Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo mbalimbali wasio na ajira ambao wamepatiwa fursa ndani ya GGML kupata mafunzo tarajali kwa muda wa mwaka mmoja sambamba na wahitimu 10 wa mafunzo huo kwa mwaka jana ambao wamepata ajira ya kudumu ndani ya kampuni hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela akisalimiana na akamu Rais Mwandamizi - Kitengo cha masuala ya Ubia/ushirika Afrika kutoka AngloGold Ashanti - GGML, Terry Strong na Meneja Mwandamizi wa masuala ya Rasilimali watu kutoka GGML, Charles Masubi.
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu waliojiunga na program ya mafunzo tarajali katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), kujituma kwa bidii, kuwa wabunifu na nidhamu.
Pia ametoa wito kwa wahitimu hao, kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya mgodi huo ili kujiendeleza na kuondoka wakiwa tofauti na namna walivyoingia kwenye program hiyo ya mwaka mmoja.
Shigela ametoa wito huo hivi karibuni mjini Geita katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo vikuu ambao wamejiunga na GGML kwa mwaka 2024/2025 kupata mafunzo tarajali sambamba na wahitimu wengine 10 wa program hiyo kwa mwaka jana ambao wameendelea na mafunzo ya juu zaidi baada ya kupata ajira ya kudumu ndani ya GGML.
Wanafunzi hao 10 waliomaliza program mwaka jana, wamechaguliwa kuendelea na program mpya inayofahamika kwa jina la African Business Unit Graduate (ABU) ambayo inawapa fursa ya kubadilishana uzoefu na wahitimu wa aina hiyo katika nchi nyingine za Ghana na Guine ambako AngloGold Ashanti kampuni mama ya GGML inamiliki migodi.
Shigela alisema nidhamu kwa wahitimu hao ni msingi muhimu katika utumishi wa aina yoyote hivyo wanapaswa kuzingatia nidhamu katika utendaji wao na hata wanapokengeuka kutekeleza majukumu yao nafsi inapaswa kuwasuta.
Alitoa mfano kuwa wapo wanafunzi ambao walienda kupata mafunzo tarajali ndani ya kampuni hiyo, na kufanikiwa kupata leseni za uchimbaji kwa ngazi mbalimbali nje ya mgodi na sasa ni matajiri.
Pia alisema kwa kuwa mzunguko wa manunuzi ya ndani ya GGML yanakaribia Sh trilioni moja kwa mwaka hasa ikizingatiwa kampuni hiyo inazingatia matakwa ya sheria ya ‘Local content’ ambayo inaitaka kufanya manunuzi ya bidhaa zake hapa nchini, nayo ni fursa nzuri kwa wahitimu hao kujifunza na kufungua kampuni za kusambaza bidhaa kwa mgodi huo.
Mbali na kuipongeza GGML kwa kuwa na mipango madhubuti inayofungua fursa kwa vijana wa kitanzania, pia aliwapongeza wahitimu hao ambao wamefanikiwa kupenya na kupata nafasi hiyo hasa ikizingatiwa walioomba nafasi hiyo walikuwa 2,800 lakini wamechaguliwa 40 pekee.
Naye Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya rasilimali watu, Charles Masubi alisema program hiyo ya ABU ambayo inahusu wahitimu 10 wa mwaka jana itawawezesha kupata mafunzo ya juu zaidi ya ujuzi wao wa darasani.
“Kama ni mhandisi tutamfundisha namna ya kuingia makubaliano, kuandaa bajeti lakini pia kupata ujuzi wa namna ya kuwasiliana kwa usahihi na wenzake,” alisema.
Alisema lengo la program hii ni kuwaandaa wafanyakazi wabobezi ambao wanaweza kuja kuwa viongozi wa baadae wa kampuni hiyo na hata nje ya GGML.
Mmoja wa wahitimu aliyepata fursa ya mafunzo tarajali kwa mwaka huu, Fakii Juma alisema GGML ina matarajio makubwa kwao katika uzalishaji hivyo watatumia vipaji vyao kuongeza ujuzi kwenye mgodi huo kutokana na elimu wanayoipata na wanajivunia kwamba wataongeza thamani ya mgodi huo.
0 comments:
Post a Comment