Wednesday 28 October 2015

Mambo 20 yaliyotamkwa na Edward Lowassa (UKAWA) na January Makamba ( CCM) leo Oct 28.

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA MAJIMBO
1: Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo, katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi, majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe.
———-
2: Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi, kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya.
———-
3: Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa, bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura, hata hivyo tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.

MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
4: CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi, tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru uliofanyika kwa uwazi na kwa amani na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.
———-
5: Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.
———-
MALALAMIKO YA UKAWA
6: Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari jana, tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume, hata hivyo matokeo ya Ubunge wanayakubali na kule wanakoshinda, wanayasheherekea.
———-
7: Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile, hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: urais, ubunge na udiwani.
———–
8: Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.
————
9: Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi.
————-
10: Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
————–
11: Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo.
————–
12: Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi. Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.


MAMBO 8 YALIYOSEMWA NA EDWARD LOWASSA

1: ‘Hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi mkuu ya Rais, Wabunge na Madiwani yanayoendelea kutangazwa nchini na tume ya taifa ya uchaguzi, hii ni sababu upo ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba utangazaji wa matokeo haya umevurugwa kwa makusudi na Watendaji ndani ya NEC kwa kusaidiana na wa chama cha Mapinduzi’

2: ‘Katika maeneo mengi matokeo yalikotangazwa, kilichoripotiwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais hakifanani wala kwendana na matakwa halisi ya Wananchi, matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai na yameandaliwa kwa lengo maalum la kumbeba mgombea wa CCM John Pombe Magufuli’

3: ‘Katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi kura zetu zimepunguzwa na kuongezwa kwa mgombea wa CCM… kwa aibu sana, maeneo mengine kura zilizotangazwa zimetofautiana na idadi halisi ya kura zilizopigwa, mfano Jimbo la Mkoani na Mtambile Pemba, Makunduchi, Chambani, Kilindi na kwengineko ni miongoni mwa matokeo yanayothibitisha kuwa sio kura za uchaguzi mkuu wa Rais bali mzimu wa uchaguzi’

4: ‘Katika maeneo mengine likiwemo jimbo la Ubungo, matokeo yaliyopo mikononi mwa msimamizi wa uchaguzi yanatofautiana na yale yaliyokusanywa kutoka katika vituo vyote vya jimbo hilo, hali kama hii ipo kwenye majimbo yote ambayo wagombea wa CHADEMA, NCCR na C.U.F ama wamekua na nguvu kubwa au wameibuka Washindi’

5: ‘Uko ushahidi wa wazi katika majimbo yote Wagombea wa UKAWA wameshinda, tume imechelewa kutangaza matokeo ya Urais kwa sababu zinazothibitishwa kuwepo mikakati ya hila, matukio yote haya ya NEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa yamekuja baada ya jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vitatu vya kuhesabu kura na kuwakamata Wataalamu wetu waliokua wakipokea matokeo ya nchi nzima ambako tulikua tukiongoza kwa maeneo mbalimbali’

6: ‘Tunaamini kwa dhati kwamba uvamizi huo ulifanyika kwa makusudi kwa malengo ya kufanikisha uchakachuaji ambao sasa tunauona ukiendelea kufanyika kupitia matangazo yanayoendelea kutolewa na NEC, tunapenda kuwataarifu na Jumuiya ya kimataifa kwamba hadi wakati huo uvamizi umefanyika kura zetu za Urais zilionyesha tukiongoza kwa asilimia zaidi ya 60 kabla hawajatunyang’anya documents zetu, computer zetu’

7: ‘Kutokana na makosa hayo makubwa na ya makusudi yanayofanywa na Watendaji wa NEC, mimi Edward Lowassa na mgombea mwenza, tunautangazia Umma wa Watanzania na Jumuiya ya kimataifa kwamba hatukubaliani na matokeo yanayotangazwa na NEC, tunataka wasitishe mara moja na kuanza upya kuhakiki, kinachofanywa na NEC hapa ndicho kinachofanywa Zanzibar, zinafanyika juhudi za kupora kwa hila na kwa mabavu mwelekeo wa ushindi wa Maalim Seif’

8: ‘Tunaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na amani na mshikamano, tunachosema sisi utaratibu umekosewa wasitishe na wasipositisha tutachukua hatua ambazo tutazitangaza baada ya kamati kuu ya chama chetu kukutana leo’
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger