Sunday, 6 June 2021

MBUNGE MPINA ATAKA BUNGE KUWAWAJIBISHA MAWAZIRI WALIOVUNJA KATIBA

...

 

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni Dodoma na kuitaka Serikali kuwawajibisha viongozi waliokaidi amri ya Mahakama kuhusu mifugo 6,000 iliyokamatwa na Mahakama kuamuru kurejeshewa wamiliki wake ambapo Serikali imekubali kusimamia haki hiyo.

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina ameliomba Bunge kuwawajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kwa kitendo cha kudharau Mahakama iliyoamuru wafugaji wa maeneo mbalimbali nchini walioshinda kesi mahakamani warudishiwe mifugo yao 6,000 iliyokamatwa na na Serikali.

Akichangia hotuba ya Makadirio ya mapato na Matumizi ya Wizara ya Malisiali na Utalii kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni Dodoma, Mpina amesema hadi leo viongozi hao wamekataa kutii amri hiyo ya Mahakama na kuwadhulumu haki wananchi hao na kwa makusudi wamevunja Katiba ibara ya 107A (i) inayoitaja Mahakama kuwa ndio yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki.

“Suala la wafugaji walioshinda kesi mahakamani lakini Serikali imekaidi kurudisha mifugo yao, katika Pori la Akiba la  Maswa na WMA ya Makao ng’ombe walikamatwa 1,739 walipoenda kwenye Mahakama Kuu Shinyanga wafugaji hao walishinda, wakaenda kwenye Mahakama ya Rufaa Tabora wakashinda ngombe jumla ya 1,739 mpaka leo hii hawajarejeshwa na Serikali” alisema Mpina.

Mpina alisema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwa kesi ya Jinai 136 ya mwaka 2017 ng’ombe 466 walikamatwa katika Pori la akiba la Swagaswaga ambapo ni ng’ombe 113 tu walirudishwa lakini wengine wote katika 466 hawajarudishwa mpaka sasa.

“Pori la Akiba la Muyowosi ambako ng’ombe 216 walikamatwa mpaka leo hawajarudishwa na Serikali katika ile hesabu ya ng’ombe 6,000 hii ni mifano tu Mh. Mwenyekiti ya wafugaji wetu ambao wameshashinda kesi mahakamani lakini Serikali haijarudisha mifugo yao”alihoji Mpina

Pia Mpina alisisitiza kuwa sio mara ya kwanza kulizungumza suala hilo bungeni kwani hata wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu alilizungumza suala hilo kwa uchungu mkubwa akiamini Serikali italizingatia.

“Nilizungumza wakati nachangia hotuba ya Mh. Waziri Mkuu hapa kwa uchungu mkubwa nikijua kwamba Serikali italichukulia hili maanani lakini nimesoma hotuba ya Waziri hakuna hata mstari mmoja alipozungumzia juu ya mifugo hawa, Mh. Mwenyekiti wewe unajua kwamba haki inatolewa na chombo gani nanukuu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107A(i) Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano  itakuwa ni Mahakama” alisema Mpina

Mpina alihoji iweje Mahakama imeshaamua ng’ombe warudishwe kwa wahusika lakini Serikali hawajarudisha mpaka leo ng’ombe hao wa wafugaji jambo lilioacha huzuni na umasikini mkubwa kwa wananchi hao.

“Waziri wa Malisiali na Utalii hajarudisha mifugo ya wananchi, Waziri wa Katiba na Sheria amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) amekataa kurudisha mifugo ya wananchi hawa wote Mh. Mwenyekiti wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wao wameapa kuitetea na kuilinda” alisema Mpina.

Mpina alihoji tayari wananchi hawa wameshinda kesi Mahakamani, Mahakama za Kuu zimeamua mifugo warudishwe, Mahakama ya rufaa imeamua mifugo warudishwe nani tena mtoa haki mwingine ambaye anasubiriwa.

“Mh. Mwenyekiti naomba Bunge lako liamua leo hatma ya mifugo ya wananchi hawa irudishwe kwa wananchi ambao wamepata mateso makubwa sana kwa muda mrefu na Serikali imeshindwa kurudisha mifugo yao hawa Mawaziri wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 107A(i) na Kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano imevunjwa na mawaziri hawa Mh. Mwenyekiti Bunge lako lichukue nafasi”alisema Mpina.

Akihitimisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujibu hoja za wabunge kuhusu bajeti hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro ameliambia Bunge kuwa wafugaji wote walioshinda kesi Mahakamani watarudishiwa mifugo yao kama hukumu zilivyoelekeza.

“Mh. Naibu Spika imeongelewa hapa watu wameshinda kesi lakini mifugo yao haijulikani ilipo hawajakabidhiwa Mh Naibu Spika nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria na sheria inatafsiriwa Mahakamani mtu akienda mahakamani ameshinda kesi lazima apate kile alichokishinda mahakamani” alisema Waziri Ndumbaro.

Hivyo Waziri Ndumbaro akaahidi kupitia Bunge kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu kesi zote ili kila mmoja aweze kupata haki inayostahili.

“Mimi niwaahidi waheshimiwa wabunge na niliahidi bunge lako tukufu tutafuatilia kesi zote hizi ili haki za wale walioshinda kesi mahakamani zisipotee, nimelichukua jambo hilo kwa umakini wa hali ya juu na niwaahidi tutakwenda kutekeleza”alisema Waziri Ndumbaro.

Bunge limepitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ya jumla ya sh 571,623,424,000.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger