Friday 18 September 2020

Shule 28 Bariadi Zanufaika Na EP4R

...


SHULE 28 za wilaya ya Bariadi zikiwemo 11 za msingi na 17 za sekondari zimenufaika na mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana (Alhamisi, Septemba 17, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkololo, wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nkololo 'A'.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wakazi hao, Mheshimiwa Majaliwa alisema awali zilitolewa sh. bilioni 2.3 na Septemba, mwaka huu zimetolewa sh. milioni 457 ili kukamilisha uwekaji miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi za Halawa, Kilabela A, Tunge, Mwauchumu, Bukiliguu, Byuna, Chungu cha bawawa, Damidami, Masewa C, Mwashagata na Banemhi zilizoko wilayani humo.

“Kwa upande wa shule za sekondari, shilingi bilioni 1.07 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa, maabara, majengo ya utawala na matundu ya vyoo kwa sekondari za Dutwa, Mwantimba, Gegedi, Miswaki, Mwamlapa, Nkololo, Nyasosi, Nyawa, Sapiwi, Banemhi, Gasuma, Igaganulwa, Ikinabushu, Itubukilo, Mwadobana, Sakwe na Nkindwabiye.”

Kuhusu mpango wa elimu bila malipo, Mheshimiwa Majaliwa alisema shule za msingi 79 zilipatiwa shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ukarabati wa majengo, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Alisema shule za sekondari 23 zilipatiwa shilingi bilioni 1.43 kwa ajili ya kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

Akielezea miradi ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.2 zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, na ujenzi wa barabara zenye urefu wa km. 246 ambazo zimefanyiwa matengenezo kwa kiwango cha udongo, km. 37.6 kwa kiwango cha molamu. Pia, makalvati 108 yamejengwa.

Alizitaja barabara zilizofanyiwa matengenezo hayo kuwa ni za Ikungulyabashashi – Ditima; Byuna - Nkindwabiye - Halawa; Igegu - Matongo Gibishi - Halawa; Dutwa- Gilya - Mwauchumu; Nyakabindi - Mwadobana - Gasuma; Kasori Centre - Kasori Ginnery na Nyamswa - Mwasubuya - Bwawani.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi, Injinia Kundo Mathew, mgombea udiwani wa kata ya Nkololo, Nyamwela Sinda na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Bariadi waliokuwepo kwenye mkutano huo.

(mwisho) 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger