Sunday, 5 July 2020

Waziri Lukuvi Ataka Wamiliki Wa Ardhi Wenye Hati Za Miaka 33 Kuzihuisha Ofisi Za Ardhi Za Mikoa

...
Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi ambao hati zao za ardhi zinaishia miaka 33 kwenda ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni kuzihuisha ili kupatiwa za miaka 99.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Mara wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Mara ambayo ni ofisi ya kumi na mbili kuzinduliwa ikiwa ni mfululizo wa kuzindua ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Alisema, kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi kwenye mikoa mbalimbali ambao viwanja vyao vimepimwa na michoro kuidhinishwa lakini hati zao ni za miaka 33 na wamiliki hao watakapoenda kuzichukua wanatakiwa kuziangalia ili zibadilishwe na  kupatiwa hati za miaka 99.

‘’ Hati nyingi za wale wamiliki ambao hawajazichukua zimekwisha muda wake, muende kwenye ofisi za ardhi za mikoa, huko mtaelekezwa na Wasajili Wasaidzi wa ardhi katika ofisi hizo namna ya kuzibadilisha ili mpatiwe za miaka 99’’ alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi,  zaidi ya wamiliki wa ardhi 50,000 kwenye mkoa Mara hawajachukua hati za ardhi wengi muda wa hati zao unaishia miaka 33 na kutaka kufika ofisi za ardhi mkoa wa Mara kurekebishiwa na kupatiwa za miaka 99 ili iwe rahisi kupata mikopo mikubwa .

Akizungumzia uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Mara, Lukuvi alisema mkoa huo umekuwa na migogoro mingi ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo utawawezesha wananchi wa Mara kumaliza migogoro kupitia ofisi hiyo badala ya kuipeleka migogoro kwake.

Waziri Lukuvi aliongeza kuwa, pamoja na Wizara yake hapo awali kushughulikia kero na migogoro ya ardhi lakini tatizo la kimfumo lilikuwa kubwa na kuweka wazi kuwa uzinduzi wa ofisi za mikoa unakomesha kero ambapo sasa hakutakiwa na gharama yoyote kwa mmiliki wa ardhi zaidi ya ile atakayolipia wakati wa kuomba hati.

‘’Mgogoro wa kimfumo ulikuwa mkubwa zaidi na leo hii tumekomesha kero na hakuna gharama yoyote mmiliki wa ardhi ataingia kufuatilia hati zaidi ya ile aliyolipa wakati wa kuomba hati, serikali ya awamu ya tano imeondoa kero zote kwa wananchi kwenye utawala wa ardhi’’  alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima alisema, ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko na kero nyingi na kati ya malalamiko kumi na mbili anayopokea kwa siku sita yanahusiana na ardhi na kusisitiza kuwa, mingi ya migogoro ya wananchi lazima nguvu hutumika jambo alilolieleza kuwa linaongeza gharama za kiafya katika masuala ya matibabu  na kubainisha kuwa uwepo ofisi ya ardhi katika mkoa huo utarahisisha huduma katika sekta ya ardhi..

‘’ Kila malalamiko kumi na mbili ninayopata ofisini kwangu sita ni ya ardhi na mengi yana sura ya kijamii na hapa kuna neno la msamiati ukisikia vyesi ujue ni kesi’’ alisema Malima.

Mmoja wa wakazi wa Musoma aliyepatiwa hati katika uzinduzi ofisi ya ardhi Bi. Mara Sophia Lugera alifurahishwa na usogezwaji huduma za ardhi mkoani Mara na kubainisha kuwa aliifuatilia kwa muda mrefu hati yake iliyokuwa ofisi ya Kanda Mwanza na kusema, baada ya kuipata hati ataitumia kuchukulia mkopo benki ili aendeleze biashara yake ya ujasiriamali.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara inayojulikana kama Mawalimu Nyerere Memorial Hospital iliyopo eneo la Kwangwa Musoma mkoa wa Mara.

Akiwa katika mradi huo, Lukuvi aliagiza kukamilika kwa jengo ya Huduma ya Mama na Mtoto kufikia mwisho wa mwezi huu ili lianze kutumika kwa wananchi wa mkoa huo na Mikoa jirani.

Alisema, ujenzi wa jengo hilo umechukua muda mrefu na anataka kuona sehemu ya jengo hilo inakamilika kufikia julai 31 mwaka huu na Agosti mosi 2020  atamuagiza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenda kuona kama agizo lake limetekelezwa kama alivyoahidiwa.

Mhandisi na Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Hosiptarli ya Rufaa mkoa wa Mara Renald Kazyoba alisema, kimsingi sehemu ya ujenzi wa mradi huo sehemu ya Huduma ya Mama na Mtoto (Wing C) itakamilika kama alivyoagizwa kwa kuwa kazi kubwa imefanyika.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger