Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya, amewataka wananchi wake kupuuza upotoshaji unaoendelea mitandaoni kuhusu suala la Bandari, na kuzuka kauli za kwamba Mhe. Rais Samia ameuza nchi.
Mhe. Dkt. Chaya ameyasema hayo leo Julai 20, 2023 wakati wa ziara yake Katika Kata ya Chikola na Sasilo, Wilayani Manyoni ambapo amefanya Mikutano ya hadhara, baada ya kuulizwa Maswali na Wananchi juu ya maswali waliyonayo kuhusu ukakasi uliopo juu ya Bandari
Amefanya Ziara Katika Vijiji vya Ipululu, Mwitikila, Chidamsulu na Chikola
Mhe. Chaya ameeleza kuwa kinachokwenda kufanyika ni Ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Dp World ya Nchini Dubai na haina tofauti na ilivyokuwa kwa Kampuni ya Ticts ambayo imetekeleza Mkataba wake kwa Miaka 25.
"Kinachokwenda kufanywa na Rais Samia ni Ubia sio ubinafsishaji, sasa kuna watu wanaanza kupotosha, mara tunauza bandari, huyu anapokuja tunakuja kukubaliana nae kwamba wewe unachukua sehemu gani na unatekeleza kwa asilimia kadhaa, na asilimia kadhaa atatekeleza Tanzania yaani TPA, na hicho ndo kinachofanyika"
Akiendelea kuwaasa wananchi wake, Mhe. Dkt. Chaya amesema wengi wanapotosha kwamba Mama Samia ameuza Bandari, jambo ambalo wao kama Wabunge hawawezi kukubali, ni lazima wangepiga kelele kupinga.
"Ubia ni makubaliano kwamba nachukua sehemu hii, wewe chukua sehemu hii baadae mnaweka utaratibu mzuri wa mgao, hakuna tofauti kabisa Kati ya anachokuja kufanya Dp World na Ticts"
Amesema anashangaa kumekuwa na Siasa nyingi kwenye jambo hilo, na kuwaomba Watanzania kumuunga Mkono Mhe. Rais na wao kama Viongozi Vijana wanapaswa kuaminiwa na Wananchi kwani hawawezi kukubali jambo ambalo linaihatarisha nchi.
"ninachofurahi kote huko nilikopita sijakutana na upotoshaji wa aina yoyote, wengi wanasimama kwakweli wanakiri kabisa kwamba huyu Mama anafaa, anatosha na chenji inabaki" amesema Dkt. Chaya
Mbunge huyo amewaambia wananchi hao kuwa, hakuna sehemu ambayo ilikuwa na Madudu mengi kama Bandarini, hata enzi za Hayati Rais Magufuli wengi walifukuzwa katika bandari.
Ameongeza kuwa, watu wengi wametajirika kupitia Bandari ya Dar es salaam na ukifuatilia wanaopinga wengi ni wale wanaofanya Kazi katika Bandari hiyo na wanajua kwa sababu wananufaika.
"Niwaombe kama kuna maeneo mazuri ya kuboresha, toeni mawazo yenu tuboreshe huu uwekezaji ambao Rais wetu anataka kuufanya, tunataka tupate Fedha ili tutekeleze miradi mingi ya maendeleo"
Amesema, maendeleo yanayofanyika katika Jimbo lake yanatokana na mapato, na mojawapo ikiwa ni ya Bandari kwani ni eneo ambalo mapato mengi yanatoka huko, hivyo uwekezaji huo utakaokwenda kufanyika utaongeza utekelezaji wa miradi katika Taifa.
"Ukicheza na bandari usipoweka uwekezaji mzuri hautavuna chochote mapato ,Mimi nimetembelea pale bandarini, hatuna uwezo wa kushusha mizigo kwa muda muafaka, mizigo ikifika inakaa muda mrefu sana na matokeo yake wawekezaji wengi wanahama"
Ametaka Rais Samia aungwe mkono kuhusu suala la Bandari kwani ana nia njema na hapaswi kukatishwa tamaa
"Ndugu zangu wana Chikola na sisi tusiwe watu wa kufuata mkumbo, tusikubali kupotoshwa na Wazushi" Mbunge Dkt. Chaya.
Aidha, Mbunge Dkt. Chaya alipopita Katika Vijiji hivyo, ameeleza Miradi ambayo Serikali inatekeleza, na itaendelea kutekeleza Katika maeneo yao.
Ziara ya Mhe. Mbunge Dkt. Chaya bado inaendelea katika Vijiji mbalimbali Jimbo la Manyoni Mashariki.
0 comments:
Post a Comment