Mabweni mawili ya
Shule ya Sekondari Ambassador iliyopo Tabata Segerea, yameteketea kwa
moto juzi saa tatu usiku na kusababisha hasara ya takriban Sh1.5
bilioni.
Mkurugenzi
wa shule hiyo, Omary Mkwarulo alisema makadirio ya hasara hiyo
yanatokana na thamani ya jengo na mali zilizokuwamo ambazo ni vitanda
400, mashuka 1,200, taulo, mito pamoja na mali nyingine za wanafunzi.
“Shule
yangu ina wanafunzi 240 lakini wote walikuwa wamefunga shule tangu
tarehe 10, mwezi huu na kwa kuwa ilikuwa ni likizo fupi wengi waliacha
mali zao ambazo nazo zimeteketea kwa moto,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema mpaka sasa uchunguzi wa chanzo cha moto huo bado unaendelea.
Licha
ya kwamba chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, Mkwarulo
alilihusisha tukio hilo na wivu wa kibiashara kwa madai kwamba huenda
wapinzani wake ndio wamechoma majengo hayo. “Nahisi ni wivu wa
kibiashara kwani hivi karibuni nilipata wanafunzi wa kigeni wenye asili
ya Australia... sasa labda watu wanaona wivu shule yangu kuendelea
kuaminiwa,” alisema Nkwarulo.
Hata
hivyo, alisema timu ya wataalamu itafanya kazi ya tathmini leo kujua
hasara iliyopatikana na baada ya hapo ujenzi au ukarabati wa majengo
hayo utaanza mara moja ili shule itakapofunguliwa Septemba 19 wanafunzi
wakute mazingira yao ya kulala yameshatengenezwa.
Mmoja
wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, Jumanne Ahmad alisema ajali hiyo
itamgharimu kiuchumi kwani atalazimika kununua baadhi ya mahitaji ya
mtoto wake ambayo alikuwa ameshayatimiza.
“Uzuri
ajali imetokea watoto wakiwa likizo, hivyo hakuna madhara kiafya,
lakini kwa upande wa mwanangu nimepata hasara ya kifedha kwani
nitalazimika kutafuta ada na pesa ya mahitaji mengine kwani karibia
vitabu vyote na baadhi ya nguo vimeteketea,” alisema Ahmad.
Tukio
hilo limetokea siku chache baada ya bweni la wasichana la Shule ya
Sekondari Mwanzi wilayani Manyoni Mkoa wa Singida, kuteketea kwa moto na
kusababisha hasara ya zaidi ya Sh50 milioni huku wanafunzi 42
wakinusurika. Bweni hilo la shule pekee wilayani humo yenye kidato cha
tano na sita, liliteketea juzi saa 2.20 usiku.
0 comments:
Post a Comment