Sunday, 29 November 2020

Wafugaji Na Wakulima Kunufaika Kupitia Kiwanda Cha Nyama Nguru Hills


 Na. Edward Kondela
Serikali imesema katika kuboresha na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro, inasisitiza uwepo wa miradi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote mawili.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro alipotembelea ujenzi wa mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills na kubainisha kuwa mradi huo unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na wakazi wa Mkoa wa Morogoro.

“Tumekuja kuangalia shughuli zinazoendelea kutokana na kikao ambacho tulikuwa nacho katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa na mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika kuboresha shughuli za mifugo kwenye mkoa huo na kuondoa changamoto za migogoro ya wafugaji ambapo uongozi wa mkoa waliniambia juu ya mradi huu ambao utakuwa na msaada mkubwa sana kwa wakulima na wafugaji wa mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla.” Amesema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel amebainisha kuwa mradi huo wa kipekee ambao mara baada ya kiwanda hicho kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja mbuzi zaidi ya 200 na ng’ombe zaidi ya 1,000 kwa siku, kumejengwa mabwawa makubwa ambayo yatakuwa yanakusanya maji yanayotoka kwenye machinjio, kisha kutibiwa kabla ya kutumika tena kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

“Mradi huu una jambo mahsusi kuliko mingine, maji haya ya mabwawa yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji huu ni moja kati ya miradi ambapo wafugaji na wakulima watanufaika ili wote waone huu mradi ni wa kwao kwa ajili ya uchumi wetu.” Ameongeza Prof. Gabriel

Aidha, amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 25, ambao unashirikisha wabia mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ni azma ya serikali katika kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mifugo hivyo kuwataka wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufuga ng’ombe bora wa kisasa na kupitia miradi ya kunenepesha mifugo ili waweze kuuza mifugo yenye ubora katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo hapa nchini ili sekta izidi kukua na kuchangia pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda.

Pia katibu mkuu huyo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo mingi na bora kwa kuhakikisha mifugo inaogeshwa ili kujikinga dhidi ya magonjwa na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kote nchini, kuhakikisha maeneo yao yana majosho ya kutosha kwa ajili ya kuogeshea mifugo na kuwataka wayafanyie ukarabati majosho ambayo hayafanyi kazi.

“Tufuge kisasa Namibia, Botswana wana ng’ombe wachache lakini wanauza kwa wingi nyama nje ya nchi, ndiyo maana tunaimarisha afya za mifugo, ndiyo maana nchi nzima tunashughulika na masuala ya uogeshaji niwatake wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe kwenye maeneo yao kuna majosho ya kutosha na niwatake yale ambayo hayafanyi kazi vizuri yaboreshwe. Ameongeza Prof. Gabriel

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amelitaka pia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo pamoja na Idara ya Uzalishaji na Masoko kwa kushirikiana na PSSSF kukutana haraka ili kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mradi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Hassan Chama Hassan amemwambia katibu mkuu huyo kuwa, mradi huo ukikamilika kwa wakati wafugaji watanufaika kwa kuwa wanakabiliana na changamoto ya kuuza mifugo yao kupitia minada ambapo wanakutana na madalali ambao wanafanya bei za mifugo kuwa chini, huku Meneja Ujenzi wa mradi huo kutoka PSSSF Mhandisi Grayson Bambaza akibainisha kuwa wafugaji watakuwa wanauza mifugo yao kwa kilo na siyo kwa kukadiria kulingana na umbo la mfugo.

Mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021, unategemewa kutoa ajira kwa wafanyakazi 120 hadi 200 kulingana na uzalishaji.

MWISHO.


Share:

Waziri Mkuu Apiga Marufuku Tozo Ya Unyaufu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza waendesha maghala kuacha kukata tozo ya upungufu wa uzito wa korosho ghafi zilizohifadhiwa ghalani (unyaufu) kwa wakulima na wanunuzi kwa kuwa tozo hiyo imeshaondolewa na suala hilo halijathibitishwa kitaalamu.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Novemba 28, 2020) katika kikao kati yake na Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Kilimo, Viwanda na Biashara pamoja Mrajisi wa Ushirika.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mtendaji Mkuu wa  Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya  Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala na Waendesha Maghala wote wa mikoa hiyo. Kikao kilifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.

“Mimi niliwaita kuwaambia kuwa wasimamizi wa maghala hampaswi kukata tozo ya unyaufu iwe ni kwa wakulima au wanunuzi kwasababu tozo hii haina uhalisia na haijathibitishwa na na vyombo husika, hakuna unyaufu unaotokea katika kipindi kifupi cha kuhifadhi korosho, hayo yote ni mawazo yenu tu”,”Amesema.

Waziri Mkuu amesema “Hizi Korosho wala hazikai miezi mitatu (3) kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni hii, korosho zinazoanza mwezi wa kumi mnada unaanza mwezi wa kumi uleule na baada ya hapo kuna minada ya kila wiki, minada ipo mingi, korosho hazikai kutoka siku zinaanguka na kuokotwa mpaka kwenda kuuzwa, unyaufu mnaoukata unatokana na nini?”.

Hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kumuondoa katika nafasi yake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala Bw. Odilo Majengo kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu kusitisha tozo ya unyaufu katika zao la korosho.

“Mkurugenzi wa Bodi ya Maghala ulidharau maagizo ya Serikali na hatuwezi kuishi hivyo katika Serikali, tulikwambia uache lakini ukaendesha zoezi hili kwa sirisiri na unasema hayo ni matamko ya kisiasa, kwanini tubaki na wewe kwenye nafasi hiyi”.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku tano kwa waendesha maghala kuandaa taarifa kuhusu ni kiasi gani cha korosho ambazo wamechukua kutoka kwa wanunuzi kama tozo ya unyafu, hivyo atatuma timu maalum kwa ajili ya kazi hiyo.

“Na ninyi waendesha maghala naleta timu huko kuja kupita kila ghala kuona msimu huu wote mmechukua korosho za unyaufu kiasi gani, kwahiyo nawapa siku tano kila mmoja akaandae taarifa ya korosho zilizochukuliwa kutokana na unyaufu katika ghala lake, kwa maghala yaliyopo mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma kuona nani amechukua unyaufu na kwa kiasi gani”.


Share:

Wizara Ya Ardhi Yawashukia Wasioendeleza Viwanja Na Kulipia Kodi Ya Ardhi


 Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa rai kwa wamiliki wote wa ardhi walio na viwanja visivyoendelezwa na kulipiwa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipia viwanja vyao ndani ya siku kumi na nne baada ya kupokea ankara ya madai na wasipotekeleza watanyanganywa viwanja vyao na kupatiwa watu wengine.

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Denis Masami wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mtaa wa Chidachi jijini Dodoma ikiwa ni Mkakati wa Wizara kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.

Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi zake za ardhi za mikoa imeanzisha utaratibu wa kuwatembelea wamiliki wa ardhi kila mwisho wa wiki kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi na kutoa elimu ili kuwawezesha wamiliki wa ardhi nchini kutekeleza jukumu hilo bila shuruti.

‘’Maeneo mengi nchini yana viwanja visivyoendelezwa na wakati huo wamiliki wake hawavilipii kodi ya pango la ardhi jambo linaikosesha mapato serikali, baada ya siku kumi na nne tutaanza utaratibu wa kuzitwaa, kuvinadi ili kufidia deni na kumilikishwa kwa watu wengine’’ alisema Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema, Wizara ya Ardhi inatekeleza mkakati wake wa kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kushirikisha wataalamu wa sekta ya ardhi na Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika mikoa kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwapelekea wadaiwa Ankara za madai ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine yatokanayo na sekta ya ardhi ili waweze kulipa.

Akiwa eneo la Chidachi jijini Dodoma na timu yake, Masami alibaini maeneo kadhaa yasiyoendelezwa na wamiliki wake kudaiwa kodi ya pango la ardhi sambamba na ukubwa wa eneo la shule ya St Merys Dodoma kuonesha kuwa na ukubwa wa Square mita 900 wakati uhalisia ni hekta 3.5 jambo alilolieleza kuwa limeifanya shule hiyo kulipia kiasi kidogo cha kodi ya pango la ardhi.

Kwa upande wake Afisa Ardhi wa Jiji la Dodoma Ruta Rwechugura alisema, wakati wa zoezi la kuwafuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi walibaini kukiukwa kwa baadhi ya taratibu na wamiliki wa ardhi na kutolea mfano ubadilishaji matumizi ya umiliki sambamba na baadhi ya wananchi kuuziana viwanja bila kubadilisha jina.

Aliwataka wamiliki wote wa ardhi walionunua viwanja kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wanabadilisha umiliki kwa kufika ofisi za ardhi katika halmashauri husika ili kuiweka ardhi yao salama na kuwasisitizia wamiliki kutobadili matumizi ya kiwanja vyao bila kufuata taratibu.

Hata hivyo, wakati wa zoezi la kuwafikia wadaiwa wa kodi ya ardhi mmoja wa wananchi aliyefikiwa na zoezi hilo Faustine Mwakalinga aliipongeza Wizara Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wake wa kuwafikia wamiliki wa ardhi kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na kuuelezea kuwa utaratibu huo unapaswa kuigwa na watendaji wengine wa  serikali katika kudai kodi kwani ni utaratibu ulio rafiki na unamhamasisha mdaiwa kulipa badala ya kuogopa.


Share:

TETESI ZA SOKA LEO JUMAPILI NOVEMBA 29,2020


Arsenal iko tayari kumuuza winga wa Ivory Coast Nicolas Pepe ikiwa kutapatikana mnunuaji mzuri wa mchezaji huyo, 25. (Daily Star on Sunday)

Mlinzi wa Barca raia wa Uhispania Gerard Pique, 33, anatumai kuwa klabu ya Nou Camp "itazungumza vizuri" na Messi ili asalie klabu hiyo. (ESPN)
Kipaumbele kwa Real Madrid ni kumsajili mshambuliaji wa Paris St-Germain na Ufaransa Kylian Mbappe, 21, mwaka 2021 kabla ya kujaribu kumsajili mshambuliaji wa Norway Erling Braut Haaland, 20, kutoka Borussia Dortmund mwa 2022. (AS)

Manchester City imekuwa ikimnyatia Martinez kwa zaidi ya mwaka huku Barcelona na Real Madrid pia zikionesha nia ya kumtaka mchezaji huyo, 23. (Sunday Mirror)
Chelsea "inatathmini" ikiwa itamsajili mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi kama mchezaji huyo, 33, ataondoka timu ya mabingwa Uhispania Barcelona. (Spanish football expert Guillem Balague, via Sunday Express)

Mkuu mtendaji wa Inter Milan Giuseppe Marotta amesema kuwa kiungo wa kati wa Denmark Christian Eriksen, 28, ataondoka klabu hiyo Januari wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa. (Sky Sports)
Philippe Coutinho ameiwakilisha Brazil mara 55

Ajenti wa kiungo wa kati mshambuliaji wa Brazil Philippe Coutinho anasema mchezaji huyo, 28, hana mpango wa kuondoka Barcelona baada ya kuhusishwa na upande wa Italia Juventus. (Mundo Deportivo - in Spanish)

Ajenti wa Domenico Berardi wa Sassuolo anasema mshambuliaji huyo wa Italia thamani yake ni euro milioni 50 na kwamba mchezaji huyo, 26, hana mpango wa kulazimisha kuondoka upande wa Serie A. (Football Italia)
Mshambuliaji wa Inter Milan Lautaro Martinez

Mshambuliaji wa Argentina Lautaro Martinez anataka kuondoka Inter Milan na amemuweka ajenti wake Jorge Mendes kusimamia utafutaji wa klabu mpya atakayo hamia. (Marca)

Watu sita wameonesha nia ya uwezekano wa kununua klabu ya West Bromwich Albion lakini mmiliki wa klabu hiyo Guochuan Lai huenda akawa na wakati mgumu wa kufikia lengo lake la kuiuza kwa pauni milioni 150 kwa klabu hiyo ya Ligi ya Premier. (Mail on Sunday)
Mkurugenzi wa michezo wa Borussia Dortmund Michael Zorc anasema anatazamia kumuona mshambuliaji wa Norway Erling Braut Haaland katika klabu hiyo "kwa muda mrefu". Nyota huyo aliye na miaka 20- ana mkataba na klabu hiyo ya Bundesliga hadi mwaka 2024, lakini anaweza kuondoka kwa euro milioni 75 (£67m) mwaka 2022 kwasababu ana kifungu kinachomruhusu kufanya hivyo katika mkataba wake wa sasa. (Bild Sport - in German)

Winga Muingereza Angel Gomes, 20, anasema aliondoka Manchester United 'kutafuta mwanzo mpya' baada ya kukataa ofa yao na kujiunga na Lille. (Independent)

Matej Vydra (Kulia) amekuwa na Burnley tangu mwaka 2018

Mshambuliaji wa Burnley na Jamhuri ya Czech Matej Vydra, 28, anataka kuondoka Turf Moor ili kupata nafasi ya kucheza soka ya kikosi cha kwanza. (Accrington Observer)

Mkufunzi wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson ameahidi kuongeza msaada wake wa chakula kwa shirika la watoto na kutoa wito kwa wachezaji zaidi wa soka kumsaidia mshambuliaji wa England na United Marcus Rashford, 23, katika kampeni yake ya kuwakinga watoto dhidi ya njaa. (Times - subscription required)

Mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford anasema kusaidia watoto "ni muhimu sana" wakati wa Janga la corona

Beki wa kushoto na nyuma wa Argentina Nicolas Tagliafico ambaye amehusishwa na Chelsea na Manchester City, amekubali kurefusha mkataba wake na Ajax ambayo unatarajiwa kumfanya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kusalia katika klabu hiyo hadi angalau mwisho wa msimu . (De Telegraaf - in Dutch)

Kipa wa Fulham Marcus Bettinelli, 28, ananyatiwa na klabu kadhaa za Ligi ya Primia. Kipa huyo ambaye kwa sasa yuko Middlesbrough kwa mkopo alijumuishwa katika kikosi cha kitaifa cha England na Gareth Southgate mwaka 2018. (Mail)

CHANZO- BBC SWAHILI

Share:

HIKI NDIYO KIJIJI MAARUFU CHENYE WATU WENYE SURA MBAYA ZAIDI DUNIANI


Piobbico Itali: Kijiji kinachowasherehekea watu wenye sura mbaya zaidi duniani

Kijiji kimoja kinachofahamika kama Piobbico kimekuwa maarufu kwa kuwa na watu wenye sura mbovu zaidi duniani na kwa sasa dhana hiyo imekifanya kuwa maarufu zaidi duniani.

Kijiji hicho ambacho kimekuwa kikienzi utamaduni huu kwa miaka 140 sasa, kiko katikati ya milima ya Apennine na bahari ya Adriatic katikati mwa Italia.

Piobbico ni kijiji cha zamani kilichozungukwa na majengo ya matofali na misitu iliyostawi. Lakini licha ya muonekano wake wa kuvutia, kijiji hicho kinafahamika sana kwa kuwa na watu wenye sura mbaya zaidi duniani.

Tangu mwaka 1879, kijiji hichi chenye watu karibia 2,000 kiliunda chama kwa jina ''Club Dei Brutti'' cha watu wa kutisha na kinaamini kwamba ''mtu ni vile alivyo wala siyo vile anavyoonekana''.

Wazo hilo lilianza zamani na kuchukuliwa kama wazo la kawaida tu lakini limegeuka na kuvutia ulimwengu kiasi kwamba watu wengine wanaomini kwamba wanasura mbaya zaidi pia nao wanatuma maombi ya kutaka kujiunga na chama hicho.

Wakati huu, chama hicho kinajumuisha watu karibia 30,000 kote duniani.

Namna ya kujiunga na chama chenye watu wa sura mbovu zaidi duniani

Chama hicho cha Club Dei Brutti awali kiliundwa kwa ajili ya wanawake wasio na wachumba.

Lakini kadiri siku zilivyoendelea kusonga mbele, wanavijiji walichukua jukumu na kukumbusha jamii kwamba uzuri wa ndani ni muhimu zaidi kuliko unaoonekana kwa nje na mwaka 2007, kijiji cha Piobbico kikazindua kinyago kwa ajili ya watu wenye sura mbaya kwenye eneo hilo.

Leo hii, ni rahisi kabisa kwa mtu kujiunga na chama hicho. Wachohitajika kufanya wanachama waandamizi ni kuchagua sura ya anayetaka kujiunga kama ni mbaya kiasi cha kuridhisha na kutazama watakuweka katika kundi gani. 

Makundi yamegawanywa kuanzia lile la kutisha kidogo hadi la watu wanaotisha kisawa sawa.

Hata hivyo chama hicho kimeamua kutojikita zaidi katika ubaya wa sura badala yake kuangalia uzuri wa moyoni bila kujali kile watu wanachokifikiria kukuhusu.

Jumapili ya kwanza ya Septemba 2019, wanachama kutoka kila pembe ya dunia walikusanyika katika kijiji cha Piobbico kwa ajili ya tamasha la mtu mwenye sura mbaya zaidi duniani na kumchagua rais wa chama hicho, wakasajili wanachama wapya na kula vyakula vya eneo kama vile kuvu, aina ya ugali na tambi.

Katika nchi ambayo inatilia mkazo zaidi kuhakikisha unaonekana mzuri, kijiji hiki kinathibitisha kwamba mtu anatakiwa kujithamini vile alivyo na kufurahia uhalisia bila kujali ubovu wa sura mbako vilevile, bado kutavutia wengi.

CHANZO- BBC SWAHILI
Share:

TIGO YAENDELEA KUKABIDHI ZAWADI ZA SIMU KWA WASHINDI MBALIMBALI WA #JAZATUKUJAZETENA


TunakabidhiTena: Tigo yaendelea kukabidhi zawadi za Simu kwa washindi mbalimbali wa #JazaTukujazeTena ambapo wateja hujishindia pia bonus za dakika, MB na SMS na kubwa zaidi kupata Simu Janja. 

"Bado tunaendelea kutoa simu kwa wateja wetu ikiwa ni ishara ya shukrani kwa kuwa pamoja nasi katika kipindi chote. Wanachotakiwa kufanya ni kununua kifurushi wapate bonus na zaidi wanaingia kwenye droo ambapo wanaweza kushinda simu janja mbalimbali" Joseph Mutalemwa-Mkurugenzi wa Tigo kanda ya pwani. @jotiofficial
"Mbali na Bonus wanazojipatia wateja wetu kila siku pindi wakijiunga kifurushi pia wanajiwekea nafasi ya kushinda simu janja ikiwemo Samsung Note 20 yenye thamani ya zaidi ya milioni 2" Joseph Mutalemwa-Mkurugenzi wa Tigo kanda ya pwani.
Amani Adami kutoka Kiwalani Dar es salaam ndiye mshindi wa Samsung Note 20. Mshindi mmoja kati ya watatu wa wiku hii. Ukiwa na Tigo wewe ni mshindi.
Nunua kifurushi chochote na Tigo itakupa Bonus za Dakika, SMS na Mb's na kubwa zaidi utajiwekea nafasi ya kushinda smartphone kila siku. #ItelT20 #TecnoKitochi4G kumi kila siku na #SamsungNote20 Tatu kila wiki. Joseph Mutalemwa -Mkurigenzi wa Tigo kanda ya Pwani pamoja na @jotiofficial wakimkabidhi simu.
"Huu mzigo ukiibiwa huu lazima uweke msiba huu maana ni balaa, bei yake ni balaa" @jotiofficial

Ukinunua kifurushi Tigo unapata Bonus za Dakika, SMS na MB's na zaidi unajiwekea nafasi ya kushinda smartphone #ItelT20 #TecnoKitochi4G kumi kila siku na #SamsungNote20 tatu kila wiki.
Mama Kashinda! Hongera wewe ni mmoja wa washindi wa Itel T20 wiki hii @jotiofficial Bado wengine Wengi..
Nunua kifurushi chochote na Tigo itakupa Bonus za Dakika, SMS na Mb's na kubwa zaidi utajiwekea nafasi ya kushinda smartphone kila siku. #ItelT20 #TecnoKitochi4G kumi kila siku na #SamsungNote20 Tatu kila wiki.
BURE: Ukinunua kifurushi kutoka Tigo unapata Bonus ya MB, SMS au Dakika na zaidi unapata Burudani kali kutoka kwa wasanii kibao kwenye tamasha la Wasafi Tumewasha na Tigo kesho uwanja wa Taifa-Kahama.
Piga *147*00# kujiunga. @wasafitv


Share:

RAIS MAGUFULI AFANYA UTEUZI WA WABUNGE...YUMO HUMPHREY POLEPOLE



Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili Novemba 29



Share:

Saturday, 28 November 2020

TAMASHA LA 'SIMIYU JAMBO FESTIVAL' LATIKISA BARIADI...KILANGI ATAKA WANANCHI WASHIRIKI MICHEZO KUIMARISHA AFYA


Baadhi ya waendesha baiskeli wanawake wakiondoka eneo la kuanzia mashindano ya baiskeli kilomita 80 Salunda Mjini Bariadi, Mashindano yaliyofanyika wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Paul Michael kutoka mkoani Shinyanga akishangilia baada ya kuibuka mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kilomita 140 wanaume katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga akimkabidhi zawadi ya fedha taslimu shilingi 600,000/= mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kilomita 80 wanawake, Bi. Laurencia Luzuba kutoka mkoani Mwanza , katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washindi nane wa kwanza katika mashindano ya mbio za baiskeli kilomita 80 wanawake, wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Duba Masunga kutoka Mkoa wa Simiyu Mshindi wa tatu mbio za baiskeli kilomita 140 wanaume akipokea zawadiya fedha taslimu shilingi 500,000/= kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ), wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Baadhi ya viongozi, watumishi na wananchi wa mkoa wa Simiyu wakikimbia mbio fupi za kilomita tano katika ufunguzi wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA) Dkt. Amir Batenga akimkabidhi Emmanuel John zawadi ya fedha taslimu shilingi 200,000/= baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika mbio za baiskeli kilomita tano (kwa watu wenye ulemavu), wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (katikati walioketi) ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo(kushoto), Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga na washindi nane wa mbio za baiskeli kilometa 140 wanaume, wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Kwiyeya Buluba mwanafunzi wa Kidato cha kwanza kutoka shule ya sekondari Simiyu, akipokea zawadi ya fedha taslimu kutoka kwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ), mara baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika uandishi wa isha, wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Ngoma za asili kutoka kundi la Wagalu wakitoa burudani wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi. 

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Mhe. Benson Kilangi ametoa wito kwa wananchi na viongozi mkoani Simiyu kuona umuhimu wa kushiriki michezo kwa ajili ya kuimarisha afya.

Kilangi ameyasema hayo Novemba 28, 2020 katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, likihusisha mashindano ya baiskeli, mbio fupi , ngoma za asili na mashindano ya taaluma kwa wanafunzi wa shule za sekondari; alipokuwa akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.

"Hii michezo tunayoifanya pamoja na kwamba ni burudani tunapaswa kuelewa kwamba michezo ni afya; ni wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anashiriki michezo, siyo lazima iwe kama hii tu, hata nyumbani tunaweza kufanya mazoezi madogo madogo kama kukimbia, kuruka kamba na mengine kwa afya," alisema Kilangi.

Aidha, Kilangi aliongeza kuwa michezo ni ajira kwakuwa wapo watu wanajipatia vipato kupitia michezo na vile vile michezo ni biashara na inasaidia kujenga mahusiano na undugu katika jamii.

Akizungumzia Kauli Mbiu ya Tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2020 inayosema, “WAWEZESHE WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE ILI KUWA NA DUNIA BORA” Kilangi amesema ni vema watoto wa kike na wanawake wakawezeshwa kwa kuwa ni wakombozi wa familia na ndiyo wanaorudisha maendeleo nyumbani kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na wanaume.

Katika hatua nyingine Kilangi ametoa rai kwa wadau wakashirikiana na mkoa wa Simiyu kuona namna ya kuwa na matamasha yanayohusu michezo, sanaa na utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuendelea kuujenga Mkoa wa Simiyu katika nyanja mbalimbali.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga amesema kwa sasa Tamasha hilo limekuwa likishirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, huku akibainisha kuwa nia ya Mkoa ni kupata washiriki wa ndani na nje ya nchi ili litumike pia katika kutangaza na kukuza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Simiyu.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani ( UNFPA) ambao ndiyo wadhamini wakuu, Dkt. Amir Batenga amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na mkoa wa Simiyu katika masuala mbalimbali ya kuwawezesha watoto wa kike na wanawake katika nyanja mbalimbali kama kauli mbiu ya tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2020 inavyosema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), Mhe. Lucy Sabo ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa maandalizi mazuri na kutoa rai kuwa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liwe endelevu kwa ajili ya kuinua vipaji kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika utamaduni, sanaa na michezo.

Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival ambalo linafanyika kwa mara ya tatu mkoani Simiyu, wamewashukuru waandaji kwa maandalizi mazuri na ambapo wamebainisha kuwa mwaka huu ulinzi umeimarishwa zaidi.

"Tunawapongeza waandaaji mwaka huu mashindano ni mazuri, Ulinzi umeimarika sana kuanzia tulipoanza, njiani kote mpaka tulipofika eneo la kumalizia, kwa hali ilivyokuwa hakuna ambaye angeweza kubebwa kwa namna yoyote ile ili kutafutiwa ushindi," alisema Paul Michael mshindi wa kwanza mbio za baiskeli wanaume kilomita 140.

Katika mashindano ya baiskeli washiriki kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga wameonekana kung'ara zaidi ambapo Paul Michael kutoka Shinyanga ameibuka mshindi na kujinyakulia kitita cha shilingi 800,000/= na Laurencia Luzuba ameongoza upande wa wanawake na kujinyakulia shilingi 600,000/= , upande wa walemavu Emmanuel John kutoka Simiyu ameibuka kidedea na kujipatia kitita cha shilingi 200,000/=
Share:

TAMWA YAONESHA NJIA YA KUMALIZA UDHALILISHAJI ZANZIBAR

Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali kisiwani Pemba wakionesha bango lenye ujumbe wa kukataa kupinga vitendo vya udhalilishaji katika viwanja vya Gombani ya kale Pemba.
***

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa kusini Pemba  Rashid Khadid Rashid ameelezea kutoridhishwa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya mahakama, polisi pamoja na wanaharakati wanaoshiriki kufanya suluhu dhidi ya kesi za udhalilishaji na kusema hali hiyo inachangia kukwamisha juhudi za serikali za kuyatokomeza matendo hayo.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja wa Gombani kisiwani Pemba yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar).

Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka kamati za kupinga udhalilishaji za wilaya kushirikiana na Ofisi ya Mufti kutoa elimu ya ndoa kwa wanandoa  pamoja na sehemu zenye mikusanyiko ya watu ikiwemo maskulini.

Amesema kesi nyingi za udhalilishaji zinashindwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka kutokana na kuwepo na baadhi ya watumishi wa vyombo vinavyosomamia sheria kukosa uadilifu.

“Miongoni mwa mambo yanayochangia kesi hizi ziendelee kutokea ni uwepo wa baadhi ya watumishi ambao sio waadilifu wanaoshiriki kufanya suluhu, pamoja na hukumu ndogo zinazotolewa dhidi ya watuhumiwa,”alisema.

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa matukio hayo Kisiwani Pemba amesema bado tatizo hilo lipo kwa kiwango kikubwa katika jamii licha ya matukio hayo kuanza kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita ikiwa ni kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na wanaharakati mbalimbali wakiwemo TAMWA Zanzibar.

“Naomba niiambie hadhira hii kuwa vitendo vya udhalishaji bado ni tatizo kubwa na matukio haya yanaripotiwa kila siku katika jamii zetu, kwa mwaka huu hadi sasa tuna  kesi 218 ambazo zinafanyiwa kazi ktika ngazi mbalimbali ambapo kwa wilaya ya Wete ni 57, Micheweni 30, Chake Chake 84, na Mkoani 47 ambapo kesi za ubakaji ndizo zinazoongoza kwa wingi katika kesi hizi.” alisema.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said amesema lengo la kuandaliwa kwa mazoezi hayo ya hiari ya siku moja ni kubadilisha tabia hasa za vijana dhidi ya fikra potofu za kubaka na kudhalilisha kwa ujumla kupitia ufanyaji wa mazoezi.

“TAMWA Zanzibar kwa kuwa ni wadau wakubwa wa kupambana na udhalilishaji wa wanawake na watoto tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kufanya mazoezi ya hiari ili kupaza sauti za wanyonge kupitia kampeni  ya siku 16 za  kuhamasisha  jamii  kubadili tabia juu ya ukatili wa mtoto wa kike.''

Katika hatua nyingien Mratibu huyo amesema, TAMWA itaendelea kushirikiana wadau mbali mbali, ili kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi bila ya ukatili na udhalilishaji.

Akitoa salama za wanawake, Mkuu wa Idara ya wanawake Pemba, Mwanaisha Ali Massoud, alisema siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike ni muhimu kwa jamii, ili kutafakari namna ya kuyakinga makundi hayo dhidi ya ukatili.

Alisema, udhalilishaji na ukatili huathiri sana wanaofanyiwa ikiwa ni pamoja na kukatisha ndoto zao ziwe na kielimu au biashara kutokana athari zake.

Alisema, “njia rahisi ya kupambana na matendo hayo ni kwa jamii kuondoa muhali na kushirikiana na vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja Polisi na mahakama.”

Tatu Abdalla Msellem kutoka jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE)ametoa wito kwa taassi na idara za serikali kuongoeza ushirikiano na asasi za kiraia hasa suala la upatikanaji wa takwimu ili kufanikisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

“Ili kufanikisha kupiga vita matendo hayo, wakati mwengine tunapoomba miradi huhitaji takwimu, ili kupata ithibati, lakini huwa vigumu, sasa lazima hili lionekane na liondolewe,’’aliesema.

Awali kwenye mkutano huo ulinogeshwa na kikundi cha mazoezi cha Gombani, usomaji wa utenzi pamoja na mchezo wa kuigiza kutoka kundi cha ‘Thesode’ la Ngwachani wilaya ya Mkoani Pemba.

Maadhimisho ya siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto huadhimishwa kila ifikapo tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba ya kila mwaka ambapo Ujumbe wa mwaka huu ni TUPINGE UKATILI WA KIJINSIA , MABADILIKO YAANZE NA MIMI. Sambamba na ujumbe maalum wa TAMWA ZNZ ‘Fanya mazoezi zuia mihemuko: Muache mtoto wakike salama.


Share:

MTATURU AANZA KUTEKELEZA AHADI ZA WANANCHI KWA KASI YA 4G

 

Wachungaji na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kiaskofu Msalaba Mrefu mjini Singida, wakiwa na pikipiki walizokabidhiwa hivi karibuni na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu kwa ajili ya kazi za kanisa hilo,
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mkuu wa Jimbo la Kusini Usharika wa Issuna, Mchungaji, Obedi Msele.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mchungaji Joyce Madadi wa Usharika wa Ikungi.
 Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mchungaji, Felix Kibiriti.


Na Dotto Mwaibale, Singida.

MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameanza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa kasi ya 4G.

Mtaturu ametekeleza ahadi yake  kwa kutoa pikipiki tano kwa Usharika wa Kiaskofu Msalaba Mrefu mjini Singida ambazo alimkabidhi Mchungaji Felix Kibiriti kwa niaba ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati Dkt. Alex Mkumbo kwa ajili ya matumizi ya shughuli mbalimbali za kanisa hilo mkoani Singida.

Mbali ya kukabidhi pikipiki hizo zenye thamani ya sh.milioni 11, Mtaturu pia alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo pikipiki mbili zenye thamani ya sh.milioni 4.6 kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Wilaya hiyo ili ziweze kusaidia kwa kazi.

Akizungumza hivi karibuni katika hafla ya kukabidhi pikipiki hizo Mtaturu alisema utoaji wa pikipiki hizo ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kusaidia kanisa hilo kupata usafiri wa uhakika kwa watumishi wake wanapo kwenda kuhubiri neno la Mungu.

 "Nitaendelea kutimiza ahadi zangu na kushirikiana na wananchi kwa kasi ili kuunga mkono jitihada ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutekeleza miradi ya maendeleo" alisema Mtaturu.

Aidha Mtaturu alisema kuwa pikipiki hizo zitatumika katika sharika za Mang'onyi, Issuna, Mungaa na Ikungi zilizopo Jimbo la Singida Mashariki.

 Mtaturu alitoa ahadi hiyo Novemba 8, 2020 wakati akizindua kitabu cha Misemo na Methali za Wanyaturu kilichoandikwa na Mchungaji Dkt.Syprian Yohana Hilinti (PhD) kilichozinduliwa katika Kanisa Kuu la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Singida mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi huko mshereheshaji katika hafla ya  uzinduzi wa kitabu hicho akiwa ni Mbunge wa Iramba  Mwigulu Nchemba.

Share:

TARURA YADHAMIRIA KUUNGANISHA WILAYA YA RUANGWA NA LIWALE

Ujenzi wa Daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa Mita 75 lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi linalojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ukiwa unaendelea. Daraja hili ni mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale kwa lengo la kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
**


Na Bebi Kapenya - Lindi

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi ikiwemo ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa mita 75 linalojengwa katika barabara ya Chikwale hadi Liwale kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.5.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Nalupi alisema mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru umetokana na mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale kwa lengo la kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo na kuwezesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa haraka.

“Wilaya hizi mbili ni maarufu sana katika kilimo cha korosho na ufuta, lakini pia wananchi wa vijiji vya Nangurugai, Mirui, Narungombe, Machang’anja na Chikwale watapata faida ya kiuchumi kwasababu mazao yao ya biashara yataweza kuvushwa kutoka upande wa Liwale kwenda Ruangwa ambapo kuna soko kubwa la mazao ya biashara pale Ruangwa mjini”, alisema Meneja huyo.

Mhandisi Nalupi alieleza kuwa hadi sasa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imeshapokea fedha Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru na ujenzi utakuwa wa Awamu II ambapo Awamu ya I itakuwa ujenzi wa daraja lenyewe kwa kutumia Mkandarasi anaitwa Nyumbani Construction Company Limited kwa mkataba wa Bilioni 1.6 na Awamu ya II itakuwa ni ujenzi wa Makalavati makubwa upande wa Liwale kwa Mkandarasi anaitwa Lumo Cones ambaye ameshaingia mkataba na ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni.

Naye, Bw. Abdallah Nampundai Mkazi wa Ruangwa ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo kwani utanufaisha wananchi kusafirisha mazao yao na kufanya biashara zao.

“Kwa sisi wafanyabiashara na wakulima tunatoa mazao yetu kutoka Ruangwa kupeleka Liwale na tunatoa Liwale kupeleka Kilwa hivyo kukamilika kwa daraja hili kutatusaidia sana kupitisha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Bw. Nampundai.

Kwa upande wake, Bw. Leonard Abel Mkazi wa Kijiji cha Nangurugai ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakapokamilika litarahisisha usafiri kwasababu wanapata changamoto nyingi mvua ikinyesha ikiwemo kupoteza ndugu zao kwavile Mto huo una mamba wengi hasa kipindi cha mvua hivyo kukamilika kwake kutawasadia sana kwenye suala la usafiri.



Mbali na ujenzi daraja la mto Mbwemkuru, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imekamilisha ujenzi wa Barabara za Lami Ruangwa mjini jumla ya Kilomita 8.32 kwa fedha za Mfuko wa Barabara pamoja na fedha za mradi wa Mfuko wa Umoja wa Ulaya, pia wameweka taa za barabarani jumla ya Km 7.62 mradi uliofadhiliwa na REA (Wakala wa Umeme Vijijini).

Aidha, Meneja huyo alisema kuwa wameweza kuunganisha sehemu kubwa ya Mji wa Ruangwa kwa barabara za Lami ambapo imeweza kurahisisha mawasiliano kwa watumiaji wa barabara na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo kwavile biashara zimeendelea kufanyika hadi nyakati za usiku kwasababu ya uwepo wat aa za barabarani.

TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inaendelea na kazi mbalimbali za kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi.
Share:

KAMATI YA USALAMA WILAYA YA IKUNGI SINGIDA YAKAGUA MIRADI YA ELIMU NA AFYA

 

Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakijadiliana wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Elimu na Afya wilayani humo. Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.
Moja ya chumba cha darasa kilicho kaguliwa na kamati hiyo.
Baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa.
Muonekano wa vyoo vya Shule ya Msingi vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Ukaguzi ukiendelea. 

Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua ujenzi wa Chuo cha Veta. Kushoto mbele ni  Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.


Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.


Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.


Moja ya chumba cha darasa cha shule ya sekondari kilicho kaguliwa na kamati hiyo.


Jengo la Maabara lililokaguliwa na kamati hiyo.


Muonekano wa vyoo vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.



Na  Mwandishi Wetu, Ikungi


KAMATI ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Elimu na Afya ambapo mbali na kupongeza usimamizi wa fedha zilizoletwa na Serikali juu ya miradi hiyo, iliwataka baadhi ya wasimamizi wa miradi hiyo kukamilisha kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wa miradi ya Elimu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Edward Mpogolo, alisema ni lazima madarasa na vyoo vikamilike kwa wakati ili yaanze kutumika mapema mwakani na kuondoa changamoto ya vyumba vya madarasa iliyokuwepo kwenye shule hizo .

Aidha pamoja na mapungufu machache yaliyobainishwa na kamati wakati wa ukaguzi, kamati iliridhishwa na miradi hiyo kwa kuwa thamani ya fedha za serikali katika miradi inaonekana ambapo pia ilimtaka Mhandisi wa Halmashauri kuhakikisha anasimamia  maboresho na mapungufu yaliyojitokeza na kutoa msaada wa kitaalamu kwa kila mradi uliokutwa na dosari. 

Kwa shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, Mpogolo alizielekeza Serikali za vijiji na Kamati za Maendeleo ya Kata kuanza mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo na kuongeza kuwa serikali itaunga mkono katika ukamilishwaji wa majengo ya shule hizo huku akiagiza afisa Mipango Miji na Mhandisi wa wilaya kukagua na kupima maeneo yote yenye shule shikizi na kupeleka mapendekezo  katika vikao vya halmashauri juu ya ukamilishwaji wa shule hizo.

Katika mradi wa ujenzi wa  Hospitali ya Wilaya, Mpogolo, aliitaka kamati ya ujenzi iliyoteuliwa na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya usimamizi wa mradi ambao unaendeshwa kwa mfumo wa  “Force Account” kuhakikisha wanakuwepo  eneo la mradi kila siku kwa ajili kushauri kitaalamu na kusikiliza changamoto ambazo mafundi wanakumbana nazo wakati wa ujenzi. 

Alisisitiza mradi huo, ambao ulitengewa kiasi cha sh. Bilioni 1.5 unatakiwa ukamilike kwa wakati na kwa thamani halisi kama ambavyo iliagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, katika ziara yake ya kampeni, ambapo alitoa siku 60 ili kukamilika kwa mradi huo na kuahidi kufika kwa ajili ya uzinduzi.

Katika ziara hiyo ya siku tatu, kamati pamoja na wataalamu wa halmashauri walitembelea na kukagua miradi yote ya Afya na Elimu inayotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi katika mwaka wa fedha 2019/2020  na  yote ikiwa na thamani ya zaidi ya  sh. Bilioni 4.5.

Wakati huo huo, mkuu wilaya hiyo amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kuchunguza taratibu zote za ujenzi wa Madarasa Matatu na vyoo vya Shule ya Msingi Matongo baada ya kubainika ukiukwaji wa taratibu mbalimbali za ujenzi. 

Ukiukwaji huo ulibainika baada ya kamati ya usalama kufika katika shule hiyo kukagua ujenzi unaoendelea wa madarasa na vyoo hivyo na kubaini mapungufu mengi na hivyo, Mpogolo kuagiza kufanyika kwa uchunguzi na ikibainika hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika wote wa usimamizi wa mradi huo na katika kipindi hicho cha uchunguzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo amtafute mwalimu atakaekaimu nafasi ya mwalimu mkuu.

Hata hivyo, Kamati ya Usalama ilimshukuru Rais Magufuli kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya 4.5 bilioni za maendeleo kwa muda mfupi. Pia imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justice Kijazi, kwa kuendelea kusimamia vizuri fedha ya serikali katika miradi inayoletwa katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. 

Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari na msingi, mabweni, mabwalo, ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyoo, maabara na ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Veta.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger