Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho Philemon Mutabilwa akiwasilisha mada katika majadiliano jana Dar es Salaam
**
CHUO Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimekutana na wadau wa Nishati Jadilifu lengo likiwa kujadili mitaala ya nishati hiyo inayotarajiwa kuanzishwa mwaka wa masomo 2021/22.
Katika majadiliano hayo chuo hicho kimebainisha mitaala hiyo ni Shahada ya kwanza ya nishati hiyo , Astashahada ya uhandishi mitambo na Nishati Jadilifu pamoja na Astashahada ya uhandishi umeme na nishati.
Akizungumza katika mjadala huo Dar es Salaam jana Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho Philemon Mutabilwa alisema nishati hiyo ni muhimu ila haijawekewa mkazo hivyo endapo malengo yatatimia yatachochea kupata wahitimu wenye ujuzi wa kutosha watakaonufaisha taifa.
"Mitaala itajikita katika namna ya kutumia nishati jadilifu kabla haijaanzishwa walimu watajengewa uwezo ili wakafundishe kuzalisha wahitimu wenye sifa stahiki kwenye soko la ajira," alisema Mutabilwa.
Alibainisha kuwa MUST haitaishia kwenye kujikita katika mitaala hiyo badala yake miaka ijayo wataangalia uanzishwaji wa mitaala ya nishati ya upepo pamoja na masalia ya chakula.
Alifafanua kuwa Serikali ya Uholanzi ndio wafadhili wa mradi wa mkakati wa uanzishaji mitaala hiyo ambapo Sh.bilioni 1 zimetolewa kugharamia huku walengwa wakiwa MUST na Chuo cha Teknolojia Arusha (ATC).
Alisisitiza kuwa mradi wa mitaala hiyo imejikita kuwajengea uwezo walimu watakaofundisha pamoja na kujenga miundo mbinu hivyo aliishauri serikali kujiandaa endapo kutatokea ukosefu wa vifaa baada ya mradi kukamilika.
Alimshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kukamilisha na kufanikisha ujenzi wa Jengo kubwa la Maktaba .
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati hiyo Mhandisi Dkt . Mathew Matimbwi alizishsuri taasisi za elimu ya juu zinazotoa mitaala hiyo kujenga miundombinu bora ya utendaji kwa vitendo ikiwemo maabara za kisasa ili kuwapa wahitmu ujuzi utakaowasaidia wanapokwenda sehemu za kazi.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Nkotage Hamisi alisema walimu wa kozi za uhandisi wawekewe utaratibu wa kwenda kushiriki mafunzo kwa vitendo ili kuwasaidia kuwajengea uwezo.
Wakati huo huo Mtafiti kutoka UDSM Brenda Kazimili alishauri kuwa MUST kujenga utamaduni wa kutembelea shule za sekondari za wasichana ili kuwajengea hamasa na kuwahimiza kuyapenda masomo ya sayansi na uhandisi.
Katika hatua nyingine Mdau kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Sylivester Mwambije alishauri kuwepo utaratibu wa kuwapeleka wanafunzi wa mitaala hiyo kwenye taasisi binafsi wapatiwe mafunzo ili kuwapa ujuzi utakaosaidia kuendana na solo la ajira.
Vile vile imeelezwa na Rehema Mbugi ambaye ameshiriki kama wadau kutoka baraza la ujuzi la Nishati kutoka TPSF kwa ajili ya kusapoti MUST kuja na mitaala huo mpya alisema itachochea ajira kwa wahitimu kupata nafasi nzuri katika kuajirika.
Bi . Rehema Mbugi (katikati) ambaye ameshiriki kama wadau kutoka baraza la ujuzi la Nishati kutoka TPSF .
0 comments:
Post a Comment