Tuesday 12 March 2024

JAPAN YASHAURI MABORESHO KATIKA UCHUMI

...

 


 Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa JATA jijini Dar es Salaam
                       ***********

BALOZI wa Japan nchini Yasushi Misawa amesema ili Tanzania kuendelea zaidi ihakikishe inaboresha maeneo ya kimkakati ikiwemo viwanda, afya, mazingira, elimu na sekta muhimu kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa shirikisho la watanzania wanufaika wa program za mafunzo ya JICA ( JATA,) Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa, amesema hatua ya maendeleo ambayo nchi nyingi za bara za Asia zimepitia ikiwemo Japani kukua kwa uchumi wa Nchi na jamii kwa ujumla kunatokana na uboreshaji wa miundombinu, sera za maendeleo ya viwanda, sekta ya rasilimali watu pamoja na mafunzo ya ufundi.

Aidha Balozi Yasushi, amesema kupitia Shirika la Maendeleo la Japan Tanzania(JICA ) wataendelea kutoa mafunzo ya ujuzi kwa Watanzania na kuwezesha miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi huku akidai kuendelea kufanikisha miradi kupitia wanafunzi waliowapa ufadhili ikiwemo mradi wa Hatua project.

“JICA imechangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikijikita katika rasilimali watu na kumekuwa na fursa nyingi za mafunzo na miradi na siku ya leo ninafuraha kushiriki na kujua kutoka kwa wanachama wa JATA ambapo kuna miradi kama HATUA ulioanzishwa kutatua matatizo ya wananchi nah ii inaendana na mikakati yetu,”amesema.

Amesema tayari wadau kutoka Japan na serikali walijadili kuhusu changamoto za kiuchumi na kijamii ambapo wataweza kufanikiwa kutokana na ujuzi waliotoa na uzoefu walionao.

Katika hatua nyingine Misawa amesema, Uhusiano bora baina ya Tanzania na Japan umekuwa ukichangia maendeleo ya kijamii na uchumi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya Hatua inayotekelezwa na wanachama wa JATA ambayo ina manufaa kwa watanzania kwa kuwa inalenga kutatua changamoto za kijamii ambayo ni moja ya mkakati wa JICA.

Pia ametumia wasaa huo katika kusherekea siku ya wanawake duniani kuwapongeza wanawake wa Tanzania kwa utendaji kazi uliotukuka na kueleza kuwa uhusiano wa ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Japan umelenga wanawake pia katika kuchukua nafasi sawa na wanaume.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA,) Ara Hitoshi amesema, JATA watumie fursa za jukwaa hilo kubadilishana ujuzi, uzoefu na maarifa kwa mafunzo waliyopata na hiyo ni pamoja na kujitolea ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Ameeleza kuwa uhusiano wa jukwaa hilo ni muhimu kwa JICA ambayo itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi za Umma na sekta binafsi ili kuendelea kuleta matokeo chanya ya maendeleo.

" Uhusiano wa Tanzania na Japan ni imara na kupitia JICA imekuza ushirikiano huu na kupitia JATA tunaamini ujuzi mliopata kutoa mawazo, fursa na kwa jamii na kuleta matokeo yenye tija zaidi katika sekta sekta mbalimbali." Amesema.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Utumishi Leila Maviki amesema Serikali ya Tanzania inathamini jitihada za Serikali ya Japan katika kuchochea maendeleo ya Tanzania kupitia fursa za masomo na mafunzo yatolewao wa watanzania ikiwemo watumishi wa Umma ambao wamepata mafunzo kupitia JICA katika uga za afya, TEHAMA, sekta ya maji na kilimo.


Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa JATA Gregory Mlay amesema kuwa shirikisho hilo limewakusanya watanzania waliopata fursa ya kusoma nchini Japan ikiwemo waliopata kupitia ufadhili wa JICA umelenga kuendeleza uhusiano wa kimaendeleo, uhusiano, ushirikiano, kubadilishana uzoefu pamoja na kudumisha uhusiano na kuendelea kufanya kazi na JICA.

Mradi wa Hatua ulianza mwaka 2022 kwa miradi mitano ambayo miradi miwili ilitekelezwa mwaka 2022 na mitatu ilitekelezwa mwaka 2023 kwa lengo na kupata fursa ya kutumia Teknolojia waliyoipata Japan kwa manufaa ya Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwa JICA 1962 hadi mwaka 2022 jumla ya wanafunzi wa Kitanzania 147,863 wamepewa ufadhili wa masomo na shirika hilo katika nchi mbalimbali duniani.  
Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa (wa pili kulia) Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA, wa pili kushoto) wakifuatilia mada wakati wa mkutano huo. Kulia ni Mwenyekiti wa JATA Gregory Mlay na kushoto ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Utumishi, Leila Maviki.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger