Zanzibar, 18 Novemba, 2021 – Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma za kibenki zinazozingatia misingi ya kiislam “CRDB Al Barakah Banking,” akibainisha kuwa kupatikana kwa huduma hizo kupitia matawi ya Benki ya CRDB kutasaidia kuongeza ujumuishi wa kifedha visiwani humo na Tanzania kwa ujumla.
Rais Mwinyi amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Michenzani Mall na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Benki Kuu ya Tanzania, Benki ya CRDB, pamoja na wateja wa benki hiyo na wananchi.
“Nafahamu wapo watu ambao walikuwa hawajajiunga na mfumo rasmi wa kibenki kutokana na kutokuwepo au kutopatikana kwa urahisi kwa huduma zinazoendana na imani yao ya kiislam. Huduma hii ya CRDB Al Barakah itakwenda kuwa jibu kwa changamoto zao na kuwawezesha kunufaika na huduma za kibenki,” alisema Rais Mwinyi.
Aidha aliwahimiza wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Benki hiyo kupitia CRDB Al Barakah akisema zitawawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo nchini. Alisema kwa kiasi kikubwa maendeleo yanahitaji fedha ambazo zinaweza kupatikana aidha kwa kujiwekea akiba benki au kupitia uwezeshaji wa mikopo, hivyo ni vema wananchi wakitambua fursa hizo na kuzitumia vizuri kujipatia maendeleo.
Akitoa mada kuhusu huduma zinazopatikana kupitia CRDB Al Barakah, Mkuu wa Kitengo cha Islamic Banking Benki ya CRDB, Rashid Rashid alibainisha kuwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na utunzaji wa amana ambapo kuna akaunti zaidi ya kumi na tano zinazogusa makundi mbalimbali ya wateja ikiwamo watoto, wanafunzi, wakinamama, wajasiriamali, wafanyabiashara na taasisi.
Aliongezea kuwa ili kuhakikisha misingi inafuatwa Benki hiyo pia imeunda Bodi ya Ushauri na Usimamizi wa CRDB Al Barakah ambayo imejaa wataalamu na wabobezi wa huduma za kibenki zinazozingatia misingi ya dini ya kiislamu kutoka ndani ya nchi, ukanda wa Afrika Mashariki na duniani.
Rais Mwinyi alisema Benki hiyo imeonyesha uzalendo wa hali juu katika kubuni na kutekeleza mpango huo ambapo mbali na fedha zinazotolewa na GCF yenyewe pia imetenga dola za kimarekani milioni 100 na hivyo kufanya jumla ya fedha kufikia dola za kimarekani milioni 200 sawa na shilingi bilioni 460.


0 comments:
Post a Comment