Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dkt.Harrison G. Mwakyembe amesema mashindano ya kombe la mataifa barani Afrika mwaka 2019 yanayoendelea kufanyika nchini Misri, yamebeba uzito wa kipekee kwa nchi ya Tanzania baada ya kukaa nje kwa miaka thelathini na tisa(39) na kufuzu kushiriki katika mashindano hayo ambayo Timu ya Taifa ya Tanzania imetupwa nje katika hatua ya makundi baada ya kupambana na timu za Senegal, Algeria na Kenya.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari tarehe 6 Julai, 2019 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Raia wa Nigeria Emmanuel Amunike katika hotel ya Protea Courtyard Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa bado ana imani kubwa na Kocha huyo kuendelea kufanya vizuri ,kinachohitajika ni swala la muda tu, kwani amemueleza mipango mikubwa ya kiufundi aliyonayo kwa Timu ya Taifa hili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo.
“Ndugu waandishi wa Habari kwanza kabisa niseme tu kwamba, nimefurahi sana kukutana na kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, ambapo lengo la kukutana naye ni kunieleza kilichotokea kule nchini Misri katika mashindano ya Afcon ambayo tumeshiriki baada ya miaka 39 kupita,
"Mashindano haya yamebeba uzito wa kipekee kwa nchi yetu, na niseme tu kwamba nina imani kubwa sana na kocha Amunike kuendelea kufanya vizuri na yetu, nimeongea naye mambo mengi sana kuhusu mashindano, na tumeona kama Wizara tumpe muda zaidi kwa mipango mizuri ya kiufundi aliyonayo kwa Timu ya Taifa hili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo,”.
“Mimi nimefurahi sana kukaa na mwalimu, na yeye pia amefurahi kukaa na Serikali, ili tujuwe mwenzetu maoni yake ni nini kuhusu timu ya Taifa, tufanyaje kujipanga hili kesho, kesho kutwa turejee tena Afcon lakini safari hii tukirejea kila mtu awe na wasiwasi kuwa hii sio timu nzuri kukutana nayo
"Ametupa mfano mzuri sana, kwamba Uganda mwaka 2015 iliposhiriki mara mwisho haikufanya vizuri hata kidogo, lakini wenzetu wakarudi wakaanza kuyafanyia kazi mapungufu katika mchezo wao, badala ya kukaa mwaka mzima mnalumbana na kunyoosheana vidole, mapungufu kwenye timu ya kiufundi na sisi kwa upande wetu yamejitokeza sana,
"Mengi sitayasema kwa sababu ni mambo ambayo tutakaa na vyombo vinavyohusika, lakini cha msingi tunafurahi sana mwalimu ana moyo chanya kwamba tunaweza, tumeonyesha watanzania kwamba tunaweza, lakini kiufundi inatakiwa na sisi tujiongeze,” alisema Mheshimiwa Mwakyembe.
Aidha Mheshimiwa Mwakyembe amesema Kocha Amunike amependekeza mazoezi zaidi kwa wachezaji wa Timu ya Taifa pamoja na kucheza mechi za kirafiki kimataifa mara Tatu kwa Mwaka hili kuweza kupata uzoefu zaidi katika mashindano ya kimataifa.
“Tatizo lililojitokeza ambalo mwalimu anadhani linaweza kutatuliwa ni mazoezi kwa timu ya Taifa,kwamba angalau mara tatu timu ya Taifa kila mwaka ikawa na mechi za kirafiki, wanaitwa leo wanacheza na Zambia , na Afrika Kusini, tumewakaribisha pengine Spain wanakuja na kuangalia mbuga za wanyama, tunajenga imani ya wachezaji wetu, kwenye mashindano haya yaliyopita tumeona kuna wakati wachezaji wetu walikosa kujiamini, unaona mchezo kadri unavyoendelea ndio sasa hata pasi za uwakika ndio zinapigwa, kwa hiyo ni kujiamini lakini vijana wa Tanzania walicheza vizuri sanaa,” alisema Mwakyembe.