Tuesday, 21 June 2016

Maofisa Utumishi 1,500 Hatarini Kutumbuliwa

SERIKALI imeagiza wote waliotengeneza watumishi hewa wafunguliwe mashitaka mahakamani huku ikionya kuwa iko tayari kusimamisha kazi maofisa utumishi wote nchi nzima wanaofikia 1,500 katika sakata hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo jana alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 bungeni mjini Dodoma. 
Amesema tayari serikali imeshatoa agizo hilo la kuwashitaki maofisa wote waliotengeneza watumishi hewa na ikibidi iko tayari kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 1,500 waliofundishwa kazi hiyo na serikali.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mpaka mwishoni mwa Mei, serikali ilikuwa imebaini uwepo wa watumishi hewa 12, 246 waliokuwa wakitafuna Sh bilioni 25.06 kila mwezi. 
Katika kuelezea athari za ufujaji huo wa fedha za serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema hata katika ulipaji wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais John Magufuli aliagiza uhakiki ufanyike, kabla ya kulipa kwa kuwa penye wafanyakazi hewa, kuna malipo hewa ya wastaafu.

Alitoa mfano wa deni la Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh trilioni 2.67 lakini uhakiki wa deni hilo ulipofanyika, deni hilo likabainika ni Sh trilioni 2.04, hatua iliyosaidia Serikali kuepusha wizi wa karibu Sh bilioni 600 za wastaafu hewa. 
January na uthubutu 
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba alizungumzia ahadi ya Rais ya kutoa Sh milioni 50 kila kijiji na kufafanua kuwa Sh bilioni 59 zilizotengwa, zitatumika kujifunza namna ya kutekeleza ahadi hiyo.

Aliwataka wabunge wa CCM kukumbuka kuwa chama hicho kilipomtangaza Dk Magufuli kuwa ndiye mgombea urais, kilitoa taarifa duniani ya aina ya Serikali, uongozi na mabadiliko wanayotaka Watanzania. 
Alisema mabadiliko ya kweli hayawezi kutokea bila kuwepo kwa hatua kubwa na uthubutu ndio maana serikali imethubutu kuwa na Bajeti ya Sh trilioni 29.5 na uthubutu wa kutenga asilimia 40 ya bajeti hiyo katika maendeleo.

Kwa mujibu wa January, mahali popote kwenye uthubutu, lazima kutakuwa na watu watakaotia shaka na kuwataka wabunge wa CCM wasitilie shaka uwezo wa serikali katika kukusanya Sh trilioni 29.5 zilizokusudiwa. 
Alisema wabunge wa CCM ndio wengi katika Bunge na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezwa ni ya chama hicho, hivyo ni muhimu wamuunge mkono Rais Magufuli kwani akifanikiwa Rais na Tanzania imefanikiwa.

Alikumbusha kuwa maendeleo yanahitaji kujitoa sadaka na viongozi wao wamekubali kujitoa sadaka, hivyo wabunge, wafanyabiashara mpaka wadogo wakiwemo bodaboda, wajitoe sadaka kwa kulipa kodi. 
Alitumia kauli ya Rais John Kennedy wa Marekani aliyoitoa miaka ya mwanzo ya 1960, alipowataka wananchi wa nchi hiyo, kutouliza nchi hiyo itawafanyia nini, bali wajihoji wao wataifanyia nini nchi yao.

Watanzania wanune 
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alieleza namna Serikali ya China ilivyoridhia kutoa Sh trilioni tano nje ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwa sekta binafsi, huku ikiahidi kutoa fedha nyingine Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.

Alihitimisha kwa kusema ujenzi wa uchumi wa viwanda ni sawa na vita na wakati wa vita, hakuna anayecheka hivyo Watanzania wote lazima wanune, ili kutimiza malengo ya kuongeza pato la jumla la taifa. 
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema pato la jumla la Taifa kwa sasa ni Dola za Marekani bilioni 55 na ili Tanzania ifike katika uchumi wa kati, inatakiwa kuongeza uzalishaji utakaoongeza pato la jumla la Taifa kuwa Dola za Marekani bilioni 200.

Alisema injini za kupeleka uzalishaji na uchumi katika kipato hicho, ziko nyingi na mojawapo ni sekta ya nishati ya umeme ambayo katika bajeti hiyo ya serikali, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh trilioni 1.43 ambapo asilimia 94 ya hizo ni za maendeleo na kati ya fedha hizo za maendeleo, asilimia 95 inakwenda kwenye umeme.

Katika kudhihirisha nia ya serikali katika sekta hiyo, Profesa Muhongo alisema katika bajeti inayomaliza muda wake, wizara hiyo imeshapata asilimia 80 ya fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu unaoisha huku Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ikiwa imeshapata asilimia 80 ya fedha iliyotarajia. 
Aliwaeleza wabunge kuwa katika bajeti waliyopitisha, usambazaji wa umeme vijijini umepangiwa Sh bilioni 534.
Share:

Vigogo Kuondolewa kwa Nguvu nyumba za Serikali


VIGOGO wakiwamo wabunge na wananchi wengine, walionunua nyumba za serikali na kutomaliza kulipa madeni yao kwa wakati kama mikataba yao inavyoelekeza, wameanza kuondolewa kwa nguvu kwenye nyumba hizo na nyumba kupigwa mnada ili kupata fedha za kulipa madeni ya Sh bilioni sita.

Madeni hayo serikali inadai kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). 
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart ambayo imepewa kazi ya kukusanya madeni hayo ya TBA kutoka kwa wadaiwa sugu hao, Scholastica Kevela alisema kazi ya kuwaondoa vigogo walionunua nyumba hizo au kupangisha bila kulipa, inaanza leo jijini Dar es Salaam.

Kevela alisema katika kazi hiyo, TBA wamewapa orodha ya zaidi ya nyumba 3,000 nchi mzima za walionunua na wengine kupangisha nyumba za TBA ambao wanadaiwa madeni na muda wa kurejesha ulishapita.

“Tuna orodha za nyumba zaidi ya 3,000 nchi nzima, juzi tulianza Mwanza tumeshikilia nyumba zaidi ya 20, kwa kuwatoa watu nje, na juzi Dodoma tumefanya hivyo, tumeshashikilia nyumba 40 zikiwemo za vigogo, kesho (leo), tunaanza zoezi hilo hapa Dar, hatutakuwa na huruma kwa mdaiwa, wote tulishawapa taarifa za kimaandishi, kazi yetu ni utekelezaji tu,” alisema Kevela.

Alisema wanatekeleza kazi waliyopewa kwa sababu hata Rais John Magufuli anasisitiza wananchi kulipa kodi ili nchi iendelee na kuacha utegemezi, hivyo wadaiwa sugu hao muda wa kulipa na hata muda wa ziada waliopewa kuhakikisha wamemaliza madeni yao nao ulipita na wengi hawakulipa, hivyo Yono inaingia kazini kupiga mnada nyumba hizo.

Alisema walionunua nyumba za serikali na hawajamaliza kulipa madeni wakiwemo wabunge, vigogo na wananchi wengine wanajitambua, hivyo kuanzia leo wanapaswa kuondoka kwani zitauzwa ili kulipa deni la serikali.

Kadhalika alisema waliopanga kwenye nyumba hizo na bado wanadaiwa kodi msako huo unawahusu na kwamba wataondolewa wote na vitu vyao kupigwa mnada ili kupata fedha za kulipa kodi wanayodaiwa na serikali.

“Sisi tunatekeleza agizo kulingana na mkataba wetu na pia tunamsaidia Rais kukusanya kodi, hivyo wote wanaodaiwa wafahamu tutawafuata walipo na kupiga mnada mali zao ili kulipa kodi ya serikali,” alisema Kevela.

Hata hivyo, alisema mchanganuo wa nyumba hizo na majina ya vigogo na wabunge watatoa baadaye baada ya kufanya upembuzi kwa sababu nyumba za wadaiwa ni nyingi. 
Awali akizungumzia madeni ya wakwepa kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), waliokwepa kulipia kontena zaidi ya 320 zilizogunduliwa na Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Yono Kevela alisema wanaendelea kukusanya madeni ya wadaiwa hao.

Alisema Yono imekamata mali za wadaiwa hao na baadhi zimeshapigwa mnada na nyingine zinaendelea kuuzwa ili kupata fedha za kulipa kodi, na hadi sasa takribani Sh bilioni saba zimeshalipwa kati ya Sh bilioni 18 zilizokuwa zinadaiwa.
Share:

CHADEMA Wataka Mkutano Mkuu wa CCM Kumkabidhi Uenyekiti Magufuli Nao Uzuiliwe


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa tamko zito kikitaka Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika mwezi ujao, vinginevyo watatumia nguvu ya umma kuuzuia.

CCM kimeitisha mkutano mkuu maalumu unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mjini Dodoma, kwa lengo la Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kumkabidhi uongozi wa chama, Rais John Magufuli.

Kauli ya kutaka Polisi kuzuia mkutano huo kama inavyofanya kwa vyama vingine vya siasa, ilitolewa juzi mjini Moshi na Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Julius Mwita.

Msimamo huo wa Chadema ambao uliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalim unafuatia Polisi kuzuia mahafali ya wahitimu wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wao.

Akizungumza na wanahabari, Mwita alikwenda mbali na kudai kuwa, Chadema watalifungulia Jeshi la Polisi kesi ya madai ya fidia kwa kuvuruga mahafali ya Chaso mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Ukisoma barua yao wamesema wamezuia mikutano ya hadhara sasa kama wanakuja hadi kwenye vikao vya ndani, hatuwezi kuendelea kukubali jambo hili.Tumetumia busara sana,” alisema Mwita na kuongeza: 

“Msipouzuia Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma Julai 23 tunakuja kuuzuia sisi... yaani muwe tayari kusafiri kwenda Dodoma tukauzuie ule mkutano la sivyo, wauzuie kama walivyouzuia mikutano yetu.” 

Mwita alimgeukia Mwalimu na kumweleza kuwa hiyo ni lugha ya ujana na inatekelezeka, akawahoji vijana wa Chaso waliokuwapo: “Wangapi mko tayari kuja Dodoma?” Wote wakaafiki.

“Intelijensia ya polisi ni ya kiumbea, inayoweza kujua tu Chadema wanakwenda kwenye mkutano, haiwezi kujua watu wamejificha wana bunduki na risasi 300 kwenye mawe kule Mwanza,” alidai.

Mwalimu alisema utaratibu wa Polisi na Serikali lazima ukome na kwamba wao ni viongozi.
Share:

Kesi ya Mauaji ya Mwanahabari, Daud Mwangosi Kuendelea Leo


Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, jana iliahirisha kesi ya mauaji ya mwanahabari, Daud Mwangosi inayomkabili askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Iringa (FFU), Pasificus Simon hadi leo. 
Kesi hiyo iliahirishwa baada ya upande wa Serikali kufunga ushahidi wake. Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Februari 12, mwaka 2012, leo inaendelea kwa upande wa utetezi kuleta mashahidi wake mbele ya Jaji Paul Kihwelo anayeisikiliza.

Katika kesi hiyo ambayo haikuchukua muda mrefu mahakamani hapo jana, mawakili wa Serikali wakiongozwa na Sandy Hyra na Ladislaus Komanya walisema wamefunga ushahidi kwa mashahidi wanne wa awali.

Baada ya wakili wa utetezi, Rwezaura Kaijage kukubaliana na maombi ya upande wa Serikali kufunga ushahidi wao, Jaji Kihwelo aliiahirisha kesi hiyo hadi leo.

Awali, mtuhumiwa Simon alifikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao hawaruhusi apigwe picha na waandishi wa habari.

Mwangosi aliuawa kwa kupigwa bomu Septemba 2, 2012 katika Kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Share:

magazeti ya leo jumanne june tarehe 21.6.2016

Share:

Basi la NBS kutoka Dar - Tabora na Basi la Kisbo, yamepata ajali Mbaya Gairo,Morogoro






Basi la NBS linalotoka DAR kwenda TABORA limepata ajali mbaya maeneo ya Gairo Morogoro. Watu 4 wafariki na 10 kujeruhiwa katika ajali ya basi la NBS.


Huku ajali nyingine ya basi la KISBO likijeruhi watu kadhaa Morogoro. Basi la Kisbo T895CYL Limepata ajali ya kuparuzana na trailer flatbed eneo la Magubike Kilosa.










Share:

Bajeti Kuu Ya Serikali 2016/2017 Yapitishwa Bungeni Kwa Asilimia 100,Serikali Yasema Kodi ya Kiinua Mgongo Itakatwa kwa Watumishi Wote Akiwemo Rais



Serikali ya Tanzania imepitisha bajeti ya shilingi trilion 29.5 kwa kupigiwa kura huku wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika huyo

Katika vikao vya Bunge la 11, wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku 23 sasa kwa madai ya kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa Bunge Dkt.Ackson Tulia.

Wakichangia bajeti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika Bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha katika ofisi ya mkaguzi wa serikali CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na kuachana na mpango wa kuanza kuwakata kodi wabunge katika mafao ya kiinua mgongo ya Wabunge, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema msimamo wa serikali upo pale pale.

Kuhusiana na makato ya kodi kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata kodi hiyo kwa viongozi wote wa kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi nchini.

Baadaye jioni wabunge walipiga kura mmoja mmoja kupitisha bajeti hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo bungeni walipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu "Ndiyo" akimaanisha anaipitisha bajeti hiyo.

Mapema Asubuhi mara baada ya dua, wabunge wa upinzani waliziba midomo yao kwa karatasi na Plasta na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.

Mbunge wa Vunjo Kupitia chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. James Mbatia kwa niaba ya wabunge hao alisema hawataacha kulalamikia ukiukwaji wa sheria unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.
Share:

Majibu Ya Hoja Za Wabunge Yaliyotolewa Leo Bungeni Na Waziri Wa Fedha Na Mipango Dkt. Philip I. Mpango (Mb)






JUNI 20, 2016
DODOMA
A.          UTANGULIZI
1.          Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru  wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8 Juni, 2016.
2.          Mheshimiwa Spika, Kipekee,  ninampongeza sana Mhe. Naibu Spika kwa umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika viwango vyake ni vya kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda, mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri, (nadhani alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!),  nataka niliambie Bunge lako tukufu kwamba kwa viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi za haki asilimia 100 kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT. Hongera sana.
3.          Mheshimiwa Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na: Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.
4.          Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 158 wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza na 25 kwa maandishi.
B:        HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI
5.          Mheshimiwa Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala juu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:
·        Kuthubutu kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za abiria;
·        Kuongeza ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na Hazina kutoa fedha hizo kama ilivyopangwa;
·        Kusimamia nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwa pamoja na safari za nje, posho, sherehe, kuondoa watumishi hewa katika utumishi wa umma;
·        Kuhimiza azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa;
·        Kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;
·        Kuanzisha mahakama ya kushughulikia mafisadi;
·        Kuweka kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili kupanua fursa za ajira na wigo wa kodi; na
·        Kujielekeza kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi wakuu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kutatua kero za wananchi, hasa masikini.
Share:

Monday, 20 June 2016

KIFARU CHA KIVITA CHA JESHI LA WANANCHI KIKOSI CHA 83KJ MKOANI PWANI CHAIBIWA






Watu 20 wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuiba KIFARU cha Kivita cha jeshi la Wananchi kikosi cha 83 KJ mkoani Pwani. - Unadhani hawa wanaotuhumiwa kuiba kifaru walikuwa na nia gani?
Share:

Breaking News: Wabunge wa Upinzani Waziba Midomo yao Kwa Karatasi na Plasta na Kisha Kutoka Nje


Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni leo wametumia mtindo mpya kueleza hisia zao baada ya kuamua kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakiwa wamejifunika midomo kwa karatasi.

Hii ni wiki ya pili mfululizo wabunge hao wamekuwa wakitoka bungeni baada ya kutangaza kutohudhuria kikao cha bunge kinachoongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema wameamua kutumia mtindo huo mpya kwa sababu Bunge limekataa kuwasikiliza hoja zao.
Share:

MPYA:SERIKALI YASITISHA AJIRA ZOTE

John Magufuli
SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila malipo.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema kuwa Serikali imesitisha kwa muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi zake.
Alisema utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.
“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na tathmini ya muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini utekelezaji utaendelea,” alisema.
Taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, zililiambia gazeti hili kuwa maelekezo hayo yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa mikoa, kwa wakuu wa idara za Serikali zinazojitegemea.
Waliotakiwa kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote wa majiji, manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali kwa upande wa Tanzania Bara.

Kamatakamata

Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao wamekuwa wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo  ambapo mtumishi mmoja wa moja za za Mkoa wa Kigoma, alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao Ubungo Kibangu jijini Dar e Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia miongoni mwa majirani ambao waliliambia gazeti hili kuwa, askari hao walifika nyumbani kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.
Kutokana na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, zililieleza gazeti hili kuwa walimu watano wastaafu nao walikamatwa na polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.
Mbali na walimu hao pia alikuwepo muuguzi mmoja.
Akizungumzia na MTANZANIA kuhusu tukio hilo la kamatakamata mmoja wa waliokumbwa na hali hiyo, Marco Nyimbi ambaye ni mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Muungano wilayani Nyasa mkoani Ruvuma alisema hatua ya kukamatwa kwake ilimfanya apigwe na butwaa na kushangazwa na hatua ya kukamatwa yeye na wenzake watano kwa kudaiwa kuwa ni watumishi hewa.
Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba.
Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.
Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Alifafanua kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu
 
chanzo: Mtanzania
Share:

Kahama kupata neema ya umeme



Wakazi wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga wanatarajia kupata umeme kutoka mgodi wa Buzwagi. Hayo yalisemwa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Kahama, Sule Kabati amesema hayo alipokuwa akitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya hiyo, Vita Kawawa aliyetembelea mradi wa mtambo wa kuunganisha umeme kutoka katika mgodi huo. Meneja huyo alisema kuunganishwa na kuwashwa kwa mtambo huo kutamaliza tatizo la kukatika umeme uliokuwa ukiukabili mji huo na vitongoji vyake. “Pia, mtambo huu utaongeza uwezo wa Tanesco wa kuhudumia wateja wengi zaidi kulinganisha na awali,” amesema Kabati. Umeme huo unatarajiwa kuwashwa Juni 24, mwaka huu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Share:

Kubenea Amshitaki Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson



Wakati Kamati ya Haki, Maadili na Madara ya Bunge imepokea mashtaka dhidi ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mbunge mwingine wa upinzani ameamua kumshtaki kiongozi huyo kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge.

Mbunge wa kwanza kumshtaki Dk Tulia, alikuwa Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James ole Millya aliyewasilisha kusudio lake kwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai mashtaka sita na tayari yamewasilishwa kwenye kamati husika.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alitangaza jana uamuzi wake wa kumshtaki Dk Tulia, ambaye ndiye anayeliongoza Bunge kwa sasa.

Dk Tulia atakuwa na kesi mbili, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na kwenye Kamati ya Kanuni.

Dk Tulia anakuwa Naibu Spika wa kwanza tangu kuanza Bunge linalojumuisha wabunge wa upinzani, kushtakiwa kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za Bunge.

Kubenea alisema ameamua kumshtaki Dk Tulia katika kamati hiyo akidai kuwa alivunja kanuni na taratibu wakati akiwasilisha malalamiko ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa mbunge huyo alisema uongo bungeni.

Akizungumza na wanahabari, mbunge huyo alisema hakuridhishwa na hatua ya Dk Tulia aliyoifanya Mei 13 na kwamba tayari alishawasilisha barua yake yenye hoja tano za mapungufu ya kikanuni kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah tangu Ijumaa iliyopita.

Kubenea alieleza kuwa Dk Tulia alitumia kanuni ya 71 kupokea malalamiko ya Dk Mwinyi kinyume na utaratibu kwa kuwa kanuni hiyo huruhusu watu wasio wabunge kupeleka malalamiko yao kwa Spika, iwapo masuala yaliyojadiliwa bungeni yamewaathiri.

Alisema wakati akichangia hoja ya wizara hiyo Mei 10, alimtaka Dk Mwinyi aeleze juu ya kuwapo kwa mkataba baina ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Kampuni ya Heinan Guoji Industry & Investment Limited na kama upo haoni kama kuna mgongano wa masilahi kutokana na kushiriki kumjengea nyumba yake.

Hata hivyo, alidai hakuna mbunge aliyesimama kudai hoja hiyo ilikuwa ya uongo kama kanuni ya 63(3) inavyotaka, badala yake siku tatu baadaye alitakiwa kufuta bungeni jambo ambalo anaona Dk Tulia hakumtendea haki.

“Naibu Spika wakati akitoa mwongozo wa Spika alinukuu sehemu tu ya maelezo yangu jambo lilipotosha misingi na mantiki ya mchango wangu bungeni hivyo kuashiria alikuwa na nia mbaya dhidi yangu,” alisema Kubenea na kuongeza: “Hata nilipoomba kufanya hivyo siku aliposoma mwongozo na kunipa nafasi ya kufuta maneno yangu au kuyathibitisha, alikataa na endapo angezingatia mchango wangu wote angetenda haki.”

Katika barua hiyo, Kubenea amelalamika kuwa wakati Dk Tulia anapokea malalamiko kutoka kwa Dk Mwinyi hakumpelekea nakala ili kurahisisha utetezi wake.

Pia, alieleza kuwa Naibu Spika aliamua kimakosa kuwasilisha tuhuma dhidi yake kwenye kamati hiyo bila kuzingatia maelezo aliyowasilisha kwake na vielelezo huku akijua Waziri huyo wa ulinzi alikiuka kanuni ya 63 (3) na 64(2).

Kubenea alisema anaiomba Kamati ya Kanuni yenye nguvu kuliko Spika kusimamisha mchakato unaoendelea kufanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya suala lake hadi pale itakapofanya uamuzi iwapo ilifuata kanuni ama la.

Katika barua hiyo, Kubenea anamuomba Dk Kashililah amjulishe Spika ili aweze kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ili kuona kama kulikuwa na uhalali wa shauri lake na anaamini Katibu huyo wa Bunge atamtendea haki.

Kubenea alishahojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Alhamisi iliyopita na kueleza kuwa alikubali kufanya hivyo kwa kuwa kamati hiyo ina nguvu kubwa ya kikanuni ikiwamo kukamatwa.

Kubenea alisema hana wasiwasi na aliyoyasema ila anataka haki itendeke kwa kufuata kanuni na hadi sasa ana vielelezo vya kutosha kuhusu suala lake.

Dk Kashililah alieleza jana kuwa hawezi kuzungumzia kwa kina jambo hilo kwa kuwa taratibu zote za kufuata zinafahamika.

 “Inawezekana ameandika, lakini mpaka ifike tuipokee. Mimi nilikuwepo Ijumaa hadi saa tano usiku sikuiona. Huenda ipo njiani ikifika tutaipokea na tutaifanyia kazi,” alisema Kashililah.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger