Tuesday, 29 June 2021

Mpango Wa Tatu Wa Maendeleo Wa Taifa Wazinduliwa

...


 Na. Saidina Msangi, WFM,
Serikali imezindua rasmi Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26 unaotarajiwa kugharimu shilingi trilioni 114.8 ambapo Serikali itachangia Sh. trilioni 74.2 na sekta binafsi itachangia Sh. trilioni 40.6.

Mpango huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi umezinduliwa jijini Dodoma na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri kuu Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), alisema kuwa Mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, matokeo ya tafiti zilizofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali hapa nchini pamoja na dira ya Afrika Mashariki ya 2050.

“Mpango huu una dhima ya kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi na kuimarisha ukuaji wa uzalishaji wa ndani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu”, alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa alisema kuwa katika mpango huu wa tatu Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo kama ilivyokuwa katika mpango wa pili hususani ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Standard Gauge (SGR), Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Julius Nyerere (JNHPP) – 2,115 MW, Ujenzi wa Bomba la Mafuta - East African Crude Oil Pipeline (EACOP) na Ununuzi wa Meli na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani).

“Mpango huo una ushirikishwaji wa kitaifa na kimataifa na kuwa wote kwa pamoja tuna jukumu la kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa kikamilifu”, alisisitiza Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa ameielekeza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha ili kuwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.

Aidha Mhe. Majaliwa ameagiza wizara zote, taasisi za umma, idara zinazojitegemea wakala wa Serikali, sekta binafsi na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha kuwa ofisi zao zina nakala ya mpango huo ili kuwezesha utekelezaji wa viwango.

Amesisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa malengo ya mpango huo yatafikiwa na kuwa Serikali haitafumbia macho ukwepaji kodi, uzembe kazini, ufujaji wa fedha na rushwa.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Massauni (Mb) alisema kuwa mpango huo ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.

Alisema maandalizi ya mpango huo yameshirikisha kikamilifu makundi mbalimbali ya wadau wakiwemo sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, washirika wa maendeleo na jamii kwa ujumla umezingatia mahitaji halisi ya makundi yote.

“utekelezaji wa Mpango huu utahitimisha utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2011/12 – 2025/26) ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo ni: maisha bora kwa wananchi; amani, utulivu na umoja; utawala bora; jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza; na uchumi imara na shindani”, alisema Mhandisi Massauni.

Alifafanua kuwa  Serikali imeanza maandalizi ya Dira mpya itakayotekelezwa baada ya kuhitimishwa kwa Dira ya sasa mwaka 2025. Dira hiyo itaendeleza maono na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira 2025 ikijumuisha kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu.

Awali akizungumza katika ufunguzi huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa mpango huo umejikita katika maeneo makuu Matano ya kipaumbele ikiwemo kuchochea uchumi shindani na shirikishi.

Pia mpango huo umejikita katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa viwanda na utoaji wa huduma ambapo itajikita katika kujumuisha miradi ya viwanda  inayolenga kuongeza thamani kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumia rasilimali za ndani.

“Serikali inalenga kujumuisha programu za kuimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini kukuza uwekezaji na biashara”alisema Bw. Tutuba.

Aliongeza kuwa mpango huo pia unalenga kuchochea maendeleo ya watu ambapo Serikali inakusudia kutekeleza miradi itakayoboresha maisha ya watu ikijumuisha eneo la elimu na mafunzo eneo la afya na ustawi wa jamii, upatikanaji wa huduma za maji na uhifadhi mazingira.

Alisema katika kuendeleza rasilimali watu Serikali inajumuisha programu na mikakati mbalimbali ambayo inalenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini katika ngazi zote za elimu ili kuwawezesha vijana waweze kujiajiri.

Aidha katika kuhakikisha vipaumbele vilivyoelezwa vinatekelezwa kwa ufanisi na fedha zinazopatikana kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati mpango huo umeainisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ili kuwezesha uwepo wa uwajibikaji.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Nchini (UNDP) Bi. Christina Musisi, alipongeza Serikali kwa kukamilisha mpango huo kwa wakati na kueleza kuwa wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali watatumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji katika kufikia malengo ya dira ya maendeleo 2025 na ajenda 2030.

Alisema kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yatashirikiana na Serikali katika kutekeleza mpango huo wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Sekta Binafsi Bw. Zaki Mbena alisema kuwa mpango huo umetoa nafasi na fursa kwa sekta binafsi kutekeleza majukumu yake na kupata wigo mpana wa kufanya kazi na kupata maelekezo ili kufanikisha mpango huo kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa Sekta binafsi nchini itatoa mchango wake kwa Serikali unaokadiriwa kuwa shilingi trilioni 40.6 na hata kuzidi kwa kuwa sekta hiyo imeshirikishwa ipasavyo wakati wa maandalizi ya mpango huo ambao ameuelezea kuwa ni muhimu na unaungwa mkono.

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na unatarajiwa kuanza utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha 2021/22.

Mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya Maisha ya Watanzania wote.

MWISHO.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger