Friday, 22 March 2019

RAIS MAGUFULI ASAINI SHERIA YA VYAMA VYA SIASA..CHADEMA WASISITIZA KUTINGA MAHAKAMANI

...


Wakati Rais wa Tanzania, John Magufuli akitia saini Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya siasa na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Februari 22, 2019, Chadema wamesisitiza wataipinga sheria hiyo mahakamani.

Marekebisho hayo yaliyopelekwa bungeni mwishoni mwa mwaka 2018 yalizua mjadala mkali ambapo baadhi ya vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia na haki za binadamu walihofu ukandamizwaji wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Akizungumzia sheria hiyo leo Ijumaa Machi 22, 2019 Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema sheria hiyo ni mbaya kutokana na vifungu vyake na inakiuka Katiba na misingi ya utawala bora pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Hata hivyo, CCM wamepokea vizuri marekebisho hayo, ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho kimejipanga kufuata Katiba na sheria.

Katika maelezo yake, Mrema aligusia jinsi sheria hiyo kifungu cha 3(b) kinavyompa Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia chaguzi za ndani ya vyama ikiwa ni pamoja na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali.

“Hii inampa Msajili mamlaka ya kuingilia vyama na kuviamulia ni nani awe kiongozi wa chama husika au mgombea wa nafasi ndani ya Serikali kama mgombea Urais na ubunge. Hii ni kinyume na Katiba ya nchi ambayo imetoa fursa na haki ya kujumuika kwa wananchi wake,” amesema Mrema.

Pia amegusia kifungu cha 3 (g) cha sheria hiyo akisema si rafiki kwa kuwa kinamfanya Msajili kuwa mshauri wa Serikali kuhusu vyama vya siasa, “huyu anaenda kuwa mshauri wa Serikali badala ya vyama na hivyo kumuondolea sifa muhimu ya kuwa mlezi wa vyama.”

Mrema pia aligusia kifungu cha 5B (i) kinachompa Msajili mamlaka ya kudai taarifa yoyote kutoka ndani ya chama cha siasa, na kifungu cha 8C (2) kinachompa mamlaka ya kukisimamisha chama kwa sababu tu hakijampelekea kwa ufasaha orodha ya wanachama wake.

“Kifungu cha 21E kinampa Msajili mamlaka ya kumsimamisha uanachama wa chama cha siasa mwanachama yeyote na kumzuia kushiriki shughuli za kisiasa. Huu ni ukiukwaji wa Katiba,” alisema Mrema.

“Kama ilivyokuwa dhamira yetu ya awali ya kupeleka shauri mahakamani, nia na dhamira hiyo iko palepale na tunaendelea kushauriana na vyama vingine vya siasa na wadau mbalimbali njia nzuri zaidi ya kufungua shauri hilo mapema iwezekanavyo.”

Licha ya vyama vya upinzani na wadau mbalimbali kukosoa muswada wa sheria hiyo kabla na baada ya kuwasilishwa bungeni, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza mara kadhaa amekaririwa akisema kuwa sheria hiyo haina shida yoyote na mapendekezo mengi yamezingatiwa.

Na Elias Msuya, Mwananchi 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger