Kwa siku tatu sasa, kumekuwepo na taarifa za TCU kutoa matokeo ya nafasi hizo huku wanafunzi wengi wakilalamikia kushindwa kuyaona matokeo hayo katika tovuti ya tume hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu jioni ya leo, Edward Mkaku, afisa habari mwandamizi wa TCU amesema, TCU tayari imeweka matokeo ya awali ya nafasi hizo lakini matokeo hayo ni awali tu na siyo rasmi mpaka pale yatakapothibitishwa.
“Tumetoa matokeo ya awali (provisional results), ambayo mwanafunzi anatakiwa kuingia katika akaunti yake ya TCU na kuona kama amepangiwa Chuo au la, lakini matokeo hayo siyo rasmi mpaka pale yatakapokuwa yamethibitishwa (approved),” amesema Mkaku na kufafanua zaidi kuwa;
“Katika matokeo ya sasa tuliyotoa, mwanafunzi hawezi kuona amepangiwa chuo gani wala kitivo au taaluma aliyopangiwa kusoma, ila tu anajulishwa kuwa amepangiwa kusomea kitu kimoja kati ya vile vitano alivyoomba.”
Akitolea ufafanuzi juu ya wanafunzi ambao wamekosa nafasi za kuchaguliwa katika hatua ya sasa, Mkaku amesema wanafunzi hao wanayo fursa ya kuomba tena nafasi hizo.
“Tayari zoezi la kuomba vyuo kwa awamu ya pili limeanza tangu jana (Jumatatu), wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza wanaweza kuomba tena katika awamu hii ya pili,” amesema.
Uombaji wa nafasi kujiunga na vyuo vikuu unaofanyika mwaka huu, utakuwa chini ya vigezo vipya vya kujiunga na elimu ya ngazi hiyo tofauti na miaka iliyopita. Hii ni kufuatia mabadiliko yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Profesa Joyce Ndalichako.
Lakini pia uombaji wa mwaka huu, unafanyika wakati serikali ikiwa katika mchakato wa kuwasaka wanafunzi waliopo vyuoni pamoja na waliohitimu vyuo bila kuwa na vigezo. Vyuo vikuu mbalimbali visivyokidhi matakwa ya kitaaluma pia vimechukuliwa hatua.
0 comments:
Post a Comment