Thursday, 10 November 2022
CHADEMA WAPINGA TUME YA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA UCHUNGUZI BWAWA LA MGODI WA MWADUI KUPASUKA, TOPE KUZAGAA KWA WANANCHI
Muonekano wa Tope likiendelea kusambaa kwenye makazi ya watu, mara baada ya bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui Kupasuka leo asubuhi, na kusababisha athari kwa wananchi
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) MKOA WA SHINYANGA.
TAARIFA KWA UMMA
*Tamko la kupinga uundwaji wa Tume ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kuchunguza kupasuka na athari za kimazingira kwa Bwawa la Maji machafu la Mgodi wa Almasi wa Mwadui.*
Mnamo tarehe 07.11.2022 Bwawa la kuhifadhia maji machafu la mgodi wa Mwadui lilipasuka na kusababisha maji na matope kuzagaa kwenye vijiji vya Ng’wang'holo na Nyenze, Kata ya Mwadui Lohumbo Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.
Aidha, Maji machafu na tope yamesambaa katika eneo la zaidi ya kilometa nane na kuathiri sana nyumba kadhaa, mashamba, mifugo, mimea, visima na hata baadhi ya watu kuathirika kiafya.
Mara baada ya kutokea kwa hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mh Sophia Mjema amejitokeza kwenye vyombo vya habari akisema ameunda Tume ya watu kutoka kamati yake ya ulinzi na usalama, baadhi ya wataalamu na kushirikiana na wataalamu wa mgodi wa Mwadui. Na kwamba wanajukumu la kutazama chanzo cha kupasuka kwa Bwawa hili, kufanya tathmini za athari na mwisho kuangalia namna jambo hili lisijirudie.
CHADEMA Mkoa wa Shinyanga tunapinga uundwaji wa Tume hiyo na Mkuu wa Mkoa, kwa kuzingatia aina ya wajumbe pamoja na hadidu za rejea kwa Tume Kwa sababu;
Mosi, kwa mujibu wa muundo wa serikali, Nchi yetu tuna wizara ya Muungano na Mazingira ambayo ina majukumu ya kutazama mazingira na ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Waziri wake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira hivyo ni busara wizara hii ikahusika na jambo hili nyeti ambalo mpaka sasa limeathiri makazi na mali nyingi za wananchi.
Kwamba, tuna Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambalo limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya usimamizi wa Mazingira namba 19 ya Mwaka 1983. Kwamba Baraza hili lina jukumu la usimamizi wa mazingira.
Kwamba, Kifungu cha 17 cha Sheria hiyo, inaipa NEMC majukumu pamoja na Kutekeleza shughuli za uzingatiaji na usimamizi (enforcement and compliance) wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira;
NEMC inawajibu wa Kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kushirikisha umma na si ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Kifungu cha 18(2) cha Sheria ya Usimamizi wa mazingira inatoa mchanganuo mpana wa majukumu ya NEMC ambayo kwayo tunaamini wanaweza kuja na majibu sahihi juu ya nini kimetokea.
CHADEMA, tunajiuliza kama NEMC ilitekeleza wajibu wake kwa kufanya uhakiki wa mazingira wa mara kwa mara kwenye Bwawa hilo yaani Environmental Audit. Lakini pia kama kulikuwa na ukaguzi na ufuatiliaji yaani Audit and Monitoring katika Bwawa hilo na Mgodi wote kwa ujumla.
Kwani tunaamini lengo la kuanzishwa kwa NEMC ni kulinda na kuthibiti ajali kama hizi zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kimazingira kama huu kwani kwa taarifa za awali tumeelezwa ni zaidi ya Nyumba13, zimezingirwa na tope na zingine kudondoka, huku ikisadikiwa watu zaidi ya 50 kuathirika kwa kukosa malazi na chakula mpaka sasa, na watoto wapatao wanne wakiwa wanaumwa.
