Wednesday, 8 April 2020

DC WA SINGIDA AJA NA OPERESHENI TOKOMEZA CORONA


    Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akiwa ndani ya basi la Kampuni ya Kiazi Kitamu akiwaeleza abiria mbinu za kujikinga na Virusi vya Corona (COVID-19) alipokuwa kwenye Operesheni maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Kituo Kikuu cha mabasi. (Picha na. Peter Kashindye).
Madereva na Mawakala wa mabasi kwenye Kituo Kikuu cha mabasi ya Mkoa wa Singida (Misuna) wakionyesha jinsi ya kutumia vitakasa mikono ili kukabiliana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (Hayupo pichani) alipofanya Operesheni Maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kuona utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huo (Picha na. Peter Kashindye).



  Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (aliyenyanyua mkono) akihoji uelewa wa kujikinga na virusi vya Corona (Covid-19) mahali pa kazi kwenye maduka ya kuuzia nyama alipofanya Operesheni Maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Soko Kuu la Singida Mjini. (Picha na. Peter Kashindye).




1.  Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akiwasisitiza wafanyabiashara wadogo juu ya matumizi sahihi ya vitakasa mikono alipofanya Operesheni maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Soko Kuu la Singida Mjini. (Picha na. Peter Kashindye).


1  Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (aliyenyanyua mkono) akitoa maelekezo kwa madereva na mawakala kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19). (Picha na. Peter Kashindye).

Na John Mapepele ,Singida

Mkuu wa Wilaya ya Singida Injinia Paskasi Damian Muragili amefanya Operesheni Maalum kwenye maeneo mbalimbali ya Mji wa Singida kutoa elimu na kuona jinsi wananchi walivyotekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu ya kujikinga na ugonjwa unaoambukizwa na Virusi vya Corona (Covid 19).


Licha ya kutoa elimu hiyo pia amewapiga faini za hapo hapo watu waliobainika kukiuka maagizo huku akisisitiza kuwa Serikali itawanyang’anya lesseni za biashara na kufunga biashara hizo wote ambao wataendelea kukaidi maelekezo hayo
 

Mhandisi Muragili amefanya Operesheni hiyo maalum akiwa na Kikosi Kazi cha wataalam mbalimbali kwenye Wilaya yake ambapo ilianza alfaji hadi usiku wa kuamkia leo ambapo alitembelea maeneo yote ya huduma katika Mji wa Singida iliyojumuisha maeneo ya Standi Kuu ya Mkoa wa Singida ya Misuna, Soko Kuu la Singida na maeneo ya biashara ya Bajaji.

Akiwa katika Soko Kuu la Singida, Mkuu wa Wilaya alifanikiwa kukuta maduka ya nguo ya Kikundi cha Ushonaji cha Singida yakiwa hayana vitakasa mikono lakini wauzaji walikuwa wakiendelea na shughuli za biashara na kuwatoza faini ya shilingi elfu 50 papo hapo.

Akilipa faini hiyo baada ya kukiri kosa hilo, Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko Kuu Singida Amina Msaghaa aliomba samahani kwa Mkuu wa Wilaya na kuahidi kutoendelea kufanya kosa hilo na kwamba faini hiyo imekuwa fundisho kwao na kwa hiyo wao kama kikundi watakuwa mfano wa kuwafundisha wafanyabiashara wengini

“Mhe. Mkuu wa Wilaya naomba kukueleza kuwa tumetoa faini hii kwa masikitiko makubwa, lakini hii inatupa ujasiri wa kushirikiana na Serikali yetu kuhamasisha kuhusu kujikinga na ugonjwa huu, naahidi tutakuwa walimu wazuri” alisitiza Msaghaa

Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji Mkoa wa Singida Hemed Juma amesema katika kupambana na ugonjwa wa Corona chama chao kimechukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Serikali kuhusu ugonjwa huu na kwamba yoyote atakayekaidi atashughulikiwa kikamilifu na chama chao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye Vyombo vya Sheria.

Akifanya ukaguzi kwenye mabasi yanayoingia na kutoka kwenye Stendi Kuu Mkuu wa Wilaya amesema abiria wanatakiwa kutumia vitakasa mikono wanapoingia na kutoka kwenye mabasi hayo kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huu

Aidha amesema Operesheni hiyo imeanza na itakuwa endelevu na ya kushitukiza kila wakati hadi ugonjwa huu utakapoisha.

Amewataka kila mwananchi wa Wilaya ya Singida kuwa mzalendo kwa kuzingingatia maelekezo ya Wizara ya Afya ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kujitenga na kuchukua hatua zinazotakiwa ili kujilinda na kuwalinda wengine na kwamba wanapohisi kuwa kuna mgeni ambaye ameingia na hajapimwa watoe taarifa kwenye Mamlaka zilizo katika maeneo yao

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika siku za hivi karibuni ameanza ziara maalum ya kuhamasisha wananchi wa mkoa wake kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya za kudhibiti na kujikinga na ugonjwa, wa Covid-19, kumwomba Mungu na kuendelea kuchapa kazi ili kunusuru kupoteza maisha na kushuka kwa uchumi wa nchi yao

Akiwa kwenye Soko maarufu la viazi lishe kwenye Kitongoji cha Kideka katika Kijiji cha Nkunikana aliwapongeza wafanyabiashara hao kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kuandaa miundombinu ya maji ili kunawa mikono kwa sabuni katika maji yanayotiririka wakati wote.


Aidha  aliwataka wakulima wa viazi lishe kuendelea kulima kwa bidii ili wananchi wapate lishe bora kutokana na viazi hivyo na majani yake ambapo alisisitiza kuwa katika kipindi hiki ni muhimu kusanitaizi mikono na kusanitaizi afya zao

“Naelekeza wakulima waache visingizio nao waendelee kwenda mashambani kujitenga na kulima kwa bidii katika kipindi hiki ili waweze kupata mazao mengi na wakati huo huo watekeleze matakwa ya Serikali ya kujitenga na mikusanyiko isiyo ya lazima ambayo ingeweza kusababishia maambukizi endapo mmoja ana maambukizi.”


Share:

Wadau Wamkabidhi Waziri Mkuu Sh. Bil 6.226 Kukabili Corona

Wadau Wamkabidhi Waziri Mkuu Sh. Bil 6.226 Kukabili CoronaWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 6.226.

Baada ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa watano wamepona.

Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi Waziri Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma. Amewataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Amesema hadi sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.

Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona.

“Serikali inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona nchini.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh. bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh. bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa.

Wengine ni kampuni ya TEHAMA ya Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging Temperature Measuring System moja vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.

Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.

Awali, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga.

Pia, Mfanyabiashara huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine. Amempongeza Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Serikali Yaipa Mwezi Mmoja Benchmark Kumlipa Mshindi wa BSS 2019

Na Shamimu Nyaki – WHUSM.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Juliana Shonza ametoa mwezi mmoja kuanzia Aprili 08, 2020 kwa Kampuni ya Benchmark Production inayoendesha mashindano ya Bongo Star Search chini ya Mkurugenzi wake Madam Ritha Paulsen kumlipa kiasi cha Shilingi milioni 50 mshindi wa kwanza wa mashindano hayo kwa mwaka 2019, Bw.Meshack Fukuta. 

Naibu Waziri ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma baada ya kupokea barua kutoka kwa familia ya mshindi huyo iliyoeleza kutokutekelezwa kwa ahadi hiyo kwa takriban miezi minne sasa ilioanisha utaratibu wa malipo hayo kuwa milioni 30 ni kwa ajili kutengeneza kazi za muziki na matangazo kwa kipindi cha mwaka mmoja na milioni 20 ni ya kukabidhiwa mkononi ambapo Mhe. Naibu Waziri amesisitiza makubaliano yote yalioanishwa kufanyiwa kazi. 

“Mimi kama mlezi wa tasnia ya Sanaa ambaye pia nilikua mgeni rasmi siku ya fainali nimesikitishwa sana na malalamiko haya, hivyo naitaka kampuni ya Benchmark kutekeleza ahadi hiyo na wasipofanya hivyo ndani ya muda huo, Serikali haitasita kufungia mashindano hayo”, alisema Mhe.Shonza. 

Mhe. Naibu Waziri ameongeza kuwa Wizara iliwasiliana na uongozi wa Benchmark kuhusu malalamiko hayo mbapo Kampuni hiyo ilieleza kuwa imeshindwa kumlipa msanii huyo kutokana na viongozi wa Kampuni iliyodhamini shindano hilo ya Startimes  kuwepo nchini China na kushindwa kusafiri kuja nchini kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Corona. 

Hata hivyo Mhe.Naibu Waziri ameleeza kuwa Wizara iliwasiliana na uongozi wa Startimes ambao umekiri kuwa umeshalipa fedha kwa Kampuni ya Benchmark tangu mwezi Januari 2020. 

Aidha,  Mhe.Shonza ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inamtengenezea msanii huyo wimbo bora pamoja na kuufanyia matangazo ya kutosha katika kipindi cha miezi miwili kuanzia leo  pamoja na kuwasilisha nakala ya mkataba wa washiriki waliofikia hatua ya kumi bora ndani ya wiki moja kuanzia leo machi 08,2020. 

Katia hatua nyingine Mhe.Shonza ameliagiza Baraza la Sanaa na Taifa (BASATA) kusimamia utaratibu wa uaandaji wa mashindano mbalimbali  ikiwemo kuwepo kwa mikataba kati ya wasanii na wanaondesha mashindano  au shughuli yoyote ya sanaa na wasanii pamoja na kuhakikisha ahadi wanazopewa washindi ikiwemo zawadi  zinakuwepo na zinakabidhiwa kwa wahusika mara baada ya mashindano. 

Kwa upande wake Bw.Meshack Fukuta mshindi wa shindano hilo kwa mwaka 2019 ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo imechukua hatua katika malalamiko yake ambapo ameahidi kufanya juhudi katika Sanaa yake ili kuitangaza nchi vizuri ndani na nje ya nchi pamoja na kujipatia kipato kupitia kipaji hicho.


Share:

Serikali Na Wadau Waja Na Elimu Juu Ya Corona Kwa Watoto

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) kwa kushirikiana na Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN), Taasisi ya Chakula na Lishe, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) wameandaa mkakati wa kufikisha ujumbe kwa watoto kuhusu kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.

Akizungumza leo katika kikao kazi kilichowakutanisha wadau hao jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN) Bruno Ghumpi amesema kumekuwepo na ujumbe mbalimbali katika kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona ila kumekosekana ujumbe maalum unaolenga makundi maaalum ikiwemo wanawake wajawazito na watoto wadogo kuanzia miaka 0 hadi minane.

Ameongeza kuwa kuwepo kwa elimu sahihi kwa watoto hao kuhusu ugonjwa wa COVID 19 itawasaidia wazazi au walezi na watoto wenyewe kupata taarifa zitakaziwasaidia kujikinga na Virusi hivyo ili kupunguza au kuondokana na maambukizi ya Virusi hivyo katika maeneo yao.

“Ujumbe huu kwa watoto ni muhimu sana kwani kundi hili kwa sasa lipo nyumbani kutokana na kufungwa kwa shule hivyo ni vizuri wazazi na walezi wakazingatia masuala muhimu ya kuwafundisha watoto wao kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona” amesema

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bw. Mathias Haule amesema kuwa ni muhimu kwa wadau kuhakikisha wanafikisha elimu katika ngazi ya chini kuanzia familia, kijiji/mtaa ili kuwezesha watu hao kupata taarifa na elimu sahihi juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

“Elimu ifike katika ngazi ya familia hasa katika maeneo ya vijijini ambako bado elimu haijawafikia kwa kasi inayotakiwa ili kuondokana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini.” Amesema

 


Share:

Mmiliki Jamii Forom ahukumiwa kwenda jela au alipe faini Milioni 3

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxece Mello kulipa faini ya Sh.Mil 3 ama kwenda jela mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulizuia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake.

Pia Mahakama hiyo, imemuachia huru mshitakiwa mwenzake Mickie Mushi baada ya kutotiwa hatiani katika makosa yao.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo upande wa utetezi umedai kuwa utakata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Melo yupo chumba cha mahabusu kusubiri kulipa faini hiyo ama akishindwa atumikie kifungo cha mwaka mmoja.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia Polisi kufanya uchunguzi kinyume na kifungu cha 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016  katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.


Share:

LUKUVI AAGIZA KUFANYIKA UHAKIKI WA KINA UTEKELEZAJI MAAMUZI YA KUTOONDOLEWA VIJIJI 920


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa kina utakaoshirikisha sekretarieti za mikoa katika utekelezaji maagizo ya kutoondolewa vijiji 920 vilivyokuwa na mgogoro maeneo ya hifadhi nchini.



Lukuvi alitoa maagizo hayo jana jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya Makatibu Wakuu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kwa Mawaziri wa Wizara zinazohusika katika utekelezaji huo kufuatia uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 kwenye maeneo ya hifadhi yaliyokuwa na mgogoro.

Wizara ambazo Makatibu Wakuu wake wanashiriki kazi ya utekelezaji maagizo hayo ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Kilimo, Maji, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Makamu wa Rais ambazo Mawaziri wake walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo yaliyopelekea Rais kuchukua uamuzi huo.

Awali wananchi waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi ya misitu walionekana wavamizi wakati serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji na wananchi wake kushiriki shughuli mbalimbali zikiwemo za uchaguzi jambo lililomfanya Rais Magufuli kuchukua uamuzi wa kuvibakisha vijiji 920 baada ya kupata ushauri wa mawaziri wa sekta husika.

Lukuvi alisema, katika kipindi hiki ambacho kamati za wataalamu zinapitia taarifa za utekelezaji maamuzi kuhusiana na suala hilo lazima ufanyike uchambuzi wa kina ili kuja majibu yatakayokidhi malengo ya uamuzi uliofanyika hasa ikizingatiwa baadhi ya maeneo ya vijjiji hayahitaji kupunguzwa.

‘’Ufanyike uchambuzi wa kina kuona faida itakayopatikana na vijiji vingapi vitanufaika na tupate taarifa itakayoainisha kila eneo na makubaliano yake’’ alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, kila sekta inayohusika inatakiwa kufanya uchambuzi katika eneo lake na kutolea mfano Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza kuja na uchambuzi utakaoainisha maeneo ya EPZA yaliyorudishwa kwa wananchi huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiainisha maeneo yaliyopunguzwa kwa shughuli za ufugaji na kilimo na Kamishna wa Ardhi akibainisha maeneo yaliyofutwa.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema wakati wa utekelezaji kazi ya uchambuzi ikiendelea wasimamizi wa sheria katika maeneo ya hifadhi wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na kuwatahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji majukumu yao ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema kamati ya Makatibu Wakuu imeendelea kufanyia kazi utekelezaji maamuzi ya vijiji 920 kama walivyoelekezwa.

Kwa mujibu wa Mary, kamati ya Makatibu Wakuu katika kutekeleza maagizo ya Mawaziri inatarajia kukamilisha kazi ya tahmini ya vijiji 920 katika muda wa wiki mbili na kuwasilisha taarifa yake kwa mawaziri wa sekta kama ilivyoelekezwa mwisho wa mwezi huu wa Aprili.

Kwa muda mrefu wananchi wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa katika mgogoro kwa kudaiwa kuwa wavamizi na kusababisha nyumba zao kuchomwa moto huku baadhi yao wakiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini.

Mgogoro huo ulisababisha Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji 920 kubaki maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya. Pia Rais Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli za ufugaji.


Share:

Trump aionya India kuhusu kusitisha mauzo ya Hydoxy-chloroquine....Asema Atalipa Kisasi

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kulipiza kisasi dhidi ya India ikiwa nchi hiyo itapiga marufuku mauzo ya dawa aina ya Hydoxy-chloroquine. 

Trump amedai kwamba dawa hiyo inaweza kutibu maradhi ya homa ya mapafu yanayosababishwa na virusi vya corona. 

Hata hivyo India ambayo ni mzalishaji mkuu wa dawa hiyo duniani imepiga marufuku kuuzwa daqa hiyo nje.

 Rais Trump amesema amezungumza na waziri mkuu wa India Narendra Modi na kumwambia kuwa Marekani inapendelea kuzipata dawa ilizoagiza. 

Dawa hiyo ya Hydroxy-chloroquine inatumika kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa malaria. 

Hata hivyo sasa inafanyiwa majaribio kubainisha iwapo inaweza kutumika kutibu ugonjwa wa Covid -19 unaosababishwa na maambukizi wa virusi vya corona.


Share:

Taarifa Kwa Umma Kufuatia Kuondolewa Karantini (LockDown) Katika Mji Wa Wuhan Vilikoanzia Virusi Vya Corona

Baada ya lock down ya wiki kadhaa, sasa rasmi Wuhan,China imeanza kuruhusu Watu kusafiri kutoka eneo hilo ambalo linaaminika kuwa kitovu cha virusi vya corona hii ni baada ya maambukizi kupungua




Share:

Taarifa Kwa Umma Toka Baraza la Mitihani Tanzania-NECTA




Share:

Wasio Chukua Tahadhari Ya Corona Songwe Kutozwa Faini

Watu wote ambao hawachukui hatua za tahadhari za kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona kwa kutofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya, watatozwa faini kwakuwa wana hatarisha maisha yao na ya wengine.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa amebainisha hayo jana mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Songwe kufanya ukaguzi wa utayari wa kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona katika Wilaya hiyo.

Opulukwa amesema, “Sasa tunaanza kutoza faini wote wasiofuata maelekezo ya wataalamu wa Afya kuhusiana na Corona, mfano tukipita dukani au sehemu ya biashara na hakuna maji na sabuni, tuta toza faini na kufunga kwa mda biashara hiyo mpaka mtu huyo azingatie maaelekezo hayo”.

Ameongeza kuwa lengo la Wilaya hiyo ni kuhakikisha kuwa mahali pa kufanyia biashara ni salama kwa wafanyabiashara na watumiaji wa huduma hizo huku akieleza kuwa wanawa fuatilia wageni wote wanao toka nje ya wilaya waliopo katika nyumba za kulala wageni na kuchukua maelezo yao kwa ajili ya tahadhari  endapo wana dalili za Ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Opulukwa ameongeza kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi wote wa Wilaya ya Songwe hususani katika maeneo ya migodi ambapo kuna mikusanyiko ya watu wengi pia ameielekeza kamati inayohusika kutoa elimu ifanye ufuatiliaji wa kina endapo wananchi wanazingatia wanayo waelekeza.

Aidha amesema mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kufanya ukaguzi wa utayari wa Wilaya hiyo katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona, Kamati hiyo imebaini baadhi ya mapungufu ambayo kama wilaya itasimamia kuyarekebisha.

Amefafanua kuwa yote yaliyoonekana kama mapungufu yapo ndani ya uwezo wa Wilaya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha eneo la kuwatenga washukiwa wa Corona lina vitanda vya kutosha na kujenga kichomea taka katika Zahanati ya Saza ambayo itatumika kutibu wagonjwa wa Corona.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe Dkt Humphrey Masoke amesema wameshaagiza vifaa kinga na tiba vyote muhimu katika Bohari kuu ya Dawa ili kuongezea katika vifaa vichache walivyo navyo tayari.

Dkt. Masoke ameongeza kuwa wana endelea kutoa maelekezo na elimu kwa jamii  juu ya tahadhari ya ugonjwa wa Virusi vya Corona kwakuwa bado baadhi ya wananchi wanaamini ugonjwa wa Corona ni wa wazungu hivyo hauwahusu.

Estin Nyangito Mkazi wa Mkwajuni Songwe amesema wamesha pewa elimu ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na Virusi vya Corona na elimu hiyo wataisambaza kwa wananchi wengine ili nao waweze kuchukua tahadhari.

Kwa upande wake Jakson Mwampashi Mkazi wa Songwe amemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kutoa elimu mara kwa mara na kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia magari ya matangazo ya barabarani ili wananchi wote waweze kupata elimu ya Corona


Share:

ASKOFU MWAKIPESILE AWATAKA WANANCHI KUENDELEA KUTII MAELEKEZO YANAYOTOLEWA KUHUSU CORONA BADALA YA KUBEZA


Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Mwakipesile
***
Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Mwakipesile ameiasa jamii kuendeleea kutii maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona na kuhakikisha nchi inakuwa salama na kuondokana watu wanaopuuza maelekezo yanayotolewa.

Ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ibada ya jumapili (5 Aprili, 2020) katika kanisa la EAGT Mlimwa West Jijini Dodoma kuhusu uwepo wa ugonjwa huo na namna Kanisa lilivyopokea maelekezo yanayoendelea kutolewa na Serikali na kuyaishi kwa vitendo.

Dkt. Mwakipesile alieleza kuwa kila Mtanzania ananafasi ya kujali maelekezo muhimu ya kuzingatia wakati wa janga hili la corona na kuwa watii ili kuendelea kupambana na ugonjwa huu na kuhakikisha kila mmoja anakuwa balozi mwema kwa kupambana na janga lililopo nchini.

Aidha alieleza kuwa, majanga yanapotokea ni muhimu kuwa na utulivu na tafakari juu ya hali iliyopo na kuangalia namna bora ya kuenenda na kukubali uwepo wa Mungu katika maisha ya kila mwandamu ili aweze kuponya na kuweka nchi katika hali ya usalama.

“Usalama wa kila mwanadamu upo katika mikono ya Mungu hivyo majanga yanapotokea hatuna budi kuwa watii katika maelekezo yanayopaswa kufuatwa na kuendelea kumgeukia Mungu katika changamoto hii ya corona,”Alieleza

Mwakipesile alieleza kila mmoja ahakikishe anaiombea nchi kwa bidii na kuipenda kwa kuwa Mungu alituweka ndani ya nchi hii kwa makusudi ili kuwa waombezi na walinzi wa nchi yetu wenyewe.

Alifafanua kuwa, ni wakati sahihi wa kuendelea kuunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuamini Mungu pekee ndiye mwenye Mamlaka na uweza wa kuponya na kuokoa nchi ya Tanzania ikiwa ni sambamba na kuruhusu Watanzania kuendelea kufanya ibada huku wakifuata miongozo na melekezo yanayotolewa na Serikali.

Sambamba na hilo ameendelea kupongeza viongozi wa dini kwa mwitikio chanya wa kutii na kuweka taratibu za kujikinga na maambukizi ya virusi hivi kwa kuwahimiza waumini wao kunaa mikono kila wakati, matumizi sahihi ya sanitizer, kuhakikisha wanapokuwa ndani ya nyumba za ibada wanakaa umbali wa mita kati mtu mmoja na mwingine ili kuzuia maambukizi hao.

“Kipekee ninampongeza Mkuu wa Nchi yetu kwa kuona umuhimu wa kuruhusu Wananchi kumwabudu Mungu na kuomba kwa bidii, hii ni ishara tosha kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuzingatia nguvu iliyopo katika maombi na uhakika wa uponyaji wa Mungu nchini,”alisema Dkt. Mwakipesile

Dkt. Mwakipesile alieleza miongoni mwa sababu zinazoruhusu uharibifu ndani ya Taifa ni endapo watu wakashindwa kujizui kutenda dhambi na kugeukia mambo maovu na kuruhusu nguvu za shetani kutesa watu badala ya kumruhusu Mungu kutawala na kuendelea kuponya nchi yao.

“Lazima ifahamike kuwa, nchi itakuwa huru na mahali salama endapo watu wake wataendelea kumgeukia Mungu na kuachana na matendo maovu katikati yao naye Mungu ameahidi kuliangalia Taifa la jinsi hiyo na kuponya uharibifu wa kila aina ikiwemo magonjwa,”alisema Dkt. Mwakipesile

Aidha Dkt. Mwakipesile alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wote wa dini kuendelea kutii Mamlaka zilizopo kwa kuwa zimewekwa na Mungu Dunia na kuwataka Watanzania kuendelea kutambua na kuunga mkono jitihada za viongozi wetu kwa matendo.

“Rais wetu amekuwa wa kipekee na mfano kwa kutambua uwepo wa Mungu na ni lazima tumuombee sana pamoja na viongozi wote na kuzingatia uwepo wetu Tanzania ni kwa makusudi kaisa pasipo kubeza hilo,”alisema

Sambamba na hilo aliwatoa hofu wananchi wote kwa kuzingatia maombi yanayoendelea nchini kuhusu ugonjwa huo na kueleza ni wakati pekee wa kujitenga na dhambi na uovu wa kila namna kisha kumgeukia Mungu pekee ili kupata rehema na haki ya kuponywa.

“Jambo la Msingi katika maisha ya mwanadamu aendelee kutambua nafasi ya Mungu kwa maana ukiacha kumhofu Mungu unapoteza haki ya kupokea uponyaji wake na kubaki katika mateso ambayo hayakuwa mpango wa Mungu kwa wanadamu,”alisisitiza Dkt. Mwakipesile.

Share:

WALIOFARIKI KWA CORONA MAREKANI WAFIKA 12,722.....TRUMP AZIMWAGIA LAWAMA WHO NA CHINA


Marekani imerekodi vifo vingi vya ugonjwa wa corona kwa siku huku watu 1,736 wakifariki siku ya Jumanne.


Idadi hiyo inaweka watu waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini humo kufikia 12,722 kulingana na data za chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Marekani ina wagonjwa 398,000 wa virusi hivyo waliothibitishwa , ikiwa ndio idadi kubwa zaidi duniani . 

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Marekani Trump ametishia kulikatia fedha shirika la afya Duniani WHO kwa sababu amesema shirika hilo halikutilia maanani kwa namna ilivyopasa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. 


Trump amelilaumu shirika hilo kwa kuegemea zaidi upande wa China.  Rais huyo wa Marekani amedai kwamba asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China katika miezi kadhaa iliyopita kupuuza hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Akitoa taarifa juu ya hali ya maambukizi hayo nchini Marekani, Trump alipuuza umuhimu wa taarifa ya mshauri mwandamizi iliyotolewa mapema mwaka huu kutahadharisha juu ya uwezekano wa kulipuka kwa maambukizi hayo. Rais huyo amedai kwamba hakuiona taarifa hiyo.

Badala yake Rais huyo wa Marekani amelishukia shirika la afya duniani WHO na kulitishia kulikatia fedha.Trump amesema asasi hiyo inaegemea sana upande wa China kuhusu mkakati wake wa kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. 



Amedai kwamba Shirika la WHO lilishirikiana na China katika juhudi za nchi hiyo za kupunguza hatari ya mlipuko wa maambukizi hayo.

Rais Trump amesema Shirika hilo limeisifu China ingawa pana sababu ya kuwa na mashaka juu ya idadi rasmi  iliyotolewa na serikali ya China juu ya vifo vilivyotokana na mambukizi ya virusi vya corona.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano April 8



















Share:

Tuesday, 7 April 2020

Mbunge aiomba serikali kumshughulikia Waziri wa Zanzibar aliyedaiwa kugoma kukaa karantini ya corona

Mbunge wa Konde(CUF) Khatib Said Haji ameiomba Serikali kumchukulia hatua Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib aliyekataa kukaa kwenye karantini na kusababisha maambukizi kwa watu wawili kwenye familia yake.

Akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021 amesema matokeo ya Hilo nyumbani kwake kuna watu wawili amewaambukiza na huko hospitali haijulikani matokeo yake nini.

“Ndani ya siku tatu ameng’ang’ana kukaa hospitali ya Mnazi Mmoja matokeo yake akatolewa kwa nguvu baada ya kuona jambo hili limekuwa kubwa sana. Baada ya malalamiko makubwa ndio alikubali kuwekwa kwenye karantini,”amesema.

Amesema alifanya hivyo kwa sababu ya kiburi cha madaraka yake na kumpongeza makamu wa pilli wa Rais Zanzibar kwa kukubali kukaa karantini alipotoka nje ya nchi bila kulazimishwa.

“Huu ndio utu, huu ndio ubinadamu leo waziri huyu ni nani anayekataa uamuzi wa Serikali hata uamuzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.Hatuwezi kumchekea mtu mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu ni waziri ulichukulie hatua haraka."


Share:

Mbowe Ashauri kuundwa kwa kikosi kazi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi zinazotokana na Ugonjwa wa Corona

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Bunge, Freeman Mbowe, ameshauri  kuundwa kwa kikosi kazi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi za ugonjwa huo.

Mbowe aliyasema hayo jana April 6, 2020  wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/21.
 
Alibainisha kuwa sekta ya utalii imeanguka kwa asilimia 99 na kwamba kuna makampuni yamefungwa huku mapato ya nchi yatapungua kwa asilimia 40 kwa miezi sita ijayo.

“Kumekuwa na kauli tofauti,mikusanyiko ambayo haifai na kwamba kuna mikusanyiko ambao wakuu wa mikoa ndio wamekuwa wakiifanya, wanakusanya watu, wanahutubia watu kwamba ugonjwa uko mbali hii ni hatari,”amesema.

Aliongeza “Ningetamani tumsikilize Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Afya kama nchi ikienda kwa kila kiongozi kutoa taarifa ugonjwa huu utawafikisha mahali pabaya.”

Alisema jambo hilo linahitaji kikosi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi na kijamii na pia kuangalia vipaumbe vya Taifa hivi sasa ni vipi.


Share:

Serikali kutoa vitabu Msingi, Sekondari kwa mtandao bure ili Wanafunzi Wajisomee Wakiwa Nyumbani

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Joyce Ndalichako amesema kwasasa serikali inatoa huduma ya upatikanaji wa vitabu vyote kuanzia shule za msingi na sekondari kwenye maktaba bila malipo yeyote kwa njia ya mtandao

“Tunatambua kwamba wanafunzi wapo nyumbani na wanahitaji kuendelea kupata elimu hata wakiwa nyumbani, tunayohuduma ya maktaba inayotolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo kiutaratibu ili uweze kupata vitabu ilipaswa mtu kulipa, sasa serikali inatoa huduma ya upatikanaji wa vitabu vyote kuanzia shule za msingi na sekondari bila malipo yeyote,”amesema.

Amewataka wanafunzi kutumia muda wao kusoma vitabu ambavyo serikali imewapa fursa bila gharama yeyote badala ya kuzurura mitaani na kujiweka  kwenye hatari ya kupata maambukizi ya corona.


Share:

Trump na viongozi wengine duniani wamtakia ahueni Waziri Mkuu Uingereza Ambaye Yuko ICU Kwa Corona

Rais wa Marekani Donald  Trump ameungana na Viongozi wengine Duniani, kutoa pole kwa swahiba wake, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kutokana na kuugua corona. 

"....tumehuzunika kusikia ameingizwa ICU,Marekani inamuombea, tumewasiliana na Madaktari wake kuona kama tunaweza kusaidia"

Waziri Mkuu Johnson alipelekwa hospitali na kulazwa baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya kutokana na kuambukizwa Virusi vya Corona.

Kansela wa Ujerumani Angela merkel na rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi wa ulimwengu waliotuma salamu za kumtakia afya Waziri mkuu wa Uingereza.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amemtumia salamu waziri mkuu Johnson na amemtakia kupona haraka.

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema anasimama pamoja na bwana Johnson, familia yake na watu wa Uingereza katika wakati huu mgumu.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO bwana Tedros Adhanom Ghebreyesus amemtumia kiongozi huyo wa Uingereza salamu za dhati wakati anapopambana na maambukizi ya virusi vya Corona.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger