
Meneja Mkazi wa Barrick nchini Dk. Melkiory Ngido akiongea katika mkutano wa saba wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania unaondelea jijini Dar es Salaam ambao umefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ukijumuisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali nchini na duniani.

Picha ya pamoja ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi na viongozi wa makampuni yaliyodhamini mkutano wa saba wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania unaondelea jijini Dar es Salaam.
#Uwekezaji wake kuendelea kuwanufaisha Watanzania
Kampuni ya Barrick yenye ubia nchini na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga, imebainisha kuwa itaendelea kufanya shughuli zake za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia weledi, ufanisi na kufuata sheria na kanuni huku ikihakikisha sehemu kubwa ya manufaa ya uwekezaji yanabakia hapa nchini.
Barrick inashiriki na ni mdhamini mkuu wa mkutano wa saba wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania unaondelea jijini Dar es Salaam ambao umefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Deogratius Ndejembi,ukiwa unajumuisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali nchini na duniani.
Akizungumza kwenye huo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt Melkiory Ngido amesema kuwa jambo kubwa linaposwa kuangaliwa kwa kina katika sekta ya madini ni namna inavyochangia katika uchumi wa nchini na kuboresha maisha ya watanzania.
Amesema ubia wa serikali ya Tazania na kampuni ya Barrick ambao ulianza mwaka 2019 unaendelea kuleta matokea chanya mbalimbali na kwa kiasi kikubwa kuchangia pato la taifa sambamba na ukuaji wa uchumi wa kijamii.
“Tangu tulipoanza kusimamia migodi ya Barrick nchini Tanzania mwaka 2019, imekuwa faraja kuona kampuni yetu ikiendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania,” amesema Dkt. Ngido.
Amesema katika kipindi cha miaka sita, mchango wa kampuni ya Barrick katika uchumi wa Tanzania umefikia zaidi ya shilingi trilioni 16, ambazo zimeingizwa katika mzunguko wa uchumi wa ndani.
Dkt. Ngido ameongeza kwamba kwa mwaka 2025 pekee, mchango wa kampuni ya Barrick hapa nchini umefikia takribani shilingi trilioni 2.2 huku kiasi cha shilingi trilioni 4.7 zimelipwa kama kodi kwa mamlaka za serikali na zaidi ya shilingi 700 bilioni zimelipwa kwa Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) kama sehemu ya gawio la serikali linatokana na faida inayopatikana.
Amesema migodi ya Barrick-Twiga ya North Mara na Bulyanhulu ina jumla ya wafanyakazi zaidi ya 6,400, ambapo asilimia 95 ni Watanzania na kati yao asilimia 77.7 wanatoka katika maeneo yanayozunguka migodi hiyo.
Kuhusu uwekezaji katika miundombinu na huduma za jamii alisema migodi ya Barrick imefanikisha miradi mbalimbali ya kijamii ya kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo yanayozunguka migodi yake kupitia fedha za uwajibikajinkwa jamii CSR hususani katika sekta za afya,elimu,maji safi na miundombinu na kutolea mfano mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha laimi kahama- kakola yenye urefu wa kilomita 73 inayoghalimu shilingi za kitanzania 104 bilioni.
Dkt. Ngido amewaleleza washiriki wa mkutano huo wa kimataifa jinsi kampuni inavyoendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kusongesha mbele mustakabali wa elimu nchini ujulikanao kama Barrick-Twiga Forward Future Education program utakaogharimu zaidi ya bilioni 70 hadi kukamilika ambao unaolenga kuboresha miundombinu ya shule za sekondari ikiwa ni jitihada za kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kupata elimu nchini.
“Kwenye kuunga mkono juhudi hizi za Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na serikali tumefanikisha ujenzi wa madarasa 1,021 na mabweni 270 nchini nzima,” amesema Dkt. Ngido.
Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Dkt. Ngido ameongeza kwamba kampuni ya Barrick pia iliingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia mkataba wa miaka 10 wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 26 kwa ajii ya kusaidia kujenga ujuzi, utaalamu na weledi kwa wanafunzi , wanataaluma na wanajumuiya wa chuo katika kuchangia maendeleo ya sekta ya madini hapa nchini vilevile katika kufanikisha dhamira yake ya kusuka kizazi kipya cha wataalamu wa tasnia ambapo imeanzisha programu ya kutoa udhamini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kusoma taaluma ya madini nje ya nchi ambapo hadi sasa wanafunzi 5 wa kitanzania wanasomeshwa katika chuo kikuu cha Johanessburg nchini Afrika ya Kusini.
Amesema Barrick inaamini kuwa mustakabali wa sekta ya madini ni mzuri na kwamba uwekezaji katika elimu na utaalamu ni muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Uendelevu wa migodi na uwekezaji wa baadaye
Amefafanua kwamba pamoja na mafanikio hayo, Barrick inaendelea kuwekeza katika kuhakikisha kuwa migodi yake inaendelea kuzalisha kwa muda mrefu.
“Tunaendelea kufanya tathmini na uwekezaji katika kuongeza muda wa uhai wa migodi yetu, ikiwemo migodi ya North Mara na Bulyanhulu,’ amesema.
Makamu wa Rais – Deogratias Ndejembi
Mgeni rasmi kwenye mkutano huo wa saba wa uwekezaji kwenye sekta ya madini ,Makamu wa Rais , Deogratias Ndejembi amesema kuwa ni muhimu kwa sekta hiyo ifunganishwe na sekta zingine ili kukuza mnyororo wa thamani.
"Sekta ya madini imeanza kuwa na mchango mkubwa kwenye mapato ya nchini , ajira na uchumi ila ni muhimu kuhakikisha kwamba sekta hiyo inakuza mnyororo wa thamani kwenye sekta zingine hapa nchini na matokeo yake yawe ni chanya kwa wananchi wote",amesema.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kwamba kwa mara ya kwanza mkutano huo wa kimataifa wa uwekezaji kwenye sekta ya madini umeweza kuwaleta washiriki takribani 1,715 kutoka ndani na nje ya nchini.
“Idadi kubwa ya washiriki kwenye mkutano huu wa saba ya kimataifa wa uwekezaji kwenye sekta ya madini ni tafsiri kubwa na pana kwenye diplomasia ya kiuchumi hapa nchini,” amesema Mavunde.
Ameongeza kuwa sekta ya madini nchini inaendelea kukua kwa kasi na mchango wake kwenye Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 10.3 na imeingiza fedha za kigeni takribani dola za kimarekani bilioni 5.40.

0 comments:
Post a Comment