha zote za maendeleo Ndani ya Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, utaratibu utakuwa ni 'Force Account'. Kibali cha kwenda kwa wakandarasi kitatoka kwa mawaziri, kwasababu mwisho wa siku ninayewajibika ni mimi", amesema Dkt. Faustine Ndugulile.

Naibu Waziri Ndugulile amefikia hatua hiyo baada ya kupokea taarifa ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa baadhi ya majengo na ukuta wa Chuo cha Waganga mkoani humo, ambao ungegharimu zaidi ya shilingi milioni 900, akisema kwamba endapo ungetumika mfumo wa 'Force Account' zingejenga jengo hilo na ukuta.

Chanzo:Eatv





Share:

KATIBU MKUU WA CCM : VYAMA VINAVYOTAFUTA WAFUASI MITANDAONI,MAHAKAMANI VITAKUFA




Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania Dkt. Bashiru Ally amesema vyama vinavyotafuta wafuasi kwenye nyumba za ibada,mahakamani,mitandaoni safari yao siyo ndefu vitakufa kifo cha mende.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo leo Jumatatu Januari 7,2018 wakati akizungumza na wanachama wa CCM mkoa wa Shinyanga katika ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga.

Amesema kutokana na vyama vya siasa kutafuta wafuasi kwenye misikiti,makanisa,mahakamani na mitandaoni haviwezi kufika mbali basi vitakufa kwa sababu ya kujitakia wao wenyewe.

Ameviomba vyama vya siasa kutoshinda mahakamani kutafuta ruzuku na kwamba wanahitaji ushindani wa kweli wa maendeleo. 

“Tunahitaji kujenga chama kwa misingi ya kidemokrasia,tunataka ushindani utawavutia watanzania kuendelea kutuamini,Kadri tutakavyojiimarisha tutakuwa chama mfano kwa vyama vingine 

Aidha amewataka wanachama wa CCM kuacha tabia ya kutafuta ubunge na nafasi zingine za uongozi na badala yake wawaache viongozi waliochaguliwa watekelezea majukumu yao na muda utakapofika wa kufanya uchaguzi. 

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania Dkt. Bashiru Ally  akizungumza na wanachama wa CCM katika ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga leo - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

SERIKALI YA GABON YAPINDULIWA NA JESHI

Kundi la wanajeshi nchini Gabon limetangaza kwamba limetekeleza mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita wanashika doria katika barabara za mji mkuu Libreville. Shirika la habari la AFP inasema milio ya risasi imesikika jijini humo. Amri ya kutotoka nje imetangazwa. Tangazo kutoka kwa kundi la vijana wa umri wa makamo linatangazwa na kurudiwa katika kituo cha redio cha serikali nchini humo, ambapo wanasema kumekuwepo na wasiwasi kuhusu uwezo wa Rais Ali Bongo kuongoza nchi hiyo. Walichukua udhibiti wa kituo hicho cha…

Source

Share:

TUNDU LISSU AACHIA WARAKA,SPIKA NDUGAI AJIBU

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu amemlalamikia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kwenda kumuona hospitalini kama alivyoahidi.

Lissu ameyasema hayo kupitia Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ .

Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wala watumishi wa Bunge licha ya kuahidiwa.

“Kabla sijahamishiwa nchini Ubelgiji (Januari 6 mwaka jana) kutoka Kenya, Spika Ndugai aliahidi hadharani, kwenye mahojiano na Azam TV, kwamba atafika kunitembelea, mahali popote nitakapokuwa nimelazwa hospitalini.

"Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au ofisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali.”

Akizungumzia kuhusu madai hayo, Spika Ndugai amesema wameshayatolea ufafanuzi malalamiko hayo mara kadhaa.

Amesema alipanga kwenda kumtembelea Nairobi lakini, “tarehe zangu nilizokuwa nimezipanga, akawa amehamishiwa kwenda Ubeligiji, kwa hiyo safari yote ikawa imevurugika.”

Kuhusu Bunge kugharamia matibabu yake, alisema ni kwa sababu hakufuata utaratibu unaotakiwa kwa mbunge kutibiwa nje.

“Mbunge hatibiwi katika nchi anayotaka mwenyewe kama yeye anavyofanya, unatibiwa nje pale inapobidi, pale unapokuwa na recommendations (ushauri) ya madaktari bingwa watatu wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.

Alisema kuna wabunge wanaotibiwa nchi za mbali kama Ujerumani, Uingereza na Marekani kwa gharama zao.

“Sasa nashangaa analalamika kitu gani wakati ukishachagua jambo si unaenda na chaguo lako?” alihoji.

Aliongeza kuwa Bunge linaendelea kumlipa mshahara kwa sababu hajafukuzwa kazi.

“Tumempenda sana huko aliko na ndiyo maana anauliza kwa nini tunaendelea kumlipa, angesema ahsante kwa upande huo, angalau mmenijali,” alisema.


Aidha, Tundu Lissu amelalamika tangu kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi Septemba 7, 2017 hakuna mtu yoyote aliyehojiwa na wapelelezi wala Jeshi la Polisi kutofanyia uchunguzi shambulio hilo.


“Katika shambulio hili, hakuna anayeshukiwa na Jeshi letu la Polisi hadi sasa. Hakuna aliyehojiwa na wapelelezi mahiri wa Jeshi letu la Polisi. Hakuna aliyekamatwa na kwa hiyo, hakuna aliyeshtakiwa” alidai Lissu.

Hata hivyo, Oktoba 2017, akizungumza na vikosi vya jeshi hilo Mbeya, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alitangaza kufunga mjadala kuhusu kupigwa risasi kwa Lissu huku akiwaonya wanasiasa kuacha kuuendeleza na waliachie jeshi lifanye kazi yake.


Katika waraka wake huo, Lissu amesema anaendelea vizuri na matibabu, kwa sasa ameanza mazoezi ya kutembea bila magongo.
Share:

MKUU WA MKOA WA TABORA AWAONYA WANAOUNGANISHA SAUTI NA RAIS MAGUFULI..SOMA HIYOOO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Aggrey Mwanri amewataka Watu wanaounganisha sauti yake na kuchanganya sauti ya Rais Magufuli, kuacha mara moja tabia hiyo kwani inaleta picha mbaya kwa viongozi.

Mwanri amesema kuwa kitendo hicho sio kizuri, kwani viongozi wa juu kama Rais ni taasisi na mamlaka yake ni kubwa.


Mwanri ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu kusambaa kwa kipande kifupi cha video ambayo inamuonesha kiongozi huyo, na Rais Magufuli wakijibishana kwa maneno.


Mwanri amesema; "wakati mwingine huwa naona wanavyotuweka pamoja na viongozi ambao nawaheshimu sana, si kitu kinachonifurahisha sana, licha ya kuunganisha kuleta kichekesho lakini mimi binafsi sifurahishwi nao."


"Kuhusu wanaotumia sauti yangu kutengeneza muziki sina shida nao ila muhimu mimi matokeo yangu ipatikane kwa wananchi wa Tabora na wala sitakimbilia kwenye biashara eti wanilipe." ameongeza Mwanri.


Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri amekuwa maarufu kupitia mitandao ya kijamii hivi karibuni kwa kuanzisha misemo mbalimbali ikiwemo, sukuma ndani, fyekelea mbali, pamoja na Injinia soma hiyo.
Share:

Sunday, 6 January 2019

WAZIRI WA KILIMO: IFIKAPO JUNI 2019 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMESAJILIWA NA KUWA NA VITAMBULISHO


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo; Tunduru-Ruvuma
Wizara ya Kilimo imeanza kuandikisha wakulima nchini kwa lengo la kuwatambua ili kuwarahisishia huduma mbalimbali zikiwemo uhitaji wa pembejeo za kilimo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati akizungumza na Wenyeviti na makatibu wa Vyama vya Msingi kwenye kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 6 Januari 2019 katika Ukumbi wa Claster Mjini Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma.

Akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Tunduma Waziri huyo amesema kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa taarifa zinazohusu uandikishwaji wa wakulima kuwa una lengo baya, hivyo amewataka wakulima hao kutosikiliza propaganda hizo zisizo na tija kwani utambuzi wa wakulima ni jambo la kawaida kufanya utambuzi.

