Tuesday, 5 May 2020

Ndege iliyobeba vifaa vya kupambana na corona yaanguka na kuua 6 Somalia

...
Watu sita wameaga dunia katika ajali ya ndege ya mizigo iliyokuwa imebeba misaada na vifaa vya kupambana na janga la corona katika mji wa Bardale, kusini mwa eneo la Bay nchini Somalia.

Shirika la Habari la Somalia limetangaza kuwa, ndege hiyo ni ya shirika la African Express Airways yenye makao makuu yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi na kwamba ilianguka jana katika mji huo, ikiwa njiani kuelekea Baidoa ikitokea mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mohamed Salad, Waziri wa Uchukuzi wa Somalia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, sita waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni rubani na msaidizi wake, rubani mwanagenzi, mhandisi wa ndege pamoja na wahudumu wawili.

Msemaji wa serikali ya Somalia, Ismael Mukhtar Omar amethibitisha kuwa, ndege hiyo ndogo ya Kenya iliyokuwa imebeba watu sita ilianguka jana kusini magharibi mwa Somalia wakati wa kutua. Vyombo vya usalama vya Somalia vinachunguza chanzo cha ajali hiyo.

Duru za habari zimearifu kuwa, ingawaje kuna uwepo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika mji huo wa Bardale, lakini eneo palipotea ajali hiyo hususan uwanja wa ndege wa  Bardale unalindwa vikali na askari wa Somalia wakishirikiana na wanajeshi wa Ethiopia.

Baadhi ya ripoti zinadai kuwa, ndege hiyo iliyokuwa imebeba misaada ya kibinadamu ilitunguliwa kimakosa na askari wa jeshi la Ethiopia wanaofanya chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger