Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (SACP) Willbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari. Mezani ni simu zilizokuwa zinatumiwa na mtuhumiwa Awadhi Lugoya kusambaza taarifa za upotoshaji kuhusu Corona.
Na Jackline Lolah Minja - Malunde 1 blog
Mkazi wa Mtaa wa Mazimbu Manispaa ya Morogoro Awadhi Lugoya anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani morogoro kwa tuhuma ya matumizi mabaya ya mitandao kwa kufungua akaunti kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook inayofahamika kwa jina CORONA VIRUS TANZANIA na kutoa taarifa za upotoshaji za ugonjwa wa Corona.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo aprili 4,2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (SACP) Willbroad Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo baada ya kufungua akaunti hiyo amekuwa akitoa taarifa zisizo sahihi na zenye upotoshaji mkubwa kwenye jamii licha ya serikali kutoa onyo kuhusu utoaji wa taarifa za upotoshaji kuhusu ugonjwa huo.
"Mnamo tarehe 1 mwezi aprili mwaka huu majira ya saa 11 jioni jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata kijana mmoja aitwaye Awadhi Lugoya kwa matumizi mabaya ya mtandao wa kijamii ( facebook) kutoa taarifa zisizo rasmi za upotoshaji kuhusu ugonjwa wa corona, mahojiano yanaendelea yakikamilika atafikishwa mahakamani",alisema Kamanda Mutafungwa.
Aidha Kamanda Mutafungwa ametoa tahadhari kwa wakazi wa Morogoro hasa wanaotumia mitandao ya kijamii kuwa makini kuhusu utoaji wa taarifa juu ya ugonjwa wa corona.
Katika hatua nyingine jeshi la polisi limefanikiwa kumkamata mwanamke mmoja maeneo ya kata ya tungi kwa tuhuma za wizi wa bodaboda kwa kutumia nguvu akishirikiana na watu wengine.
"Siku ya tarehe 3 mwezi wa nne mwaka huu majira ya saa tano usiku maeneo ya kata ya Tungi Udhuruni ndani ya manispaa ya Morogoro tulifanikiwa kumkamata bwana Geofrey (30-35)akiwa ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na tulibaini alikuwa na mwanadada aitwaye Lightness John ambaye kwa sasa ni majeruhi amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro akiwa amevunjika mguu, hawa nia yao ilikuwa ni kuiba bodaboda ila wananchi waliwawahi dada huyo yuko chini ya ulinzi mkali upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani",amesema.
0 comments:
Post a Comment