Alisema kuwa kuandikisha kwa wakulima ni njia pekee ya kuwa na takwimu sahihi kwa kutambua idadi ya wakulima, vijiji na Kata wanazolima ikiwa ni pamoja na kutambua ukubwa wa mashamba yao kwani kufanya hivyo serikali itakuwa na urahisi wa kuwahudumia wakulima hao.

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera kwa kusimamia vyema sakata la korosho kwa kusikiliza kesi 11 huku zikifikishwa mahakamani kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

“Nakupongeza sana Mhe Homera kwa usimamizi madhubuti katika kudhibiti kangomba nilipata taarifa kuwa Kg 17,679 za korosho mmezikamata pamoja na zingine Kg 2,779.2 jambo hilo ni zuri endeleeni kusimamia vyema majukumu ya serikali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM yam waka 2015-2020” Alikaririwa Mhe Hasunga

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanza kuwalipa wasafirishaji wa korosho kutoka maghala ya vyama vya msingi, kuwalipa gharama za uendeshaji kwa vyama vya masingi, kuwalipa watunza maghala na magunia sambamba na kuondoa mzigo kwa wakati kutokana na ghala kuezuliwa na upepo lililokuwa na jumla ya Tani 536.

Pamoja na pongezi hizo pia Homera amezitaja changamoto mbalimbali katika Oparesheni korosho kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya wananchi waliofanyiwa uhakiki, utaratibu wa upatikanaji wa miche ya korosho kwa msimu wa mwaka 2018/2019, na mkanganyiko wa upatikanaji wa mapato ya Halmashauri 3% ya bei ya korosho.
Share:

KINYWAJI KILICHOWEKEWA VIAGRA 'KUONGEZA NGUVU ZA KIUME' CHAZUA BALAA..JAMAA APATA TABU

Shirika la kupima viwango vya ubora wa bidhaa nchini Uganda The Uganda National Bureau of Standards (UNBS) linatarajiwa kufanya utafiti na vipimo zaidi kuhusu ubora wa kinywaji cha Natural Power SX , kinywaji cha kuongeza nguvu mwilini kinachodaiwa kuwa na dawa ya Viagra.

Kulingana na gazeti la The Sunday Monitor nchini Uganda vipimo vya maabara vilivyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti matumizi ya dawa nchini Uganda NDA ,vilibaini kwamba kinywaji cha Natural Power SX kina Sildenafil Citrate, ambayo hukuzwa kama Viagra.

The Sunday Monitor linasema kuwa, NDA mnamo mwezi Disemba 28 kupitia barua iliotiwa saini na bwana David Nahamya kwa niaba ya katibu wa mamlaka hiyo bi Dona Kusemererwa, liliripoti kwa Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la ubora wa bidhaa nchini Uganda Dkt. Ben Manyindo kwamba mlalamishi alidai kwamba baada ya kutumia kinywaji hicho nguvu zake za kiume ziliongezeka kwa muda mrefu mbali na kiwango cha mipigo ya moyo pamoja na kutokwa na jasho kusiko kwa kawaida.

Kufuatia malalamishi hayo mamlaka ilichukua sampuli ya bidhaa hiyo na kuichunguza.

Kwa mujibu wa gazeti hilo matokeo yake yalionyesha kuwa bidhaa hiyo ya Slidenafil Citrate iliwekwa katika kinywaji hicho kulingana na barua hiyo .

Slidenafil , inayouzwa kwa jina maarufu kama Viagra ni dawa inayotumika kutibu matatizo ya nguvu za kiume pamoja na tatizo la shinikizo la damu. Hutumika kwa kula ama kudungwa moja kwa moja katika mishipa ya damu

Kwa mujibu wa gazeti la The Sunday Monitor kisa hicho kinajiri wakati ambapo mamlaka ya NDA inayosimamia dawa nchini Uganda mwezi uliopita ilionya kwamba dawa ya Viagra ilipatikana imechanganywa katika dawa za miti shamba.

Vyombo vya habari vilinukuu mamlaka ya NDA ikisema kwamba asilimia 55.08 ya dawa za mitishamba pamoja na dawa za vyakula tofauti zimechanganywa na Sldenafil pamoja na dawa nyengine hatari.

Swala hilo liliwasilishwa kwa shirika la ubora wa bidhaa na mamlaka ya kudhibiti utumizi wa dawa ambao wanasema kuwa walipata sampuli za Natural Power SX ambazo zilikuwa zimetiwa dawa ya Viagra baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa mteja aliyekuwa na wasiwasi.

Chanzo- BBC
Share:

DIWANI WA CHADEMA AVULIWA UANACHAMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Ukonga kimemvua uanachama diwani wa viti maalum manispaa ya Ilala, Dorcus Lukiko kwa madai ya kukihujumu chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Januari 6, 2018 mwenyekiti wa Chadema jimbo la Ukonga, Omary Sweya amesema Lukiko amevunja kanuni na katiba ya chama kwa kutoshiriki vikao mbalimbali vya chama na kutosimamia sera zake kama katiba inavyoelekeza.

Amesema Lukiko ambaye pia mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Guluka Kwalala, amedhihirika kukihujumu chama hicho wakati wa uchaguzi mdogo katika jimbo hilo, uliofanyika Septemba 16, 2018.

"Ameonekana pia baada ya uchaguzi mdogo akimzungusha maeneo mbalimbali aliyekuwa mgombea wa CCM kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushindi alioupata bila kujali hujuma alizopata mgombea wetu na chama kwa ujumla," amesema Sweya.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa Lukiko amekuwa akiwadhalilisha na kuwatuhumu viongozi wa chama bila kufuata taratibu na kanuni za chama kama zinavyoelekeza.

Amesema alitumiwa barua ya kuitwa mbele ya kamati tendaji ya jimbo lakini kwa dharau alitupa barua hiyo na kutoa maneno ya kejeli kwa viongozi na chama kwa ujumla.

"Kwa niaba ya kamati tendaji ya jimbo iliyoketi kikao Januari 5, napenda kuwataarifu kwamba kuanzia sasa ninapozungumza, Dorcus Lukiko si mwanachama wa Chadema. Tunatoa tahadhari kuwa kazi zozote zitakazofanywa na yeye, Chadema isihusishwe kwa namna yoyote ile," amesema.
Share:

MGONJWA MAHUTUTI KWA MIAKA 10 AJIFUNGUA MTOTO....HAJULIKANI ALIYEMPA MIMBA HOSPITALINI

Maafisa wa polisi mjini Arizona nchini Marekani wameanzisha uchunguzi wa unyanyasaji wa kingono baada ya kupokea ripoti kuhusu mgonjwa aliyekuwa katika koma kwa muongo mmoja kujifungua.



Mwanamke huyo ni mgonjwa katika kliniki moja inayosimamiwa na shirika la afya la Hacienda , karibu na mji wa Phoenix.

Klinki hiyo ya Hacienda haijatoa maelezo kuhusu tukio hilo lakini ikasema kuwa inaelewa kisa hicho.

Chombo kimoja cha habari kiliripoti kwamba mtoto aliyezaliwa yuko katika afya nzuri na kunukuu vyanzo vikisema kuwa wafanyikazi wa kliniki hiyo hawakujua kwamba mwanamke huyo alikuwa mjamzito.

Mgonjwa huyo bado hajatambulika.

Msemaji wa kituo cha polisi cha Phoenix alisema kuwa kuwa kisa hicho kwa sasa kinafanyiwa uchunguzi, lakini hakusema ni lini uchunguzi huo ulianzishwa ama hata kutoa maelezo ya kesi hiyo.

Mwanamke huyo iliripotiwa kwamba amejifungua mnamo mwezi Disemba 29. Kulingana na duru ambayo haikutajwa: hakuna aliyejua kwamba mwanamke huyo alikuwa mjamzito hadi alipoanza kuonyesha dalili za kutaka kujifungua.

Duru hizo pia zilisema kuwa mwanamke huyo alihitaji kuangaliwa kwa saa 24 na kwamba watu wengi wamekuwa wakiingia na kutoka katika chumba chake.

Mikakati ya kiusalama.

Itifaki katika hospitali hiyo imebadilika kilisema chanzo kingine na sasa wanaume wanaoingia katika vyumba vilivyo na wanawake ni sharti waandamane na wafanyakazi wanawake.

Katika taarifa, kliniki ya Hacienda ilisema '' hivi majuzi tuliarifiwa kuhusu kisa kibaya kinachohusisha afya na usalama wa ndani.

Imesema kuwa inashirikiana vizuri na maafisa wa polisi. David Leibowitz, ambaye ni msemaji wa Hacienda, aliongezea kwamba shirika hilo lilikuwa likitumia kila njia kubaini ukweli.

Idara ya afya katika jimbo la Arizona imesema kuwa imetuma wakaguzi kuwachunguza wagonjwa katika hospitali hiyo kwa lengo la kuweka sheria kali za kiusalama.

Katika tovuti yake, Kliniki ya Hacienda inasema kuwa inawaangalia vizuri wagonjwa wenye magonjwa sugu, wagonjwa vijana , watoto wachanga pamoja na wale walio na ulemavu.
Chanzo - BBC
Share:

LUGOLA AMPA WIKI MBILI KAMISHINA UHAMIAJI NCHINI KUWAONDOA WAHAMIAJI HARAMU MIKOA YA KAGERA NA KIGOMA KABLA YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Na Mwandishi wetu-Karagwe Kagera. WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amempa wiki mbili Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt Anna Makakara, awe amefika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu. Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Karagwe katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Changarawe mjini humo, Lugola alisema kuna idadi kubwa ya wahamiaji haramu katika…

Source

Share:

KOCHA MBELGIJI WA SIMBA AMEPANIA AISEE ,AZIPANGA BUNDUKI HIZI HATARI KWENYE MECHI YA KMKM.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ameamua kupanga kikosi Full Masinondo katika mechi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM, ikielezwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Saoura ya Algeria. Mashabiki wengi walishangazwa baada ya kikosi cha Simba kuonekana kikiwa sawa na kile ambacho Simba hukitumia kwenye Ligi Kuu Bara. Sehemu ya benchi la ufundi la Simba limeeleza: “Kocha ameamua kufanya match fitness. Kutaka wachezaji wawe fiti zaidi. Baada ya mechi hiyo wataendelea na mazoezi. “Lengo ni kujiandaa na Waalgeria halafu pia…

Source

Share:

CCM YAWAONYA WALIOTEULIWA NA RAIS MAGUFULI KUANZA KUTAFUTA UBUNGE KABLA YA WAKATI


Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi katika Mji mdogo wa Lamadi, mara baada ya kuwasili Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoaniSimiyu Januari 05, 2019

Na Stella Kalinga, Simiyu

Katibu Mkuu wa Chama cha Mpinduzi (CCM) Taifa Dkt. Bashiru Ally amewaonya baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, ambao wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo kabla ya wakati wa Chama hicho kutangaza mchakato wa kutafuta wagombea wapya wa ubunge na udiwani.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo Januari 05, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM pamoja na Viongozi na watendaji wa Serikali katika wilaya ya Bariadi na Itilima wakati akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu.

Dk Bashiru amesema ikiwa viongozi hao wataendelea kufanya hivyo atawataja hadharani na akasisitiza kuwa ni vema wakaridhika na nafasi walizopewa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwani kushindwa kufanya hivyo ni kumdharau aliyewateua.

“Wapo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, Makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo, CCM hatujatangaza mchakato wa kutafuta wabunge au madiwani wapya, uko wakati nitawatangaza hadharani, mridhike na nafasi zenu mlizopewa na Mhe. Rais”, alisema

Katika hatua nyingine Dkt. Bashiru amesema kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu 2019 Viongozi wa CCM wajipange katika kuhakikisha viongozi wa Vijiji na Mitaa wanachaguliwa katika misingi ya demokrasia kwa kuzingatia sifa zao na si fedha zao(rushwa).

