Saturday 15 May 2021
RAIS SAMIA AMTEUA MGOMBEA URAIS TANZANIA 2020 QUEEN SENDINGA KUWA RC IRINGA
RAIS SAMIA AMTEUA MWAKITALU KUWA MKURUGENZI WA MASHTAKA 'DPP'... DK. MHEDE MABASI YA MWENDOKASI 'UDART'
HUYU NDIYE DK. PHILEMON SENGATI MKUU MPYA WA MKOA WA SHINYANGA...ZAINAB TELACK AHAMISHIWA LINDI
RAIS SAMIA AMTEUA ACP SALUM RASHID HAMDUNI KUWA MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU....AMKUMBUKA MAKONGORO NYERERE
Breaking News : RAIS SAMIA AMEFANYA UTEUZI WA WAKUU WA MIKOA NA WATENDAJI WA TAASISI..WENGINE WAHAMISHWA
MREMBO AFUNGA VIRAGO NA KUMKIMBIA MME WAKE AKIDAI NI MLAFI SANA
OFISI YA WAZIRI MKUU YASHEREKEA EID NA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU
*******
Na Mwandishi Wetu
Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitr.
Akimwakilisha Waziri Mkuu katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema lengo la kuandaa chakula hicho ni kuendeleza umoja na kutoa faraja kwa kundi hilo la watu wenye ulemavu.
Katika kusherekea sikukuu hii ya Idd El Fitir, Ofisi ya Waziri Mkuu iliona ni muhimu kuandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na vijana wetu wa chuo hiki cha watu wenye ulemavu hivyo Waziri Mkuu pamoja na Waziri wetu wa Nchi, Mhe. Jenista Mhagama wamenituma niwawakilishe katika tukio hili kwasababu wao wapo katika majukumu mengine ya kitaifa, amesema Ummy Nderiananga.
Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Prof. Jamal Katundu, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuyajali na kuyasaidia makundi mbali mbali ya watu wenye mahitaji maalum kikiwemo chuo hicho cha watu wenye ulemavu.
Hili jambo kubwa sana na ndio maana mimi kama Naibu Katibu Mkuu nimepewa jukuma la kuratibu suala hili na kama mlivyoona vijana wetu wamefurahishwa sana na tukio hili hivyo natumie fursa hii kutoa wito kwa watu wenye uwezo na taasisi mbali mbali zenye mafungu ya kusaidia jamii kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuja kuwasaidia vijana wetu, Prof. Jamal Katundu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, amesema menejimenti pamoja na wanachuo wamelipokea tukio hilo kwa furaha sana ambapo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa tukio hilo.
Aidha, baadhi ya wanachuo wakiwemo Joseph Baraza na Evodia Mwombeki wameelezwa kufurahishwa na tukio hilo na wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walijumuika nao katika chakula hicho.
Tumefurahi sana kwa namna moja ama nyingine kwasababu huwa tunajisikia furaha sana kujumuika na watu tofauti tofauti na kujiona kwamba hatujatengwatunawashukuru sana kwa tukio hili la leo na Mungu awabariki sana, amesema Evodia Mwombeki, Mwanafunzi katika fani ya Kilimo na Ufugaji.
Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Kwasasa kina jumla ya wanafunzi 76 na kinatoa kozi mbali mbali zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.
NEC YAVIONYA VYAMA VINAVYOSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MUHAMBWE, BUHIGWE NA KATA 5
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, vina wajibu wa kuweka mawakala kwenye vituo vya kupigia na kujumlisha kura lakini mawakala hao na wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia Sheria za Uchaguzi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2021 na kushirikisha kata za Buziku (Halmashauri ya Wilaya ya Chato), Bugarama (Halmashauri ya Wilaya ya Geita), Igunga (Halmashauri ya Wilaya ya Igunga), Ligoma (Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru) na Kata ya Miuta iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.
Jaji Mst. Kaijage amesema Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.
Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na kata tano za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua wabunge na madiwani wanaowataka.
Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zinakamilika leo jioni saa 12:00 hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.
“Pili upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”alisema Jaji Mst. Kaijage na kuongeza:
“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye majimbo na kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Kifungu cha 62 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.”
“Mojawapo ya vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura anaweza kutumia ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura anapokwenda kupga kura. Aidha majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala”
Jaji Mst. Kaijage amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nuktanundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.
Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
Amewakumbusha wapiga kura kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka jana yaliyokubaliwa na wahusika wote vikiwemo vyama vya siasa, kuwa wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura, hivyo Tume imewashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, itahusisha idadi ya wapiga kura watakaopiga kura 303,965 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kupigia kura ni vituo 793.
Friday 14 May 2021
Wadau Wa Mabwawa Watakiwa Kuzingatia Sheria
WADAU wa mabwawa wamesisitizwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo na kuhakikisha mabwawa yanasajiliwa kwenye Mamlaka husika ili yatambulike kisheria kwa lengo la kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa hivi karibuni Jijini Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo vya Maji kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa wakati wa kufunga warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
“Zingatieni Miongozo ya Usalama wa Mabwawa, tunahitaji uwepo wa mabwawa yenye manufaa na ambayo ni salama kwa viumbe hai na mazingira na si vinginevyo,” alielekeza Rwebugisa.
Rwebugisa alisisitiza umuhimu wa kutumia Watalam wa Mabwawa waliosajiliwa kuanzia hatua za awali za usanifu hadi hatua ya usimamizi wakati tayari yameanza kazi ili kuepukana na changamoto zinazoweza kusababisha madhara.
Alisema baaadhi ya mabwawa hukutana na changamoto kadhaa huku mengine yakishindwa kukidhi matakwa ya matumizi yaliyokusudiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoshirikisha wataalam.
“Kabla hamjaanza kuchimba ama kujenga mabwawa hakikisheni mnashirikisha wataalam ili wajiridhishe kulingana na utaalam wao kama bwawa linalotarajiwa kujengwa mahali hapo linastahili na pia namna gani lijengwe ili kuepukana na changamoto zinazozuilika,” alisisitiza Rwebugisa.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza endapo bwawa litajengwa bila ushauri wa kitaalam ni pamoja na kuvuja, jambo ambalo alisisitiza kuwa ni hatari kwa afya na maisha ya viumbe wanaozunguka eneo husika.
Alisema jamii pia inapaswa kuelimishwa na kutambua umuhimu wa mabwawa hasa ikizingatiwa kwamba mabwawa yanazo faida lukuki ambazo baadhi yake alizitaja kuwa utunzaji wa mazingira kwa kuhifadhi taka hatarishi lakini pia ni chanzo cha mapato kutegemeana na aina ya bwawa.
“Mabwawa yana faida nyingi sana, ni muhimu jamii ikaelimishwa juu ya faida hizo lakini pia namna ya kuyalinda na kuyatunza ili kuepusha madhara,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu warsha, Rwebugisa alisema imejikita kujadili Miongozo ya Usalama wa Mabwawa na kwamba wadau walioshiriki wajitahidi kufuata miongozo walioijadili.
Alielekeza washiriki kuhakikisha wanaendelea kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha usalama wa mabwawa na kuendeleza mawasiliano ya karibu na ya kila mara na Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wake.
“Mapendekezo yenu tumeyachukua kwa maboresho kwani miongozo iliyopo sio misahafu hivyo tutakuwa tunaboresha kila tunapoona kwa pamoja umuhimu wa kufanya hivyo,” alisema.
Warsha hiyo imeshirikisha Viongozi kutoka Wizara ya Maji, Wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), Wizara na Taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.
Wizara ya Madini yaagiza ukaguzi leseni za Madini Njombe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe kufanya ukaguzi wa Leseni zote 245 za Uchimbaji Madini mkoani humo ili kujua maendeleo ya uendelezwaji wake.
Agizo hilo linafuatia ombi lililowasilishwa na wachimbaji wadogo wa Madini mkoa wa Njombe ambao wameiomba Wizara kuwapatia maeneo ya kuchimba kutokana na sehemu kubwa kushikiliwa na wawekezaji kwa kipindi kirefu pasipo kuyaendeleza.
” Nakuagiza RMO fanya uchambuzi wa Leseni zote kujua zina hali gani, ikiwa zinalipiwa, ni maendeleo gani yamefanyika ili kuanzia hapo wizara ichukue hatua. Tunapotoa leseni tunataka watu waziendeleze na wachimbe siyo kuzifungia kabatini,’’amesisitiza Prof. Msanjila.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, moja ya vipaumbele vya Serikali na kama alivyoeleza Waziri wa Madini katika Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ni pamoja na kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo ili wachimbe, hivyo, wizara itahakikisha inalifanyia kazi kwa karibu suala hilo.
Amefanunua kuwa, endapo mmliki wa leseni ana nia ya kuiuza leseni yake hakatazwi isipokuwa anapaswa kuiendeleza kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine. ‘’ Ukitaka kuuza leseni lazima useme uliifanyia nini kabla ya kuiuza. Huu ndiyo utaratibu wa Sheria,’’ amesema.
Akizungumzia mwenendo wa makusanyo katika mkoa huo amesema bado kiwango kiko chini ikilinganishwa na rasilimali madini zinazopatikana katika mkoa huo ikiwemo chuma na makaa ya mawe na kuongeza kwamba, hadi sasa Mkoa wa Njombe umekusanya kiasi cha shilingi milioni 240 kati ya shilingi bilioni 1 uliyopangiwa kukusanya huku akitaja moja ya sababu ikiwa ni wamiliki kutozifanyia kazi leseni zao.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachimbaji wadogo katika mkoa huo kwa kufanya shughuli zao huku wakishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Madini pamoja na ofisi ya Mkoa wa Njombe suala ambalo limepelekea kutokuwepo kwa migogoro inayozuia maendeleo ya Sekta.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Njombe Alfred Luvanda, amemhakikishia Prof. Msanjila kuwa, wachimbaji mkoani humo wako tayari kimitaji ikiwemo kulipa kodi za serikali pindi itakapowapatia leseni za kuchimba madini, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Madini.
‘’ Kwanza tunashukuru sana kwa ujio wako, tunaamini kilio chetu kimefika sehemu sahihi. Tunakuahidi tutachimba, tutalipa kodi za serikali na tutaipa serikali heshima,’’ amesema Luvanda.
Naye, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe Henry Mditi amewaeleza wachimbaji hao kuwa ofisi ya madini mkoani humo haitomuonea mtu yoyote na hivyo akawataka wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria.
Prof. Msanjila amekutana na wachimbaji hao Mei 13, 2021, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wachimbaji pamoja na watumishi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aongoza swala ya Eid al-Fitr kitaifa
Swala hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini akiwemo Mufti wa Tanzania, Sheikh Abiubakar bin Zuberi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge.
Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na makamu wake, Dkt. Philip Mpango kwa waumini hao, waziri mkuu amesema viongozi hao wanawatakia Waislamu na Watanzania wote nchini sikukuu njema.
Ametumia jukwaa hilo kuwahisi Waislamu kusherehekea siku kuu ya Eid al-fitr kwa kuiishi miiko ya dini hiyo.
Awali, akihutubia maelfu ya Waislamu waliofika katika ibada hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesisitiza umuhimu wa amani, upendo na kutosherehekea katika mazingira ya kupata dhambi.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza Kuu la Waislamu leo alasiri.