Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza
vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama
Kikuu cha Ushirika cha Nyanza ambazo zilinunuliwa na kutwaliwa na watu
binafsi kwa njia za ujanja ujanja.
Rais
Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa
akiwahutubia wananchi wa Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.
Dkt.
Magufuli alisema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu
wachache waliovifilisi vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha
mali za ushirika yakiwemo majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali
hizo zirudishwe mikononi mwa wananchi.
"Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma" Alisema Rais Magufuli.
Katika
Mkutano huo Rais Magufuli pia alisema Serikali itafanya oparesheni
kubwa ya kuteketeza Makokoro katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za
kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki
na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika
viwanda.
Alibainisha
kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana
ili lengo la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo
viwanda vya kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.
Kabla
ya kuhutubia mkutano huo Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi
wa daraja la waenda kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya
Uwanja wa Ndege kwenda katikati ya Jiji la Mwanza.
Daraja
hilo litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta
5.5 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 6.455
Akizungumzia
ujenzi huo Rais Magufuli alimtaka Mkandarasi anayejenga Daraja la
Furahisha kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa
mkataba, na pia ameagiza Mkandarasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja
wa Ndege wa Mwanza kuendelea na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa
Serikali imejipanga kumlipa fedha za kazi hiyo.
Pia
Dkt. Magufuli ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia
nne kutoka Katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza
ili barabara hiyo ifike hadi uwanjani badala ya kuishia eneo la
Pasiansi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
11 Agosti, 2016