“ Katika mwaka huu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere baada ya miaka 20 tunataka kufanya mchakato wa kusimamia uchaguzi uwe tofauti, wakati wa kuteua tuzingatie sifa na tuwapime viongozi kwa maisha yao na vitendo vyao......”, alisema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 26 katika kipindi cha miaka mitatu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga, ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo amebainisha kuwa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) barabara katika jimbo hilo zimetengenezwa zinapitika na zipo ambazo zinaendelea kufanyiwa matengenezo.

Naye Katibu wa CCM Mkoa, Bw. Donald Magesa akitoa taarifa ya Chama, utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani humo umefanyika vizuri huku akisisitiza kuwa Viongozi wa Chama na Serikali wamejipanga kwa kushirikiana na wananchi kukamilisha maboma yaliyojengwa ili kila mwanafunzi aliyefaulu darasa la saba mwaka 2018 aweze kuanza kidato cha kwanza.

Share:

KATIBU MKUU WA CCM ASHAURI WAKUU WA MIKOA KUJIFUNZA SIMIYU


Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally amewashauri Wakuu wa Mikoa hapa nchini kwenda(kuja) mkoa wa Simiyu kujifunza namna ya kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kati ya Chama na Serikali sambamba na ubunifu na uchapakazi wa viongozi wa mkoa huo.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo Januari 05, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM pamoja na Viongozi na watendaji wa Serikali, Mjini Bariadi wakati akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu.

Dkt. Bashiru amewapongeza Viongozi wa Serikali wakingozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa namna wanavyoshirikiana na viongozi wa Chama kwa namna wanavyosimamia shughuli za maendeleo.

“Niwapongeze kwa namna mnavyosimamia shughuli za maendeleo, nilikuwa hapa mwaka 2005 kama msimamizi wa uchaguzi nilizunguka maeneo mengi mengine yalikuwa hayapitiki, leo nimekuja nikazungushwa maeneo machache tu, nimeona mambo mengi sana ya tofauti kwa hiyo uongozi wa mkoa huu kwa Chama na Serikali umefanya kazi kubwa na bado mna nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa zaidi”, alisema.

Aidha, amesema ili uchumi uwe imara, wa kisasa na wenye manufaa ni lazima uwe jumuishi na uwalenge watu walio wengi ambao ni wazalishaji wadogo hususani katika katika sekta ya kilimo na viwanda huku akisisitiza umakini zaidi ili uwepo wa viwanda na maendeleo ya kilimo viwanufaishe wengi.

Ameongeza kuwa wakati Mkoa wa Simiyu unapanga mipango mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi ni vema kukawa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, ili kuondoa migogoro kwa watumiaji ambayo inakuwa chanzo cha chuki na watu kuishi kwa wasiwasi.

Katika hatua nyingine Dkt. Bashiru amesema CCM imejipanga kuhakikisha kuwa itasimamia na kuimarisha ushirika ambao utasimamiwa na wataalam wenye taaluma na maadili ili uweze kuwanufaisha wanaushirika na kutatua changamoto zao.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa Viongozi na watendaji wa Serikali Mkoani humo watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM huku akisisitiza kuwa fedha zote zinazoletwa katika mkoa wa Simiyu zitasimamiwa vizuri na zitafanya kazi iliyokusudiwa.

Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu unafanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF) ili kubaini fursa za kiuchumi zilizopo katika katika kila kijiji kwa Vijiji vyote 470, ambapo utekelezaji wa Falsafa ya Kijiji Kimoja Bidhaa Moja(OVOP) unatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi Februari.

Ameongeza kuwa viwanda vikubwa vitatu vyenye uwezo wa kuajiri takribani wafanyakazi 2000 kikiwepo kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio (Maswa) kiwanda cha bidhaa 18 za afya zitokanazo na pamba(Bariadi) vitajengwa mwaka huu 2019 Simiyu.

“Ndugu Katibu Mkuu mwaka jana wakati Mhe. Rais anapokea ndege ya Air Bus alicheza muziki na ukiangalia ilikuwa ni kitu kinachotoka moyoni kuonesha furaha yake, ninaamini mwaka 2019 Mhe. Rais ataucheza muziki huo hapa Simiyu”, alisema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Simiyu amesisitiza viongozi na wanachama kuimarisha uhusiano mzuri, kusaidiana na kupendana katika maisha ya siasa huku akiwasihi viongozi kulinda na kuheshimu dhamana walizopewa kwa kutimiza wajibu wao.

Akitoa salamu kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Bariadi,Mhe. Andrew Chenge ametoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM mkoani Simiyu kudumisha upendo, umoja na mshikamano hususani katika kipindi cha kueleka uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Share:

MAHAKAMA YABARIKI WANAWAKE WAPEWE TALAKA KWA NJIA YA SIMU

Sheria mpya nchini Saudia inawalinda wanawake kutopewa talaka bila kujua. Kuanzia siku ya Jumapili , mahakama zitatakiwa kuwaelezea wanawake kupitia njia ya ujumbe wa simu kwamba wamepewa talaka.

Mawakili wanawake wanapendekeza kuwa hatua hiyo itamaliza kile kinachotajwa kuwa talaka za siri - ambapo wanaume hutoa talaka bila kuwaelezea wake zao.

Amri hiyo itahakikisha kuwa wanawake wanajua hali ya ndoa yao na itawalinda dhidi ya masurufu.

Mwaka uliopita marufuku ya wanawake kuendesha magari iliondolewa na mahakama nchini Saudia.

Hatahivyo wanawake bado wako chini ya usimamizi wa wanaume.

''Sheria hiyo mpya itahakikisha kuwa wanawake wanapewa haki zao za masurufu wakati wanapopewa talaka'', alisema wakili Nisreen al-Ghamdi.

Pia ina hakikisha kuwa uwezo wowote utakaotolewa na mahakama hautumiki vibaya.

''Wanawake wengi wamewasilisha malalamisihi yao katika mahakama za rufaa kwa kupewa talaka bila ya wao kujua'' , kulingana na wakili Samia al-Hindi.

Hatua hiyo mpya inasemaekana kuwa miongoni mwa mabadilikio ya kiuchumi na kijamii yalioshinikizwa na mwanamfalme Mohammed bin Salman, ikiwemo kuwaruhusu wanawake kuingia uwanjani na kutazama mechi za kandanada mbali na kufanya kazi ambazo awali zimekuwa zikifanywa na wanaume pekee.

Ni mambo gani ambayo wanawake wa Saudia hawawezi kufanya?

Kuna vitu vingi ambavyo wanawake wa Saudia bado hawaruhusiwi kufanya bila ya kuomba ruhusa kutoka kwa wasimamizi wao wa kiume kama vile waume zao , baba zao ndugu wa kiume ama watoto wao.

Vitu hivyo ni:
  • Kuwasilisha maombi ya pasipoti.
  • Kusafiri katika mataifa ye kigeni.
  • Kuolewa
  • Kufungua akaunti ya benki.
  • Kuanzisha biashara
  • Kuondoka jela
Hali hiyo ya kusimamiwa na wanaume imesababisha taifa hilo kuwa miongoni mwa mataifa ambayo usawa wa kijinsia umekandamizwa mashariki ya kati.

Chanzo- BBC
Share:

TAASISI YA PROJECT ISPIRE YAENDELEA KUWAINUA WANAFUNZI KUPENDA MASOMO YA SAYANSI.

  Na, Karoli Vinsent. Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Taasisi ya Project Inspire imehaidi kuwainua wanafunzi Katika somo la teknolojia ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili. Akizungumza mwishoni mwa wiki kwa niaba ya barozi wa Uingereza Marc Thayre ambani ni Mkuu wa Masuala ya siasa, Habari na mambo ya ndani alisema wamehamua kuwainua vijana kwa sababu ndiyo nguvu kazi ya baadae. Alisema wapo kwa ajili ya kuwainua vijana kupitia mawazo yao mpya ya teknolojia ambayo ambayo yataweza kuleta maendeleo Katika jamii. “Tupo kwa ajira ya kuwainua vijana kupitia teknolojia…

Source

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger