Na Neema Nkumbi, Kahama
Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa ajili ya kuwakopesha wasanii nchini, hatua inayolenga kuinua vipaji, kukuza sekta ya ubunifu na kuwawezesha vijana kiuchumi.
Akizungumza katika mafunzo ya uelimishaji kuhusu namna ya kupata mikopo hiyo yaliyofanyika leo februari 18, 2026 katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Afisa wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Jovita Godwin, amesema mfuko huo unatoa fursa kwa wasanii wa nyanja mbalimbali ikiwemo muziki, filamu, sanaa za maonyesho, fasihi na ufundi wa kazi za sanaa ili waweze kukuza kazi zao na kufikia malengo yao ya kisanaa na kibiashara.
Amesema serikali imekusudia kuona sekta ya sanaa inakuwa chanzo cha ajira na mapato kwa vijana wengi, hivyo amewahimiza wasanii wa Kahama kujitokeza kwa wingi na kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili wanufaike na mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela, amesema halmashauri imejipanga kuibua na kukuza vipaji kupitia matamasha, makongamano na ziara katika kata mbalimbali kwa lengo la kuwatambua wasanii na kuwaunganisha na fursa zinazotolewa na serikali.
Naye Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki Mataluma, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi kwa vijana, akiwataka wasanii kutumia mikopo hiyo kama chachu ya maendeleo yao binafsi na ya taifa.
Baadhi ya wasanii waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kuanzisha mfuko huo wakisema utawasaidia kupanua shughuli zao za kisanaa, huku wakiiomba serikali kuendelea kuboresha masharti ya mikopo ili kuwafikia wasanii wengi zaidi.


















0 comments:
Post a Comment