Emmy Mutaboyerwa (katikati) na wanae Daniela na Damita Mutaboyerwa.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia kijana mmoja aliyefahamika kwa majina ya Shedrak Kapanga (34), ambaye alikuwa ni msaidizi wa kazi za ndani ' House Boy' kwa tuhuma za kumuua bosi wake na watoto wake wawili kwa madai ya kwamba amekuwa akimgombeza mara kwa mara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Juni 12, 2021 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na baadhi ya vitu alivyoviiba baada ya kufanya tukio hilo.
"Tukio hilo limetokea Juni 9, 2021, mtaa wa Maryknol Masaki Dar es Salaam na mtuhumiwa Kapanga ambaye ni msaidizi wa kazi za ndani tumemkamata jana Juni 11, 2021, maeneo ya Magomeni akiwa kwenye harakati za kutoroka baada ya kuwaua Emilly Mutaboyerwa ambaye ni mama na Damita (13) na Daniela Mutaboyerwa (15)",amesema Kamanda Muliro.
Amesema vitu alivyokutwa navyo wakati akitoroka ni pamoja simu za marehemu, televisheni, king’amuzi cha DSTV na rimoti.
Amesema upelelezi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la mauaji Juni 9, 2021 baada ya kuwapiga kila mmoja kwa wakati tofauti kwa kitu kizito na kuwa sababishia kuvuja damu nyingi na kupoteza maisha.
"Baada ya kuwaua aliwafungia ndani na kutoroka. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ili kujua sababu za msingi za mauaji hayo na mara utakapokamilika mhusika/wahusika watafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo", ameeleza Kamanda Muliro
0 comments:
Post a Comment