Baadhi ya watalii kutoka Israel wakipita kuangalia kikundi cha utamaduni kutoka kabila la Wamasai katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kuondoka kurejea Israel
Baadhi ya watalii kutoka Israel wakiwa katika eneo la kuondokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kabla ya kuondoka kurejea Israel
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemedi Mgaza akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel
Kaimu Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Christina Kamuzola akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel
Afisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Michael Makombe akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya watalii kuondoka kuelekea Israel
*****************************
Na Waandishi wetu, Arusha
Mamia ya watalii kutoka Israel waendelea kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii licha ya changamoto ya Ugonjwa wa UVIKO-19 ambao umeikumba dunia hivi sasa.
Kuja kwa watalii hao kunatokana na sio tu Tanzania kubarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, bali pia hatua za tahadhali zinachokuliwa na Serikali dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO-19.
Hatua hizo ambazo zimewejengea imani watalii kuendelea kuja nchini zimetambuliwa na Baraza la Wasafiri na Utalii Duniani (World Travels and Tourism Council-WTTC) ambapo Mwezi Agosti 2020 baraza hilo liliitangaza Tanzania kuwa nchi salama ya kuitembelea.
Akizungumza Jijini Arusha, wakati wa hafla ya kuwapokea watalii takribani 100 kutoka Israel na wengine 150 waliokuwa wanaagwa, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemedi Mgaza amesema ujio wa watalii hao umetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel na wadau wengine wa utalii za kutangaza vivutio vya utalii nchini humo.
Juhudi hizo ni pamoja na kushiriki maonesho ya utalii yanayofanyika kila mwaka nchini Israel ambapo kwa mwaka huu yamepangwa kufanyika mwezi Oktoba, kushiriki katika vyombo vya habari mbalimbali nchini humo pamoja na kuwatumia mawakala wa utalii, kampuni za kuongoza watalii na waandishi wa habari.
Mmoja wa watalii waliokuwa wanaagwa leo, Bw. Lior Ziegler aliwahakikishia Watanzania kuwa Watalii kutoka Israel wataendelea kuja nchini kwa sababu Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, huduma bora ikiwemo na mapokezi mazuri ya kuridhisha.
“Nimefurahia kutalii katika vivutio mbalimbali vya utalii hapa Tanzania kwa kweli ni vizuri sana…..nitaendelea kuhamasisha Waisrael kuja kutembea hapa na kujionea wenyewe vivutio hivyo adhimu,” Amesema Bw. Ziegler
Kauli hiyo imeungwa mkono na Afisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Michael Makombe ambapo alieleza kuwa watalii hao wamevutiwa na Bonde la Ngorongoro kutokana na mazingira yake ya upekee, wanyama kuonekana kwa urahisi pamoja na historia ya Olduvai Gorge ambapo ni eneo linaloaminika kuwa fuvu la mtu wa kale zaidi duniani limegunduliwa.
Kwa upande wa Kaimu Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Christina Kamuzola amesema TTB kwa kushirikiana na Serikali na wadau kutoka sekta binafsi itaongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii ili kufikia malengo ya Serikali ya kuleta watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni 600 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya 2020-2025.
Juhudi hizi ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Tarehe 27 Julai, 2021 akiwaapisha mabalozi wapya 13 na kuwaagiza pamoja na mambo mengine, kutangaza vivutio vya utalii, fursa za kiuchumi pamoja na uwekezaji zinazopatikana nchini.
0 comments:
Post a Comment