Na Salvatory Ntandu - Shinyanga
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imelipatia ufumbuzi tatizo la wakazi wa mkoa wa Shinyanga la kufuatilia hati za nyumba katika ofisi za ardhi Kanda ya Magharibi zilizopo mkoani Simiyu kwa kufungua ofisi mpya mkoani humo ambayo itakuwa na mamlaka ya kutoa nyaraka hizo mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Machi 13,2020 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika kikao maalumu na viongozi waandamizi wa mkoa wa Shinyanga cha Kumtambulisha Kaimu kamishina wa ardhi wa mkoa huo, Hezekiel Kitilya.
Alisema kuwa hapo awali wananchi wa mkoa wa Shinyanga walikuwa wanatumia fedha nyingi kufuatilia hati za nyumba zao mkoani Simiyu na kutumia gharama kubwa jambo ambalo linasababisha wananchi wengi kutopata hamasa ya kuwa na hati za nyumba kutokana na usumbufu huo.
“Kuanzia sasa masuala yote ya ardhi mkoani Shinyanga yatafanyika hapa na Ofisi yangu imeleta maafisa wenye mamlaka ya kutatua migogoro ya ardhi,upimaji,upangaji wa miji,na utoaji wa hati bila ya kutegemea ofisi za kanda zilizopo mkoani Simiyu”,alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa Ofisi hiyo itasaidia kuipunguzia gharama serikali ya mkoa huo kwa maafisa wake kufuatilia hati au kupeleka nyaraka za ardhi mkoani Simiyu ambapo kwa mwaka mmoja halmashauri za Mji Kahama na Manispaa ya Shinyanga zimetumia zaidi ya shilingi milioni 40 kufuatilia nyaraka hizo.
Awali akimkaribisha Waziri Lukuvi, Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela alisema kuwa kwa sasa mkoa huo umejipanga kutatua changamoto za ardhi kwa kupima,kupanga na kuwarasimishia makazi wanachi katika wilaya zote.
“Halmashauri zetu zimeshaanza kupima viwanja katika mji na vijiji ambayo inakua kwa kasi ili kuwapa fursa ya kupata hati miliki za ambazo zitawasidia kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha hapa nchini”,alisema Msovela.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza katika kikao maalumu na viongozi waandamizi wa mkoa wa Shinyanga cha Kumtambulisha Kaimu kamishina wa ardhi wa mkoa huo, Hezekiel Kitilya.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza katika kikao maalumu na viongozi waandamizi wa mkoa wa Shinyanga cha Kumtambulisha Kaimu kamishina wa ardhi wa mkoa huo, Hezekiel Kitilya.
0 comments:
Post a Comment