CHADEMA tunasikitika kwa kutokuchukuliwa hatua mahsusi na za haraka kwa wahanga hawa, ambao hawana makazi na chakula huku wakiwa wamepoteza mifugo na hawana hata sehemu ya kupata maji ya kunywa. Tunaitaka Serikali na Mgodi wa Mwadui kuwatafutia sehemu salama za kuishi kwa muda na kuwapatia waathirika wote hudumu muhimu za kibinadamu.
Mwisho tunatoa wito kwa Serikali, kuivunja tume hii na jukumu hili lifanywe na Wizara ya Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na NEMC pamoja na wadau na wataalamu wa mazingira nchini, kwani tunaamini tope na maji hayo yatakuwa na athari kubwa kwa jamii yetu. CHADEMA tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu jambo hili, na kuona hatua kali zikichukuliwa, pamoja na kuangazia stahiki zote za waathirika.
Imetolewa leo Alhamisi 10 Novemba, 2022 na
Emmanuel Ntobi,
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga.
WAZIRI WA MADINI DOTTO BITEKO ATEMBELEA WAATHIRIKA WA TOPE BWAWA LA MGODI WA ALMASI MWADUI
Na Marco Maduhu. KISHAPU
WAZIRI wa Madini Dotto Biteko ametembelea wananchi ambao wameathirika na Tope la Mgodi wa Almasi Mwadui mara baada ya bwawa lake kupasuka na kutiririsha tope kwenye makazi yao na kutaka wananchi waelezwe ukweli kama tope hilo linasumu ama laa.
Biteko amefanya ziara hiyo leo Novemba 10, 2022 kwa kutembelea waathirika hao pamoja na kuona eneo ambalo limeathiriwa na tope la mgodi huo wa Mwadui.
Akizungumza na uongozi wa Mgodi huo, amewataka wafanya tathimini ya haraka ya kubaini athari ambao wamezipata wananchi na kuwalipa fidia, pamoja na kudhibiti tope hilo lisiendelee zaidi kwenda kwenye makazi ya wananchi hasa katika kipindi hiki cha mvua.
“Nawapongeza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mgodi mara baada ya bwawa hili kupasuka kitu cha kwanza kabisa mlijali usalama wa wananchi na hakuna ambaye amepoteza maisha zaidi ya kupoteza mashamba yao pamoja na nyumba zao na visima vya maji kuzingirwa na tope,”amesema Biteko.
“Kwa sasa Serikali haiwezi kutoa majibu juu ya hatua ambazo itazichukua sababu bado kuna uchunguzi unafanyika na majibu yakitoka ndipo tuta tamka adhabu ambayo mgodi huu unapaswa kuwajibishwa na liwe fundisho kwa wengine kwa kuonyesha uzembe wa hali ya juu, kwa sasa tuna angalia usalama wa wananchi kwanza, na pia waelezwe ukweli kama tope hilo lina sumu au hapana”ameongeza
Aidha, amesema kwa taarifa za awali alizokuwa nazo bwawa hilo la Mgodi wa Almasi Mwadui lilipata hitilafu tangu mwezi wa Tisa mwaka huu, lakini Mgodi huo uliendelea kulitumia na hatimaye limeleta athari kwa wananchi.
Mhandisi Mkuu wa Mgodi huo Mwadui Shagembe Mipawa, amekiri bwawa hilo la mgodi kuwa na hitilafu mwezi huo wa tisa, na walilitolea taarifa kwa uongozi wakaziba sehemu ambazo zilikuwa zina vuja na wakajiridhisha kuwa lipo salama, lakini wanashaghaa siku hiyo novemba 7 likapasuka na tope kuvamia makazi ya wananchi.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Ayubu Mwenda, amesema kitu cha kwanza walichokifanya baada ya kupasuka kwa bwawa hilo ni kuwahi usalama wa wananchi kwanza, pamoja na kuweka matuta ya kuzuia tope hilo lisiendelee kwenda kwenye makazi ya watu zaidi.
Amesema kwa watu ambao wameathirika na tope hilo wapatao 115 wamewahamishiwa kwenye hosteli za mgodi huo na wanaendelea kuwapatia maradhi yote, pamoja na watoto wao kuwapeleka shule na kuwarudisha ili wasiathirike kimasomo huku wakiwatimizia mahitaji yote.
Amesema mgodi huo bado unaendelea kufanya tathimini ili kujua ni kiasi gani wananchi wameathirika ikiwamo kupoteza nyumba pamoja na mashamba, na kuangalia namna ya kuwapatia fidia, huku wakiendelea kuwapatia huduma ya chakula, maji, na matibabu
Akizungumzia tope hilo kuwa na sumu, amesema Kemikali ambazo wanazitumia kwenye mgodi huo hazina madhara kwa binadamu, sababu uzalishaji wa Almasi ni tofauti na dhahabu na kuwatoa wasiwasi wananchi juu ya afya zao.
Naye Meneja wa Mamlaka ya udhibiti na uhifadhi wa mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Kayombo Jarome, amesema kuna uharibifu mkubwa wa mazingira ambao umetokea, lakini bado wanasubili majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kujua kama tope hilo kama lina kemikali ambazo zina madhara kwa wananchi ndipo watatoa taarifa kamili.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, ameiomba ifanyike tathimini ya haraka ili wananchi wapatiwe maeneo mengine ya mashamba na kufanya shughuli za kilimo, ili kukabiliana na baa la njaa hapo baadae, pamoja na kutekelezewa miradi ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.
Nao baadhi ya wananchi akiwamo Meya Ndole, amesema nyumba yake imezingirwa na maji na amepoteza mbuzi wawili ambao walisombwa na tope hilo na kuishukuru Serikali kwa kuwatoa kwenye maeneo ambayo ni hatarisha na kuja kuishi ndani ya mgodi kwa muda.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amewatoa wananchi wasiwasi kuwa Serikali ipo pamoja nao na kila mtu atapata haki yake na hakuna ambaye atapoteza na kuwataka wawe na subira wakati taratibu zingine za kisheria zikifuata.
Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi Mwadui, ambao kwa sasa wanaishi ndani ya Mgodi huo.
Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi Mwadui, ambao kwa sasa wanaishi ndani ya Mgodi huo.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akizungumza na waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Mwadui, ambao kwa sasa wanaishi ndani ya mgodi huo.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo akisalimia na waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza na waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Mwadui, ambao kwa sasa wanaishi ndani ya mgodi huo.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Almasi Mwadui Ayubu Mwenda akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Madini Dotto Biteko.
Wananchi ambao ni waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui wilayani Kishapu wakiwa kwenye makazi yao ya muda ndani ya mgodi huo.
Wananchi ambao ni waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui wilayani Kishapu wakiwa kwenye makazi yao ya muda ndani ya mgodi huo.
Wananchi ambao ni waathirika wa Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui wilayani Kishapu wakiwa kwenye makazi yao ya muda ndani ya mgodi huo.
Waziri wa Madini Dotto Biteko wapili (kushoto) akiangalia eneo ambalo limeathiriwa na Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui mara baada ya kupasuka kingo zake.
Waziri wa Madini Dotto Biteko wapili (katikati) akiangalia eneo ambalo limeathiriwa na Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui mara baada ya kupasuka kingo zake.
Muonekano wa Kingo ambayo imepasuka kwenye Bwawa la Mgodi wa Alamsi Mwadui la kuhifadhia maji machafu.
Muonekano wa Tope ambalo limesambaa na kwenda kwenye makazi ya watu likitoka kwenye Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui.
Muonekano wa Tope ambalo limesambaa na kwenda kwenye makazi ya watu likitoka kwenye Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui.
Ziara ya kuangaliwa eneo ambalo limeathitika na Tope la Bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui ikiendelea.
KIJANA AKAMATWA AKIMRUSHIA MAYAI MFALME WA UINGEREZA











