Monday, 3 August 2026

MBUNGE WA JIMBO LA ITWANGI AZZA HILLAL HAMAD ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI BUTINI

 

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wazee kwenye kijiwe cha Kahawa Butini na kusikiliza kero zao na kuzitolea majibu.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amefanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Butini Kata ya Itwangi Wilaya ya Shinyanga, wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitolea majibu.

TAZAMA VIDEO HAPA👇👇



Akizungumza leo Agosti 3, 2026, wakati wa mkutano huo, amesema baadhi ya kero tayari ameshazifanyia kazi, ikiwamo ukarabati wa barabara ya Itwangi–Mwakasomwe–Welezo, ambapo amesema mkandarasi tayari amepatikana na utekelezaji wa mradi huo utaanza muda wowote.

Pia amesema, barabara ya Butini–Nsalala, ambayo daraja lake lilikatika na kuchukua takribani miaka sita hadi saba bila kutengenezwa, sasa inakwenda kujengwa baada ya kazi hiyo kutangazwa rasmi, huku makalavati yakitarajiwa kujengwa katika maeneo husika.
“Nimekuja kusikiliza kero zenu ambazo ndizo vipaumbele vyenu, na kabla ya kuanza kusikiliza kero zenu, baadhi tayari nimekwisha anza zifanyia kazi zikiwama za ubovu wa miundombinu ya barabara na madaraja,” amesema Azza.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, amesema tayari ameshaliwasilisha suala hilo kwa Waziri husika, na pia alilizungumzia bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maji.
Aidha, amesema ataendelea kupigania kuboreshwa kwa huduma za afya katika Jimbo la Itwangi, akieleza kuwa ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wananchi watashuhudia mabadiliko makubwa katika Jimbo hilo.


“Jimbo la Itwangi lina kata 14, lakini lina vituo vya afya viwili tu. Tuna vijiji 58, lakini zahanati zinazotoa huduma ni 23 pekee, ninaamini ndani ya miaka mitano kutakuwa na mabadiliko makubwa chini ya uongozi wa Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana aliligawa jimbo hili ili kuharakisha maendeleo,” amesema Azza.
Katika hatua nyingine, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Butini, Nsalala na Jimbo la Itwangi kwa ujumla, akisema ndani ya kipindi cha miezi sita tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Baadhi ya wananchi wa Butini waliowasilisha kero zao katika mkutano hu, wamelalamikia ukosefu wa maji safi na salama, uchakavu wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji, ukosefu wa nyumba za watumishi wa afya, kutofikishwa kwa huduma ya umeme katika baadhi ya vitongoji, pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, makalavati na madaraja.

TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akiwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi Rais Dk. Samia Suluhu Haasan katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, pamoja na kumpigia kula yeye na Diwani wa Itwangi Ldya Pius.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wazee kwenye kijiwe cha Kahawa Butini na kusikiliza kero zao na kuzitolea majibu.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wazee kwenye kijiwe cha Kahawa Butini na kusikiliza kero zao na kuzitolea majibu.
Diwani wa Itwangi Lidya Pius akizungumza.
Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mkola Kabali akizungumza.
Diwani wa Viti maalumu Anastazia Njile akizungumza.
Share:

MZUMBE YATOA USHAURI WA UCHAGUZI WA KOZI KATIKA KAMBI YA UDAHILI MLIMANI CITY


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu Mzumbe kimewahimiza wanafunzi na wazazi kutumia fursa ya kambi maalumu ya udahili inayoendelea katika viwanja vya Mlimani City ili kupata ushauri wa kitaaluma na kufanya maamuzi sahihi kuhusu uchaguzi wa kozi za masomo ya juu.

Akizungumza katika kambi hiyo leo Agosti 2, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Aziza Juma, amesema huduma zinazotolewa zinajumuisha elimu kuhusu uchaguzi wa kozi, vigezo vya kujiunga na chuo, ushauri wa kitaaluma pamoja na udahili wa papo kwa papo kwa waombaji wanaokidhi sifa.

Amesema kambi hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi kuelewa kwa kina kozi zinazotolewa na chuo na kuhakikisha wanaomba programu zinazolingana na sifa walizonazo.

"Tunatoa ushauri kuhusu uchaguzi wa kozi kwa sababu baadhi ya wanafunzi huomba programu ambazo haziendani na masomo waliyosoma shule, diploma au cheti. Tunawasaidia kufanya uchaguzi sahihi kulingana na sifa zao," amesema Aziza.

Ameongeza kuwa kambi hiyo pia ni fursa ya kuhamasisha jamii kufahamu programu mbalimbali zinazotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe, kwani bado kuna watu wengi hawana taarifa za kutosha kuhusu fursa za masomo zinazopatikana chuoni hapo.

Kuhusu programu za teknolojia, amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha masomo yanayohusiana na sayansi na teknolojia ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa.

"Teknolojia ndiyo mwelekeo wa dunia ya leo. Tunawahamasisha vijana kujiandaa kwa kuchagua kozi zitakazowawezesha kupata ujuzi wa kisasa, kuchangia maendeleo ya jamii na kushindana katika soko la ajira," amesema.

Aziza amesisitiza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kutoa elimu na ushauri kwa waombaji ili kuhakikisha wanafanya uchaguzi sahihi wa taaluma unaoendana na ndoto na uwezo wao wa kitaaluma.

Kambi hiyo imeanza Julai 28 hadi Agosti 3, 2026 ambapo hadi sasa muitikio unaridhisha kwa wananchi ambao wamepata fursa ya kutembelea eneo hilo na kupatiwa huduma.

Baada ya hapo zoezi litaendelea katika kampasi za Morogoro, Mbeya na hapa Dar es Salaam hivyo wazazi walezi wasisite kutembelea kampasi au kuomba online. 

Share:

Sunday, 2 August 2026

WAZIRI KAPINGA: UWEKEZAJI WA AZANIA GROUP UTAONGEZA AJIRA NA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA


Serikali imeipongeza Azania Group kwa kutimiza miaka 25 ya mafanikio katika sekta ya viwanda na biashara, huku ikieleza kuwa kampuni hiyo imeendelea kuwa mfano wa uwekezaji wa wazawa baada ya kutangaza mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi trilioni moja katika miradi mbalimbali ya uzalishaji nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Judith Kapinga (Mb) wakati akizindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Azania Group yaliyofanyika Agosti 01, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Kapinga amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika utekelezaji wa agenda ya uchumi wa viwanda.

Aidha, kukuza kwa uwekezaji huo unaonesha imani kubwa ya sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania na utaongeza ajira, kukuza uzalishaji wa viwandani, kuinua kipato cha wakulima na kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa kipindi cha robo karne, Azania Group imejijengea rekodi ya mafanikio kupitia uwekezaji katika viwanda, uongezaji wa thamani ya malighafi za ndani, utoaji wa maelfu ya ajira na mchango mkubwa katika mapato ya Serikali kupitia kodi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR, bandari, barabara, nishati na TEHAMA, hatua zilizopunguza gharama za uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Kapinga amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Hivyo amewataka wawekezaji kuendelea kuwekeza katika teknolojia, tafiti na ubunifu ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuifanya Tanzania kufikia azma ya kuwa uchumi wa dola trilioni moja.

Hata hivyo Waziri Kapinga ameipongeza Azania Group kwa mafanikio ya miaka 25 na kueleza kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya Shilingi trilioni moja ni hatua muhimu itakayochochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger