Hafla ya utiaji saini hati za Maelewano (MOU), imefanyika leo Ikulu Jijini Zanzibar ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alishuhudia utiaji saini huo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya INTERTORCO yenye makao makuu yake mjini Madrid Hispania.
Utiaji saini Hati ya Maelewano kuhusu kazi ya Upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa Nishati ya Gesi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulisainiwa na Katibu Wizara ya Maji na Nishati Dk. Mngereza Mzee Miraji ambapo kwa upande wa Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP ilisainiwa na Allan Kessler Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ambaye pia ni mkuu wa Kampuni ya “Monitor Power System” .
Aidha, kwa upande wa Hati ya Maelewano juu ya ujenzi wa Bandari ya uvuvi aliyesaini kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Katibu Mkuu, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dk. Aboud Suleiman Jumbe ambapo kutoa Kampuni ya TANGEN & INTERTORCO GROUP , aliyesaini ni Injinia Michael Angaga ambaye ni wmakilishi wa Kampuni hiyo.
Mara baada ya utiaji saini hati hizo za Maelewano, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwahutubia wananchi waliofika katika hafla hiyo pamoja na wale waliokuwa wakifuatilia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambapo alisema kwamba Zanzibar imeanza safari mpya ya uchumi wa buluu.
Alisema kuwa amefurahishwa na utiaji saini mradi huo mkubwa ambao unajumuisha bandari za uvuvi Unguja na Pemba ambao utahusisha ujenzi wa maegesho ya meli za uvuvi zenye gati tano kwa upande wa Mpigaduri Unguja na gati mbili katika bandari ya Mkoani Pemba.
Aidha, alisema kuwa kutakuwa na ununuzi wa meli za uvuvi kwa ajili ya uvuvi bahari kuu, ujenzi wa chelezo cha kujenga na kutengeneza meli, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza boti ndogo kwa wavuvi, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nyavu na zana za uvuvi.
Ujenzi mwengine ni kiwanda cha kusindika minofu ya sakami, kiwanda cha kutengeneza mbolea itakayotokana na mabaki ya samaki, ujenzi wa soko la mnada wa samaki la Kimataifa, ujenzi wa majokofu mbali mbali ya kuhifadhia samaki, pamoja na Chuo Kikuu cha kufundishia uvuvi na ubaharia.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mradi huo ukitekelezwa uchumi wa Zanzibar utakuwa kwa haraka sana ambapo Serikali itatekeleza Mradi huo kwa mashrikiano na Kampuni 12, kutoka nchi tano za Norway, Hispania, Ujerumani, Korea Kusini na Marekani.
0 comments:
Post a Comment