Jeshi la Polisi mkoani Kagera linamshikilia kinyozi wa Arusha, anayedaiwa kuiba na kuvaa sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) za baba mkwe wake na kuzitumia mkoani hapa kutapeli vijana kuwa anaratibu uandikishaji kwa wanaohitaji kujiunga na jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amemtaja mtuhumiwa kuwa ni Mrisho Ibrahim (34) mkulima na kinyozi, mkazi wa Mtaa wa Kimandolu jijini Arusha.
Alisema Ibrahim ambaye alikwenda mkoani Kagera kwa lengo la kumtembelea rafiki yake wa kike, alikamatwa Mei 5, mwaka huu Kamachumu wilayani Muleba akiwa na sare kamili baada ya kujitambulisha kwa uongo kuwa ni mwajiriwa na askari wa JWTZ mwenye cheo cha Private kikosi cha Mizinga Arusha.
“Baada ya kufika mkoani Kagera na kumkosa mpenzi wake ambaye alikuwa amehama nyumba, aliishiwa fedha ndipo akaamua kutumia sare hizo kufanya utapeli.
“Mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Ruto, ambako alipangishiwa na mwenyeji wake ambaye ni askari mgambo aliyemtaja kwa jina moja la Rweyemamu,” alidai Kamanda Malimi.
Alidai kuwa katika mahojihano mtuhumiwa alikiri kuwa si mwajiriwa wa JWTZ na kwamba sare hizo ni mali ya baba mkwe wake ambaye ni askari wa jeshi hilo.
Kamanda Malimi alidai kuwa Ibrahim alisema kwamba alizichukua sare hizo baada ya kukabidhiwa jukumu la kuwa mwangalizi wa makazi ya baba mkwe ambayo yapo Arusha Kimandolu.
“Aliamua kuvaa sare hizo na kuja nazo hadi Muleba Kagera ambako alimfuata rafiki yake wa kike (mchepuko), lakini akamkosa baada ya kuwa amehama, ndipo kutokana na kukosa fedha akamuona huyo askari mgambo na kumdanganya kama anataka kazi ya JWTZ atafute pesa na hata kama kuna vijana wengine apelekewe wakiwa na fedha.
“Hadi anakamatwa alikuwa anatafutiwa vijana hao. Hivyo tunaendelea na upelelezi, ushahidi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Malimi.
0 comments:
Post a Comment