Wednesday 16 September 2020

Serikali Yawatoa Hofu Wamiliki Wa Malazi Wa Kanda Ya Kaskazini Kuhusu Usajili Wa Wageni Kwenye Mfumo Wa MNRT Portal

...
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewatoa hofu Wamiliki wa Huduma za Malazi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa usajili wa Wageni kwenye mfumo wa MNRT PORTAL utakaoanza kutumika nchini kote Oktoba 1, 2020 umelenga kupata takwimu sahihi za Wageni zitakazosaidia katika  kuboresha sekta ya Utalii nchini na si vinginevyo.

Pia, Imesema Usajili huo  utalinda siri za Wageni  na  zitatumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali pekee na sio  kwa maslahi binafsi.

Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga alipokuwa akihitimisha mafunzo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili ya usajili   Wageni kwenye Mfumo wa  MNRT PORTAL  kwa Watoa Huduma za Malazi zaidi ya 250 wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara

Amesema Usajili wa Wageni katika Mfumo huo utahusisha Wageni wa ndani pamoja na Wageni kutoka nje ya nchi ambapo lengo kuu ni kupata takwimu zitakazosaidia kuboresha sera, mikakati na mbinu za kukuza utalii nchini.

Amesema Usajili huo mbali ya kusaidia kujua idadi ya Watalii wa ndani bali utawasaidia hata Wamiliki wa malazi hayo kuweka rekodi ya  Wageni waliolala katika malazi yao kwa kipindi chote ambacho anafanya biashara hiyo ya malazi.

Chitaunga amesema katika sekta ya utalii mfumo huo umekuwa ukitumika sehemu nyingi Duniani kama vile Uingereza, Marekani na Kanada  na si kitu kipya kilichoanzishwa hapa nchini.

Pia amesema mfumo huo utasaidia kurahisisha kazi kwa Wamiliki wa malazi ambapo badala ya kubeba karatasi na kwenda katika ofisi za Wizara ya Maliasili na utalii kwa ajili ya kulipia leseni ataweza kutumia  kompyuta yake akiwa ofisini kwake  kufanya usajili huo

Mkurugenzi huyo amesema mfumo huo utakaonza kutumiwa na Watoa Huduma za malazi nchini kote mwezi Oktoba 1, 2020 utahusisha hoteli, loji, nyumba za Wageni pamoja na mahema ya watalii.

Ametaja vitambulisho vitakavyotumika katika usajili huo kuwa ni Kitambulisho cha Taifa kwa wageni ambao ni Watanzania na Pasi ya kusafiria kwa Wageni wa kutoka nchi za nje.

Naye Anne Sosteness ambaye ni miongoni mwa Wamiliki wa Malazi katika mkoa wa Arusha aliyeshiriki mafunzo hayo, Amesema mafunzo ni mazuri na ni salama kwa mteja na mtoa huduma kwa ssbabu Mteja anatakiwa kuonesha kitambulisho chaTaifa au pasi ya kusafiria ili aweze kusajiliwa.

Aidha, Amesema mfumo huo unapunguza matumizi ya karatasi ambayo ni rahisi kupotea na kuchanika.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger