Wednesday, 11 March 2020

Bilioni 66.5 zapatikana tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nCHINI

...
Na Greyson Mwase, Dodoma
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini mapema Machi mwaka jana jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 66.5 zimepatikana na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Profesa Manya ameyasema hayo leo tarehe 11 Machi, 2020 kupitia mahojiano maalum jijini Dodoma na kueleza kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mwezi Machi, 2019 hadi kufikia mwezi Januari, 2020 usimamizi wa masoko ya madini nchini umeendelea kuimarika ambapo, katika kipindi husika kilogramu 9,237.34 za dhahabu; karati 12,973.14 za madini ya almasi; kilogramu 20,099.17 za madini ya bati; na kilogramu 514,683.28 za madini ya vito mbalimbali ziliuzwa kupitia masoko hayo na kuipatia Serikali jumla ya shilingi bilioni 66.57.

Akielezea mfano wa masoko yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuipaisha Sekta ya Madini, Profesa Manya alielezea Soko Kuu la Dhahabu Geita ambapo alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, ukusanyaji wa mapato ulikuwa wastani wa Shilingi 599,046,378.47 yaliyotokana na wastani wa mauzo ya Kilogramu 101.97 kwa mwezi kwa takwimu za kipindi cha miezi mitano kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Alisema kuwa, baada ya kuanzisha soko, makusanyo yaliongezeka hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 2.39 kwa mwezi yaliyotokana na wastani wa mauzo ya Kilogramu 360.94 zilizouzwa katika kipindi cha miezi 11 tangu soko hilo kuanzishwa Machi, 2019 hadi Januari, 2020 na kuongeza kuwa ongezeko hilo lilitokana na uwazi katika biashara ya madini ya dhahabu kwa kuwepo kwa soko hilo.

Aliongeza kuwa, kwa kipindi cha mwezi Oktoba, 2019 pekee katika Soko Kuu la Dhahabu Geita, Serikali ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kutokana na mauzo ya kilogramu 537.6 zilizouzwa.

Akitolea mfano wa soko jingine la madini la Chunya lililopo Mkoani Mbeya, Profesa Manya alifafanua kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, kiasi cha wastani wa Shilingi 177,965,811.06 kilichotokana na mauzo ya dhahabu yenye uzito wa wastani wa Kilogramu 29.67 kilikuwa kikipatikana kwa mwezi kwa takwimu za kipindi cha miezi minne (4) kabla ya kuanzishwa kwa soko.

Aliendelea kusema kuwa, mara baada ya kuanzishwa kwa Soko la Madini la Chunya mapema Mei, 2019 ndani ya kipindi cha miezi tisa Serikali ilikusanya kiasi cha wastani wa Shilingi 961,009,348.85 kilichotokana na mauzo ya dhahabu kwa wastani wa Kilogramu 176.24 kwa mwezi.

Awali akielezea uanzishwaji wa masoko ya madini 28 na vituo vya ununuzi wa madini 28 nchini Profesa Manya alisema kuwa kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kulitokana na changamoto kubwa iliyokuwa inaikabili Sekta ya Madini kwa kipindi kirefu, hasa ya utoroshaji na biashara haramu ya madini.

Akielezea manufaa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini Profesa Manya alieleza kuwa ni pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata huduma ya masoko na upatikanaji wa bei stahiki za madini yanayouzwa na wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uwazi katika biashara ya madini, kuimarika kwa ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli na kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini na hivyo kusaidia upatikanaji wa mapato stahiki ya Serikali kupitia tozo za mrabaha (6%) na ada ya ukaguzi (1%) za mauzo ya madini kwenye masoko.

Mafanikio mengine ni pamoja na upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo ya madini yanayozalishwa na kuuzwa na wachimbaji pamoja na wafanyabiashara wadogo wa madini nchini kupitia masoko.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger