Thursday 24 September 2020

Mazingira ya malezi ni sababu ya watoto wengi kubaki mtaani.

...

Na Samirah Yusuph, Bariadi. 
Watoto ni miongoni mwa vibarua wanaoupamba mji wa Bariadi mkoani Simiyu, ambapo wamekuwa wakifanya shughuli mbali mbali mtaani kwa ajili ya kijipatia kipato.

Wapo walioacha shule kwa sababu mbali mbali na kuingia mtaani lakini pia wapo wanaosoma huku wakiendelea kufanya shughuli hizo kwa ajili ya kujiingizia kipato na kuendesha maisha ya familia zao.

Baadhi ya watoto hao walisema kuwa mazingira ya nyumbani na malezi ni sababu ya ongezeko hilo kwani kuna baadhi ya wazazi wanawatuma watoto kufanya kazi mitaani ili waweze kusaidia familia.

"Unakuta mtoto hapati mahitaji yake yote kutoka kwa mzazi pengine mtoto anakuwa na uhuru uliopitiliza hata akirudi usiku wa manane mzazi hawezi kumuiliza alikuwa wapi hiyo inachangia sana mtoto kuharibikiwa," alisema Yohana Daud (19) mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari biashara.

"Hata hapa tunaona mtoto anatoka nyumbani hafiki shule anaenda mtaani kutafuta pesa na mzazi hajui wala hafuatilii na hapo ndipo ndoto zinaanza kufifia na mwisho anajikuta anaharibikiwa," aliongeza Yohana.

Matarajio ya watoto wengi ni kutimiza ndoto zao kama inavyokuwa tangu awali wanapoanza kwenda Shule licha ya wengi kutokufikia malengo yao na kuishia mtaani jambo ambalo linawakatisha tamaa.

"Binafsi sijisikii vizuri ninapoona wasicha wenzangu wanashindwa kwenda shule na kubaki kufanya kazi mitaani, sisi sote ni sawa lakini inashindikana ni wapi watoe taarifa waweze kutimiza ndoto zao,"alisema Beatrice Baraka (18) mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kidinda.

Wakati huo baadhi ya watoto walio katika vibarua hivyo walisema kuwa, wao hawapendi kuwa katika mazingira hayo kwani wao pia wanatamani wasome ili waweze kufanikiwa na kutimiza ndoto zao jambo ambalo kwao limekuwa haliwezekani tena.

 Adela 15 (jina sio halisi) ambae ni mfanyakazi za ndani alisema kuwa baada ya kumaliza darasa la saba shule ya msingi Mbiti wilayani Bariadi mwaka 2019, hakutakiwa kuendelea na shule tena kwa sababu baba yake hakuwa na uwezo wa kumnunulia sare za shule hivyo ilimlazimu kutafutiwa kazi za ndani ili aweze kusaidia familia.

"Nilikuwa natamani kuwa daktari lakini kwa sasa sitaki tena kwa sababu najua haiwezekani, ninafanya kazi ninalipwa tsh 30,000 ambayo inatumwa nyumbani ninabaki na tsh 10,000 kwa ajili ya matumizi yangu," alisema Adela.

Adela anatamani pesa anayopata walau abaki nayo ili aweze kununua vitu ambavyo vitamsaidia katika maisha yake ya baadae.

Agatha 15 (jina sio halisi) ambaye ni mhudumu wa ukumbi wa starehe, alisema baada ya kumaliza darasa la saba hakufanikiwa kuendelea na masomo kwa sababu familia yake ilihitaji mtu wa kusaidia ili wapate chakula hivyo ikamlazimu yeye kutafutiwa kazi ili asaidie familia.

"Siku ya mtihani wa darasa la saba nilipigwa nikavimba jicho, nilipokuwa kwenye mtihani sikuweza kufanya chochote hata matokeo yalivyoka nimefeli nilimuomba baba nirudie shule lakini hakuniruhusu kwa sababu ilibidi mimi nitafute pesa ili ndugu zangu wengine wasome," alisema Agatha.

Aliongeza kuwa anatamani kuwa Mfanyabiashara lakini haiwezekani kwa sababu malipo yake ya mwezi ni tsh 30,000 ambayo inatumwa kwa wazazi wake na anabakiwa na tsh 5000 pekee kwa ajili ya matumizi.

Wakati huo huo Ramadhani 14 (jina sio halisi) mtoto anayejishughulisha na kazi ndogo ndogo mtaani alisema kuwa, amezoea changamoto za mtaani na hivyo anafurahia maisha hayo kwa sababu hawezi kukaa nyumbani akaishi kwa kuongozwa na mzazi.

"Nikiwa darasa la nne niliacha shule nikaanza kufanya kazi na nikawa ninarudi nyumbani jioni, baadae nikaona isiwe shida baada ya kunisema sana ninalala kwenye banda la video na ninaishi tu mtaani lakini sifikilii kurudi nyumbani hata siku moja," Alisema Ramadhani

Uwepo wa kundi hilo la watoto katika mji wa Bariadi baadhi ya wazazi wametafsiri kuwa ni namna ya kumnyima mtoto uhuru lakini pia ni malezi ambayo watoto wanakuwa wanayapata tangu wakiwa katika familia ndiyo yanapelekea hali hiyo.

"Watoto hawa sio kama hawana kwao, lakini kunabaadhi wameamua kuishi maisha hayo japo kuna wale wanaotumwa ili kusaidia familia, na kingine kinacho haribu watoto ni hawa ma dada poa ambao wanapokuja kujiuza na baada ya kuondoka tabia hiyo wanakuwa wameiambukiza kwa watoto wetu waliopo kwenye makuzi," alisema Mama Najima.

Jambo hilo lilitolewa ufafanuzi na Afisa ustawi wa jamii mji wa Bariadi Janeth Jackson, Ambapo amesema tatizo hilo lipo lakini kwanza wazazi ama Jamii inatakiwa kujua wajibu wao kwa watoto, hasa pale wanapoona vitendo vya kikatili vinapotokea ama kufanyika kwa watoto Jamii inayo wajibu wa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika.

" Ninachoamini ni kwamba unapotoa taarifa fulani ni ngumu sana kwamba kila mtu itamfikia hasa ya kufikisha ujumbe kwa jamii na watoto walioko mashuleni,nikiwa na maana kwamba kwa wale ambao hawako shule ni sehemu ya jamii na hata kama hakuipata kupitia mimi basi yule aliyeipata tunahakikisha wanakuwa mabalozi wazuri kwa waliobaki," alionheza Janeth.

Aliongeza kuwa sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu Cha 95 kinaitaja jamii kutoa taarifa kwa kitendo chochote Cha ukatili kikitokea ama kuhisi ukatili wa aina yoyote kutokea na jamii hailewi  juu ya wajibu wao wa kutoa taarifa kwa vitendo hivyo.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger