Monday, 23 August 2021

MAMA MARIAM MWINYI AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA TAMASHA LA KIHISTORIA LA KIZIMKAZI

...

 

Mke wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Ujasiriamali kwa wananchi wa Mji wa Kizimkazi pamoja na Uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2021, uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Skuli wa Sekondari ya Kizimkazi, Zanzibar leo Agosti 23, 2021, kwa udhamini wa Benki ya CRDB.
 
==========    =========
 
Mke wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kufanikisha uandaaji wa Tamasha la Kizimkazi 2021. Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi ambapo alikua mgeni rasmi katika uzinduzi huo ulioanza kwa semina ya wajasiriamali 300 iliyoratibiwa na Benki ya CRDB.
 
Akizungumzia katika uzinduzi huo Mh. Mariam Mwinyi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwaongezea maarifa wajasiriamali jambo ambalo litakwenda kuongeza tija katika uendeshaji wa biashara zao.  Aliongeza kuwa malengo ya semina hiyo kwa wajasiriamali yanaendeana na malengo ya Serikali ya Awamu ya 8 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya uwezeshaji wa wajasiriamali.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuwawezesha wajasiriamali ambapo pamoja na mambo mengine Serikali imeanzisha mfuko wa uwezeshaji kwa wajasiriamali, imefanya uteuzi wa Katibu Mkuu maalum anaeshughulikia masuala ya uwezeshaji lakini pia imeendelea na juhudi za kuhamasisha taasisi za fedha ikiwemo Benki ya CRDB kusaidia uwezeshaji kwa wajasiriamali” alisisititiza Mh. Mariam.
 
Pamoja na kupongeza shughuli za kitamaduni, sanaa na michezo zitakazofanyika katika tamasha hilo, Mh. Mariam Mwinyi ameiomba Benki ya CRDB kuendelea kusaidia wakazi wa Kizimkazi katika eneo la elimu hasa kwa kusaidia upatikanaji wa vifaa ya maabara mashuleni. Sambamba na wito huo kwa Benki ya CRDB, Mh. Mariam alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanasimamia vyema malezi ya watoto na kuwahimiza katika elimu ambayo itawasadia  katika maisha yao huku akitoa mfano wa Rais wa Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania,       Mhe. Samia Suluhu Hassan ambae ni mzaliwa wa Kizimkazi.
Nae Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Benki ya CRDB, TullyEsther Mwambapa alisema Benki ya CRDB imedhamiria kubadirisha maisha ya wana Kizimkazi kupitia sera yake ya kurudisha kwenye jamii ambapo kila mwaka Benki hutenga asilimia moja ya faida yake kuwekeza katika jamii. Sambamba na ufadhili wa tamasha la Kizimkazi, Benki ya CRDB  imekamilisha ujenzi wa miradi miwili ya maendeleo ambayo itakabidhiwa kwa Mgeni Rasmi  wa Tamasha la Kizimkazi 2021 ambae ni Rais Samia Suluhu Hassan  siku ya kilele cha tamasha Agosti 28.
 
“Imani yetu ni kuwa fursa zitakazopatikana kupitia Tamasha la Kizimkazi zitaleta hamasa kubwa na kuchochea shughuli za kiuchumi hapa Kizimkazi na hivo kuongeza mchango wa wana Kizimkazi katika kutekeleza dhana ya Uchumi wa Bluu ambayo inaongoza Serikali ya Awamu ya 8 ya Mapinduzi ya Zanzibar” aliongeza Tully.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mh. Rashid Hadid Rashid alisema tamasha la mwaka huu litakua la kihistoria kutokana na kupewa nguvu kubwa na Benki ya CRDB ambayo imekua mdau mkubwa wa Kizimkazi tangu tamasha hilo lilipoanza kama Samia Day mnamo mwaka 2016.
 
“Nawashukuru sana Benki ya CRDB kwa kutoa ufadhili mkubwa kwenye tamasha la Kizimazi kwa mwaka huu ambalo pamoja na mambo mengine ya kimaendeleo pia litajumuisha usafi wa mazingira, mashindano ya michezo mbali mbali ikiwemo  mpira wa miguu na pete, kufua na kukuna nazi, nage, karata , bao, kuvuta kamba, resi za baskeli, resi za ngalawa, shomooo , na mashindano ya kuhifadhi Qurani”alisema Mh. Rashid.
 
Pamoja na shughuli hizo za kimaendeleo, utamaduni, sanaa na michezo, wananchi ambao watahudhuria Tamasha la Kizimkazi watapata fursa ya kupata chanjo ya UVIKO 19 ambapo itatolewa katika viwaja vya Kizimkazi Dimbani Mji Mpya. Zoezi hilo litaongozwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Ahmed Nassor Mazrui.
Mke wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi akiwapungia wananchi wa Mji wa Kizimkazi, wakati alipowasili kwenye Ukumbi wa Skuli wa Sekondari ya Kizimkazi, Zanzibar leo Agosti 23, 2021 kwa lengo la ufunguzi wa Mafunzo ya Ujasiriamali Tamasha la Kizimkazi 2021. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, ambao ndio wadhamini wakuu wa Tamasha hilo.
Sehemu ya Wananchi wa Mji wa Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar wakimsikiliza Mgeni Rasmi Mke wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Ujasiriamali kwa wananchi wa Mji wa Kizimkazi pamoja na Uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2021, uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Skuli wa Sekondari ya Kizimkazi, Zanziba.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger