Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe
19 Desemba, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi 3
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,
amefanya uteuzi wa Wenyeviti 7 wa Bodi za Taasisi za Serikali, na pia
ameteua Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania na
Mjumbe mmoja wa Baraza la Taifa la Biashara.
Taarifa iliyotolewa
leo tarehe 19 Desemba, 2016 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi
imewataja walioteuliwa kama ifuatavyo;
1. Rais Magufuli amemteua
Bw. Ali Mufuruki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa
wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira.
Ali Mufuruki ni Afisa Mtendaji
Mkuu wa Kampuni za Infotech Investment na Mwenyekiti wa Taasisi ya
Afrika inayojihusisha na uendelezaji wa vipaji vya uongozi katika ukanda
wa Afrika Mashariki.
2. Rais Magufuli amemteua Mhandisi
Christopher Kajolo Chiza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade)
Mhandisi Christopher Kajolo Chiza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Sabetha Mwambenja ambaye amemaliza muda wake.
3. Rais Magufuli amemteua Bw. Peter M. Maduki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
Peter M. Maduki anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Idrissa Mshoro ambaye amemaliza muda wake.
4. Rais Magufuli amemteua Dkt. Yamungu Kayandabila kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Dkt.
Yamungu Kayandabila ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Peter
Ilomo ambaye amemaliza muda wake.
5. Rais Magufuli amemteua Prof. Godwin Daniel Mjema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Fedha na Mikopo (UTT-MFI)
Prof.
Godwin Daniel Mjema ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Fadhili D. Mbaga ambaye
amemaliza muda wake.
6. Rais Magufuli amemteua Kepteni Ernest Mihayo Bupamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Bahari (DMI)
Kepteni Ernest Mihayo Bupamba ni Mwendesha Meli Mkuu (Principal Captain) Katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
7.
Rais Magufuli amemteua Dkt. Aloyce S. Hepelwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi
ya Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID)
Dkt. Aloyce S. Hepewa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. John Jingu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Tanzania.
Dkt. John Jingu ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Halikadhalika, Rais Magufuli amemteua Dkt. Rashid Adam Tamatama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI).
Dkt. Rashid Adam Tamatama ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia, Rais Magufuli amemteua Bibi. Zuhura Muro kuwa Mjumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Council – TNBC).
Bibi. Zuhura Muro ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojihusisha na huduma za ushauri wa ubora na mafunzo (Service Limited) katika ofisi zake za Dar es Salaam.
Wateule wote waliotajwa hapo juu, uteuzi wao umeanza tarehe 17 Desemba, 2016
Mwanamuziki Darasa amepata ajali maeneo ya Ntobo barabara yakuelekea
mgodi wa Bullyanhulu wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga. Waliokuwa
garini wote wamenusurika.
Katika gari hiyo pamoja na watu wengine alikuwa na mtayarishaji wa video aliye kwenye chart Hanscana.
WAKUU wa Wilaya (Ma-DC) na Wakurugenzi nchini, ambao hawajakamilisha
kutengeneza madawati, yanayokidhi idadi ya wanafunzi katika shule za
maeneo yao, wamepewa siku 14 kukamilisha kazi hiyo. Imeelezwa kuwa wanafunzi watakapofungua shule, lazima wakae kwenye madawati hayo. Wakuu wa wilaya na wakurugenzi, watakaoshindwa kutimiza agizo hilo
hadi ifikapo Desemba 30, mwaka huu, watakuwa wamejifukuzisha kazi
wenyewe. Aidha, wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kwenda
kidato kwanza mwakani, wanaanza masomo yao kwa awamu moja, badala ya
awamu mbili tofauti. Agizo hilo lilitolewa jijini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Arumeru katika
ziara yake ya kikazi mkoani hapa. Aliagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote nchini kuwa hadi Desemba
30, mwaka huu wilaya zote zenye upungufu wa madawati ziwe
zimekamilisha. “Wale ambao watashindwa kufanya hivyo, watakuwa wamejifukuzisha kazi
wenyewe” alisema. Akizungumzia ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo,
Majaliwa alisema kuwa hadi Desemba 30, mwaka huu, wawe wamefikia
asilimia 50, tofauti na hali ya sasa ambapo wamekusanya asimilia 30 tu.
“Ongezeni kasi ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zenu na
mhakikishe kila mtu anafanya kazi zake kwa kumheshimu mwenzie,” alisema
Waziri Mkuu. Serikali inahitaji haraka madawati ili kuondoa uhaba unaozikabili
shule za sekondari na msingi wa madawati. Hali halisi ikoje? Hadi sasa,
zaidi ya madawati milioni moja, sawa na asilimia 88 ya madawati
yanayohitajika katika shule za msingi na asilimia 95 kwa shule za
sekondari, yamepatikana. Kwa shule za msingi, imebaki asilimia asilimia
12 kumaliza tatizo la madawati, huku shule za sekondari imebaki asilimia
5. Mikoa sita ambayo ina hali mbaya na haijatekeleza kikamilifu agizo
hilo la madawati ni Mwanza, Kigoma, Mara, Rukwa, Simiyu, Dodoma na
Geita, ambapo Geita inadaiwa madawati zaidi ya 80,000 ya shule za msingi
na sekondari. Mwanza inadaiwa madawati 41, 438, Kigoma madawati 31,171, Mara
madawati 16,978, Dodoma madawati 14,873, Rukwa madawati 10,978 pamoja na
Mkoa wa Simiyu. Mkoa wa Mwanza unaundwa na wilaya za Nyamagana, Ilemela, Misungwi,
Kwimba, Ukerewe, Magu na Sengerema, wakati wilaya za mkoa wa Kigoma ni
Buhigwe, Uvinza, Kakonko, Kasulu, Kibondo na Kigoma. Wilaya za mkoa wa Mara ni Tarime, Bunda, Butiama, Musoma, Serengeti
na Rorya na Mkoa wa Rukwa una wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi. Mkoa wa Simiyu wilaya zake ni Bariadi, Maswa, Busega, Meatu, Itilima
na Mkoa wa Dodoma wilaya zake ni Kondoa, Bahi, Mpwapwa, Kongwa, Dodoma,
Chamwino na Chemba, wakati mkoa wa Geita wilaya zake ni Geita, Chato,
Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale. Mikoa ambayo imemaliza tatizo hilo la madawati kwenye shule za msingi
na sekondari ni 14 ambayo ni Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Arusha,
Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Manyara, Pwani, Shinyanga,
Singida na Tabora. Mikoa mingine iliyosalia, imebakiza idadi ndogo ya madawati ambayo inakaribia kukamilika. Tanzania Bara ina mikoa 26.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku watu binafsi wenye
uwezo kifedha kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na kuwanyanyasa
wananchi kwa kuwapiga mabomu wanachi wasio na silaha. Ameagiza nguvu hizo wazitumie kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi. Aidha amewaambia wananchi wa Kata ya Bwawani Kitongoji cha Omapinu
kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
atafika kijijini hapo wiki ijayo, kuzungumza nao namna ya kutatua
mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation na wananchi hao. Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo baada ya kusimamishwa na wananchi
wa kitongoji hicho, wakati alipokuwa akiendelea na ziara yake mkoani
hapa jana. “Kuanzia sasa ni marufuku kwa watu binafsi wenye uwezo wa fedha
kutumia Jeshi la Polisi kuwapiga mabomu na kuwanyanyasa wananchi kwa
kuwapiga mabomu wakati hawana silaha. “Polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu
hizo kwenye maeneo ambayo yanahatarisha usalama wa nchi na wananchi na
si vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu. Kuhusu mgogoro wa shamba la Tanzania Plantation, Waziri Mkuu alihoji;
“Ni kwanini polisi wawapige mabomu wananchi wanaozuiwa kulima au
kuchota maji katika eneo hilo la shamba hadi kufikia hatua ya wanawake
kuharibu mimba? “Nyie polisi kwanini mnawapiga mabomu hawa watu, nani
anatoa amri ya kupigwa mabomu wananchi hawa. Nasema kuanzia leo
msiwapige mabomu watu hawa na pia nawasihi nyie wananchi msifanye fujo,
subirini Waziri Lukuvi anakuja wiki ijayo kwa ajili ya kutatua mgogoro
huu wa shamba.” Alisema polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu, pale tu panapotokea jambo
linaloweza kuhatarisha maisha au vurugu, ila si kuwanyanyasa wananchi
wanaodai ardhi yao kwa kuwapiga mabomu. Alisema Lukuvi atafika mkoani humo kwa ajili ya kushughulikia
migogoro ya ardhi, ambayo ipo zaidi wilayani Arumeru, na atakaa muda
mwingi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi. Alisema kuanzia sasa mwekezaji ambaye ana mashamba wilayani humo na
hayaendelezi, mashamba hayo yatachukuliwa na serikali ili kugawanywa kwa
wananchi. Alisema Waziri Lukuvi akiwa wilayani humo pamoja na kushughulikia
migogoro mingine, pia atatatua mgogoro huo baina ya shamba la Tanzania
Plantation na wanachi hao. Awali, Ofisa Ardhi Wilaya ya Arumeru, Rehema Jato alikiri kuwepo kwa
mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa wa Shamba la Tanzana Plantation,
Pradeep Lodhia na wananchi. Alisema kuna kesi mahakamani na wanachosubiri sasa ni uamuzi wa
Mahakama ndipo hatua zingine zichukuliwe. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,
Alexander Mnyeti alisema wilaya hiyo ni moja ya wilaya nchini zenye
migogoro mingi ya ardhi na wakati mwingine watu wanauana.
UCHAGUZI wa kumpata Meya wa Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam, umefanyika na hatimaye Diwani wa Kata ya Pemba Mnazi kutoka
Chama cha Mapinduzi (CCM), Maabadi Hoja amechaguliwa kuwa Meya wa
kwanza. Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, ambaye alikuwa
msimamizi wa uchaguzi, alisema mgombea huyo wa CCM ndiye aliyeshinda. Washiriki wengine walitoka vyama vya CCM, Chama cha Wananchi (CUF) na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mhando alisema Hoja
alipata kura tisa dhidi ya Celestine Maufi (CUF) aliyepata kura tano na
kura moja iliharibika. Pia, Mhando alisema katika uchaguzi huo, Amini Sambo ambaye ni Diwani
wa Kata ya Kibada, pia kutoka CCM, alishinda nafasi ya Naibu Meya,
akipata kura 10 dhidi ya Ernest Mafimbo wa CUF, aliyepata kura tano.
“Tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri Kigamboni, sasa tumepata Meya na
Naibu Meya,” alisema Mhando. Uchaguzi wa Meya na Naibu wake kwa upande wa Kigamboni, umefanywa
baada ya Wilaya ya Temeke kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Temeke na
Kigamboni. Mhando alieleza kuwa uchaguzi huo ambao ni wa mara ya kwanza kwa
halmashauri hiyo, ulifanyika kwa amani bila kuwapo na malalamiko. Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndungulile, baada ya kumalizika kwa
uchaguzi huo, alisema uchaguzi ulifanyika bila tatizo lolote na kwamba
baada ya uchaguzi kuisha, kinachofuata ni kazi. Alisema kwa muda mrefu mambo mengi katika halmashauri hiyo,
yalisimama kwa kukosa Baraza la Madiwani. Akizungumza na gazeti hili,
meya huyo, Hoja alisema anajipanga kuiweka Halmashauri hiyo mpya kimji.
Aliahidi kuanza na kusimamia mipangomiji na miundombinu. “Manispaa yetu ni mpya na haijapangwa, tunataka kuiweka kimji zaidi
na tutaanza na mipangomiji kwani kuna ujenzi holela na pia tutasimamia
miundombinu,” alisema Hoja. Hii si mara ya kwanza kuchaguliwa kushika nafasi hiyo. Alichaguliwa
kuwa Meya wa Manispaa ya Temeke mwaka 2010 baada ya kushinda udiwani wa
kata hiyo kwa mara ya kwanza. Baada ya kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana, Hoja alipata tena
udiwani katika kata hiyo, lakini aliposhindania nafasi ya meya,
hakushinda nafasi hiyo. Lakini, baada ya Temeke kugawanywa kuwa wilaya
mbili za Temeke na Kigamboni, Hoja amegombea tena na kushinda. Kwa upande wake, akihojiwa, Naibu Meya mpya, Sambo, anasema hii ni
mara ya kwanza kushika nafasi ya udiwani. Alichaguliwa mwaka jana. Sambo alisema anaishukuru Serikali kwa kusogeza huduma karibu, kwa kuifanya Kigamboni kujitegemea kama halmashauri. Alisema yeye na viongozi wenzake watashirikiana na serikali, kuifanya
halmashauri hiyo mpya kuwa ya mfano. Halmashauri ya Kigamboni inaundwa
na kata tisa za Pembamnazi, Kimbiji, Somangila, Kisarawe, Kibada,
Vijibweni, Kigamboni, Mjimwema na Tungi.
Tunakaribisha
matangazo ya aina zote.Bei zetu ni nzuri sana na kamwe
hutajuta kutangaza biashara yako kupitia mtandao huu. Kwa Siku tunafunga na Pageviews zaidi ya laki tatu kama graph inavyoonyesha hapo chini