Friday, 6 March 2026

ACHENI HEKAHEKA ZA MTANDAONI ZENYE NIA OVU, CHANGAMKIENI FURSA

...




WAKATI baadhi ya vijana wakipoteza muda mwingi mitandaoni kukuza chuki, kulalamika na kushusha hadhi ya nafsi zao, Serikali imewapigia kipyenga wasomi wa vyuo vikuu kutumia akili zao kubuni miradi itakayowaingizia "mkwanja" na kuwafanya mabilionea wa kesho.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Fatma Mabrouk Khamis, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Afrika Mashariki na India.

 Fatma ameweka wazi kuwa Serikali ya Zanzibar Awamu ya Nane imeweka kipaumbele cha kufa mtu kwenye sayansi na teknolojia, ikilenga kuwabadilisha wasomi kutoka kuwa wasaka ajira na kuwa wabunifu wa miradi inayozalisha mali.

“Wasomi wetu, wakati wa kushinda mitandaoni bila tija umepitwa na wakati. Huu ni wakati wa kuongeza ubunifu, kubuni miradi ya uzalishaji na kuingia kwenye ujasiriamali,” alisema Fatma huku akisisitiza kuwa idadi ya wahitimu ni kubwa kuliko nafasi za serikalini, hivyo njia pekee ya ushindi ni kujiajiri kupitia sekta binafsi.

Katika kile kinachoonekana kama "mchongo" wa uhakika, Joseph Evarest kutoka Shirika la UNDP kupitia programu ya FUNGUO, amebainisha kuwa wapo tayari kuviunganisha vyuo vikuu vya Tanzania na mataifa kama India na Uingereza. Mpango huu si wa nadharia tu, bali unalenga kubadilisha mawazo ya ubunifu ya wanafunzi kuwa biashara halisi zinazopata ufadhili wa fedha, ili kijana aweze kusimama mwenyewe kiuchumi badala ya kukata tamaa.

Baadhi ya wanafunzi waliochangamkia fursa hiyo, akiwemo Kelvin Hemu (UDSM) na Happy Weston, wamethibitisha kuwa tayari wapo kwenye mchakato wa kuibua mawazo yatakayowapa fedha za kuendeleza kazi zao. 

Huu ni ujumbe tosha kwa vijana: Badala ya kutumia bando lako kusononeka na hali ya maisha, tumia ubunifu wako kufungua milango ya maendeleo, kwani amani iliyopo nchini ndiyo uwanja mpana wa wewe kujiwekea akiba na kupata tija.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger