Dodoma Julai 19, 2023
Tume ya Madini imetoa siku saba kwa wamiliki wote wa leseni za madini zikiwemo leseni za utafutaji wa madini, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini, leseni za uchenjuaji wa madini, leseni za uyeyushaji wa madini na leseni za usafishaji wa madini kuhakikisha wanatekeleza masharti ya leseni zao kwa mujibu wa Sheria.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ya Sekta ya Madini.
Amesema kuwa, zipo kampuni za madini ambazo zimeaminiwa na Serikali kwa kupewa leseni za madini lakini wamekuwa wakikiuka masharti ikiwa ni pamoja na kutoendeleza maeneo ya uchimbaji wa madini hivyo kukosesha fursa kwa waombaji wengine wenye nia ya kuchimba madini na Serikali kupata mapato yake.
“ Tumetoa muda wa siku saba ( kuanzia tarehe 19 hadi 25 Julai, 2023 kwa wamiliki wote kutekeleza masharti ikiwa ni pamoja na wamiliki wote wa leseni za madini ambao leseni zao zimetoka lakini hawajazichukua kuhakikisha wamezichukua, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka kuhakikisha wamelipia na leseni ambazo hazijaendelezwa kuhakikisha zinaendelezwa ndani ya muda ulioainishwa sambamba na kuwasilisha taarifa ya kuanza kazi na taarifa za kila robo mwaka kuwasilishwa,” amesema Profesa Kikula.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka waombaji wote wa leseni za madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi, maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi na ada ya pango kwa mwaka.
Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa wamiliki au waombaji wa leseni watakaoshindwa kurekebisha mapungufu ndani ya muda wa siku saba, Profesa Kikula amefafanua hatua hizo kuwa kwa leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango ya mwaka, leseni ambazo haziendelezwi na leseni ambazo zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kwa maombi yote ya leseni ambayo hayakidhi vigezo, yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.
Aidha, Profesa Kikula amesisitiza kuwa dhumuni la Serikali ni kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wawekezaji wote nchini na kuongeza kuwa Serikali haitamfumbia macho mwekezaji wa ndani au kutoka nje ya nchi ambaye ameshikilia maeneo bila ya kuyaendeleza au kuyatumia maeneo hayo kujipatia fedha kisha kuwekeza nje ya nchi.
Pia, Profesa Kikula ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika madini ya kimkakati yanayohusika katika utengenezaji wa vifaa vya kisasa na kieletroniki ikiwemo magari yanayotumia umeme ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Wakati huohuo, Profesa Kikula ameongeza kuwa Serikali imekamilisha kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii za mwaka 2023 ambazo zitasaidia wamiliki wa leseni kuwa na mwongozo wa namna bora ya kutoa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi yao.
0 comments:
Post a Comment