Wednesday, 25 January 2017
NACTE:ORODHA YA VYUO VILIVYO RUHUSIWA KUDAHIRI WANAFUNZI KWA KIPINDI CHA MARCH / APRIL, 2017 KWA MWAKA WA MASOMO 2016 / 2017
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI
(NACTE)
ORODHA YA VYUO VILIVYO RUHUSIWA KUDAHILI WANAFUNZI KWA
KIPINDI CHA MARCH/APRIL, 2017 KWA MWAKA WA
MASOMO 2016/2017
NACTE YAANZA KUPOKEA MAOMBI YA WANAFUNZI WANAOTAKA KUJIUNGA NA VYUO VYA AFYA,UALIMU,MIFUGO,KILIMO ETC NGAZI YA CHETI NA DIPLOMA MWAKA WA MASOMO 2016/2017 -MARCH /APRIL INTAKE
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI
(NACTE)
TAARIFA KWA UMMA
KUFUNGULIWA KWA MFUMO WA PAMOJA WA UDAHILI KWA KIPINDI CHA MACHI/APRILI, 2017 KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017
Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), linapenda kuutangazia Umma na wadau
wote wa Elimu nchini, kuwa mfumo wa Udahili wa pamoja yaani “Online Central Admission System (CAS)”, umefunguliwa rasmi tarehe 23 Januari, 2017, saa 6 mchana, kwa kupokea maombi ya mwombaji katika kozi mbalimbali, ikiwemo ngazi ya, Astashahada na Stashahada kwa Kipindi cha Machi/April, 2017 kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
Maombi
yote yafanyike kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS) au kupitia
chuoni ambapo mwombaji anapendelea kwenda kusoma, ambapo chuo
kitamdahili mwanafunzi husika kwenye mfumo wa udahili kupitia “Institutional Panel”.
Mwombaji wa Astashahada na Stashahada anaweza kuomba kwa ajili ya eneo moja au zaidi katika maeneo ya taaluma yafuatayo:
- Biashara, Utalii na Mipango, mfano; Uhasibu, Meneja Rasilimali Watu, Wanyama Pori, Mipango.
- Sayansi na Teknolojia Shirikishi, mfano; Kilimo, Uhandisi, Mifumo ya Mawasiliano, Usanifu Majengo, Mifugo.
- Afya na Sayansi Shirikishi, mfano; Uganga, Maabara, Ufamasia, Uuguzi.
- Awe amehitimu kidato cha nne mwaka 2015 au kabla ya hapo.
- Awe na Astashahada ya mwaka 2016 au kabla ya hapo kwa wanaojiendeleza.
- Sifa kwa kozi mahsusi ziko kwenye mwongozo wa kozi (Guidebook) ulioko kwenye mfumo (CAS).
- Kwa eneo la Afya na Sayansi Shirikishi ada ya maombi ni Tshs 30,000/=.
- Kwa eneo moja kati ya maeneo mengine yaliyobaki, ada ni Tshs 20,000/=.
- Kwa zaidi ya eneo moja la taaluma, mfano; Afya pamoja na Biashara, ada ni Tshs 30,000/=, ambapo muombaji anaruhusiwa kuchagua maeneo yote.
Muhimu: Hakutakuwa na muda wa nyongeza wa kufanya maombi. Hivyo waombaji wanashauriwa kuwa makini wakati wa kufanya maombi yao.
Angalizo: Kwa eneo la Mafunzo ya Ualimu na kozi ya Muhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Community Health Workers) hayatakuwepo kwenye udahili wa awamu hii.
Imetolewa na:
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
23 Januari, 2017
Tuesday, 24 January 2017
WANASIASA WANAOENEZA TAARIFA ZA UONGO KUHUSU NJAA KUKAMATWA
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameonya kuwa watu
wakiwemo wanasiasa wanaoeneza taarifa za uongo za kuwepo kwa baa la
njaa, ni kosa na wachukuliwe hatua ikiwemo kukamatwa.
Masauni
amesema bado kuna watu wanajichukulia mamlaka ambayo sio yao na kueneza
uongo kuwa kuna njaa nchini, hilo ni kosa kwa kuwa kwa kueneza
propaganda hiyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
“Hizo
ni propaganda za watu wasioitakia mema nchi hii ….. mtu anapofanya kosa
lazima achukuliwe hatua …… Jeshi la Polisi liangalieni hili,” alisisitiza.
Masauni
alitoa onyo hilo wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya jana
mkoani Rukwa ambako Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven alimhakikishia
kuwa mkoa huo hauna njaa, bali una ziada ya kutosha.
“Nyie
wenyewe mmemsikia mkuu wa mkoa (Zelothe) amethibitisha kuwa hakuna njaa
mkoani hapa lakini sio hapa tu, pia mikoa ya Mbeya na Songwe
wamenithibitishia kuwa hawana njaa,” alisema Naibu Waziri Masauni na kuongeza:
“Sasa
wapo wanasiasa uchwara wanaeneza propaganda kuna njaa, sio mamlaka yao
kutangaza kuwa kuna njaa, kueneza uongo kama huo ni si sawa kwa kuwa
kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini, wanastahili kuchukuliwa
hatua ikiwemo kukamatwa,” alisisitiza.
Awali
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe alimweleza Naibu Waziri Masauni kuwa
hali ya kiusalama katika mkoa huo ni shwari ambapo amani na utulivu
umeshamiri kwa kuwa una chakula cha kutosha.
WALIMU WATATU WAKAMATWA KWA KUPIGA DILI LA KUPOKEA MISHAHARA PRIVATE NA SERKALINI
Walimu
watatu mkoani Mwanza wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la
kukimbia vituo vyao vya kazi na kufanya kazi shule binafsi huku
wakiendelea kupokea mishahara ya serikali
Taarifa
ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imewataja walimu hao waliokamatwa
jana asubuhi katika mtaa wa Buhongwa wilaya ya Nyamagana jijini
Mwanza,kuwa ni pamoja na Richard Mgendi (30), Rwiza Ntare (27) na
Gilbert Makwaya (33).
Walimu hao kila mmoja ana story yake kama ifuatavyo:-
Mwalimu Richard Mgendi
alikuwa akifundisha shule ya sekondari ya Misasi wilayani Misungwi,
mwaka 2012 alimuaga mkurugenzi wa wilaya hiyo kuwa anakwenda kusoma
Masters ya lugha (Linguistic) katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino,
kwa kipindi chote hicho inadaiwa mwalimu huyo alikwenda kusoma na
alipomaliza hakurudi katika shule yake ya awali bali alikuwa akifundisha
shule binafsi ya sekondari iitwayo Musabe iliyopo Buhongwa huku
akiendelea kulipwa mshahara kutoka serikalini.
Mwalimu Rwiza Ntare
alikuwa akifundisha shule ya sekondari iitwayo Kigongo sekondari
iliyopo wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo mwaka 2015, alimuaga
mkurugenzi wake kuwa anakwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kupatiwa
matibabu ya macho na vidonda vya tumbo lakini hakurudi tena bali
inadaiwa alikuwa akifundisha shule binafsi ya sekondari iitwayo Musabe
iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kulipwa mshahara na serikali.
Mwalimu Gilbert Makwaya
alikuwa akifundisha Runima sekondari iliyopo maeneo ya Buhongwa na
alimuaga mkurugenzi wa wilaya ya Nyamagana tarehe 27/09/2015 kuwa
anakwenda kusoma Masters ya Hesabu katika chuo kikuu cha Mwenge kilichpo
mjini Moshi lakini hakwenda bali alikuwa akifundisha shule binafsi ya
Musabe iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kupokea mshahara kutoka
serikalini.
Walimu wote watatu wapo katika mahojiano na jeshi la polisi na pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Jeshi
la polisi linaendelea kuwatafuta baadhi ya walimu ambao wametoroka
lakini inadaiwa wapo katika shule hiyo binafsi ya Musabe huku
wakiendelea kulipwa mshahara na serikali pamoja na mkurugenzi wa shule
hiyo.
MAJAMBAZI WAWILI 2 WAUAWA JIJINI MWANZA
Watu
wawili waliokuwa wakituhumiwa kwa ujambazi wameuawa wakati wakitaka
kujaribu kuwatoroka askari polisi wilayani Ilemela mkoani Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza amesema kwamba tukio hilo lilitokea
tarehe 20.01.2016 majira ya saa 2:30 usiku, katika mtaa wa kiloleli
“A” kata ya Nyasaka mkoa wa Mwanza na kuwataja majambazi waliouawa kuwa
ni Eric Magese miaka 22, na aliyejulikana kwa jina moja la Peter miaka
kati 25 hadi 27 wote wakazi wa Mecco jijini Mwanza.
Amesema
majambazi hao waliuawa wakati wakijaribu kutoroka askari polisi pindi
wakiwapeleka mahali ambapo wenzao wamejificha ili waweze kufanya
uvamizi.
Amesema
kuwa katika tukio hilo pia ilipatikana silaha moja aina ya short gun
yenye namba TZ CAR 103283 ikiwa na risasi tatu ambayo inadaiwa walipora
kwenye kampuni ya ulinzi iitwayo Malika Security Service Limited
Msangi
amesema majambazi hao walikuwa wakitafutwa na polisi baada ya kufanya
unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza
ilikiwemo tukio la Kitangiri mnamo tarehe 19.12.2016 na tukio la tarehe
02.01.2016 katika mtaa wa Nyasaka.
Jinsi walivyouawa
Msangi
amesema baada ya upelelezi uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao,
walikubali kuwapeleka askari katika eneo ambalo walikuwa wamepanga
pamoja na wenzao wawili kwa ajili ya kufanya matukio zaidi ya ujambazi.
Amesema
walipofika katika eneo hilo, watuhumiwa hao walipiga kelele kama ishara
ya kuwatorosha wenzao na kuanza kuwakimbia askari.
Askari
walifyatua risasi kadhaa hewani wakiwaamuru wasimame lakini waligoma
ndipo waliwafyatulia risasi za mguuni kwa bahati mbaya ziliwalenga
maeneo ya juu ambapo walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali.
Monday, 23 January 2017
Bibi Akutwa amekufa Huku akiwa na vibuyu 5 na kuku mweupe
Bibi
mwenye umri wa miaka 60 amekutwa amekufa mkoani Tabora huku amevaa nguo
nyeusi aina ya kaniki, akiwa na vibuyu vitano na kuku mweupe, katika
mazingira yanayoashiria kushiriki vitendo vya kishirikina.
Aidha, mwili wa mtu mwingine umekutwa pembeni ya mti aliokuwa akichimba dawa.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,
Hamis Selemani iliwataja waliokutwa wamekufa kuwa ni Nsoma Dotto (60)
mkazi wa Kijiji cha Zugimlole Wilaya ya Kaliua na Mayara Marashi (50)
ambaye ni mkazi wa Igunga.
Kamanda Selemani alisema Nsoma alikutwa akiwa amekufa umbali wa mita 200 kutoka nyumbani kwake juzi.
Alisema
bibi huyo alikutwa amevaa nguo nyeusi aina ya kaniki akiwa na vibuyu
vitano huku pembeni yake kukiwa na kuku mweupe. Uchunguzi wa awali wa
jeshi hilo, unaonesha kuwa huenda ni imani za kishirikina.
Aidha,
alisema Marashi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mwakapinga, Kata ya
Nanga, aliyekuwa mganga wa kienyeji, mwili wake uliokotwa Januari 16,
mwaka huu ukiwa umeanza kuharibika.
Kwa
mujibu wa Kamanda Selemani, mganga huyo wa kienyeji aliondoka nyumbani
kwake Januari 8, mwaka huu kwenda porini kuchimba dawa, lakini hakurudi
kijijini hadi maiti yake ilipookotwa akiwa amekufa.
Alisema
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho. Aliwaomba wananchi
wanaoenda porini kwa ajili ya shughuli zozote zile, wawe wanatoa taarifa
kwa ndugu zao ili iwe rahisi tatizo linapotokea.
Rais wa Uturuki Awasili Nchini Kwa Ziara ya Kikazi
RAIS
wa Uturuki Mheshimiwa Recep Erdogan amewasili nchini jana jioni
(Jumapili, Januari 22, 2017) kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na
kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na niaba ya Mheshimiwa Rais. Dkt. John
Magufuli.
Rais
huyo ameambatana na mkewe Mama Emine Erdogan pamoja na Mawaziri watatu
ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa
Uchumi Mheshimiwa Nihat Zeybekekci na Waziri wa Nishati na Maliasili
Mheshimiwa Berat Albayrak
Pia Rais huyo ameambatana na wafanyabiashara wapatao 85 wa nchi hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip
Erdogan aliyefuatana na mkewe, Mheshimiwa Emine Erdogan (kulia)
wakifuhia ngoma kwenye uwanja wa ndege wa Julius Kambarage jijini Dar es
salaam baada ya Rais huyo kuwasili kwa ziara rasmi nchini Januari 22,
2017. Mheshimiwa Majaliwa alimpokea Rais huyo kwa niaba ya Rais John
Magufuli. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).