Wednesday, 6 October 2021

COSTECH YATOA MAFUNZO YA UANDISHI WA HABARI ZA SAYANSI,TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

...

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Time ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika mafunzo ya waandishi wa habari na watafiti,ambaye pia ni Mkurugenzi wa Menejiment ya Maarifa katika Tums hiyo Dkt Philbert Luhunga akitoa mada ya umuhimu wa Utafiti na usambazaji wa matokeo ya utafiti wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kwa Waandishi wa habari na watafiti.

Afisa wa program ya mafunzo ya waandishi wa habari na watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (COSTECH) ,Deusdedith Leonard akieleza malengo ya mafunzo.

Na Dinna Maningo, Mwanza

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya  Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika mafunzo ya waandishi wa habari na watafiti, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Menejiment ya Maarifa katika Tume hiyo Dkt Philbert Luhunga, amesema kuwa watafiti mbalimbali wamekuwa wakifanya tafiti katika masuala ya kisayansi lakini kazi zao haziwafikii wananchi kutokana na lugha inayotumika kufikisha taarifa hizo kwa wananchi.

Dkt. Luhunga amewataka Waandishi wa Habari kuziandika taarifa za sayansi, teknolojia na ubunifu na kuzitangaza kwa lugha rahisi inayo tambulika na wananchi jambo ambalo litachochea kwa kasi utumiaji wa taarifa hizo na hivyo kuchagia kwenye maendeleo endelevu ndani ya jamii. 

Aliyasema hayo wakati akitoa mada ya umuhimu wa utafiti na usambazaji wa matokeo ya utafiti kwenye mafunzo ya siku mbili ya uandishi wa habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu yaliyotolewa na Tume hiyo kwa waandishi wa Habari 25 na Watafiti 15 kutoka mkoa wa Kagera,Mara na Mwanza yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza.

"Mfano watafiti wanafanya tafiti za mbegu nzuri za kilimo lakini wananchi wanashindwa kuzitumia mbegu hizo maana hawazifahamu mbegu hizo,waandishi wa habari mkiandika Habari za matokeo ya tafuti mtasaidia kazi za watafiti wa sayansi, teknolojia na ubunifu kutambulika na kutumiwa na jamii", alisema  Dkt. Luhunga.

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Mwanza Emilly Kasagala alisema kuwa taarifa nyingi za utafiti zinafanyika zikiwemo za kilimo lakini namna ya kuwafikia walengwa ambao ni wananchi bado ni tatizo .

Kasagala aliipongeza Costech kwa kutoa mafunzo nakwamba yatawasaidia Waandishi wa habari kuandika habari za kisayansi kwa lugha rahisi ambayo itawafikia wananchi kwa urahisi.

"Watafiti wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali za kisayansi lakini matokeo ya tafiti hizo haziwafikii wananchi kwa wakati na hivyo baadhi ya tafiti kutokuwa na matunda mazuri ndani ya jamii" ,alisema Kasagala.

Akieleza malengo la mafunzo hayo,Afisa wa Programu ya mafunzo  kutoka COSTECH Deusidedith Leonard,alisema kuwa Tume hiyo inaendesha mafunzo ya siku mbili Oktoba 5-6/2021 ya namna ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (STU) kwa Watafiti na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema kuwa lengo lingine ni kuwapa uelewa wa kuwasilisha taarifa za kitafiti kwa lugha rahisi, kisha wanahabari waweze kuchakata na kufikisha taarifa hizo kwa walengwa wakiwemo watunga Sera,Wafanya maamuzi na wananchi.

Leonard alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwahamasisha na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuandika taarifa za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu.

"Tunawajengea uwezo Watafiti na Waandishi wa Habari kama ilivyo katika nyanja nyingine kama vile Michezo, Siasa,na Biashara,mafunzo yatatoa fursa kwa waandishi wa habari kutoa maoni,ushauri pamoja na mapendekezo ya jinsi ambavyo wangependa Tume iweze kuyafanyia kazi ili kuhakikisha taarifa za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu zinasambazwa kwa urahisi kwa wananchi", alisema.

Leonard aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo ya siku mbili Tume itafanya ziara ya kimafunzo Oktoba,7-8,2021 kwa waandishi wa habari walioshiriki mafunzo kutembelea miradi mbalimbali ya utafiti na Ubunifu ili kupata maudhui ya kuandaa taarifa kwa ajili ya vyombo vyao vya habari

Waandishi wa habari na Watafiti kutoka mkoa wa Kagera,Mara na Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Menejiment ya Maarifa kutoka COSTECH.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger