Wednesday, 7 September 2016

Magufuli aipa makali NHC

...




Rais John Magufuli .
Rais John Magufuli . 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa wizara zote zinazodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ziwe zimelipa madeni yao na zikishindwa ziondolewe kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Mbowe Hotels inayomilikiwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Rais pia amefanyiwa maombi maalumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam  Paul Makonda alipotembelea Chuo Kikuu (UDSM), ambako mkuu huyo wa mkoa alisema katika maombi yake kuwa Magufuli ndiye ambaye wananchi walimtaka na kumuomba Mungu azidi kumsaidia katika kutekeleza majukumu yake.
Katika shughuli ya awali, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa taasisi hizo alipozungumza na wananchi wa Magomeni wilayani Kinondoni kwenye eneo la Magomeni Quarters ambako Manispaa ya Kinondoni ilibomoa nyumba za wakazi miaka mitano iliyopita kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa, ikiahidi kuwalipa wananchi hao kodi ya mwaka mmoja na kuwarejesha baada ya ujenzi kukamilika.
Hata hivyo, manispaa hiyo imeshindwa kujenga nyumba hizo na pia kuwalipa wakazi hao kodi za miaka iliyofuata.
 Rais Magufuli amesema atafurahi kama wizara zinazodaiwa na NHC zitaondolewa kwenye majengo ya NHC kama ilivyofanya kwa mtu ambaye hakumtaja jina na hivyo kulazimika kuhamia Dodoma mapema.
“Nakupongeza sana (mkurugenzi mkuu wa NHC, Nehemiah) Mchechu kwa kazi nzuri unayofanya,” alisema Rais Magufuli.
“Nataka ndani ya siku saba wizara zote zinazodaiwa, ziwe zimelipa madeni yote. Kama hawajalipa watoe nje kama ulivyomtoa yule jamaa.”
Siku chache zilizopita, Mchechu alitangaza majina ya wadaiwa sugu ambao ni pamoja na Mbowe Hotels, taasisi za serikali na watu binafsi na kutoa mwezi mmoja kulipa madeni hayo.
Baadhi ya wadaiwa hao Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sh2 bilioni); Wizara ya Habari (Sh1 bilioni), Wizara ya Afya (Sh1 bilioni); Mambo ya Nje (Sh613 milioni) na Mbowe Hotels iliyopanga kwenye jengo ambalo kulikuwa na ofisi za kampuni zake za Freemedia na klabu ya Bilicanas, ikidaiwa Sh1 bilioni.

Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger