Friday, 20 November 2026

SERIKALI YALENGA KAYA ASILIMIA 90 KUPATA MAJI SAFI NA SALAMA IFIKAPO 2030

...


Na Dotto Kwilasa – DODOMA

SERIKALI imesema upatikanaji wa takwimu sahihi na za uhakika ni miongoni mwa nguzo muhimu zitakazowezesha kufikiwa kwa lengo la kuhakikisha angalau asilimia 90 ya kaya nchini zinapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030.

Takwimu hizo zinatarajiwa kusaidia kutathmini hali halisi ya upatikanaji wa huduma za maji nchini, kubaini maeneo yenye upungufu na kuelekeza uwekezaji kulingana na mahitaji halisi ya wananchi.

Akizungumza katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Anna Makinda, alisema takwimu rasmi ni nyenzo muhimu katika kupima utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuwawezesha watunga sera kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi.

Alisema kufikiwa kwa lengo la kuongeza idadi ya kaya zinazopata maji safi na salama kunahitaji mifumo imara ya ukusanyaji, uchambuzi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

"Lengo la kuongeza kaya zinazopata huduma ya maji safi na salama hadi kufikia angalau asilimia 90 ifikapo mwaka 2030 linahitaji takwimu sahihi zinazopatikana kwa wakati ili kupima hatua zinazofikiwa," alisema Makinda.

Alisisitiza kuwa pamoja na kuzalisha takwimu, ni muhimu kuhakikisha zinawafikia watumiaji wa mwisho, hususan watunga sera, ili zitumike katika kupanga na kusimamia shughuli za maendeleo badala ya kubaki kwenye nyaraka za ofisi.

"Watunga sera wanapaswa kuhakikisha kuwa takwimu zote zinazopatikana zinawafikia walaji wa mwisho na siyo kuendelea kubaki kwenye makabrasha," alisema.

Makinda alisema Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti ya NBS ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzalisha takwimu zinazokidhi mahitaji ya watumiaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ally Munde, alisema matumizi ya takwimu sahihi yana mchango mkubwa katika kuboresha mipango ya maendeleo kwa kusaidia Serikali kutambua mahitaji ya wananchi na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Alisema taarifa hizo zinapaswa kutumika katika kupanga na kutekeleza miradi ili kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unakuwa na tija na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

"Takwimu sahihi ni nyenzo muhimu katika kupanga huduma za kijamii na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inazingatia hali halisi ya wananchi," alisema Munde.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu inayohusu kuimarisha mifumo rasmi ya takwimu za maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu yanayohimili mabadiliko ya tabianchi inapaswa kupewa kipaumbele katika uzalishaji na matumizi ya takwimu nchini.

Alifafanua kuwa takwimu hizo zitasaidia kubaini maeneo yenye changamoto katika upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, hatua itakayowezesha Serikali kuweka mikakati ya kuboresha huduma hizo.

Aidha, alisema upatikanaji wa takwimu kwa wakati ni muhimu katika kuandaa mipango inayozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha rasilimali zinazowekezwa zinatumika kwa ufanisi.

Munde alisisitiza umuhimu wa kutumia takwimu katika kufanya maamuzi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji unaofanyika katika sekta mbalimbali.





Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger