Wednesday, 4 December 2019

Serikali Yawafichua Watoto 16,000 Wenye Ulemavu Waliofichwa Na Kuwaandikisha Shule

...
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa amesema Serikali imewafichua na kuwatambua jumla ya watoto 16,000 wenye ulemavu wa aina mbalimbali waliokuwa na umri wa kwenda shule katika mikoa yote hapa nchini waliokuwa wamefichwa na kuwaandikisha shule kulingana na mahitaji yao ya msingi.

Naibu waziri Ikupa ameyasema hayo Desemba 03, 2019 katika Maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

“Watoto wenye mahitaji maalum waliokuwa wamefichwa Serikali imewatambua na kuwaandikisha shule kulingana na mahitaji yao ya msingi, watoto 16,000 wametambuliwa kutoka mikoa na halmashauri zote nchini isipokuwa Halmashauri tisa tu ambazo hazijafikiwa kwa kuwa zoezi hili ni endelevu kadri bajeti itakavyoruhusu nazo zitafikiwa,”alisema Ikupa.

Aidha akijibu baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na  Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) kuhusiana na kutengewa bajeti  ndogo amesema kuwa tayari serikali imetenga milioni 30 kwa ajili ya kuliwezesha baraza la watu wenye ulemavu  kufanya kazi kwa ufanisi, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuongeza nguvu katika kuwasaida watu wenye ulemavu hususani walio katika maeneo ya pembezoni.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri  Ikupa ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutenga nafasi maalum za uwakilishi bungeni kwa watu wenye ulemavu kama kilivyofanya Chama Cha Mapinduzi( CCM), huku akiwasisitiza wenye ulemavu na wao kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi badala ya kusubiri nafasi maalum pekee.

Awali akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi amesema Simiyu inawathamini na kuwajali watu wenye ulemavu huku akibainisha kuwa Halmashauri zimetenga zaidi ya shilingi milioni 231 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa watu wenye ulemavu na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo ili wajikwamue kiuchumi.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bibi. Tungi Mwanjala ameiomba Serikali   kuviwezesha viwanda vya ndani kutengeneza vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili kupunguza gharama zitokanazo na kodi ya kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi.

Naye mmoja wa Watu wenye ulemavu Bi Nuru Awadh amesema katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano watu wenye ulemavu wameaminiwa  katika nafasi mbalimbali na sheria nyingi zinazowahusu watu wenye ulemavu zitakelezwa kwa vitendo.

Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli Mbiu inayosema: “HAMASISHA USHIRIKI WA WATU WENYE UELMAVU NA UONGOZI WAO: TEKELEZA AGENDA ENDELEVU 2030”

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger