Sunday, 30 April 2023

KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA KUBORESHWA

...
Mkoa wa Rukwa waingia katika historia mpya mara baada ya Serikali kupitia Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) kuingia mkataba na Kampuni ya M/s Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd ya nchini China kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga kwa gharama ya Shilingi Bilioni 55.908 kwa muda wa miezi 18.

Uboreshaji huo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani humo na ukanda wa Magharibi mwa nchi ya Tanzania ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Zoezi la utiaji saini wa mkataba huo uliofanyika katika Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga, mkoani humo umefanyika kati ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Matavila pamoja na Mwanasheria wa TANROADS, Wakili Gurisha Mwanga na kushuhudiwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa.

Akizungumza baada ya Zoezi hilo, Prof. Mbarawa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuboresha miundombinu pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo.

Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuwa uboreshaji wa kiwanja hicho utakapokamilika utaruhusu kiwanja hicho kufanya kazi saa 24 yaani usiku na mchana na kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege aina ya Boeing Q 400 pamoja na ATR 72.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umeletwa mahsusi ili kuchochea shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, utalii, uwekezaji, uvuvi, usafirishaji wa mizigo na abiria na shughuli za kijamii kwa ujumla.

"Mapema mwakani wana Sumbawanga mtegemee ndege ya kwanza kutua hapa", amesisitiza Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amefafanua kuwa uboreshaji wa kiwanja hicho pia utahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, ununuzi na usimikaji wa taa za kuongozea ndege (AGL) na mitambo ya Usalama (DVOR/DME), barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani, maegesho ya magari na uzio wa usalama.

Aidha, amesema kiwanja hicho kwa sasa kina barabara ya kuruka na kutua ndege ya kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilometa 1,516 na upana wa meta 30 ambapo kupitia mradi huu barabara hiyo itaboreshwa kufikia urefu wa kilometa 1,750 na upana wa meta 30 kwa kiwango cha lami.

Waziri Prof. Mbarawa, ametoa rai kwa Uongozi wa Mkoa wa Rukwa kuusimamia mradi na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi huo pamoja na kuwasisitiza wananchi wetu wanaozunguka eneo la mradi kuepukana na uhalifu wa namna yoyote katika mradi badala yake waulinde mradi huu ili wafaidike na fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati utekelezaji wa mradi ukiwa unaendelea.

"Mkiulinda mradi huu utasaidia kulinda thamani halisi ya mradi lakini pia kukamilika kwa wakati na ubora unaokubalika", amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amewaagiza Wataalam wa Wizara, TANROADS, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga (TCAA) na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na wadau wote kufanya kazi kwa weledi na kusimamia utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa wakati.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Queen Sendinga, ameishukuru Serikali kwa baraka ya miradi inayoendelea mkoani kwake ambapo ukiondoa kiwanja cha ndege hicho pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Ntendo - Kizungu (km 25) na barabara ya Matai - Tatanda (km 25) inaendelea vyema.

Mkuu wa Mkoa huyo pia ameahidi kuusimamia uboreshaji wa kiwanja hicho ili uweze kukamilika kwa wakati kwani mkoa huo hauna viporo vya miradi kucheleweshwa.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, ameeleza kuwa uboreshaji wa kiwanja hicho utahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 150,000 kwa mwaka ambapo Jengo hilo litakuwa na sehemu ya kuongozea ndege.

Matavila ameeleza kwamba upembuzi yakinifu wa kiwanja hicho ulifanywa na kampuni ya Sir Fredrick Snow & Partners Ltd ya Uingereza ikishirikiana na Kampuni ya Belva Consult ya Tanzania kati ya mwaka 2007 mpaka mwaka 2009.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila akisaini mkataba wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbwanga na Mwakilishi kutoka kampuni ya M/s Beijing Construction Engineering Group ya nchini China kwa gharama ya Bilioni 55.908 kwa muda wa miezi 18, mkoani Rukwa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila pamoja na Mwakilishi kutoka kampuni ya M/s Beijing Construction Engineering Group ya nchini China wakionesha mkataba wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbwanga mara baada ya kusainiwa, mkoani Rukwa. Uboreshaji huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 18 na utagharimu Bilioni 55.908.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kusiani mkataba wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbwanga utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 55.908, mkoani humo.



Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, akitoa taarifa ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbwanga utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 55.908, wakati wa utiaji saini mkataba wa uboreshaji wa kiwanja hicho na mkandarasi kutoka kampuni ya M/s Beijing Construction Engineering Group ya nchini China, mkoani Rukwa.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendinga, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbwanga utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 55.908, mkoani humo.



Muonekano wa sehemu ya barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha changarawe katika Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ambapo Serikali imesaini mkataba wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kwa gharama ya shilingi Bilioni 55.908, mkoani Rukwa. Ukarabati wa barabara hiyo utafanyika kutoka kilometa 1,516 hadi kufikia kilometa 1,750 kwa kiwango cha lami.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger